Home Makala CHAGUZI HURU, HAKI AFRIKA: KENYA IMEJITAHIDI KUONGOZA KUTOA MFANO

CHAGUZI HURU, HAKI AFRIKA: KENYA IMEJITAHIDI KUONGOZA KUTOA MFANO

990
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Bara la Afrika bado lina safari ndefu kufikia uwepo wa chaguzi zinazoendeshwa kwa uhuru na haki na upungufu huu unatokana na si kingine bali kukosekana kwa Katiba stahiki na tawala bora zinazofuata sheria. Na kila inapotokea baadhi ya nchi kujitutumua kuvisimika vitu hivi, wapo viongozi wanaofanya kila jitihada kupiga hatua nyuma bila hata ya kujali athari zinazoweza kutokea.

Migogoro mingi huibuka wakati wa uchaguzi na hata vita ya wenyewe kwa wenyewe, kutokana na utayarishaji mbovu tena mara nyingi wa kimakusudi, lakini lengo kuu ni kwa watawala (waendeshaji wa chaguzi) kutumia kila njia kwa kutenda au kutotenda ili wabakie madarakani.

Katika nchi nyingi barani humu, chaguzi huwa ni kama kitu kinacholazimishwa tu na mataifa fadhili na mara nyingi wao ndiyo huchangia fedha za kuendesha chaguzi zao. Hapa kwetu mwaka 2015 tuliona jinsi uchaguzi mkuu ulivyoandaliwa kwa njia za zimamoto na hasa katika uandikishaji na uandaaji wa daftari la wapigakura. Hadi kufikia 2014, utawala ulionekana kutokuwa na habari kuwepo uchaguzi mkuu mwaka unaofuata.

Hadi sasa utawala wa Rais Joseph Kabila wa Congo (DRC) bado unajizungusha kufanya uchaguzi mkuu ambao ulitakiwa ufanyike tangu Desemba mwaka jana, ambapo kikatiba kipindi chake cha pili kilimalizika. Ajabu kabisa ni kwamba Kabila anaonekana kutojali iwapo nchi yake itaingia kwenye ghasia kubwa. Lakini huenda ni kwa sababu nchi hiyo haijapata kuwa tulivu kabisa tangu uhuru miaka 57 iliyopita.

Uganda nayo ina sehemu yake ya mapungufu tajwa, kwani Rais Yoweri Museveni ambaye yupo madarakani tangu 1986, amekuwa anaichokonoa Katiba kumwezesha kuendeleza vipindi vya urais, utadhani hakuna wananchi wengine wenye uwezo wa kuwa rais isipokuwa yeye. Sasa hivi yuko mbioni kuondoa kihunzi kimoja cha umri ambacho kikiachwa kilivyo hataweza kugombea tena urais mwaka 2021.

Lakini nchi jirani ya Kenya ni mfano mzuri wa ninayozungumza. Mwaka 2007 nchi hii ilitumbukia katika ghasia kubwa baada ya utulivu wa miaka mingi ulioifanya nchi hiyo kuwa kama nanga ya kidemokrasia na maendeleo katika ukanda huu wa Afrika. Haijatulia sawasawa hadi leo hii.

Miaka kadhaa iliyopita katika moja ya makala zake kuhusu Afrika, Tajudeen Abdul-Raheem (marehemu), raia wa Nigeria na mwanahabari mahiri na mwanaharakati kuhusu masuala ya utawala bora barani Afrika, alitaja sababu za kwanini viongozi wengi barani Afrika hawakwenda kuhudhuria maadhimisho ya miaka 200 tangu upigwaji marufuku wa biashara ya utumwa iliyoshamiri kupitia Bahari ya Atlantiki.

Alisema sababu kubwa ni kwamba pamoja na historia, utumwa haujafa umejibadili na kuwa aina nyingine ya unyonyaji na ukandamizaji ambao watu wa Bara la Afrika bado wamebakia kuwa chini katika vielelezo vyote vya kupima maendeleo ya watu duniani.

