Home Makala CONFUCIUS INAVYOWAJENGA WANAFUNZI TANZANIA

CONFUCIUS INAVYOWAJENGA WANAFUNZI TANZANIA

2226
0
SHARE
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Mathew ya Jijini Dar es Salaam, James Edward (kushoto) na mwenzake Abdulaziz Ahmed wakibadilishana mawazo na Mkufunzi wa somo la lugha ya kichina, Zhu Yajing

NA FARAJA MASINDE


USHIRIKIANO wa China na Tanzania unazidi kuimarika kufuatia kuwepo mipango mbalimbali inayogusa shughuli za kukuza maendeleo kwa oande hizi mbili. Kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, mahusiano ya China na Tanzania kwenye sekta ya elimu nayo yanatanuka.

China inawekeza kwenye elimu hapa nchini kwa kasi kubwa. Kwa sasa inaangalia Tanzania kama rafiki katika utamaduni lakini pia kama ndugu ambaye anapaswa kufahamu kila kinachofanyika China ili kukuza zaidi uhusiano baina ya nchi hizi mbili.

Ili kudhihilisha kuwa imelenga kunyanua elimu ya Tanzania, China kupitia Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, imekuwa mstari wa mbele kubuni na kutengeneza mazingira bora ya kujifunzia kwa baadhi ya shule hapa nchini hasa shule za Msingi na Sekondari.

Taasisi hiyo katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wa kitanzania wanapata utajiri wa lugha hasa zile zinazotumika kwenye soko la ajira, biashara, uchumi na mambo mengine, imeamua kusogeza mafunzo ya Kichina kwenye shule za Sekondari.

Miongoni mwa shule hizo ni pamoja na Baobab ambayo iko Bagamoyo mkoani Pwani pamoja na St. Mathew iliyoko jijini Dar es Salaam. Shule hizi zote zimeanza kutoa mafunzo ya lugha ya Kichina yanayosimamiwa na taasisi ya Confucius.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Zhang Xaozhen anazibainisha sababu ambazo zinasukuma taasisi hiyo kutanua fursa za wanafunzi wa kitanzania kujifunza lugha pamoja na utamaduni wa kichina, kuwa ni kuwasaidia wanafunzi kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia hasa kiuchumi na kukabiliana na soko la ushindani.

“Duniani kote kwa sasa kujua lugha nyingi kumekuwa na tija kubwa mno jambo ambalo limekuwa na faida, kwani hatuwezi kupinga kuwa lugha ya kichina ni miongoni mwa lugha maarufu zaidi duniani kwa sasa achilia mbali China kuwa na uchumi mkubwa.

“Hivyo iwapo mwanafunzi hasa wa kitanzania ambaye yuko ngazi ya chini kwa maana ya shule ya Msingi au sekondari atakuwa na utajiri wa lugha ikiwamo kichina, itakuwa ni rahisi zaidi kwake kuweza kukabiliana na ushindani duniani ikiwamo pia kuweza kumudu kufanya biashara.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunashikamana na kizazi hiki cha kitanzania katika kukisaidia kuifahamu lugha hii wakati wakiwa shule. Hii itakuwa na faida kwao kuweza kujifunza tangu wakiwa chini ambapo inakuwa ni rahisi zaidi  kukariri misamiati ikilinganishwa na watu wazima.

“Hivyo lengo ni kuhakikisha kuwa tunazifikia shule nyingi kadri tutakavyoweza, kwani sisi ndiyo tunaosimamia gharama zote ikiwamo kuwaleta walimu hapa kutoka China. Hii ni fursa kwa wazazi kuweza kuwaruhusu watoto wao kujifunza lugha hii, ambayo inaelekea kuwa miongoni mwa lugha adhimu duniani,” anasema Profesa Zhang.

Mmoja ya walimu wanaofundisha lugha hiyo ya kichina kwenye shule ya Baobab ni, Wang Jie anasema kuwa licha ya kwamba programu hiyo imeanza mwaka huu shuleni hapo, lakini kumekuwa na mwitikio mkubwa unaoendana na uelewa wa haraka zaidi miongoni  mwa wanafunzi hao wapatao 220 wanaosoma lugha hiyo.

