Home Habari Corona itufunze kukabili majanga tunayoishi nayo

Corona itufunze kukabili majanga tunayoishi nayo

1131
0
SHARE

DK. HELLEN KIJO BISIMBA

HIVI sasa ukifuatilia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na hata mazungumzo ya kawaida watu, mjadala mkubwa ni ugonjwa wa corona.

Ugonjwa huu unatajwa kuwa ni hatari na haujapatiwa kinga wala tiba. Nilimsikia mtaalamu mmoja akieleza kuwa, huenda tiba au kinga ikapatikana baada ya miezi 18 yaani mwaka mmoja na nusu kuanzia sasa.

Aidha nchi ambazo zimekumbwa na ugonjwa huu na tayari umetangazwa kuwa janga la kimataifa na Shirika la Afya Duniani. Sasa, inasemekana ugonjwa huu umefika nchini mwetu baada ya watu walioambukizwa wakiwa nje ya nchi kuingia nao nchini na kuna watu kadhaa tayari wameonekana kuwa na maambukizi.

Nimeangalia jinsi ugonjwa huu kwanza, ulivyokuwa kama hauelewekieleweki na pamoja na kusikia madhara yake ulikuwa haujawa tishio sana kwetu, lakini ghafla ulitokea kuwa tishio na taarifa zake zikasambazwa sana shule zimefungwa kuanzia chekechea hadi vyuo, tahadhari zinatolewa kila upande.

Nimeona pia mwitikio mkubwa wa kujikinga kwani sehemu za nyumba za ibada, nje ya maduka, hospitali na kwingineko yapo maji ya kunawa mikono na sabuni pamoja na vitakatishi, sehemu nyingine watu wanavaa barakoa kama wazee wa kanisa wanaohesabu sadaka.

Kama alivyosema Rais Dk. John Magufuli akiwa kanisani huko Dodoma Jumapili iliyopita, alisema pamoja na kuwepo ugonjwa corona hapa nchini yapo magonjwa mengine ambayo nayo yanaua watu zaidi hata ya hiyo corona, sasa kwanini corona ndio iwe vinywani kiasi hiki?

Inatubidi tufanye uchambuzi kidogo. Hapa nchini magonjwa ya mlipuko hutokea kama kipindupindu, kuharisha hasa kwa watoto wadogo na watu wengi tu hufa. Yapo magonjwa yasiyo ya mlipuko ambayo pia huua kama saratani, malaria, ukimwi na mengine mengi na huenda mengi yanaweza kuepukika kwa mfano, vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja na chini ya miaka mitano.

Wapo wanawake wajawazito ambao taarifa zao zingekuwa zinatolewa kwa siku tungeweza kuzizima kuwa kila baada ya saa moja yupo mama mjamzito anafariki yaani vifo 24 kila siku.

Kila jambo lina kuja na uchanya wake na uhasi wake. Corona ni janga la kimataifa, huko lilikoanzia na huko lilikofika wameweza kulitangaza na kuonyesha athari zake kwa kiasi kikubwa.