Tajudeen alisema: “Kama vile ilivyokuwa kwa wafalme na wafanyabiashara wakuu wengine wa utumwa katika karne zile, leo hii marais na mawaziri wetu wakuu wanaendesha mifumo ya tawala ambayo zinaendeleza watu wetu kuwa ‘watema kuni na wachota maji’ wakati utajiri wa bara letu unazidi kuchotwa na watu wa mabara mengine. Viongozi wetu wanakubali kuwa washiriki wa ngazi za chini ili mradi watahakikishiwa maisha yao ya anasa na yale ya wanafamilia wao na maswahiba.”

Kenya ilikuwa ni kielelezo cha yote haya. Nchi hiyo haitatizwi na suala la ukabila, kama vile wengi wanapenda kuuaminisha ulimwengu,k wamba ni mapambano kati ya Waluo na Wakikuyu katika kuwania madaraka ya nchi.

Ni mapambano baina ya nguvu zinazotokana na matakwa ya demokrasia na wezi wanaofanya kila mbinu kupora madaraka hayo. Ni vita kati ya ‘walionacho’ na ‘wasionacho’. Ni jitihada nyingine za ‘watema kuni na wachota maji’ kuwatokomeza wakandamizaji wao.

Kenya ni nchi moja barani Afrika ambayo hali kama hii ilikuwa itokee muda mrefu sana nyuma, ingawa nchi za magharibi zilikuwa zinatuambia kwamba ikilinganiswa na viwango vya majirani zake kama vile Tanzania, Uganda, Somalia na Ethiopia, Kenya ni nchi iliyokuwa imetulia na kupiga maendeleo makubwa.

Wanataja kwamba mwonekano wa Kenya duniani ulikuwa unaonewa wivu na nchi nyingi barani Afrika. Kenya ni nchi pekee ya dunia ya tatu ambayo yapo makao makuu ya taasisi za Umoja wa Mataifa na kitovu cha mashirika ya misaada yanayohudumia nchi zilizo jirani.

Kwa kuongezea nchi za magharibi zilikuwa zinaisifu sana Kenya kwa uchumi imara na wamekuwa wakitaja pato lake la zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja katika sekta ya utalii pekee. Hivyo kwa viwango hivi, Kenya ilikuwa ni tumaini kubwa kuwa mfano kwa nchi nyingi barani Afrika. Hivyo nchi hiyo kutumbukia ghafla katika ghasia kubwa mwaka 2007 haikueleweka na hivyo ikaanza kutajwa kuwa nayo kumbe ni kama nchi nyingine tu zenye migogoro.

Uchaguzi wao wa mwezi uliopita na hususan tukio la Ijumaa iliyopita ni mwendelezo tu wa mapambano ya pande mbili nilizotaja hapo juu. Mahakama ya Juu kabisa (Supreme Court) nchini humo ilifutilia mbali matokeo ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8, yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta, Rais aliye madarakani wa chama cha Jubilee.

Kwa kura 4-2, Mahakama hiyo iliridhishwa bila chembe ya shaka kwamba mchakato wa kuhesabu kura haukuzingatia Katiba ya nchi, sheria na kanuni kwa namna inavyotakiwa. Hivyo uchaguzi wa urais, baina ya Uhuru Kenyatta na mshindani wake Raila Odinga urudiwe ndani ya siku 60.

Kwa hali ya kawaida na kutokana na namna Katiba mpya ya Kenya ilivyopatikana (kwa umwagaji damu), Katiba ambayo iliweka misingi bora ya utawala bora na mgawanyo wa ile mihimili mitatu ya dola, maamuzi ya Mahakama yangepaswa kuheshimiwa na uchaguzi wa marudio ufanyike kwa amani pasipo manung’uniko yaliyopitiliza. Lakini sivyo hivyo. Kuna kila kiashiria cha kuwaweza kutokea duru jingine la ghasia.

Hebu angalia: Baada tu ya Uhuru Kenyatta kutangazwa kuwa mshindi, mpinzani wake akaanza kulalamika mapungufu ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), malalamiko ya kawaida tu baada ya chaguzi katika nchi nyingi barani Afrika.

