Home Makala Corona inaweza kuibomoa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

Corona inaweza kuibomoa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

204
0
SHARE

NA JAVIUS KAIJAGE

TANGU kuibuka na kusambaa kwa virusi vya Corona ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwanzoni mwa Machi mwaka huu, yapo mambo mengi yamejitokeza na mengine kuashiria kuharibu uhusiano mwema wa mataifa katika jumuiya hiyo.

Kimsingi tangu virusi vya Corona kutangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni janga la kimataifa, pamekuwepo na ushauri/maelekezo mengi kutoka kwa wataalamu wa afya na wanasayansi kwa ujumla kuhusu namna ya kujikinga na virusi hivi hatari.

Miongoni mwa ushauri/maelekezo hayo ni kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka, kutumia sanitizers, kukaa umbali wa takribani mita moja kati ya mtu na mtu, kutogusana mikono, kuvaa barakoa, kuepuka kujigusa usoni na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.

Ushauri mwingine wa kitaalamu ambao umekuwa ukitumika hasa katika siku za mwanzo baada ya kuibuka ugonjwa huu wa Covid-19,  ilikuwa ni kutumia mfumo wa ‘lock-down’ au ‘lock-in’, kufunga mipaka ya nchi na viwanja vya ndege.

Mbali na ushauri wa kitaalamu kwa mujibu wa wataalamu, pia watu, jamii na serikali mbalimbali zimekuwa na mikakati mingine ya ziada katika kukabiliana na tatizo hili kwa mfano hapa Tanzania, Rais Dk. John Magufuli amekuwa akiwasihi Watanzania watumie maombi ili kushinda janga hili.

Pia serikali yetu ilienda mbali mpaka kuwaambia wananchi watumie njia ya asili ya kujifukiza madawa ya mitishamba kwa lengo la kusambaratisha virusi hivi.

Yote katika yote hatua zote hizi za kukabiliana na janga la Corona, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kila nchi imekuwa ikichukua hatua zake ambazo  kimsingi zinaonekana kuwa sahihi kulingana na mazingira husika.

katika jumuiya hii yapo mataifa yaliyoamua kuchukua hatua za ‘lockdown’ kwa lengo la kulinda wananchi wake.

‘‘Lockdown’’ ni kanuni ya dharura ambayo huzuia watu kuondoka eneo fulani mfano kutotoka majumbani mwao.  Kimsingi kuzuiwa kabisa humaanisha mtu/watu kukaa mahali walipo bila kuingia majengo mengine au maeneo mengine.

Mbali na ‘lockdown’ pia mataifa kadhaa ndani ya jumuiya hii yalienda mbali hadi kufikia hatua ya kufunga viwanja vyake vya ndege pamoja na mipaka kwa lengo lile lile.

Katika hatua zote hizi Tanzania haikuchukua hatua ya ‘lockdown’, wala kufunga mipaka yake ya nchi kama mataifa mengine yalivyofanya na badala yake imechukua hatua nyingine kama ilivyoshauriwa na wataalamu mfano kuhimiza wananchi kunawa mikono, kutumia sanitizers, kutogusa uso na kusisitiza uvaaji wa barakoa.

Hatua nyingine zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania ni kuwahimiza watu kujiepusha na misongamano isiyo ya lazima na ndiyo maana serikali ilifikia hatua ya kufunga shule, vyuo na michezo mbalimbali kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa kasi virusi vya Corona.

Hata hivyo mbali na hatua hizi zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kuzuia kusambaa kwa virusi hivi, bado mataifa jirani yakiwemo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yamekuwa yakilaumu kwamba Tanzania imeshindwa kuchukua hatua zinazostahili.

Kimsingi Tanzania kushindwa kufunga mipaka yake na kushindwa kutumia mfumo wa ‘lockdown’ ambao kimsingi umetumiwa na mataifa takribani yote ndani ya jumuiya, ndicho chanzo kikuu cha manung’uniko.

Manung’uniko haya yamekwenda mbali hadi mataifa mengine katika jumuiya hii kufikia hatua ya kusema Watanzania ndio wanasambaza virusi vya Corona.

Ushahidi huu unajidhihirisha pale madereva wa Tanzania wanapokuwa wamekwenda katika mataifa hayo kwa lengo la shughuli za kibiashara kwani wamekuwa wakilalamika sana kuwa hawatendewi haki bali wananyanyaswa ikiwemo kunyanyapaliwa.

Huko Rwanda,hali hiyo imejitokeza sana kwani kupitia vyombo mbalimbali vya habari tumekuwa tukiona kwa macho yetu jinsi ambavyo madereva wanafanyiwa ikiwemo kuzuiwa kufanya matembezi ndani ya taifa hilo au wakati mwingine kuzuiwa kuingia kabisa ndani ya taifa hilo pindi wafikapo mpakani.

