Home Habari CHADEMA YAMALIZANA NA EDWARD LOWASSA

CHADEMA YAMALIZANA NA EDWARD LOWASSA

2238
0
SHARE

*Dk. Mashinji ataka CCM iendeleze ushawishi

NA GABRIEL MUSHI


JOTO la ghadhabu na hasira lililokuwa limewapanda baadhi ya viongozi na makada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wiki iliyopita dhidi ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, hatimae sasa limeshuka. RAI linaripoti.

Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Vincent Mashinji amethibitisha kumalizana na Lowassa na kusema kuwa mjadala juu ya suala hilo umefungwa na ambaye hajaridhika akate rufaa.

Dk. Mashinji aliliambia RAI kuwa,wamemalizana na Lowassa kwa  sababu alilolifanya ni kosa la kwanza, lakini  pia hakuwa na uzoefu sana na vyama vya upinzani kwa hiyo suala hilo limeishia hapo.

“Tumelimaliza hilo suala na tayari limeshafungwa, ameshaeleza nini kilitokea, sasa anayeendelea kujadili, labda huyo mtu ana vitu vyake sasa,” alisema.

Aidha, alisema hawana adhabu yoyote watakayoitoa kwa Lowassa kwa sababu kutoa adhabu hasa ya kusimamishwa uanachama haiwezi kutekelezwa kirahisi.

Alisema ufafanuzi alioutoa Lowassa mbele ya Kamati kuu ya chama ilipokelewa vizuri na wajumbe wa Kamati hiyo ambao pamoja na mambo mengine walimuonya na kumueleza asili ya maisha upinzani.

“Kwa sababu ukiishi kwenye msitu wenye wanyama wakali mnatakiwa kuwa kama timu, mnatakiwa kujua mnachokipigania ni nini, sasa unapoongea lugha zinazoonesha kumuunga mkono adui inaleta picha mbaya. Ni sawa na mwaka 1978 aliyekuwa waziri mkuu Sokoine angemsifia nduli Idd Amin, sijui Nyerere angemfanyaje!

“Kwa kawaida mtu unayeshindana naye unamsifia kwa lipi, wakati alikushinda na anachofanya ni wajibu wake! Wananchi wamsifie, lakini sisi ambao tuna jukumu tofauti tuelezee kulingana na majukumu yetu,” alisema Dk. Mashinji.

Hata hivyo, Dk. Mashinji alisema anawaomba CCM waendelee kumshawishi Lowassa na makada wengine wa upinzani.

“Naomba waendelee kumshawishi ahamie CCM kwa sababu ndiyo kazi pekee waliyobakisha na wasimshawishi yeye tu, waendelee kushawishi wengine na wengine kwa sababu ndio uwezo wa akili zao za kufikiri uliposhia kwamba siasa zao ni siasa za kuhamisha watu.

“Tutambue kuwa hili suala lina hasara kubwa  kwa Taifa, nina hakika wananchi wakielezwa hasara ambayo wanaifanya wangewaadhibu CCM, kwa sababu kumrudisha mbunge mmoja kwenye kiti chake inaligharimu Taifa si chini ya bilioni moja ambayo ni sawa na kuchima visima 500 vya maji ambavyo kila kimoja kinaweza kugharimu milioni tatu.

“Ukienda majimbo kama Chato ni kukame, maji hakuna, ningekuwa na uwezo ningewaambia wananchi wapige kura za hasira kuonesha kuwa huu mchezo wanaoufanya CCM hauna tija. Tunatumia mabilioni ya fedha kurudisha viongozi ambao hawana maana kwani hata wale wanaowapigia chapuo wanajua kabisa wamewanunua kwa rushwa.

“Kwa hiyo nadhani tusaidiane kuwaelimisha wananchi kuwaeleza ukweli kuwa hii ni hasara kwa Taifa letu hata kama wanafikiri ndio kiki ya kuishinda Chadema, nadhani wamekosea,” alisema Dk. Mashinji.

