Home Habari CHADEMA YAJIPANGA KUDHIBITI WABUNGE WAKE

CHADEMA YAJIPANGA KUDHIBITI WABUNGE WAKE

992
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

WIMBI la kuhama kwa makada wa vyama vya upinzani hasa wale wanaoshikilia nafasi za Ubunge na Udiwani, limeonekana kukitisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). RAI linachambua.

Katika siku za karibuni Chadema kimepoteza idadi kubwa ya madiwani wake, huku pia kukiwa na taarifa za baadhi ya wabunge wao kutimkia CCM.

Miongoni mwa wabunge waliohusishwa na kukihama chama hicho ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea ambaye tayari amekanusha kuwa na mpango huo.

Ilielezwa kuwa Kubenea anaondoka Chadema kwa sababu kuu mbili ambazo ni uhusiano wake mbaya na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho, pamoja na kwenda vibaya kwa biashara zake huku akidaiwa kukabiliwa na madeni.

Kama Kubenea ambaye alitazamiwa kujivua uanachama huo jana angefanikiwa ungekuwa ni mwendelezo wa vuguvugu la wabunge na madiwani wa upinzani kutimkia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kile kinachoitwa kuunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli.

Hatua hiyo ingemwondolea sifa ya kuwa mbunge huyo wa Ubungo pamoja na kupoteza nafasi zake zote ndani ya chama hicho.

Taarifa za kuondoka kwa Kubenea zilienea kwa kasi mwanzoni mwa wiki hii, mara baada ya aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi-CUF, Maulid Mtulia, kujivua uanachama wa chama hicho.

Mmoja wa watu wa karibu na Kubenea, aliliambia RAI kuwa mpango wa mbunge huyo kuondoka Chadema ulikuwepo, lakini kutokana na kusambaa kwa taarifa ndipo ilipoibuka hoja ya kusitisha kwa zoezi hilo.

Kutokana na hali hiyo RAI limeelezwa kuwa tayari viongozi wa juu wameshajipanga ili kuweka mipango thabiti itakayowaondolea wabunge na madiwani wake uwezo wa kujivua uanachama.

Imeelezwa kuwa tayari vikao vya ndani vya chama vinavyowahusisha viongozi wa juu vimeshaanza kufanyika ili kuhakikisha dawa ya kukomesha suala hilo inapatikana.

Pamoja na ukweli huo, hivi karibuni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema chama chao hakiwezi kutetereka au kufa kwa sababu ya kuondoka kiongozi au mwanachama wake.

Mbowe alisema wanajua upo mkakati mkubwa unaohusisha fedha unafanywa na wenzao ili kuwalaghai viongozi na wanachama wake kukihama chama hicho.

Alisema chama kipo imara na hakitatetereka kwa sababu hiyo si mara ya kwanza watu kuondoka, hivyo ni vema wanachama wakaondoa woga badala yake waendelee kujenga chama kwa nguvu zote.

Katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii, zinabainisha kuwa mbali ya Kubenea, lakini pia upo mkakati wa kuhama kwa mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Kaliua Magdalena Sakaya na Mbunge wa Moshi Mjini, Japhary Michael.

Hata hivyo, tayari Mnyika amekana kuwa na mpango huo kama alivyofanya Kubenea.