Home Makala CHE GUEVARA- Mpiganaji aliyesalitiwa kwa kutaka kukomboa Afrika kutokea DRC

CHE GUEVARA- Mpiganaji aliyesalitiwa kwa kutaka kukomboa Afrika kutokea DRC

3781
0
SHARE

 NA JOSEPH MIHANGWA

WIKI iliyopita tuliangazia juhudi za mmoja wa mashujaa wa Mapinduzi ya Cuba dhidi ya ubeberu wa Kimarekani, mzaliwa wa Argentina, “Ernesto” Che Guevara, za kujaribu kudidimiza ubeberu huo barani Afrika kwa staili ya Mapinduzi ya Cuba na yale ya Zanzibar mwaka 1964, ni mfano usioweza kusahaulika juu ya mshikamano wa “walala hoi” dhidi ya ubeberu.

Misaada ya Cuba ya Fidel Castro, iliotoa kwa harakati za ukombozi kwa nchi changa na zenye kuonewa Barani Afrika unazidi kipimo cha ukarimu, kisiasa na kijeshi kwa nchi za Algeria na Sahara Magharibi hadi Eritrea; Ethiopia, Zanzibar na kwa makoloni ya Kireno ya Guinea Bissau, Angola na Msumbiji, Endelea…

Jimbo la Katanga liligombewa na mataifa ya Ulaya kwa utajiri wake wa madini, ambapo mwaka 1961 lilifikia kujitenga kutoka Serikali ya Congo iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa kwanza, Patrice Emery Lumumba na kuwa chini ya kibaraka wa Wabelgiji, Moise Tshombe. Kuuawa kikatili kwa Lumumba mwaka 1961 kwa msaada wa Shirika la Kijasusi la Marekani [CIA] kulitokana na Kiongozi huyo mzalendo wa Afrika kujipambanua na upande wa nchi za Kikomunisti katika mgogoro huo wa Congo, na kibaraka wa nchi za Magharibi, Mobutu kuchukua madaraka.

Hata yule jasusi mkubwa wa CIA, kitanzi cha Wakomunisti Congo na nchini Portugal aliyepewa jina la “The Hangman of Portugal” – Mnyongaji wa wazalendo nchini Ureno”, Frank Carlucci, alipelekwa Zanzibar mwaka 1964 akitokea Congo yenye matata [baada ya Portugal] kwenda kuratibu na kusimamia mchakato wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kwa shinikizo la Marekani na Uingereza zilizohofia Zanzibar ya Mapinduzi kuangukia kambi ya nchi za Kikomunisti.

Nasser, aliyetawala Misri kwa kumpindua Mfalme Farouk mwaka 1958, alimuonya Guevara na kumtahadharisha juu ya hatari kwa yeye kujigeuza “Tarzan” wa kingano asiyeshindwa, Mzungu mweupe kati ya watu weusi, akiwaongoza na kuwalinda badala ya kuwapa mafunzo na ujasiri waweze kupigania uhuru wenyewe dhidi ya adui.

Kuna tetesi na hisia zisizothibitishwa kwamba Che Guevara alishiriki ama kupanga au katika mapambano ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 kwa upande wa kikosi cha wanaharakati wa Kikomunisti wa Umma Party [UP] ambao wengi wao walipata mafunzo ya Kijeshi nchini Misri na Cuba. Uvumi wa aina hiyo ulikuwa hai siku ya Mapinduzi kwa duru za Kibalozi Visiwani, wageni na wapita njia walionukuliwa wakisema waliwaona Wacuba [wenye madevu]; au kwamba walisikia wapambanaji hao wakiongea Kihispaniola.  Kama hilo halikuwa kweli, basi bila shaka watu waliokuwa wakiongelewa ni wale vijana wa Abdulrahman Babu wa Umma Party, wahitimu wa mafunzo ya Kijeshi kutoka Cuba, waliorejea nchini Zanzibar wakiongea lugha ya Kihispaniola kwa ufasaha mkubwa.

Tukio lingine linalofanya watu wafikirie Che Guevara alikuwa na mkono wake katika Mapinduzi ya Zanzibar ni ziara yake mwaka mmoja baada ya Mapinduzi, Februari hadi Aprili 1965 wakati huo akijiandaa kuelekea Congo.

Uzito wa ziara yake Visiwani haukuwa wa kawaida kwani ingawa sherehe za kwanza za Mapinduzi Visiwani zilitakiwa kufanyika Januari 12, 1965,  ziliahirishwa hadi Februari 12, 1965 pengine kumsubiri awasili kwa ziara ya siri Visiwani Februari 11, 1965 ili ashiriki kwa siri siku inayofuata.

Rais Abeid Amani Karume alimpokea kwa bashasha kubwa na kumkabidhi kwa Ali Sultani [Mhitimu wa Mafunzo ya Kijeshi Cuba, 1962] akisema:  “Sikiliza Ali! Nakukabidhi mgeni huyu, “Comrade” mwenzenu uwe naye wakati wa ziara yake hapa Zanzibar na umhudumie vizuri”. Che alipewa kwa siri kubwa nyumba ya kulala na ulinzi madhubuti pale Beit-Ras hadi alipoondoka kwenda Dar Es Salaam akiwa njiani kuelekea Congo kwa mapambano.