 

Kauli ya Dk. Mashinji inamaliza mjadala wa suala hilo ambao uliibuka mwanzoni mwa wiki iliyopita Januari 9, mwaka huu, baada ya baadhi ya viongozi na makada wa Chadema kupandwa na ghadhabu na kujawa na chuki zilizosababishwa na Lowassa kufanya  ziara ya kimya kimya Ikulu, jijini Dar es Salaam na kukutana na Rais Dk. John Magufuli, ambapo pamoja na mambo mengine alimsifia kwa kufanikisha utoaji wa elimu bure pamoja na kuzalisha ajira mpya.

 

Kauli hizo zilipokelewa kwa chuki na baadhi ya makada na viongozi wa juu wa chama hicho na baadhi yao kuanza kutoa kauli nzito zilizolenga kuponda uamuzi huo, ambao ulidaiwa kutokuwa na baraka za chama.

 

Miongoni mwa makada wa Chadema waliotoa kauli za kupinga uamuzi huo wa Lowassa ni Dk. Mashinji mwenyewe, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho, Frederick Sumaye, Profesa Mwesiga Baregu na Umoja wa Vijana wa chama hicho (Bavicha).

 

MBOWE

Mwenyekiti wa chama hicho pamoja na mambo mengine alinukuliwa akisema kuwa ziara hiyo ya Lowassa haikuwa ikijulikana na chama, hata hivyo kauli alizozitoa hazikuwa za chama bali zilikuwa ni kauli zake binafsi.

 

LEMA

Mbunge wa Arusha Mjini aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kuwa Lowassa ameikosoa Tanzania.

”Mh Lowassa umeikosea Tanzania kwa kauli baada ya kutoka Ikulu. Mema yapi umeyaona katika Serikali hii? Wakati Mbunge Lissu bado anauguza majeraha ya risasi, maiti zinaokotwa, Uchumi unaanguka, Benki zinafungwa, Demokrasia imekufa Bungeni/Nje ya Bunge na Sioi mkwe wako bado yuko Magereza”

 

LISSU

Akiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu Lissu alionesha kutokubaliana na Lowassa na kutaka kitendo cha Lowassa si cha kunyamaziwa au kuhalalishwa kwa hoja nyepesi.

“Hatukatai kuzungumza na Magufuli, kuhusu matatizo mengi na makubwa yanayoihusu nchi yetu, lakini ni muhimu na ni lazima viongozi wakuu wa chama washirikiane na washauriane  kabla ya mazungumzo haya na baada ya mazungumzo ni lazima viongozi wakubalkiane juu ya kauli za kutoa hadharani kwa umma, ili wote tuwe kwenye ukurasa mmoja.

“Viongozi na wanachama wetu wanashambuliwa hadharani kwa mapanga na hata kwa risasi, kumsifia Rais ni  kumuunga mkono yeye,  katika mazingira ya kesi nyingi za kutunga dhidi yetu, kazi nzuri inayofanywa inamaana gani kama si kuhalalisha ukandamizaji tunaofanyiwa…..”Kwa vyovyote vile kitendo cha Lowassa si cha kunyamaziwa au kuhalalishwa kwa hoja nyepesi nyepesi.”

 

PROFESA BAREGU

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Profesa Mwesigwa Baregu, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu wa Chadema alisema hakuwa akijui lengo la Lowassa  na kwamba kuna mambo hakumwelewa vizuri kwa sababu Chadema inaamini katika demokrasia ya kweli.

 

“Ni mapema sana kujua alikuwa na lengo gani kwenda kule lakini kwa yale aliyoyasema mengine sijamwelewa vizuri kwa sababu tukisema Chama cha Demkokrasia tunamaanisha demokrasia ya kweli.

 

“Pia tunaamini ili maendeleo yaje lazima demokrasia iwepo kwahiyo sielewi Lowassa kama aliyoyasema ndiyo waliyoyazungumza akiwa ndani au labda kuna mengine zaidi. Maana Rais alisema kwamba wamezungumza mengi kila mmoja alisema yak wake, sasa hayo mengine ndiyo hatujayajua kama alikuwa nasema kwa kuwa maendeleo yamekuja lazima demokrasia ikandamizwe .

