Home Makala CHALAMILA: KWA JPM MAENDELEO NI BORA ZAIDI YA CHOCHOTE

CHALAMILA: KWA JPM MAENDELEO NI BORA ZAIDI YA CHOCHOTE

4143
0
SHARE

NA PENDO FUNDISHA, MBEYA


Maendeleo ni mabadiliko yanayoonekana kuboresha hali ya binadamu katika nyanja mbalimbali za maisha. Upande wa sayansi, maendeleo yanahusu ongezeko la ujuzi kutokana na utafiti na mabadilishano ya matokeo yake. Upande  wa historia yanahusishwa na utambuzi wa kwamba ulimwengu unaweza kuboreshwa zaidi kutokana na mchango wa sayansi, teknolojia na uhuru.

Upande wa jamii yanahusishwa na tarajio la kwamba binadamu anaweza kupata hali bora zaidi katika mafungamano ya siasa na uchumi lakini mara nyingi siasa inatajwa kuharibu maendeleo kama itatumika vibaya na inaweza kuharibu maadili ya uchumi, na hata kuangamiza kabisa uhai wa maendeleo.

Kuna dhana imejengeka kwa Watanzania kwamba maisha yote ya binadamu ni siasa, na hakuna mtu anayeweza kuishi bila ya siasa, wengine wanasema siasa ni mchezo mchafu na ndani yake hakuna adui wala rafiki wa kudumu, lakini ukweli ni kwamba siasa inapogeuka na kuwa kisababishi cha watu kuvunja sheria, kanuni na taratibu, inakuwa ni moja ya changamoto ya kutopatikana kwa maendeleo na kukua kwa uchumi.

Dhana hii imejengeka mkoani Mbeya ambapo wananchi wanakubali kuishi kisiasa badala kuitumia siasa kuleta maendeleo. Bado watendaji wa Serikali wanatajwa kuruhusu siasa iwatawale na kusahau sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya kazi.

Kutokana na hulka hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, anatumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa watumishi wa umma na kuwataka wasome vizuri miongozo yao ya kazi.

Anasema watumishi wa umma hawapaswi kuwa mashabiki wa kisiasa, badala  yake wanatakiwa kuishauri Serikali kwa kutoa mawazo yatakayosadia kusukuma mbele kugurudumu la maendeleo.

Chalamila, anayasema hayo kwa sababu katika kipindi kidogo alichokaa, amebaini kwamba Mkoa wa Mbeya umetawaliwa na siasa na kwa kiasi fulani zimekuwa zikikwamisha maendeleo na hali hiyo imeenda hadi kwa watumishi wa umma hasa Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

“Nimebaini ndani ya halmshauri ya Jiji la Mbeya pana UCCM na  UCHADEMA, lakini ukiwa kama mtumishi, wewe unatakiwa kubaki kwenye utumishi wako na kubwa ninaloliona hapa ni watu kuchafuana tu,” anasema.

Anasema wapo watumishi wanaojiita kuwa ni wanaccm, kazi yao ni kuchora njama za kupiga fedha wakishirikiana na baadhi ya viongozi wa Serikali na viongozi wa CCM na wanapobanwa, basi hukimbilia kuwachongea au kuwaharibia wenzao kwa kuwaita ni wanachadema.

Anasema kazi yao ni kupeleka maneno kwenye chama na kuwataka watu waondolewe kwa visingizio kwamba ni wapinzani wanashabikia CCM, jambo ambalo halina ukweli kwani watendaji hao wanagoma kutekeleza maagizo binafsi ya viongozi walafi kwa  kuzingatia  sheria, kanuni na miongozo ya kazi ili kuwaletea wananchi maendeleo.

“Niwaambieni kwamba wanaccm na wanachadema, watapata sifa baada ya wewe tu, kuwatendea wananchi vizuri, ukiwa msafi ni faida kwa wanaccm ambao ndio serikali inatekeleza ilani yake na  ukiwa mchafu atakayesulubiwa jukwaani ni viongozi wa chama tawala  ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa,” anasema.

Anasema mwaka  2014 watu walikuwa wanaomba apatikane rais anayesimamia sheria, sasa amepatikana, lakini baada ya kupatikana, wameanza kusema  ni mkali mno. Ukweli ni kwamba, rais hajabana demokrasia ya maendeleo, ila amebana demokrasia ya mdomoni.

“Ni bora mtu akaendelea kuwa Chadema kama anatekeleza taratibu, sheria za kazi na mimi nasema wazi nitamlinda, lakini si kufanya mambo kwa kupakaziana na  kama neno Chadema linakuja eti kwa sababu umezibana sheria ni vizuri wewe piga kazi na mimi nitakulinda,”anasema.

Aidha, anawataka watumishi hao kutambua kwamba wanapokuwa watumishi wa umma, wemechagua kuwa washauri namba moja wa Serikali, na si mpinzani wa Serikali na atajipambanua  kwa kuisaidia Serikali.

“Sipingi watu kuikosoa Serikali yao kwani kila mtu anahaki na uhuru wa kuongea, ila jitathimini vizuri kama unataka kuwa mpinzani wa Serikali, unapaswa kuondoka ndani ya Serikali na kwenda taasisi binafsi ili uwe huru.

