Home Habari kuu CHADEMA YAONYA WABUNGE WAKE

CHADEMA YAONYA WABUNGE WAKE

5481
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI   


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewataka na kuwaonya wabunge wake wote kuzingatia taratibu na kanuni za chama hicho hasa wanapokutana ana kwa ana na Rais Dk. John Magufuli. RAI linaripoti.

Onyo hilo limekuja siku chache baada ya wabunge wake watano kwa nyakati tofauti kukutana na Rais Dk. Rais Magufuli huku baadhi yao wakitoa kauli zilizotafsiriwa kama kumwagia sifa Rais.

Wabunge wa Chaema waliopata nafasi ya kukutana na Rais Magufuli wakati wa ziara yake kwenye mikoa ya Dodoma, Iringa na Morogoro ni mchungaji Msigwa (Iringa mjini), Joseph Haule ‘Prof Jay’ (Mikumi), Peter Lijualikali (Kilombero), Suzan Kiwanga (Mlimba) na Devotha Minja (Viti maalumu).

Wiki iliyopita wabunge hao kwa nyakati tofauti walitajwa kusifia hatua za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli tangu aingie madarakani.

Katika hafla ya chakula cha jioni kilichokuwa kimeandaliwa na Rais Magufuli kwa viongozi mbalimbali wa Iringa, Msigwa alipongeza hatua ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwmo ununuzi wa ndege, ujenzi wa barabara za lami, upanuzi wa Bandari Elimu, Afya na miradi mingine inayotekelezwa na kiongozi huyo wa nchi.

Mjadala uliibuka baada ya kusambaa kwa video inayoonesha Msigwa akihutubia na kumsifia Rais Magufuli juu ya mambo mbalimbali ya kimaendeleo ambayo ameyawezesha hata katika mikoa ambayo wabunge wake ni kutoka vyama vya upinzani.

Msigwa alisisitiza kuwa Rais hapendelei ni wa watu wote hata wa vyama vya upinzani.

“Rais umekuwa ukisisitiza katika hotuba zako kuwa wewe hujali mambo ya vyama na hii imedhirika kuwa kweli hujali vyama, umesaidia sana, hela za kutoka kwako zimekuja nyingi, kama alivyosema Mahiga, kuna barabara nzuri katika kipindi chako ambacho umekuwa Rais.

“Umejenga barabara ya lami kutoka Mlandege mpaka kwa Mkuu wa Wilaya karibu Sh bilioni 3.5, tuna stendi nzuri ipo Ipogoro ya karibu Sh bilioni tatu, tuna maji, kwa hiyo kuna vitu vimefanyika kwa kweli Rais hupendelei, hela zinakuja hata sisi ambao ni wa Chadema unaleta hela, kwa hiyo tunakupongeza sana,” alisema Msigwa.

Kauli hiyo ya Msigwa iliibua mjadala mkali miongoni mwa makada wa Chadema huku miongoni mwao wakimuona kama msaliti wa chama ambaye anatarajia kuhamia CCM.

Hatua hiyo ilimlazimu Msigwa kuomba radhi  kwa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa twitwer.

“Ufafanuzi wangu bado haueleweki na heshima kuzingatia maumivu yenu. Kwa mkanganyiko huu. Nagundua rafiki zangu na wanachama wetu wanaugua. Basi niseme nini? Naomba nisameheni sana” alisema Msigwa.

Kauli hiyo iliungwa mkono Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es salaam na Mjumbe Baraza kuu na Mkutano Mkuu Taifa chama hicho, Kileo Mwanga ambaye aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwa kuukubali msamaha huo.

Mbali na Msigwa, lakini pia Lijualikali na Haule kwa nyakati tofauti nao wanadaiwa pamoja na kuwasilisha kero zinazoyakabili majimbo yao, lakini pia walimpongeza Rais kwa jitihada zake za kuleta maendeleo kwa wananchi bila kujali itikadi za vyama vya siasa.

Hatua hiyo ya kutoa pongezi ilichukuliwa kwa sura na mtazamo tofauti na watu wa rika na kada mbalimbali hali iliyoibua mjadala uliokuwa na pande mbili, upande mmoja ukipongeza na upande mwingine ukikosoa kwa hoja kuwa hawakupaswa kufanya hivyo.