“Mpaka sasa watu wengi watakuwa katika ya sintofahamu kwahiyo ni vizuri yeye mwenyewe akatoka hadharani akawaambia watanzania ambao walimpigia kura alipogombea urais mwaka 2015 akafafanua hayo matembezi yake yalikuwa na lengo gani, je wameyafikia au la na tutegemee nini,” alisema Profesa Baregu.

 

Alisema kama lengo lake ni kutaka kurudi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwani hakuna kitu kilichomzuia maana yeye ni mtu mkubwa na ana watu wengi wanaomuamini si lazima aende kwa kinyemelea, angetoka moja kwa moja kama anahama Chadema ajitangaze kama wengine wanavyofanya kuwa huo ndio ujasili.

SUMAYE

Waziri Mkuu wa zamani na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani na Mjumbe wa Kamati Kuu, alisema Lowassa alifanya kosa.

Sumaye alisema kosa la Lowassa alilikuwa ni kuibuka na kauli ambazo kwa namna moja au nyingine ziliumiza wengine.

WAMALIZANA

Baada ya kauli hizo na nyingine nyingi zilizoonekana kupandisha joto la hasira za kisiasa hasa kwa upande wa Chadema, hatimae mwanzoni mwa wiki hii pande hizo mbili zilimalizana na kurejesha furaha kwa makada na wapenzi wa chama hicho nchi nzima.

Hitimisho la mtifuano huo ambao kwa upande mmoja ulionekana kunufaisha wapinzani wa Chadema kisiasa, lilifanyika kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya chama hicho iliyoketi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika kikao hicho RAI limeelezwa kuwa pamoja na kuwapo kwa hoja mbalimbali, lakini suala la Lowassa lilijadiliwa kwa utulivu wa hali ya juu na kupatiwa majibu ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kurejesha hali ya utulivu ndani ya chama.

Majadiliano hayo ya Kamati ya Utendaji yalimsukuma Lowassa kutoa tamko rasmi juzi lenye baraka zote za chama chake.

Lowassa aliweka wazi kuwa mazungumzo yake na Rais kamwe hayatamyumbisha kwani yuko imara na uamuzi wake wa kujiunga na Chadema mwaka 2015 haukuwa wa kubahatisha ingawa alikiri kushawishiwa kurejea CCM na Mwenyekiti wa chama hicho.

Alieleza kuwa aliitwa Ikulu kwa ghafla na aliitumia nafasi hiyo kuzungumza na Rais kuhusu masuala mbalimbali ukiwemo mustakabali wa siasa za nchi hii, kutoheshimiwa kwa Katiba na sheria, uminywaji wa demokrasia, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na hali ngumu ya uchumi kwa wananchi.

 

Tamko hilo la Lowassa limedhihirisha kumaliza mkanganyiko aliouibua na kukirudisha chama pamoja.

Ukweli wa hilo umethibitishwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema.

Mrema alisema tamko lililotolewa na Lowassa ni tamko la chama chao na wako tayari kulitetea popote pale.

“Ni tamko la chama, ikitokea kukahitajika kulitetea, chama ndio kitafanya hivyo, ni tamko la Lowassa, lakini linabaraka za chama na ni mali ya chama,”alisema Mrema.

Kuhusu kumbana Lowassa wakati wa kikao cha Kamati ya Utendaji, Mrema alisema hakukuwa na kitu kama hicho, badala yake busara kubwa ilitumika kuendesha shughuli zote za kikao hicho na hakuna aliyeshughulikiwa.

Tamko hilo la Lowassa limeonekana kubadili kabisa upepo wa kisiasa ndani ya Chadema, ambapo sasa hakuna anayemjadili mwanasiasa huyo vibaya, badala yake kila mmoja anaamini kuwa mazungumzo yake na Rais yalilenga kusaidia siasa za nchi hii hasa kwa upande wa upinzani.