Kuwekwa karantini madereva wa Tanzania wawapo ndani ya Taifa la Rwanda tena kwa masharti na wakati mwingine vitisho imekuwa ni jambo la kawaida katika kipindi hiki na zaidi ya hapo inasemekana baadhi ya wanyarwanda wamefikia hatua ya kuwarushia mawe Watanzania kisa wana virusi vya korona.

Taifa lingine ambalo limechukua hatua kali za kuwapima madereva wa Tanzania pindi waingiapo nchini kwao ni Uganda. Kimsingi hata waganda wanaamini kuwa kutokana na serikali yetu kutochukua hatua kali za kudhibiti virusi hivi kwa wao walivyofanya basi Watanzania wange wana Corona.

Uganda imekuwa ikitoa taarifa kuwa kwa mujibu wa vipimo vyake vilivyotumika kuwapima madereva wa nchi nyingine, inaonekana wanaotoka Tanzania baadhi wamekutwa wana Corona na hivyo kuwa tishio kwa waganda.

Kutokana na hali hiyo, serikali ya Uganda ilitoa utaratibu wake kwamba madereva kutoka nje ya nchi ikiwamo Tanzania, wataruhusiwa kuingia lakini wakishaingia ndani ya nchi hawataruhusiwa kufanya matembezi bali watabaki katika maeneno ya magari yao na pia si wote watakaoingia.

Si Rwanda na Kenya zilizofanya hivyo bali hata serikali ya Kenya imekuwa ikifanya hivyo kwani kwa siku za karibuni pamekuwa pakitokea maneno ya kebehi kutoka kwa baadhi ya wananchi wa Kenya wakisema ya kuwa Watanzania wanawapelekea Corona katika taifa lao.

Masharti ya madereva wa Tanzania kuingia Kenya imekuwa ni shida kwa kisingizio cha kuwa vipimo vinaonyesha madereva hao wana virusi vya Corona.

Kupitia vyombo mbalimbali vya habari vimekuwa vikionyesha msururu wa magari ya Tanzania yakiwa yamesimama mpakani mwa Kenya na Tanzania kutokana na masharti magumu ya madereva kuingia kule.

Zaidi ya hapo serikali ya Kenya kupitia Rais wake, Uhuru Kenyatta imechukua uamuzi wa kutangaza kufunga mipaka yake na Tanzania kwa muda wa siku 30 kwa kisingizio kuwa Watanzania inaonekana wana maambukizi makubwa ya Corona kwani baada ya madereva kupimwa wamekutwa na hali mbaya.

Ni dhahiri hatua hizi za mataifa jirani tena katika jumuiya moja ambayo kimsingi watu wake ni ndugu, jamaa na marafiki zetu, kuwafanyia Watanzania namna hii, imepelekea hali ya taharuki hadi kufikia hatua ya waheshimiwa wabunge kuitaka serikali Tanzania kuchukua hatua kali dhidi ya mataifa hayo.

La kujiuliza ni hatua zipi ambazo zinashauriwa kutumiwa na serikali ya Tanzania kwa mataifa yanayotufanyia hivi?

Je, ni kulipiza kisasi kwa kutumia hatua zilezile za kufunga mipaka na kuwanyanyapaa wananchi wa mataifa hayo walioko kwetu?

Je, ni serikali kuchukua fursa ya utajiri wake wa  bandari na rasilimali nyingine  kuyakomoa mataifa yanayotutendea hivi?

Je, ni kuamua kabisa kuondoa ushirikiano katika nyanja zote za Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii kwa lengo lile lile la kufanya malipizi?

Lakini pia bado kuna suala lingine la kujiuliza ya kwamba endapo Tanzania itachukua hatua kali dhidi ya mataifa hayo itapata faida gani?

Je, hakuna njia nyingine nzuri ambayo inaweza kutumika kwa ajili ya kuleta utengamano badala ya kufikiria hatua kali zinazoweza kubomoa jumuiya hii?

Kimsingi virusi vya Corona vinatisha na saikolojia ya mwanadamu imejengwa katika hofu hasa kwa kitu kinachotisha, hivyo inawezekana yote yanayotokea kwa mataifa yetu ya jirani ni hofu kutokana na janga hili.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ni kwamba kuna uwezekano mkubwa virusi vya Corona vikaendelea kuwepo kwa muda mrefu katika uso wa dunia, hivyo ni wajibu wa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutafuta njia sahihi ya kuendelea kushirikiana badala ya kubomolewa na janga hili.

Email: HYPERLINK “mailto:javiusikaijage@yahoo.com”javiusikaijage@yahoo.com, Simu: 0756521119