Home Makala Chadema wameonesha ukomavu kisiasa

Chadema wameonesha ukomavu kisiasa

1707
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA

BAADA ya vuta nikuvute ya siku kadhaa hatimaye Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefikia uamuzi wa kuwaweka chini ya uangalizi wabunge wake wawili Saed Kubenea (Ubungo) na Antony Komu (Moshi Vijijini).

Wabunge hao wamewekwa chini ya uangalizi baada ya sauti zinazoaminika kuwa ni za wabunge hao kusambaa katika mitandao ya kijamii wakisikika wakipanga kumshughulikia Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniphace Jacob na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.

Japo awali wabunge hao walikataa kuwa sauti hizo si za kwao na kudai kuwa kuna watu wanaendeleza mchezo mchafu wa kuwachafua, mara hii wamlikiri mbele ya kamati kuu kuwa ni za kwao na kwamba yalikuwa majadiliano ya kawaida kutokana na taarifa waliyokuwa wameipata jamaa yao mmoja waliyekuwa wamekutana naye.

Uamuzi wa kuwekwa chini ya uangalizi wabunge hao ulitangazwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, baada ya kumalizika kikao hicho cha dharura kilichoketi kuwajadili wawili hao.

Kwa mujibu wa Mnyika wahusika wote walikiri kuwa sauti hizo ni za kwao na hivyo wakakutwa na hatia ya kukiuka kanuni na maadili ya chama hicho.

Pamoja na kuwekwa chini ya uangalizi pia kamati hiyo iliwapa onyo kali na kuwaagiza waandike barua za maelezo na kuwataka kuwaomba radhi wahusika na chama kwa ujumla huku wakivuliwa nafasi zote za uongozi ndani ya chama.

Kabla ya uamuzi huo Kubenea alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani na Komu alikuwa jumbe wa kamati ya utendaji katika kanda ya Moshi.

Wabunge hao walikiri kuwa sauti hizo ni zao huku Komu akisema suala hilo halikuwa na agenda yoyote ya siri, na kwamba yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida tu ambayo hayakuwa na nia au dhamira yoyote mbaya.

Kubenea kwa upande wake anasema siku zote wamekuwa wakishirikiana na Meya Jackob na kwamba hawana mgogoro naye huku akiongeza kuwa Boniface ni miongoni mwa marafiki zake wa karibu.

Inadaiwa katika baadhi ya viongozi akiwamo Mbowe, Jacob na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho walitaka wabunge hao waoneshwe mlango wa kutokea wakiamini kitendo walichokifanya ni usaliti kwa chama.

Kwa mujiubu wa gazeti moja la Kiswahili lilidai kuwa viongozi hao walikuwa wanashikilia hoja kuwa wawili hao walihusika katika njama ya kuwamaliza Mbowe na Jacob kwa maana ya kula njama ili kupoteza maisha yao.

Huo ndiyo uliokuwa msimamo wao tangu wanaingia katika kikao hicho kabla ya kukumbana na ukinzani kutoka kwa baadhi ya wanachama na viongozi wengine wa chama hicho ambao hawakuafiki uamuzi huo kwa madai kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha unaodhihirisha njama ya wawili hao kutaka kuwamaliza Mbowe na Jacob.

Baadhi ya wanaodaiwa kupiga uamuzi huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vicent Mashinji, mawaziri wakuu wastaafu na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Edward Lowassa na Fredrick Lowassa na viongozi wengine wa chama hicho.

Inadaiwa kuwa Lowassa alipinga uamuzi huo kwa madai kuwa hakuna ushahidi wa kutosha na kwamba mtu mmoja kusema fulani amalizwe haina maana kwamba kupanga mauaji huku akisisitiza kuwa kumaluzwa inawezekana walipanga ya kisiasa.

Kwanza niwapongeze viongozi waliopinga uamuzi huu wa kufukuzwa wabunge hao kwa uamuzi wa busara waliouchukua na hatimaye kuzima matokeo hasi ambayo yangeweza kujitokeza si tu kwa chama bali kwa Taifa pia.

Bila shaka Lowasa anatambua fika gharama ya kiongozi kufukuzwa uanachama kutokana na uzoefu wake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alichokitumikia ujana wake wote hadi hapo alipoamua kukihama mwaka 2015 baada ya kuondolewa katika mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Ni wazi kuwa endapo chama hicho kingefikia uamuzi wa kuwafuta uanachama wabunge hao siyo tu wao ambao wangepoteza ubunge wao katika majimbo ya Ubungo na Moshi Vijijini wanakoongoza wabunge hao bali hata chama kingeyaweka rehani majimbo yake kwa kulazimika kurejea katika uchaguzi mdogo wa marudio ambao kwa historia na mwendendo wa siasa za sasa hawawezi kujipa nafasi kubwa ya kuyatetea majimbo yao.

Lakini tunapaswa kukubaliana kuwa Chadema bado ni chama kidogo ambacho kinaendelea kujijenga kuweza kutoa ushindani wa kwele kwa CCM na si ushindani wa bla bla, kwa hiyo ni lazima viongozi wake wakubali kuwa wavumilivu hata kwa mambo magumu.

Siamini kama ni sahihi kwa chama chenye wabunge 45 kati ya majibo 264 ya uchaguzi 264 kuanza kuwafukuza wanachama wake tena wanaowakilisha majimbo makosa ambayo yanaweza kuzungumzwa na kupata majawabu yenye kutoa adhabu mbadala.

Endapo wangefikia uamuzi wa kuwatimua wabunge hao wangekuwa wanajinyong’onyeza wenyewe kwa kutoa nafasi kwa chama tawala ambacho bila shaka kinayo nguvu kubwa ya kuweza kuyatwaa majimbo hayo kupitia uchaguzi na kwa kuzingatia kuwa kimekuwa na historia nzuri katika chaguzi nyingi za marudio.

Pili Chadema ilikuwa inaingia katika historia ya kuliletea Taifa hasara ya mabilioni ya fedha kwa kuandaa uchaguzi mwingine wa kupata wawakilishi wa majimbo hayo jambo ambalo wao kama chama wamekuwa wakilipinga mara kadhaa hasa pale wabunge wao na wa vyama vingine vya upinzani wanaojivua uanachama wa vyama vyao na kujiunga na CCM.

Tukio la Kubenea na Komu lilikuwa ni jaribio ambalo lilihitaji kuweka kando hisia, hasira na visasi miongoni mwa wana-kamati ili kuupata mwafaka wenye kujenga usioongozwa na mihemko.

Endapo wajumbe wangeongozwa kwa mihemko na kutazama baadhi ya matukio ya nyuma hasa yale yanayomhusisha Kubenea kutaka kukihama chama hicho na kujiunga na CCM ni wazi kuwa hadi sasa wasingekuwa wabunge.

Ukitazama majina ya Lowassa, Sumaye na Mashinji ambao wanatajwa kuwa ndiyo waliopinga na kuishinda nguvu ya mwenyekiti na wafuasi wake kuwafuta uanachama wawili hao ni wazi kuwa chama kinauona umuhimu wa kuwa na wanachama wenye ukomavu wa kisiasa na wanaoweza kuzishinda hisia za wengi pale yanapojitokeza mambo magumu.

Kwa kuhitimisha niseme wazi kuwa katika hili Chadema wameonesha ukomavu ambao ndiyo msingi wa mapambano yoyote hasa katika ulingo wa siasa.