Miongoni mwa watu walioguswa na suala hilo na kulitolea maoni ni aliyekuwa Spika wa Bunge, Pius Msekwa, ambaye alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akiipongeza hatua ya wabunge hao wa upinzani wenye misimamo isiyoyumba kumsifia Rais hadharani.

Mzee Msekwa na baadhi ya wasomi, walieleza kuwa hatua ya wabunge hao kumsifia Rais imeonesha kukua kwao kidemokrasia na kwamba walichokifanya kinapaswa kuigwa na wabunge na vionmgozi wote wa vyama vya upinzani.

Alisema Tanzania ya sasa inalenga kwenye masuala ya maendeleo na si siasa  kwa sababu watu hawaishi kwa siasa badala yake wanaishi kwa maendeleo ambayo hayatokani na kupingana pale yanapofanyika.

“Hawa wabunge wanajua wanachokifanya na kwa maendeleo ya nani…kwangu ni mashujaa wanaopaswa kuigwa na wabunge wenzao kutoka upinzani,”alinukuliwa Msekwa.

Katika mazungumzo yake na RAI, Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje ya Chadema, John Mrema alisema kilichofanywa na wabunge hao si kosa, lakini wanapaswa kuwa makini katika kauli zao hasa wanapokutana na viongozi wa Serikali.

  Mrema alisema chama chao hakiwezi kuwafunga midomo wabunge na makada wake kuipongeza au kuzungumzia mambo yoyote kuhusu Serikali ya awamu ya tano, lakini wanapaswa kuzungumzia zaidi kero zinazowagusa wananchi.

“Ni vema wabunge wakazingatia kanuni na taratibu za chama pindi wanapokutana ana kwa ana na Rais  ili kuzingatia malengo ya kufikisha kero na changamoto zinazowakabili wananchi wa majimbo yao.

 “Ni kweli tumeona hizo kauli, kama chama tunaendelea na taratibu zetu kwa sababu ni jambo ambalo hatuwezi kuwaziba midomo, ila kuna utaratibu wa kufuata, kama kuna mtu amekwazika na hizo kauli basi afuate taratibu ila sisi kama chama tunajua wabunge wana uhuru wa kusema, lakini  tunawataka wajue wananchi wanataka nini.

“Waseme kwa niaba ya wananchi na hali halisi ya maisha ya wananchi wanaijua,  wanapokutana na Rais ni vema wakajikita kumueleza matatizo  na changamoto ambazo wananchi wanakumbana nazo kwa sababu wao wanawakilisha wananchi na wanajua shida na matatizo wanayopata,” alisema.

KUWAITA WABUNGE HAO

Mrema alisema chama chao hakijafika hatua ya kumuita mbunge yeyote aliyemsifia Rais na kwamba kwao haliwasumbui kwa sababu kila mtu anaouhuru wa kusema, isipokuwa ni vema wabunge hao na wengine wote wa Chadema, wakajikita kwenye kuwasemea wananchi zaidi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Magufuli alikamilisha ziara yake ya kihistoria katika mikoa hiyo mitatu aliyoizuru kwa kutumia barabara.

Katika ziara hiyo miradi mbalimbali ya mira ya maendeleo imezinduliwa ikiwamo kuweka mawe ya msingi.

Aidha, katika ziara hiyo wabunge wote wa Chadema katika mikoa hiyo walipata fursa ya kumweleza Rais Magufuli kero za majimbo yao ana kwa ana, pamoja na kuomba utatuzi.

MAOMBI YA WABUNGE KWA RAIS

Rais Magufuli aliendelea na ziara yake mkoani Morogoro, ambapo safari hii Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule ‘Profesa Jay’ naye aliangukia mikononi mwa Rais kumuomba atatue kero za jimbo hilo.

Hata hivyo, mtindo alioutumia Profesa Jay haukutafsirika na wengi kuwa amemsifia Rais Magufuli licha ya kukubali kuwa kwa kuwa ni Rais wa wanyonge anaamini atasikiliza kero za jimbo hilo.

Alisema mikumi kuna uhaba wa maji ambao licha ya mradi kufadhiliwa na Benki ya Dunia bado waziri hajatoa fedha za kutekeleza mradi huo, ubovu wa barabara na fidia kwa wafanyakazi wanaopisha miradi.