“Lakini naamini kwamba mtendaji unafahamu jukumu lako kwamba wewe ni mshauri namba moja wa Serikali, unapokuwa mtumishi wa umma na kupoteza lengo la Serikali unakuwa unakosea sana….katika elimu yangu yote niliyoisoma sijawahi kuona demokrasia na haki ya mtumishi wa umma kuipinga serikali yake,” anasema.

Anasema Rais Magufuli amekuwa akihimiza wateule wake kusimamia mapato, ili uchumi wa nchi uweze kukua, lakini ukiangalia huko ndani wanaosababisha mambo mazuri yasiende kwa wananchi, ni watumishi wa Serikali, kwani wameshindwa kuwa watu waadilifu katika kusaidia kupeleka maendeleo mbele.

Anasema ni vema watu wakaachana na ushabiki wa kisiasa, kwani nyadhifa hizo wamezipata ikiwa ni dhamana  na vipo katika mfumo wa maji ya bahari ‘yanapokupwaa na kujaa’ lakini ni vizuri yakatowekwa kwa amani kuliko kunyanganywa kutokana na kushindwa kutenda haki itakuwa ni adhabu kubwa hata kwa Mwenyezi Mungu.

“Halmashauri hii imekuwa na malalamiko mengi sana na asilimia kubwa ni upigaji wa fedha, rais analeta maafande kuwa wakurugenzi, mjue kuna jambo, kumekuwa na aina mbili za binadamu—wapo  wanaotii amri kwa shuruti na wale wasiotii kwa shuruti, wapo waliosema nimeletwa niumalize upinzani, ieleweke tangu upinzani uanze Serikali ipo, kinachotugharimu hapa ni kuwa na watu wezi, wawe Chadema au CCM” anasema.

Anasema ametoka  kwenye chama, anafahamu mambo yaliyomo kama watu wangekuwa wanafuata misingi ya sheria mambo yangeenda vizuri.

“Watanzania hivi sasa wasingeumia, lakini mijitu ilikuwa ikijinufaisha yenyewe na kuwasahau wananchi ambao ni wapiga kura na zinazotumika ni kodi zao,” anasema.

Hata hivyo, anasema tayari amefanikiwa kutembelea halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya na kuna baadhi ya mambo ameyabaini na atahakikisha yanafanyiwa kazi, lakini anatarajia kuanza ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.

Anasema Serikali imetumia kiasi cha Sh bilioni 21 kwa ajili ya utengenezaji wa meli tatu, ambapo meli mbili za mizigo zimegharimu bilioni 11ambazo tayari zimeanza kazi ya kusafirisha makaa ya mawe kutoka nchini Malawi na kuyaleta Tanzania kwa ajili ya matumizi ya kiwanda cha saruji Mbeya, huku meli moja ya abiria ikiendelea na matengenezo itakabidhiwa Desember mwaka huu.

Anasema meli hiyo inatarajia kutumia bilioni tisa na kubeba abiria 200 tani 200 na kufanya safari zake Ziwa Nyasa, lingine ni kukamilika kwa barabara yenye urefu wa kilomita sita iendayo Matema inajengwa kwa kiwango cha lami na kwamba inatarajia kutumia sh bilioni 56, lakini kuna kipande kimeongezwa kinachofika Kyela Mjini chenye urefu wa kilomita kitakachotumia bilioni 4.5 na mkandarasi anaendelea na kazi zake.

Akizungumzia vituo vya afya, Chalamila anasema ametembelea Kituo cha Afya cha Ipinda, wilayani Kyela, ambapo kimekamilika  na kutumia milioni 625 kati ya fedha hizo milioni 500 ni fedha kutoka Serikali kuu na zilizobaki zimetoka serikali za mitaa pamoja na wadau wa maendeleo.

Anasema Wilaya ya Rungwe, ametembelea Chuo cha Elimu Mpuguso, ambacho kimepewa bilioni tisa kwa ajili ya upanuzi wa majengo ya walimu, madarasa na kujenga maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi na maktaba na kwamba mradi huo ni mkubwa.

Kwa Halmashauri ya Busokelo, Mkuu huyo anasema ametembelea kituo cha afya ambacho kimepewa Sh milioni 500 na kipo mbioni kukamilika katika Kijiji cha Mpata, huku Wilaya ya Chunya akikagua barabara yenye urefu wa kilomita 72 ambayo imetumia shilingi bilioni 99.1 na sasa kunakilomita 39 za kutoka Chunya Mjini kuelekea Makongorosi zinazojengwa kwa bilioni 56.

Anasema, viele vile Chunya kuna chuo cha afya ambacho kimepewa Sh milioni 400 kwa ajili ya ujenzi ambazo ni fedha nyingi sana za serikali lakini kuna kituo cha afya Makongorosi ambacho wananchi na halmashauri wamechanga na kufikia milioni 78 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Hata hivyo, upande wa halmashauri ya Mbarali Mkuu huyo anasema ujenzi wa barabara ya Rujewa –Ubaruku na kiasi cha shiligi bilioni tano kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo pia kituo cha afya kilichopo katika Kijiji cha Utengule Usangu kimepewa milioni 400.