Home Latest News CHANGAMOTO ZA OBAMA ZIWAONGOZE WATAWALA AFRIKA

CHANGAMOTO ZA OBAMA ZIWAONGOZE WATAWALA AFRIKA

5154
0
SHARE
Former U.S. President Barack Obama speaks during a meeting with youth leaders at the Logan Center for the Arts at the University of Chicago to discuss strategies for community organization and civic engagement in Chicago, Illinois, U.S., April 24, 2017. REUTERS/Kamil Krzaczynski - RTS13Q4A

NA HILAL K SUED     |    


Katika historia ya mahusiano baina ya Marekani na Afrika ni marais wa Marekani sita tu ndiyo wamewahi kutembelea bara hili.

Wa kwanza alikuwa Franklin Roosevelt alipofanya ziara ya siri iliyoanzia Morocco mwaka 1943 wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwa ajili ya Mkutano wa Casablanca, mkutano uliopanga namna ya kumaliza uvamizi wa Ujerumani katika nchi za Ulaya.

Nchi zingine alizotembelea ni pamoja na Gambia na Senegal (zikiwa bado zinatawaliwa na wakoloni) na Liberia. Wakati huo ni nchi zipatazo tatu tu ndiyo zilikuwa huru – Liberia, Uhabeshi sasa Ethiopia na Misri.

Tangu 1978 marais wote wa Marekani, isipokuwa Ronald Reagan wametembelea Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara na ni nchi 14 ndiyo zimetembelewa. Rais Donald Trump bado hajafanya ziara Barani Afrika.

Lakini katika hawa ni Barack Obama pekee ndiyo amevutia hisia za wengi, hasa katika hotuba zake kuhusu masuala ya demokrasia na utawala bora barani Afrika, (bara la asili yake), masuala ambayo amesema yamekuwa kizungumkuti kikubwa sana na hata kuathiri maendeleo ya nchi nyingi za Afrika.

Wiki iliyopita rais huyo wa zamani wa Marekani alikuwa Afrika ya Kusini katika maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Nelson Mandela na kutoa karipio kali kuhusu mienendo ya baadhi ya viongozi Barani.

Katika hotuba yake iliyoshangiliwa sana Obama bila kutafuna maneno alizinanga nchi kadha Barani Afrika (bila kuzitaja) zinazokuza kile alichokiita siasa za “umimi” – (strongman politics). Alisema Afrika haitaki viongozi wa nguvu, bali inahitaji taasisi za umma za nguvu na huru.

Kabla ya wiki iliyopita Obama alipata kutoa kauli hiyo mara mbili wakati akiwa rais wa Marekani – kwanza alipolihutubia Bunge la Ghana wakati wa ziara yake ya kwanza barani Afrika mwaka 2009, miezi michache tu baada ya kushika madaraka.  Mara ya pili ni alipohutubia mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Julai 2015.

Katiba hotuba yake kwa Bunge la Ghana aliisifia sana nchi hiyo kwa kuonyesha mfano wa demokrasia ya kweli kwa Bara la Afrika. Alisema katika karne hii ya 21 taasisi za utawala zilizo imara, huru, zenye uwezo, za kuaminika, na zinazoendeshwa kwa uwazi ndiyo ufunguo wa mafanikio katika maendeleo.

Aliongeza kusema Bunge lenye nguvu, kikosi cha polisi kilicho aminifu, uhuru wa mahakama, wa vyombo vya habari na sekta binafsi, na asasi za kiraia zilizo mahiri ni vitu ambavyo hutoa uhai kwa demokrasia kwa sababu hivyo ndivo vinahusika sana katika maisha ya watu.

Alirudia maneno kama hayo katika hotuba yake katika Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) pale aliposema kuna baadhi ya nchi ambazo zimeonyesha kwamba wananchi wanaweza kudhibiti hatima yao na kuleta mabadiliko kuanzia chini kwenda juu na kutolea mfano nchi ya Kenya (nchi yake ya asili) ambako asasi za kiraia na sekta binafsi kwa pamoja zilisaidia kutuliza ghasia baada ya uchaguzi wa 2007.

Alisema historia daima iko upande wa Waafrika walio na ushujaa katika kukabiliana na uonevu, ukandamizaji wa haki za binadamu na siyo wale ambao kwa matakwa binafsi hubadili katiba ili waendelee kukaa madarakani.

Hakuna ubishi kufuatana na historia yake bara la Afrika limepitia misukosuko mingi. Ni kitovu cha mwanzo wa binadamu na tawala zake za kale zilikuwa na maktaba kubwa kubwa na vyuo vikuu. Lakini uovu wa utumwa ulishika mizizi, si katika nchi za nje tu, bali pia barani hapa.

