Home Makala Kimataifa CORD YA RAILA KUMEZWA NA NASA?

CORD YA RAILA KUMEZWA NA NASA?

922
0
SHARE

Kenya inafanya uchaguzi Mkuu mwakani huku tayari ikiwa imepitisha mabadiliko makubwa katika Tume yake ya uchaguzi. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, Tume ya Uchaguzi itahusisha viongozi watakaopendekezwa na vyama vya siasa, pamoja na wale wasiohusika na masuala ya kisiasa moja kwa moja.

Tena, makamishna wa Tume hiyo, watatakiwa kuridhiwa na Bunge kabla ya kupitishwa na Rais.

Tume hiyo mpya inatakiwa kuanza kazi mapema, ili kuandaa Uchaguzi Mkuu ujao. Kabla ya kuwepo tume mpya, Tume iliyojiuzulu imekuwa ikiendelea na majukumu yake na moja ya majukumu hayo ni kutafuta kampuni itakayopewa tenda ya kuleta karatasi za kura.

Wakati hilo likifanywa na Tume inayomalizia muda wake, tayari Muungano wa vyama vya upinzani maarufu kama CORD uliochini ya Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga, umeitaka Tume hiyo kuacha kuendelea na tenda hiyo ambayo wameipatia kampuni moja ya Dubai.

Lakini tena, Muungano wa Rais Uhuru Kenyata ambao awali ulihusisha vyama mbalimbali, tayari umekuwa chama kimoja. Kwa lugha nyingine ni kuwa Jubilee badala ya kuwa muungano wa vyama, sasa ni chama kimoja. Kwa upande wa wapinzani wao nao huko wanakabiliwa na joto jipya.

Muungano wa Cord unapitia kipindi kingine kigumu kufuatia harakati za kutaka kuuvunja na kuundwa kwa muungano mpya ambao utaitwa NASA. Muungano huu mpya utajumuisha vyama vilivyokuwa CORD pamoja na KANU.

Kama muungano huu utafanikiwa, ni dhahiri kazi kubwa itakuwa katika kupata mgombea urais kupitia muungano huo, zoezi ambalo inaelezwa kama litafanikiwa, basi mazingira ya kuwepo uchaguzi mgumu kwa Jubelee yanaonekana.

Harakati za kwanza za ujenzi wa NASA ni zile ambazo zimefanyika katika mapokezi ya Gavana wa Kaunti ya Bomet, Isaac Ruto, aliyekuwa akirejea Kenya kutoka Afrika Kusini, alikoenda kwa ajili ya matibabu. Gavana Ruto alienda kutibiwa jicho kufuatia kuumizwa na bomu la machozi katika mikutano ya kisiasa.

Katika mapokezi hayo ambayo hayakuhudhuriwa na Raila kwa kuwa alikuwa nje ya nchi, alikuwepo Makamu wa Rais wa zamani wa Kenya na kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa Chama cha Amani, Musalia Mudavadi, Gavana wa Kaunti ya Kisumu, Jack Ranguma, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, Senata wa Baringo, Gideon Moi, Wabunge: John Mbadi (Gwasi), Zakayo Cheruiyot (Kuresoi Kusini), Johanna Ngeno (Emurua Dikirr) na Katibu Mkuu wa KANU, Nick Salat.

Mkutano huo uliohudhuriwa na zaidi ya wananchi 30,000 ulielezwa kuwa ni kama utangulizi tu wa kuzaliwa Umoja utakaoitwa National Super Alliance (NASA).

Wafuatiliaji wa siasa za Kenya wanaeleza kuwa, mgongano mkubwa kwa NASA hata kabla haijazaliwa, ni kuhusu nani atakuwa mgombea urais pamoja na mgombea mwenza.

Hii ndiyo huwa mbinu pekee ya mtu kushinda urais nchini Kenya, yaani kuwa na wagombea ambao wanatoka katika makabila yenye kura nyingi na hasmwishoa kuunganisha nguvu na makabila mengine.

Kwa kuwa Rais Uhuru anatokea kabila la Kikuyu na Naibu Rais wake anatokea Kalenjin, basi upo umuhimu wa kuwa na umoja utakaogawa kura zao huku wagombea wa upinzani wakitakiwa kuendelea kukamata ngome zao ili walau waweze kushinda.