Home Latest News Cliton kuweka rekodi ya pili Marekani

Cliton kuweka rekodi ya pili Marekani

2101
0
SHARE
Hillary Clinton
Hillary Clinton
Hillary Clinton

JONAS MUSHI NA MITANDAO,

HILLARY  Clinton anaweza kuwa mwanamke wa kwanza kuwa mgombea urais wa Chama cha Democratic ambapo vyombo vya habari nchini Marekani vimetangaza kuwa tayari amepata kura nyingi kumshinda mpinzani wake Bernie Sanders.

Amejihakikishia ushindi baada ya majimbo sita kufanya uchaguzi yakiwemo California ambapo kulikuwa na wapigakura 543 na New Jersey wapigakura 142.

Chombo cha habari cha Associated Press kimesema  Clinton tayari amefikisha kura 2,383 ambazo zinahitajika ukiachia mbali kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wajumbe wenye nguvu.

Wakati hayo yanatokea mpinzani wake Bernie Sanders anasisitiza kuwa ni mapema kutoa matokeo ya mbio hizo za kuwania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama cha Democratic.

AP imesema Clinton tayari ana kura 1,812 za wajumbe wa kawaida na kura 571 kutoka kwa ajumbe wenye nguvu.

Duru za siasa nchini humo zinasema atakuwa ndiye mwanamke wa kwanza kuwa mgombea urais wa moja ya chama kikubwa nchini Marekani.

Hatotangazwa rasmi kuwa mgombea wa chama cha Demokrat mpaka katika mkutano mkuu mwezi ujao, licha ya kwamba mpaka sasa ameshafikisha idadi ya wajumbe wanaohitajika kuteuliwa kuwa mwakilishi wa chama na kumshinda Seneta wa Vermont Bernie Sanders.

John Hudak, naibu mkurugenzi wa kituo cha ufanisi wa uongozi wa umma katika taasisi ya Brookings aliiambia VOA kwamba umuhimu wa tukio hilo unaweza usipewe uzito unaohitajika kwa kuwa Clinton toka mwanzo anafahamika na aliingia katika kinyang’anyiro akitarajiwa atakuwa mshindi.

Clinton alipopata habari hizo Jumatatu usiku alitahadharisha wafuasi wake akisema ingawa hesabu za vyombo vya habari zinampatia idadi ya wagombea wanaohitajika ikiwa ni tukio ambalo halijawahi kutokea lakini bado kuna mashindano katika majimbo sita yaliyobaki kufanyika siku ya Jumanne na kwamba anapigana kwa nguvu kupata kila kura katika mashindano hayo.

Majimbo mengine ambayo yalifanya uchaguzi Jumanne kwa upande wa Democratic ni pamoja na  Montana (wapigakura 27), New Mexico (43), Dakota Kusini (25) na Dakota Kaskazini (23).

Mbio hizo zitahitimishwa katika jimbo la Washington DC ambapo uchaguzi utafanyika Juni 14 huku kukiwa na wajumbe 45.

Ni historia baada ya miaka 227

George Washington alichaguliwa kuwa rais mpya wa Marekani mwaka 1789 pamoja na marais 42 waliofuata ni wanaume. Kati yao 41 walikuwa wazungu na rekodi hiyo ilivunjwa na Barack Obama kwa kuwa rais wa kwanza wa Marekani mweusi.

Inaonekana sasa Clinton anakwenda kuvunja rekodi ya pili kwa kuwa mgombea mwanamke wa kiti cha Urais nchini humo.

Ni kwa muda mrefu vyama vikubwa vya nchini humo vimekuwa vikiweka wagombea wanaume lakini Clinton alianza kubadilisha dhana iliyokuwepo mwaka 2007 alipojitosa kwenye kinyang’anyiro hicho na kuangushwa na Obama.

Hii inaonekana kama mwanga mpya katika taifa hilo kwamba sasa wanatoka katika historia ya muda mrefu na wanaandika historia mpya.

Japo Clinton amewahi kushika nyadhifa kubwa za kuwa mke wa rais, useneta na Katibu Mkuu lakini kwenye urais anaonekana ni mtu mpya kutoka na jinsia yake.