Ukaja ukoloni ambao ulipora uchumi wa Afrika na pia uwezo wa watu wake kujiamulia hatima zao. Hatimaye vyama vya ukombozi viliibuka na kukua katika harakati kubwa za kutaka kujitawala na watu wa Afrika walishangilia sana pale bendera za kigeni zilipoanza kuteremka.

Lakini nusu karne baada ya bendera hizo kuteremka, nchi hizi bado ziko katika umasikini mkubwa unaosababishwa na tawala mbovu na ufisadi ulikithiri miongoni mwa viongozi wao na migogoro isiyoisha, na hivyo kuathiri maendeleo ya wananchi. Haya yanajiri pamoja na ukweli kwamba mwishoni mwa miaka 80 kulikuwapo msukumo mkubwa kwa nchi za Afrika kuondokana na udikteta wa chama na/au wa mtu mmoja na kuanzisha.

Msukumo huo ulitokana na wimbi la upepo wa demokrasia ulioanzia Ulaya ya Mashariki pale tawala za kikomunist zilipoanza kudondoka moja baada ya nyingine, ikiwemo ‘baba’ yao Urusi ya Kisovieti. Upepo huo ulisisitiza siasa za mfumo wa vyama vingi, kufanya uchaguzi wa kidemokrasia, na kuweka ukomo wa vipindi vya marais kuwa madarakani.

Lakini miongo mitatu baada ya upepo huo wa kidemokrasia chaguzi za nchi nyingi Barani humu huwa ni kama kitu kinacholazimishwa tu na mataifa fadhili na mara nyingi wao ndiyo huchangia fedha ya kuendesha chaguzi zao.

Hapa kwetu kila mtu aliona kwamba uchaguzi wa 2015 uliandaliwa kwa kasi za zimamoto na hasa katika uandikishaji na uandaaji daftari la wapigakura. Ilikuwa kama vile watawala waligutushwa tu kunatakiwa kuwepo uchaguzi.

Dakika za mwisho mwisho mmoja wa watendaji wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuwekwa mwingine, wakati Tume yenyewe ni mgogoro mkubwa kutokana na madai ya kutokuwa huru, madai yanayotiwa nguvu na ukweli kwamba uteuzi wa tume hiyo hufanywa na mtu mmoja – mkuu wa chama tawala ambaye pia mara nyingine huwa ni mgombea wa nafasi hiyo ya urais.

Na mpangilio wa aina hiyo ndiyo huzaa kile alichosema Obama wiki iliyopita alipokuwa Afrika ya Kusini kwamba mgombea aliye madarakani hushinda kwa asilimia 90, huku wapinzani wake wakuu ama wako kizuizini, au mikutano yao ya kampeni hudhibitiwa, baadhi ya magazeti hunyamazishwa na asasi za kiraia kusakamwa.

Udanganyifu wa namna ulitokea Ethiopia katika uchaguzi wa 2015 ambako chama tawala cha Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF) kilibeba viti vyote 540 vya Bunge, upinzani haukuambulia hata kiti kimoja.

Lakini matokeo yakae twayafahamu – baada ya miaka miwili tu nchi hiyo ilishindikana kutawalika, maandamano kila siku, ubabe wa utawala uliwaweka kizuizini maelfu ya watu, hadi Waziri Mkuu Hallemariam Desaleign alilazimika kubwaga manyanga baada ya kuona udangayifu wake katika uchaguzi haumpeleki popote.

Wananchi wengi wa Ethiopia wanaendelea kuzama katika umasikini mkubwa hadi baadhi yao wanaikimbia nchi yao, na wengi wamekuwa wakipitia hapa Tanzania katika safari za hatari kubwa – huku baadhi yao wakikamatwa na mamlaka za hapa. Umasikini huo umekuwa ukiongezeka kwa sababu watawala walikazania zaidi kuendeleza vitu (miundombinu n.k.) kuliko watu.

Haya yote yanatokea kwa sababu watawala wa sasa barani Afrika hushindwa kupata yale ya ndani mwa wananchi kuhusu maisha yao kwa sababu tu misimamo yao ni tofauti na ya watawala, hivyo hawawezi kujua mawazo au hoja zao.

Watawala wanaweza kubadilisha misimamo ya watu hawa kwa njia ya hoja, au pengine wanaweza kubadili hoja na misimamo yao (watawala) – vyote kwa nia njema kwa mustakabali wa taifa. Kikubwa kinachotakiwa ni hekima na siyo ubabe.