Hata hivyo, Rais Magufuli baada ya kusikiliza kero hizo, alimuomba Profesa Jay ashushe mistari kidogo kwakuwa mbunge huyo ni mkongwe katika tasnia ya muziki nchini.

PETER LIJUALIKALI

Rais Magufuli aliendelea na ziara yake mkoani Morogoro ambapo safari hii ilikuwa zamu ya Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali naye hakubaki nyuma kuonesha ushirikiano kwa Rais na kumuomba kutatua kero mbalimbali ikiwamo eneo ambalo linahodhiwa na maaskofu lirejeshwe kwa wananchi.

“Naomba Mh. Rais utoe tamko leo mbele ya wananchi wa Kilombero, ikiwa wewe umezuia kutoza ushuru wa mazao chini ya Tani moja, Afisa Mtendaji ni nani mpaka akiuke, Mkurugenzi ni nani mpaka akiuke, basi leo toa tamko mbele ya wananchi”, alisema.

Aidha Rais Magufuli ambaye alikuwa akizindua daraja la mto Kilombero lenye urefu wa mita 384, alimuomba Lijualikali aongee na Maaskofu mwenyewe sio kusubiri hadi mtu kutoka Dar es Salaam kusuluhisha tatizo hilo.

“Nimuombe Mh. Lijualikali mgogoro upo huku Kilombero, unasubiri hadi mimi ninayetoka Dar es Salaam nije ni suluhishe mgogoro huo na maaskofu, kazi ya Ubunge ndio hiyo. Baba Askofu mimi sifanyi chochote juu yenu, Lijualikali kama unawaogopa Maaskofu basi ila njoo uongee nao mwenyewe,” alisema.

Devota Minja

Wakati akihitimisha ziara yake Rais Magufuli pia alikutana na kilio cha Mbunge wa Viti maalumu (Chadema) Devotha Minja ambaye alimuomba Rais Magufuli atumie uzoefu wake wa wizara ya ujenzi kuchunguza ujenzi wa barabara ya Kilomita nne inayojengwa mjini Morogoro kwa gharama ya Sh bilioni 13.5.

Aidha, Rais Magufuli alikubaliana na ombi la Minja na kusema haiwezekani kujenga Kilomita moja ya barabara kwa Sh bilioni tatu.

Kutokana na hali hiyo alimuagiza Waziri wa Ofisi ya Rais – Tamisemi, Selemani Jaffo kuifanyia uchunguzi wa haraka hoja iliyotolewa na mbunge huyo.

Ziara hii imewafungua wabunge wa Chadema kusini mwa Jiji la Dodoma na wananchi wameshuhudia dhana ya Maendeleo hayana vyama ikifanya kazi.

RITTA KABATI

 Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Kabati (CCM), aliwataka wabunge wa vyama vya upinzani kuacha unafiki na kutafuta ‘kiki’ kwa kumkosoa Rais John Magufuli ndani ya Bunge lakini nje ya Bunge wanamsifia.

Pia alimpongeza Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kwa kutambua kazi nzuri ambazo zinafanyiwa na serikali ya awamu ya tano na kutambua Rais Magufuli anafanya kazi bila ubaguzi.

Akichangia mjadala wa bajeti ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi bungeni jijini Dodoma alisema Msigwa sasa ameanza kukomaa kisiasa.

“Nimpongeze Rais alikuwa Iringa siku tano, amefanya kazi nzuri sana na wananchi wa Iringa wametambua uwepo wake, kwa mara ya kwanza nimpongeze Mchungaji Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini, kwa kutambua kazi nzuri ambazo zinafanyika katika awamu ya tano na kutambua Rais Magufuli anafanya kazi bila ubaguzi.

“Na maneno hayo mazuri ameongea mbele ya Waziri Mhagama (Jenister) wabunge na wananchi wa Iringa, kwa kweli nasema Msigwa sasa ameanza kukomaa kisiasa.

“Nashangaa wabunge wengine wa upinzani wanapokutana na Rais hawasemi haya maneno, hawamwambii ukweli,  lakini wanapoingia humu ndani kwenye Bunge, wanaanza kusema maneno mengine ni unafiki, hata jana wanasema Rais wetu hakosolewi, mbona mkikutana sasa hamumkosoi?

“Mnasubiri muongee humu bungeni muanze kukosoa muanze kutukana, mnataka kiki au mnataka nini,” alisema.