Home KIMATAIFA COMORO IMEKUMBWA NA MAJARIBIO 20 YA MAPINDUZI

COMORO IMEKUMBWA NA MAJARIBIO 20 YA MAPINDUZI

4680
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Nchi ya Visiwa vya Comoro, iko katika Bahari ya Hindi kusini mwa Tanzania. Ni nchi ya tatu kwa udogo wa eneo barani Afrika. Miongoni mwa visiwa vingi vinavojumuisha nchi hiyo kuna visiwa vikubwa vitatu – yaani Comoro yenyewe (jina la asili Ngazija), Moheli (Mwali) na Anjouan (Nzwani).

Kisiwa kingine ni Mayotte ambacho wakati wa uhuru mwaka 1974 wakazi wake waliukataa uhuru huo, na hivyo kubakia kuwa ‘koloni’ au kuwa chini ya ulinzi wa Ufaransa. Hawakukosea sana kwani vile visiwa vilivyopata uhuru vilikumbwa na misukosuko mikubwa ya kisiasa, ikiwemo matukio ya mapinduzi au majaribio ya mapinduzi ya kijeshi takriban mara 20.

Hata hivyo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuilazimisha Ufaransa kutoa uhuru kamili kwa Mayotte, azimio ambalo lilipingwa na Ufaransa kwa maelezo kwamba wakazi wenyewe wa kisiwa hicho wanapendelea ‘kulindwa’ na Ufaransa.

Wakazi hao walilithibitisha hilo katika kura nyingine ya maoni iliyofanyika mwaka 2011. Na kwa upande wake Umoja wa Afrika (AU) hautambui mamlka yoyote ua Ufaransa juu ya kisiwa hicho.

Comoro yenyewe ni mwanachama wa AU lakini pia ni mwanachama wa Umoja wa Nchi za Kiarabu (Arab League), hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa ni kusini zaidi duniani ndani ya Umoja huo na ni mwanachama pekee iliyeko kusini mwa mstari wa Ikweta.

MAPINDUZI YA KWANZA NA UJIO WA BOB DENARD

Kama nilivyotaja hapo mbele msururu wa mapinduzi, au majaribio ya mapinduzi ya kijeshi yaliweka madarakani marais kadha. Pamoja na Comoro kutokuwa na utulivu kisiasa, miongoni mwa wakazi wake wake wana tofauti kubwa zaidi kimapato kuliko nchi yoyote ile. Takwimu za 2014 zilionyesha kwamba zaidi ya nusu ya wakazi wake wanaishi chini ya kiwango cha kimataifa cha Dola 1.25 kwa siku.

Mapinduzi ya kwanza yalifanyika Agosti 1975 pale Rais Ahmed Abdallah alipopinduliwa na jeshi chini ya uongozi wa askari maarufu mamluki (wakati huo) wa Ufaransa Bob Denard na badala yake akasimikwa Said Mohamed Jaffar wa chama cha United National Front of the Comoros (FNUK). Miezi mitano baadaye, Januari 1976 Jaffar naye aling’olewa kutoka madarakni na badala yake akashika Waziri wake wa Ulinzi, Ali Soilih.

Ilikuwa ni wakati huu wakazi wa kisiwa cha Mayotte walipopiga kura ya maoni ya kwanza kubakia chini ya Ufaransa. Asilimia 64 ya wakazi walikubali kuendelea kuwa koloni la Ufaransa. Kura ya pili ya maoni ilithibitisha Februari 1976, na iliongeza asilimia hiyo hadi kufikia 99.

Mwezi Mei 1978 Bob Denard alirejea tena kumpindua Rais Ali Soilih na kumrejesha Ahmed Abdallah, akisaidiwa na Ufaransa, Rhodesia (ya Ian Smith) na utawala wa Makaburu wa Afrika ya Kusini. Katika kipindi kile kifupi Abdallah alikabiliana na majaribio saba ya kupinduliwa hadi hatimaye alipong’olewa na kuuawa.

Lakini tofauti na Soilih, utawala wa Abdallah ulikuwa wa kidikteta na alizidisha wito kwa wananchi kuzingatia misingi ya Kiisilam. Abdallah aliendelea kuwa madarakani hadi 1989 pale baada kuhofia kupinduliwa, alitia saini hati ya kuwaamuru askari wa ulinzi wa makazi yake, wakiongozwa na Bob Denard kuwanyang’anya silaha wanajeshi.

