Home Makala Chadema waachwe waandamane

Chadema waachwe waandamane

882
0
SHARE

Na. M. M. Mwanakijiji

KUZUIA au hata kupiga mkwara mpango wa CHADEMA katika mpango wa UKUTA wenye lengo la kuandaa maandamano na mikutano kuanzia Septemba Mosi, ni kuwapa nafasi ya umuhimu ambao naamini wameupoteza. Njia hii ya maandamano ilikuwa na mashiko wakati fulani lakini sasa hivi sitoshangaa ikawa na mashiko kwenye kundi fulani hivi.

Sasa, hakuna sababu ya kuzuia maandamano yao, binafsi ningependa Serikali siyo tu iwape ruhusa ya kufanya hivyo, iwahakikishie ulinzi mahali pote ambapo wataandamana. Lakini pia wajue kama ilivyo siasa, wapo na wengine ambao watakuwa tayari kuandamana kuiunga mkono Serikali na hili linaweza kuvuruga upinzani kwa kiwango ambacho bado hakijafikiriwa.

Inawezekana wapo Watanzania ambao wanaunga mkono hisia na maono ya wapinzani kuwa Serikali ya sasa hivi ni kali sana, inabana sana na inasimamia sana sheria kiasi kwamba inaonekana ni ya kidikteta. Inawezekana wapo watu ambao wanaona kabisa kuwa Rais wa sasa asiyecheka cheka, anayesema analomaanisha, asiyechelewa kuchukua hatua (mpya au za kusahihisha hatua za awali) anaonekana ni kama mtu wa tofauti sana kulinganisha na viongozi tuliowazoea. Inawezekana kabisa kuwa jinsi serikali inajaribu kusimamia fedha za umma na kuwashughulikia viongozi wabovu inaonekana haina huruma kweli na haina utu na hivyo ina alama zote za serikali ya kibabe.

Inawezekana watu hao wapo kweli na wanaamini hivyo, na wanapenda au wangependa Magufuli na watendaji wake walegeze kamba kidogo watu wapumue. Nimesoma tena mahali fulani kuna watu wameomba kabisa kuwa hali ni ngumu sana, zile fedha za kuchezea chezea hazipo tena na watu wanatamani warudi “Misri” ambako walikuwa wanakula nyama za kuchoma, na kufurahia maisha katika utumwa wa ufisadi!

Wako radhi warudi utumwani kwenye raha bila uhuru kuliko kwenda mahali wawe huru na kutengeneza maisha mapya wenyewe siyo ya wale wanaowatumikisha. Nakumbuka mwanasiasa mmoja alifika mahali na kutangaza kuwa kabisa anamiss zama zile za maisha yale!

Sasa inawezekana wapo pia Watanzania ambao wanakubaliana na simulizi (narrative) hili la wapinzani na wajumbe wao. Na inawezekana Watanzania hao wanaweza hata kufikia maelfu; kwamba kwa kweli wanaona nchi iko vibaya, sheria hazifuatwi, kuna kusimikwa kwa udikteta, na wanaamini kabisa kuwa hali ikiendelea hivi wao wataingia Ikulu kirahisi 2020. Inawezekana kabisa hawa ndugu zetu wanaamini wanafanya hivyo kwa sababu wanaongozwa na uzalendo!

Lakini naomba kupendekeza kuwa inawezekana kuna jambo jingine kubwa zaidi; kwamba, inawezekana wapo Watanzania ambao zama hizi kweli kwao ni mpya na zimeanza kuwapa heshima ya utu wao. Inawezekana Watanzania hawa wanafurahia kuona uongozi usio na mchezo, wenye viongozi ambao wanasimama kuinua maisha ya Watanzania na kuwaongoza kuelekea mafanikio ya kweli.

Inawezekana kabisa wapo hata viongozi na watendaji wengine ambao kwa miaka mingi walikuwa wanatamani nchi iwe kwenye mstari fulani unaoeleweka na sasa wamepewa nafasi hiyo na wao wanaanza kuonesha uongozi na kutenda kwa weledi wa kazi na majukumu yao.

