Home Makala CHAMI: SERIKALI IBORESHE MAZINGIRA YA UWEKEZAJI

CHAMI: SERIKALI IBORESHE MAZINGIRA YA UWEKEZAJI

929
0
SHARE

NA SAFINA SARWATT,  KILIMANJARO


SEKTA ya viwanda ni sehemu muhimu ya uchumi wa kisasa ambako bidhaa zinatengenezwa kwa wingi kwa kutumia mashine na michakato maalumu.

Viwanda huhesabiwa kati ya shughuli za sekta ya pili ya uchumi kwa ujumla ambako malighafi zinabadilishwa kuwa bidhaa, mfano pamba kuwa kitambaa na nguo.

Viwanda hutumia zaidi mashine na hupanga michakato yake kikamilifu na kutoa bidhaa zisizosanifishwa kwa wingi. Viwanda vimejitokeza tangu kupatikana kwa mashine tangu karne ya 19.

Kupatikana kwa mashine ya mvuke kulirahisisha gharama za kutengeneza vitu mbalimbali na kusababisha mapinduzi ya viwanda yaliyoanza nchini Uingereza yakisambaa kwa haraka Ulaya na Marekani.

Sekta ya viwanda ilipanuka sana katika karne ya 19 hadi katikati ya karne ya 20, katika nchi zilizoendelea karibu nusu ya wafanyakazi wote walikuwa katika sekta hii.

Ila tu tangu nusu ya pili ya karne ya 20, sekta ya tatu na ya nne yaani biashara na huduma zilianza kuwa na wafanyakazi wengi zaidi.

Haya ni matokeo ya kufanikiwa kwa viwanda vinavyoendelea kutoa bidhaa nyingi kwa haraka na uhitaji wafanyakazi kwa sababu uwezo wa mashine uliongezeka.

Hata hivyo, tumeshuhudia nchi zilizoendelea zikifanikiwa kubadili mifumo ya uchumi kutoka kutegemea kilimo na kukuza sekta ya viwanda kwa kasi kubwa na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.

Aliyekuwa waziri wa zamani wa viwanda na biashara ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uchumi, Dk. Cyril Chami, katika mahojiano yake na RAI wiki hii anasema nchi nyingi duniani zilizoendelea ni zile ambazo zimewekeza kwenye sekta za viwanda  na kuimarisha uwekezaji.

Tangu uhuru makusudio makubwa ni nchi kuwa ya viwanda, lakini mpaka leo bado hatujafanikiwa na Tanzania bado nchi maskini ingawa kila rais aliyeingia madarakani aliweka msisitizo mkubwa  juu ya Tanzania ya viwanda ambapo kila mmoja kwa nafasi yake alipokea kwa utashi wake.

Jukumu la ujenzi wa viwanda

Dk. Chami anasema Serikali ikiacha jukumu la ujenzi wa viwanda kwa sekta binafsi bila kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, malengo ya Tanzania ya viwanda hayatafikiwa.

Na kwamba ili Tanzania ya viwanda ifanikiwe, lazima Serikali iboreshe mazingira mazuri ya uwekezaji, kujenga mahusiano mazuri baada ya viwanda kujengwa Serikali itafute wataalamu .

Dk. Chami anasema viwanda hivyo vijengwe katika maeneo ambayo ni muhimu  kwenye nchi, kwa sababu  vikijengwa kwenye maeneo muhimu vitaweza kuajiri watu wote mpaka wale ambao hawajasoma kabisa.

“Ubora wa bidhaa unahitaji utaalamu wa hali ya juu zaidi, hivyo ni lazima kuwepo wataalamu watakaosimamia ubora na watakaoleta malighafi kwa ajili ya kuendesha viwanda,” anasema Dk. Chami.

Anasema viwanda vinatakiwa kujengwa maeneo ambayo yana muunganiko mkubwa na kwamba, viwanda hivyo pia vitakavyojengwa viweze kugusa maisha ya Watanzania wote kwa maana ya wakulima na wafugaji kwa kuwa kundi hilo ndilo pekee lipo nyuma kimaendeleo.