Wang anasema kuwa, licha ya kwamba lugha hiyo ya kichina imekuwa na changamoto kutokana na kutokuwa na Alphabeti lakini bado hakijawa kigezo kwa wanafunzi hao wa Baobab kuielewa lugha hiyo ambayo inatajwa kuanza kuzipiku lugha nyingine duniani kwa umaarufu.

“Ni kweli kuwa wakati tunaanza kulikuwa na changamoto kidogo hapa katika kuwasilisha mafunzo kwa wanafunzi na hii ilikuwa ikichagizwa hasa na kwamba lugha yetu haina alphabeti hivyo wengi walikuwa wakipata wakati mgumu zaidi kuweza kupokea mafunzo haya.

“Lakini mpaka hivi ninavyozungumza na wewe leo hii, unaweza kumwita mmoja wa wanafunzi hapa mkazungumza kichina bila tabu yeyote hali inaonyesha ni kwa namna gani wameimarisha uelewa wao.

“Na pia tunafurahi kuona kuwa wengi wanapenda na kuifurahia lugha hii, kwani imekuwa ikiwapa motisha wa kufanya vizuri kwenye masomo yao. Tunafurahia kuona kuwa wengi wanaosoma masoma haya ya lugha ya kichina ambao ni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, kwenye  hatua mbalimbali sasa hivi wanaweza kuandaa chakula  cha kichina, kuimba na mambo mengine,” anasema Wang.

Anasema kuwa wanafunzi wanaofikia hatua ya mwisho ambayo ni ya sita, wamekuwa wakipelekwa nchini China kwa ajili ya kujiendeleza. Udhamini wa safari hizo za mafunzo hufanywa kwa ufadhili. Hii ni fursa hivyo wazazi wa Kitanzania ni kazi kwao kuwaruhusu watoto wao kujifunza lugha hiyo.

“Itakuwa jambo la busara zaidi iwapo serikali ya Tanzania italiongeza somo hili kwenye mtaala wake wa elimu, kwani lina faida kubwa kwa wanafunzi,” anasema Wang.

Anaongeza kuwa, mpaka sasa shule hiyo ina walimu watatu wanaofundisha somo hilo la kichina,  ambapo mbali na shuleni hapo pia kuna shule kama St. Mathew ambayo mpango huo pia unaendelea ukiwa chini ya taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

WANAFUNZI

Valeria Godson anayesoma kidato cha tatu Sayansi, huku akiwa hatua ya pili kwenye somo la kichina shuleni hapo anasema kuwa, kujifunza lugha ya kichina ilikuwa ni ndoto ya muda mrefu ambapo anafurahi kuona ikitimia baada ya ujio ya taasisi hiyo ya Confucius shuleni hapo.

Anabainisha kuwa, anapenda kujifunza lugha hiyo ya Kichina kutokana na sababu mbalimbali hasa ikiwamo; kukua kwa teknolojia ya taifa hilo jambo analoamini kuwa litakuwa na faida kwake kwa namna yeyote ile.

“Ndoto zangu siku moja nikuwa mfanyabiashara mkubwa hivyo naamini kabisa kuwa kwa kufahamu lugha hii ya kichina, kutanisaidia kufuangua milango yangu kibiashara kwani natambua kuwa lugha hii inafursa nyingi kwasasa duniani.

“Hakuna asiyetambua kuwa China ndiyo taifa lenye idadi kubwa ya watu kwasas hivyo tunaweza pia kutumia fursa hii katika kuwa wakarimani wao pindi wanapokuja hapa Tanzania na hivyo kujikuta tukipata ajira.

“Lakini jambo jingine ninalojivunia ni kuwa, nimeweza kuimarisha uelewa wangu kwenye somo la Hesabu ambapo kwa sasa nimekuwa nikipata ufaulu wa kwanza jambo ambalo halikuwa rahisi hapo awali na hii imetokana kwamba awali walimu walikuwa wakitupa changamoto juu ya kwamba tunasoma lugha hii hivyo ufaulu wetu ungeshuka lakini tumeweza kulikosoa hilo kupitia matokeO ya mtihani,” anasema Vaileth.

Upande wake, Leila Mkenga ambaye pia anasoma kidato cha tatu akichukua mchepuo wa Biashara, huku akiwa hatua ya pili kwenye somo hilo la Kichina, anasema kuwa; lugha hiyo imemsaidia kufanya vyema kwenye masomo kama ya Uraia, Kiingereza na Sayansi kulingana kwamba wakufunzi hao wamekuwa wakiwatolea mifano hai kutoka nchini mwao juu ya mambo mbalimbali.