Na inawezekana kabisa wapo Watanzania wengi na labda kwa mamilioni ambao wanaamini kabisa kuwa huu ni wakati wa taifa letu kwenda mbio. Baba wa Taifa aliwahi kusema miaka ya sitini kuwa “Yatupasa kukimbia wakati wao (nchi zilizoendelea) wanatembea”. Labda kwa miaka ishirini na ushee hivi Watanzania waliaminishwa kuwa na wao wameendelea siyo tu waliacha kukimbia bali walifika mahali wakakaa chini na kupiga gumzo.

Sasa kaja Rais anayewaambia waamke na waanze mbio tena na wapo ambao wanaonekana wamechoka. Walizoea kukaa na kupiga soga, kula wakiamini vinatosha na wakitafuna hata vya urithi! Sasa Rais anawaambia muda wa kukaa chini haupo tena, muda wa kuchekeana na kupiga soga haupo tena, kwamba sasa ni wakati wa kufanya kazi kwani maendeleo ya kweli yanatokana na kazi na hawa watu sasa wanaanza kuona jasho linakuja. Walizoea kujipepea huku wamekunja nne lakini sasa wanaambia muda kukimbia umeanza!

NI vigumu mno kumfanya mtu asiyejua kukimbia aanze kukimbia kwani ana vikwazo vingi sana. Kuanzia vya kimaumbile hadi havi vya kisaikolojia. Mtu huyo ukimwambia twende tukimbie atakueleza mambo mengi;

“sijakimbia muda mrefu”

“Kwanini nikimbie, naweza kujaribu kutembea kwa haraka”

“tangulia ntakukuta ngoja kwanza ninyoshe viungo”

“Tukimbie tena, kwanini bana, tutembee tu na sisi tutafika”

Mtu kama huyo unahitaji kumpa sababu ya kukimbia; mtu wa namna hiyo unataka kumuwekea mnyama kama simba mwenye njaa, ndio utaona jinsi gani ataamka haraka na kuanza kukimbia! Watanzania wamewekewa uongozi mkali, usio na utani na ambao naamini unahitaji kuongeza ukali zaidi ili watu wajue kuwa zama hizi ni mpya kweli kweli!

Inawezekana hata wanaopinga watapinga huku na wao wanakimbia! Sasa wasizuiwe. Kama walivyoandamana wakati wa Dk. Slaa na wakapewa ulinzi hili linaweza kufanywa vizuri kabisa.

Waacheni waandamane, waacheni wapinge. Lakini tuwape nafasi Watanzania wengine nao wenye kuunga mkono mabadiliko na kumuunga mkono Rais na ajenda yake na wao waandamane. Ninaamini walio upande wa mabadiliko ya kweli ni wengi zaidi kuliko wale waliosalimu amri kwenye mabadiliko mengine.

Tumeshuhudia juzi juzi Uturuki ambapo yalijaribiwa mapinduzi ya kijeshi, lakini Rais alipojitokeza – Rais ambaye hata wapinzani walikuwa wanasema ni dikteta – akawaita watu kumuunga mkono na maelfu walikuja mitaani. Naamini, Njia hii ya maandamano inataka kuua upinzani mara moja daima kwa sababu wakiandamana wao, halafu na upande wa pili ukaandamana nchi nzima, ujumbe utakaotumwa utakuwa ni wa fundisho la kihistoria na utatua kwenye mioyo ya baadhi yao kama shoka la Umsolopagas!

Inawezekana labda ndio njia pekee ya kulazimisha wapinzani kurudi na kufanya siasa ya kweli na kukubali kuwa hizi ni zama mpya, na wao lazima wabadilike. Mbinu zile zile zilizowavuruga wakizirudia tena zitawavuruga kwa sababu ajenda kuu waliyokuwa nayo haipo tena na haiwezi kusimama ikaaminika tena. Na hii ya “Udikteta” itaanguka yenyewe, kwani hata Nyerere wapo waliomuita sana Dikteta, lakini nina uhakika wanashangaa hadi leo kwanini wananchi wengi wa kawaida wanamuona na kumheshimu kama Rais aliyewajali wao na maslahi yao kweli kweli labda kuliko mwingine. Labda hadi ujio wa Magufuli.

www.zamampya.com