Rais-mteule Uhuru Kenyatta akamwambia ni vyema Raila aende tu mahakamani kufuatana na Katiba, aache kulialia. Raila akafanya hivyo, akaenda mahakamani, kesi ikasikilizwa na akashinda. Sasa ni zamu ya Uhuru kulalamika lakini malalamiko yake yanachukuliwa kuwa mazito na ya kutisha zaidi. Anasema mahakama ilipendelea, majaji ni watu wa ovyo tu na atawanyoosha kwani yeye si rais-mteule tena, bali ni rais kamili.

Kwa tafsiri yoyote ile, haya ni maneno mazito sana yanayoonyesha dharau kwa Mhimili mmoja muhimu wa Dola, ule wa Mahakama na kwamba yuko tayari kuuchukulia hatua kutokana na kitendo chake cha kupora ‘ushindi’ wake uliotangazwa na IEBC.

Ile hoja ya kusema ‘haiwezekani kikundi cha ‘watu sita’ (idadi ya Majaji wa Mahakama ya Juu waliyoketi na kutoa maamuzi) wanatengua maamuzi ya zaidi ya watu milioni 6 (kura za wananchi alizopata)’ haina mashiko, kwani maamuzi ya mahakama yalizingatia zaidi ukiukwaji mkubwa katika mchakato wa kuhesabu na kusafirisha matokeo na si watu wangapi wamempigia kura mgombea yupi. Mchakato usio sahihi hauwezi kutoa matokeo sahihi.

Lakini kuna baadhi ya wanasiasa, hasa walio madarakani wamekuwa wakilielezea tofauti. Kuna baadhi yao huwatupia lawama watazamaji wa kimataifa.

Kwa mfano miaka mitatu iliyopita katika hotuba yake ya ufunguzi ya mkutano wa kimataifa wa kujadili uendeshaji wa chaguzi katika Bara la Afrika jijini Dar es Salaam, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama kinachotawala CCM, alitumia muda mwingi kuwalaumu watazamaji wa kimataifa kwamba wao ni sehemu kubwa ya kuibuka vurugu na machafuko katika baadhi ya nchi.

Alisema tabia ya baadhi ya watazamaji kuchukua upande katika vyama vinavyogombea ndiyo husababisha vurugu na hivyo kudumaza uendelezaji wa demokrasia katika Afrika.

Alitaja sababu nyingine ni matatizo yanayokabili tume za uchaguzi kama vile ya uwezeshaji wa kifedha, kitaalamu na kirasilimali-watu, vitu ambavyo uhaba wake husababisha kutofanyika kwa chaguzi zilizo huru.

Aidha, alisema kwamba tabia na mienendo ya wadau wengine katika chaguzi kama vile wanasiasa na vyama vyao, asasi za kiraia, vyombo vya habari na watu wengine nazo huchangia sana kwa namna moja au nyingine kutokea vurugu na machafuko.

Sababu zote alizozitaja zinaweza zikawa sahihi katika kusababisha vurugu katika chaguzi barani Afrika. Lakini kiini chenyewe Kikwete hakukisema na hii haikuwa kwa kupitiwa, bali ni kwa makusudi mazima na sababu kubwa ni kwamba ndiyo kimekuwa kikisababisha vurugu na malalamiko karibu katika chaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi nchini mwake, yaani nchi hii.

Sababu yenyewe ni kutokuwapo kwa tume huru za uchaguzi. Na hili lilielezwa vyema na Prof Ibrahim Lipumba katika mkutano huo huo. Ni vigumu sana kuamini kwamba tume ya uchaguzi inayoteuliwa na rais wa nchi ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala ambacho lengo kuu la chama hicho ni kubakia madarakani, kinaweza kutenda au kufanya maamuzi ya haki katika chaguzi. Na mara nyingi huwa kwamba rais anayeiteua Tume hiyo naye hugombea kiti hicho.

Tusidanganyike hapa, haiwezekani. Na mifano iko mingi sana humu humu nchini, ukiachilia mbali kwingineko barani Afrika.

Ni tatizo sugu katika kuendeleza demokrasia ya kweli barani Afrika, hasa ukizingatia kwamba viongozi wa nchi kadhaa wamekuwa wakifanya kila hila kuendelea kubakia madarakani, kwa kubadilisha Katiba kuondoa ukomo wa vipindi vya urais au ghilba nyingine, kwani akigombea tena ni lazima atapita tu.