“Nafurahi kuona kuwa hata ratiba ya masomo haya ya Kichina ni rafiki kwani iko nje ya vipindi vya masomo. Tunafundishwa mara mbili kwa wiki kwa maana ya Jumanne na Alhamisi.

“Natamani kuona serikali ikitilia mkazo wanafunzi kama sisi wa sekondari kujifunza lugha mbalimbali. Inatakiwa iongeze baadhi ya lugha za kigeni kwenye mtaala, hii kuongeza uwezo kwa vijana wa Kitanzania kushindana katika ulimwengu.

“Hata hivyo nasikitika kuona kuwa, mpaka sasa serikali imeshindwa kuyahesabu masomo haya kama sehemu ya mitihani inayotambulika, kwani yamekuwa na faida kwetu sisi wanafunzi licha ya kwamba siyo utamaduni wetu lakini itakuwa na faida kwa taifa kwa ujumla,” anasema Leila.

Leila anaongeza kuwa, iwapo wazazi na walimu watatoa sapoti ya kutosha kwa watoto wao, itakuwa na faida kubwa kwani wataweza kupiga hatua kubwa kwenye lugha hiyo jambo ambalo matunda yake watayaona baadaye.

Hata hivyo, wanafunzi hao wanalalamikia muda mchache wa kufundishwa kwa somo hilo shuleni hapo, jambo ambalo limekuwa likiwakosesha fursa ya kujifunza zaidi lugha hiyo ya Kichina.

“Tunaamini kuwa somo hili litatusaidia katika kukabiliana na soko la ushindani wa ajira duniani iwapo litatiliwa mkazo na wanafunzi hapa nchini. Confucius haina budi kuendelea kusaidia shule nyingi zaidi,” anasema Leila.

Mwalimu mkuu msaidizi

Upande wake Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo upande wa Wasichana, Alphonce Francis anasema kuwa, uwepo wa lugha hiyo ya Kichina imewasaidia wanafunzi wengi wanaosoma soma hilo kufanya vizuri darasani.

“Mafunzo ya lugha hii ya Kichina yamekuwa na faida kubwa mno ambayo tunaiona kupitia maendeleo ya wanafunzi darasani, kwani wameendelea kufanya vizuri kwenye mitihani yao.

“Pia imewasaidia kujifunza utamaduni wa Kichina kwani sasa hivi wanafunzi hawa wamekuwa wakizungumza bila tabu yeyote lugha hii, jambo ambalo tunaishukuru taasisi hii ya Confucius ambayo imewezesha uwepo wa mpango huu hapa.

“Hata hivyo kwa hapa Baobab siyo Kichina tu kwani kwa sasa tunafunzisha lugha mbalimbali kama Kiarabu, Kichina, kifaransa hivyo imekuwa ni chaguo la mwanafunzi mwenyewe kuchagua somo moja analotaka kusoma,” anasema Francis.

Anabainisha kuwa, ratiba ya lugha hizo imekuwa haiingiliani na vipindi vya kawaida vya masomo huku akiweka wazi mkakati wa shule hiyo wa kuendelea kuongeza lugha nyingine.

“Shule hii ni miongoni mwa shule bora ambazo zimekuwa zikifanya vyema kwenye eneo zima la elimu, ambapo ikiweka bayana uwepo wa mafunzo ya lugha hizi hii kuwa ni fursa kwa wanafunzi na wazazi wanatakiwa kuchangamkia fursa hii kwa kuwaleta watoto wao ili kuwasaidia kukabiliana na soko la ajira, kulingana na kiwango bora cha elimu kinachotiolewa.

“Shule ina walimu zaidi ya 80 ambao kati yao ni 10 tu ndio wenye Diploma huku waliosalia wote wakiwa na viwango vya juu vya elimu. PIa wamefuzu vigezo vinavyohitajika kwenye utoaji wa elimu wa kisasa duniani kote achilia mbali kuwa na uongozi mzuri pamoja na mfumo wa chakula na maeneo mazuri ya kulala ambayo yanastahili kwa binadamu,” anasema Francis.