Home Habari CHADEMA YAJA KIVINGINE

CHADEMA YAJA KIVINGINE

861
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)kimesema Operesheni yake ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu matendo yaliyowasukuma kuanzisha opareshani hiyo sasa yanawakuta Watanzania wengi bila kujali itikadi za vyama vya siasa, dini, rangi au kabila.

Katibu Mkuu wa Chadema, aliliambia RAI, kuwa dhamira kuu ya Ukuta ilikuwa ni kuyapinga matendo yote ya kidikteta yaliyokuwa na yanayofanywa na serikali.

Dk. Mashinji, amesema walifanya hivyo kwa sababu walishaona dalili na ishara za kidikteta, hatua iliyowasukuma kuanzisha operesheni hiyo ambayo ilionekana kuwekewa vikwazo.

Alisema hata hivyo Chadema sasa inafurahia kwa sababu tayari maamuzi yenye vimelea vya kidikteta yameanza kuonekana wazi wazi kwa watu wa upinzani na hata waliomo ndani ya CCM.

Alisema viashiria hivyo ni pamoja na wabunge kukamatwa bila sababu, watumishi kufukuzwa kazi bila kujali utu, mtu mmoja kufanya maamuzi bila kushirikisha wenzake na matendo mengine kama hayo.

Alisema matendo kama yale ya kutishia wabunge wa CCM silaha ni moja ya ishara za mafanikio ya ukuta kwani sasa jamii inajua nini Chadema ilitaka kufanya.

Alisema hatua hiyo ya jamii sasa kuijua maana ya Ukuta inafungua milango ya wao kuiendeleza operesheni yao, ambayo imeshaanza kutekelezwa kivingine kwenye mikoa mbalimbali.

“Mara baada ya kumaliza mkutano wetu wa Baraza Kuu uliofanyika mkoani Dodoma, kila mjumbe alitoka na azimio la kuendeleza oparesheni ya Ukuta na tayari imeshaanza kutekelezwa katika baadhi ya mikoa na tunaelekea kushinda,”alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu opereshenji hiyo, Dk. Mashinji alisema jamii inafikiri operesheni hiyo ilikufa, jambo ambalo si la kweli.

“Operesheni Ukuta haijafa na si kama inafufuliwa sasa, hii operesheni inaendelea, tulichokifanya sasa ni kuongeza hamasa ili kuirejeshea dhamira kuu iliyokusudiwa,”alisema.

Dk. Mashinji alisema kuwa kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo Ukuta unaendelea kumgusa kila mtu bila kujali nafasi yake.

“Hatukuwahi kusema kuwa Ukuta  umevunjika bali tunaendelea kuongeza hamasa, ukuta wetu bado unaendelea kujengwa na tunaelekea kuwa washindi.

“Sote ni mashahidi kwani kila kukicha tunashuhudia namna ambavyo Ukuta unavyoendelea  kuwagusa watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa serikali, Waandishi wa Habari, wafanyabiashara na makundi mengine, hivyo watu wanaendelea kuona dhamira yetu, lazima tukubali mambo yote  yanayoendela ni sehemu tu ya Ukuta,” alisema Dk. Mashinji.

Katika hatua nyingine, Dk. Mashinji aliongeza kuwa ni jambo lisilokubalika kuendelea kuona kunafanyika mambo na maamuzi yasiyofuata sheria liwemo suala la kuingilia mihimili ya dola.

“… ni jambo lisilokubalika kuona mtu unadharau Mahakama, Bunge, unakamata vitu bila kufuata sheria, tulichoamua ni kuuendeleza ujenzi wa Ukuta,” alisema.

Dk. Mashinji alisisitiza kuwa mbali na mamabo mengine operesheni hiyo msingi wake mkuu nji kudai haki, huku akisisitiza kuwa kampeni hiyo inaendelea kushika kasi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.

“Ukiona umenyang’anywa haki yako, unapaswa kulazimisha kuichukua maana duniani kote haki haiombwi, … kama mtu anapotea katika mazingira ya kutatanisha, unaanzaje kubembeleza arudishwe,  sasa ni lazima tuichukue, ,” alisema.

Kwa mara ya kwanza operesheni ya UKUTA iliyokuwa imepangwa kwenda  sambamba na uzinduzi wa mikutano ya hadhara nchi nzima ilizinduliwa Julai 27 mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Hatua ya kutangazwa kwa operesheni hiyo ilitokana na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa siku nne mfululizo jijini Dar es Salaam na kutoa maazimio matatu.

Pamoja na mambo mengine, chama hicho kilinukuliwa kikisema kuwa lengo la operesheni hiyo ilikuwa ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini, kiliyodai kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Hata hivyo baadaye Chadema kilistisha Operesheni hiyo kabla ya kuuibua tena kwenye kikao cha Baraza Kuu lililokutana mwishoni mwa mwezi uliopita.