Kuna nguzo moja kuu ya kutenda haki (principle of justice) inayoelezwa katika usemi mmoja maarufu katika tasnia ya sheria inayosema: “Haki su tu kwamba itendeke, bali ni lazima pia ionekane wazi inatendeka (au mwonekano wake uonyeshe haki inatendeka).”

Hivyo rais anapoiteua tume ya uchaguzi  yaani mwenyekiti wake, wajumbe na watendaji wengine wakuu wa tume na yeye mwenyewe (rais) ni mgombea chini ya usimamizi wa tume aliyeiteua, basi huwezi kupata haki hapo.

Utapata manung’uniko makubwa na vurugu tu na hata kusababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe kama tulivyoona katika nchi kadhaa na Ivory Coast ni mfano mzuri, kwani yalitokea mara mbili katika kipindi cha muongo mmoja tu.

Kenya waliibadilisha hii, lakini walifanya hivyo baada ya vurugu zilizotokana na uchaguzi wa 2007 katika Katiba mpya iliyoisimikwa mwaka 2011. Chini ya Katiba hiyo, rais ‘anateua’ tume ya uchaguzi kwa namna ya kuyataja majina hadharani, lakini mchakato mzima wa kuipata tume hiyo haimhusishi sana yeye mwenyewe au taasisi yake  yaani Mhimili wa utawala (Executive Branch). Inamhusisha kwa takriban asilimia 10 tu.

Uchujaji mkali unaojumuisha waombaji wengi, usaili wao kupitia tume maalumu na hatimaye kufikia kwa rais, hufanyika kupitia vyombo mbalimbali, likiwemo Bunge na kamati yake husika. Mchakato huu unasisitiza ile dhana ya ‘si kwamba tu haki itendeke, bali pia haki lazima ionekane ikitendeka.’

Sasa kama ilivyo katika ule usemi ‘mzoea vya kunyonga, vya kuchinjwa haviwezi’, watawala wa Afrika ni wagumu kubadilika. Kufuatana na Mahakama Kuu iliyoamua kesi Ijumaa iliyopita, mchakato na mfumo mzima wa IEBC uliingiliwa kiasi kwamba matokeo yaliyotangazwa hayakuwa sahihi.

Na kwa Kikwete kusema katika mkutano wa kimataifa na kuwalaumu watazamaji wa kimataifa kwamba ndiyo chanzo cha vurugu katika chaguzi Barani Afrika kwa kuonyesha upendeleo upande mmoja si kweli kwa asilimia 100, huenda ni kweli kwa asilimia 20 tu au chini ya hapo.

Baada ya uchaguzi wa Kenya wa Agosti 20, wengi walitangaza kwamba ulifanyika katika mazingira yaliyo tulivu, huru na haki na hivyo Raila Odinga akubali matokeo yake ya kushindwa. Tatizo kubwa la hawa watazamaji ni kutoa hukumu kwa kuangalia mambo kijuujuu tu, kwamba wapigakura wamejipanga katika mistari kwa utulivu, hakuna vurugu na kadhalika. Hivi kweli huwa hawajui kwamba wizi wa kura unafanyika zaidi katika majumuisho ya matokeo na si katika upigaji kura?

Kauli za watazamaji wa kimataifa zinaweza kuanzisha ghasia ni hii ilitokea katika uchaguzi uliofanyika Ethiopia Mei, 2005. Baada ya tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kutangaza ushindi kwa chama tawala cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Meles Zenawi (marehemu), watazamaji wa kimataifa wakiongozwa na wale wa kutoka nchi za Ulaya (EU) walitoa tamko rasmi kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

Hapo hapo vyama vya upinzani vikaingia mitaani na kufanya maandamano makubwa ambayo yalipambana na nguvu za polisi ambao walitumia risasi za moto na kuua watu zaidi 250. Viongozi kadhaa wa vyama hivyo walikamatwa na kufunguliwa mashtaka na kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Hata hivyo, EU iliingilia kati, ikatishia kusimamisha misaada yote kwa nchi hiyo na ndipo hukumu hiyo ikafutwa na hatimaye washtakiwa wote kuachiliwa.