Namna mchujo unavyofanyika marekani

Kabla ya Wamarekani kuamua nani wanayemtaka awe rais ajaye, wao kwanza huteua nani atakayewania kiti hicho.

Mchakato huo hung’oa nanga kwa mchujo wa kamati za wajumbe ambapo wananchi hupata fursa ya kumchagua mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Democratic au kile cha Republican.

Huu hapa ni mwongozo wa mchakato wa kuteua wagombea.

Je mchakato wa kuteua wagombea huwa vipi?

Kura za mchujo na mfululizo wa uchaguzi wa kamati za wabunge hufanyika katika kila jimbo na wilaya nje ya nchi ambayo huamua nani atapeperusha bendera ya kila chama.

Mshindi wa mchujo huo anawakusanya wajumbe – hawa ni wanachama wenye nguvu ya kupiga kura kumchagua mgombea katika mikutano ya chama.

Katika makongamano hayo ndipo mgombea wa urais wa kila chama huchaguliwa.

Nini tofauti kati ya kongamano la Chama na mchujo wa mashinani ?

Kongamano la chama kinahusisha wanachama wanaokusanyika katika shule, nyumba za watu binafsi na majengo ya umma kujadili wagombea sera zao na mapendekezo yao na mara nyingi wao hupiga kura waziwazi kwa kuonyesha mikono.

Hata hivyo katika mchujo wa mashinani wajumbe wa chama cha kisiasa huketi wakajadili sera na mapendekezo ya wagombea na huchagua mgombea wao kwa kupiga kura kwa siri wakitumia sanduku la kura.

Kura za mchujo wa mashinani huandaliwa na serikali ilihali kongamano la chama huandaliwa na watu binafsi vigogo wa chama, wanachama kwa jumla.

Kuna aina mbalimbali za mchujo na sheria mbalimbali:

Mchujo wa wazi -“Open”:

Mchujo huu ni wazi kwa kila mtu mwenye kadi ya kupigia kura bila kujali msimamo wa chama.

Hii inamaanisha kuwa japo mtu anaweza kuwa mwanachama wa Republican anaweza kushiriki katika kura za Demcrats. Kinyume chake pia ni sawa na halali.

Mchujo Nusu wazi: – “Semi” :

Hapa wajumbe wanaoruhusiwa kushiriki katika mchujo na upigaji kura sharti wawe ni wanachama waliosajiliwa rasmi katika chama kinachoendesha uchaguzi huo wa mchujo.

Kwa mfano wanachama wa chama cha Democrat pekee ndio wanaoruhusiwa kushiriki katika mchujo huo wa kumchagua mgombea wa tiketi ya urais kwa chama cha Democratic.

Hata hivyo kwa wale wapiga kura ”Huru/Binafsi”ambao hawaegemei upande wowote ama ni Democrat au Republican wanaweza kushiriki katika mchujo huu.

Jimbo la New Hampshire huwa linaendesha mchujo nusu .

Mchujo Uliofungwa – “Closed” :

Hapa wajumbe wa chama waliojiandikisha kikamilifu ndio wanaoruhusiwa kupiga kura katika majimbo waliojiandikisha pekee.

Kila mjumbe anaipigia chama chake kura kumchagua muaniaji tiketi wa chama hicho.

Kura za mchujo zinatofautiana katika kila jimbo.

Katika majimbo mengine, wajumbe wa chama cha Democratic huruhusiwa kukiri wazi wazi kuwa wanampendelea mgombea mmoja dhidi ya mwengine.

Mgombea lazima ashinde kwa wingi wa kura za wajumbe.

Mshindi sharti apate uungwaji mkono na nusu ya wajumbe na zaidi ili kupata uteuzi wa chama hicho.

Muaniaji kiti cha urais kwa tikiti ya Republican anahitaji kura 1236 za wajumbe iliatangazwe mshindi. Hata hivyo katika chama cha Republican mambo huwa ni ya siri.

Wakati huohuo muaniaji tikiti ya chama cha Democratic anastahili kutia kibindoni kura 2383 iliajihakikishie kupeperusha bendera ya chama chake katika uchaguzi mkuu ujao.