“Mfano pamba, wakulima watakuwa na uhakika wa kupata soko la uhakika na kwamba pamba zao hazitaathiriwa na soko la dunia kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya bei kwenye soko,” anasema.

Anasema faida nyingine ni endapo kitajengwa kiwanda cha pamba husaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kutokana na uingizwaji wa nguo kutoka nje.

“Tutakuwa tunatengeneza nguo wenyewe na kuuza nje ya nchi badala sisi kuwa soko la bidhaa ya wenzetu,” anasema Dk. Chami.

Kiwanda cha pamba kikijengwa pamba zote zitaenda moja kwa moja kiwandani, faida yake ni kwamba tunapata nguo, mafuta na mbegu na malisho ya mifugo.

“Mfano wa pili pia ni kilimo cha mazao ya michikichi eneo hilo litaweza kuchochea kilimo hicho kwa wakulima,” anasema.

“Alizeti nayo inalimwa kwa wingi katika mikoa ya Singida, Dodoma na Manyara, badala ya wakulima kukamua mafuta Serikali ichukue mazao yale na kutengezea mafuta safi ya kula ambayo hayana kemikali, kwa sababu kila mwaka mafuta ya kula zaidi ya tani 500,000 yenye kemikali huingizwa nchini lakini kama tungekuwa na kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti tusingekuwa na wimbi kubwa la uingizwaji huo wa mafuta.

“Kuna zao la korosho ambalo iwapo kukiwapo na kiwanda chenye uwezo wa kubangua korosho zote zinazolimwa kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara, manufaa yake yataonekana kwani zao hilo lina soko kubwa Uingereza, ambapo kilo moja huUzwa pauni nne hadi sita.

“Eneo la mahindi tutakuwa tunazalisha unga na pumba na kuwauzia wenzetu wa Kenya badala ya kusafirisha mahindi, kwani faida yake ni kubwa kwanza pumba tunapata malisho ya ng’ombe na  kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuongeza viwango vya ubora wa maziwa ya Tanzania.

“Ukiangalia Kenya ndiyo wanaongoza kwa uzalishaji wa maziwa wakati sisi ndiyo tunawauzia mahindi na wao wanapata faida mara tatu, kwanza wanachukua mahindi yetu kwa bei rahisi wanatuuzia unga maziwa na pumba za mahindi,” anasema Chami.

Anasema viwanda ndiyo eneo pekee ambalo linaweza kutoa ajira mpaka kwa wale watu ambao hawajasoma kabisa pamoja na wasomi wenye shahada ya uzamivu, viwanda vitakavyojengwa pia viwe vinagusa maisha ya Watanzania wote ikiwamo wakulima na wafugaji.

Dk. Chami anasema katika eneo ambalo nchi ingefanikiwa kukuza uchumi wake na kuondokana na umaskini wa hali ya utegemezi, ni pamoja na kuimarisha sekta ya viwanda.

Anasema viwanda ni njia pekee ya kumaliza umaskini na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na kudhibiti wimbi kubwa la vijana wanaojiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na pombe haramu.

Uwepo wa viwanda bila mali ghafi hauwezi kusaidia chochote ni lazima kuwepo mali ghafi za kutengenezea bidhaa, kudhibiti uingizwaji wa bidhaa feki zinazoingizwa nchini kupitia njia zisizo halali.

“Kama mazingira hayo yataandaliwa kwa kukidhi matakwa haya yote vitakuwa vivutio vikubwa kwa makundi yote.

“Fursa zikiwapo ni rahisi kuwashawishi wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake watalima kilimo bora, kwani tatizo kubwa lililopo ni kwamba wakulima wengi wamekata tamaa kutokana na kutokuwa na uhakika wa soko,” anasema.

mwisho