Muda mfupi baada ya kutia saini agizo hilo Abdallah alidaiwa kupigwa risasi na ofisa mmoja jeshi akiwa ofisini mwake. Lakini baadaye vyanzo vingine vya habari vilisema kombora la kifaru cha jeshi lilirushwa chumbani mwake na kumuua. Ingawa Denard pia alijeruhiwa katika tukio hilo, ilidaiwa kuwa muuwaji alikuwa ni askari chini ya kamandi yake (Denard).

BOB DENARD ATOROSHWA NA MAKABURU

Siku chache baadaye Denard mwenyewe alitoroshwa kwa msaada wa majasusi wa utawala wa Makaburu na kupelekwa Afrika ya Kusini. Baada ya kifo cha Abdallah binamu wa Soilih, Mohamed Djohara akashika madaraka.

Djohar alitawala hadi Septemba 1995, pale Bob Denard aliporejea Comoro kujaribu kufanya mapinduzi mengine. Lakini safari hii Ufaransa iliingilia kwa kutuma vikosi vya anga na kumlazimisha Denard kusalimu amri.

Wafaransa walimhamisha Djohar kwenda visiwa vya jirani vya Reunion na kumsimika Mohamed Taki Abdoulkarim, mtiifu kwa serikali ya Ufaransa  kupitia uchaguzi bandia. Taki alikaa madarakani kuanzia 1996 hadi kifo chake Novemba 1998.

Aliongoza kipindi cha migogoro mikubwa ya vyama vya wafanyaklazi, ukandamizaji wa haki za binadamu na majaribio ya kujitenga kwa baadhi ya visiwa. Taki alirithiwa na Rais wa Mpito Tadjidine Ben Said Massounde.

KUJITENGA KWA ANJOUAN

Mwaka 1997 visiwa vya Anjouan na Moheli vilitangaza kujitenga kutoka Comoro kwa lengo la kurudisha mamlaka ya Ufaransa, ambayo iliktaa kata kata ombi lao. Tukio hili lilisababisha mapambano makali kati ya majeshi ya waasi na askari wa serikali ya Comoro.

April 1999, Kanali Azali Assoumani, alitwaa madaraka baada ya kumpindua Tadjidine Ben Said Massounde aliyekuwa Rais wa Mpito. Tukio hili la mapinduzi au majaribio ya mapinduzi lilikuwa la 18 tangu uhuru mwaka 1975.

Azali naye alikuwa dhaifu madarakani hususan katika kudhibiti mamlaka na kuzuia harakati ya baadhi ya visiwa kutaka kujitenga, hususan kile cha Anjouan – suala ambalo liliibua shutuma nyingi kimataifa. Umoja wa Afrika (AU) chini ya usuluhishi wa Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini ulikiwekea vikwazo kisiwa cha Anjouan kwa lengo la kulazimisha suluhu.

Azali aling’atuka mwaka 2002 ili agombee uchaguzi wa kidemokrasia ulioandaliwa na ambao aliibuka mshindi. Azali alisifika sana katika kuanzisha mageuzi makubwa ya kisiasa Visiwani humo, hii pamoja na namna ya kuingia kwake madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Uchaguzi wa 2006 ulimpa ushindi Ahmed Abdallah Mohamed Sambi dhidi ya Azali. Azali alikuwa muumini mkubwa wa dini ya Kiisilam na alichukulia mafunzo ya dini nchini Iran  hadi akapewa jina la “Ayatollah.”

Mohammed Bacar, kanali muasi wa jeshi la Comoro alitwaa madaraka ya kisiwa cha Anjouan mwaka 2001 na Juni 2007 alifanya uchaguzi kisiwani humo ili kuthibitisha uhalali wa hatua yake, uongozi ambal ulikuwa unapingwa nba mamlaka ya serikali ya Comoro, na AU.

VIKOSI VYA AU VYAVAMIA ANJOUAN

Machi 25 2008 vikosi vya askari kutoka nchi kadha za Afrika (ikiwemo Tanzania) chini ya udhamini wa AU vilikivamia kisiwa hicho, na kwa ujumla vilipokelewa kwa shangwe na wakazi wa huko ambao wengi walielezea walivyo wakiteseka na utawala wa kikatili wa Kanali Bacar. Bacar alitoroka kwa boti na kwenda kisiwa cha Mayotte kuomba hifadhi.

Kufuatia uchaguzi wa 2010 Makamu wa rais wa zamani wa Comoro Ikililou Dhoinine aliapishwa na kuwa Rais wa Comoro baada ya  kampeni aliuoungwa mkono na Rais Ahmed Abdallah Mohamed Sambi. Dhoinine, mfamasia, alikuwa rais wsa kwanza wa Comoro kutoka kisiwa cha Moheli.

Na baada ya ya uchaguzi wa 2016 Azali Assoumani alishinda na kuwa rais kwa muhula wa tatu.