Jambo ambalo Karume hakuelewa ni kwamba, Che na Ali Sultani walikuwa wanajuana tangu mwaka 1961 kule Cuba wakati Chama cha kiharakati cha Zanzibar Nationalist Party [ZNP] kilipofungua Ofisi Havana, Cuba; na tena mwaka mmoja baadaye, pale Ali na wanaharakati wenzake wa ZNP walipokwenda mafunzoni nchini humo mwaka 1962 kabla ya kujiengua ZNP pamoja na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Babu mwaka 1963 kuunda Umma Party, kilichoshiriki Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Usiku wa Februari 12, 1965, Che alikutana na Makomredi waliokuwa Cuba 1962 katika karamu maalum iliyoandaliwa na kufanyika nyumbani kwa Ali Mahfoudh eneo la Migombani.  Waliokuwepo ni pamoja na Ali Mahfoudh mwenyewe, Mohamed Ali Foum, Ali Abdullah Bafaki, Salim Ali Ahmed Salim na wengine. Kanali Mahfoudh ndiye alikuwa Mkuu wa kwanza wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Zanzibar [Zanzibar People’s Liberation Army] – ZPLA kufuatia Mapinduzi. Che alisikitika kuwakosa baadhi ya Makomredi, kama Amour Dugheish, Salim Saleh, Hashil Seif Hashil, Ali Mshangama na wengine ambao wakati huo walikuwa mafunzoni nchini Urusi na Indonesia.

Ziara ya Che Guevara Visiwani ndiyo iliyoibua tetesi zilizonaswa na “vyanzo” vya Ubalozi wa Marekani mjini Dar Es Salaam kwamba, mpiganaji huyo alikuwa pamoja na Babu nchini Tanzania; lakini Mwalimu Nyerere akakanusha na kujifanya hajui kitu.

Kikundi cha waasi ambacho Guevera alidhamiria kukiunga mkono nchini Congo kiliongozwa na Gaston Soumialot, na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Waasi hao, mwenye umri wa miaka 26 tu wakati huo, aliitwa Laurent Desire Kabila [baba yake na Rais wa sasa wa DRC, Joseph Kabila], Mbunge kutoka Katanga Kaskazini na msomi mhitimu wa Paris na Belgrade, aliyetarajia kuanzisha Serikali ya Kijimbo kwa  maeneo yaliyokombolewa Congo Mashariki.  Guevara kwa upande wake, alitarajia kuyatumia maeneo hayo kwa mafunzo ya kijeshi si kwa waasi wa Congo pekee, bali pia kwa Vikosi vya Ukombozi kwa nchi za Kusini za Barani Afrika na zaidi kama ingebidi, kufanya Congo kuwa kitovu cha Ukombozi mpana zaidi.

Aprili 20, msafara wa magari matatu aina ya Mercedez Benz nyeusi, uliondoka Dar Es Salaam na kuvuka ziwa Tanganyika kwa mtumbwi na kuingia Congo, Aprili 24, 1965.

Alichokiona Che kwa Waasi kilikuwa cha kusikitisha na kukatisha tamaa: Jeshi la Kabila halikufunzwa, lilikosa nidhamu na halikupangika vizuri kwa kazi ya kivita. Lilijaa uhasama wa kikabila na masengenyo miongoni mwa wapiganaji wake na liliongozwa na Makamanda wasio na ujuzi, wenye kupenda anasa, ufuska  na maisha ya utulivu na salama kwenye nyumba za vileo, dansi na “vimwana” mjini Kigoma, badala ya kuwa mstari wa mbele kwenye uwanja wa mapambano!.

Muonekano wa Jeshi hilo, kwa jina la “Jeshi la Ukombozi la Wananchi” [People’s Liberation Army] – PLA, ulikuwa wa kukatisha tamaa pia:  lilikuwa jeshi tegemezi na la kinyonyaji, lisilotaka wala kupenda kufanya kazi, mafunzo na mazoezi; halikupigana ila kudai mahitaji na kufanyiwa kazi na wananchi jirani, wakati mwingine kwa shuruti na kwa ukatili mkubwa. Kabila mwenyewe alionekana mara moja tu akifika na shehena ya pombe kali [whisky] na kuondoka kurejea Kigoma baada ya siku tano; vinginevyo alitumia muda mwingi kwa ziara za nje au kwenye makazi yake, Dar Es Salaam.

Akielezea kutofurahishwa na haiba na muonekano wa Kabila, Che Guevara alisema: “Amejaa umbeya wa kisiasa; ni mlevi kupindukia na dhaifu kwa wanawake, hana umakini wala ujasiri wa kimapinduzi”. Na pale kikosi cha Guevara kilipojitupa uwanjani kuwasaidia waasi hao, kilijikuta kikibakia pekee kwa Jeshi la Kabila kutimua mbio, Maafisa wao wakitangulia kwa woga na hofu; wakatelekeza silaha zao na kuwaacha majeruhi wajiokoe wenyewe.  Kwa jinsi hii, Jeshi la Mobutu, lililojumuisha Askari wa kukodiwa, lilizidi kupata ushindi siku hadi siku kwa kuwanyuka Jeshi la “walevi” la Kabila.

Miezi saba ya mapambano nchini Congo haikuweza kumpa Che Guevara na kikosi chake matumaini ya ushindi ili kutimiza ndoto yake. Hivyo, kwa uchovu na kukata tamaa, alianzisha safari kurudi nyuma kuvuka Ziwa Tanganyika hadi Kigoma na kuwasili Dar Es Salaam Novemba 1965 alikopumzika kwa miezi minne hadi Februari 1966.

Ndani ya chumba kidogo kwenye Ubalozi wa Cuba alikofikia, Che aliandika maneno yafuatayo kuelezea hisia zake: “Hii ni historia chungu ya kushindwa inayoumiza”. Aliondoka Dar Es Salaam, Machi, 1966 kurejea Cuba kabla ya kwenda Bolivia kuongoza mapambano kama yale ya Cuba, ambako aliuawa vitani, Novemba 7, 1967.