Home Habari Covid-19 yatishia uwepo wa kura ya maoni Kenya

Covid-19 yatishia uwepo wa kura ya maoni Kenya

269
0
SHARE
Kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Odinga (kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya BBI, Seneta Yusuf Haji, katika mkutano wa BBI uliyofanyika Garissa Februari 23 mwaka huu. Picha ya maktaba.

NA ISIJI DOMINIC

LILE vuguvugu la kutaka kupigwa kura ya maoni Juni mwaka huu kubadilisha baadhi ya vipengele katika Katiba ya Kenya, sasa ipo shakani kutokana na janga la virusi vya corona ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO) imelitangaza kuwa janga la kimataifa. 

Muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, takribani miaka miwili iliyopita, ilibuni jopo kazi iliyopachikwa jina la Building Bridges Initiative (BBI) na kupewa maeneo tisa ya kushughulikia. 

Jopo kazi la BBI chini ya Mwenyekiti wake Seneta wa Garisa, Yusuf Haji, iliwasilisha ripoti yake ya kwanza mwishoni mwa mwaka jana katika Ukumbi wa Bomas jijini Nairobi na kupokewa vyema. 

Akihutubia wananchi baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais Uhuru aliwataka Wakenya kujisomea na kupendekeza marekebisho zaidi ambayo wanaona yanaweza kufaa, lengo likiwa ni ipatikane Katiba itakayowaunganisha na hususan itakayohakikisha nchi haiingi kwenye taharuki pindi kunapofanyika uchaguzi mkuu. 

Lakini mapema mwaka huu, baadhi ya wanasiasa wakiongozwa na Raila, walikuwa wakizunguka nchi nzima kwa kile walichodai kuhamasisha ripoti ya BBI na kushinikiza kufanyika kwa kura ya maoni Juni mwaka huu. 

Kundi lingine la wanasiasa wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, nao walipinga utaratibu wa wafuasi wa Raila ‘kuiteka’ BBI wakidai wanatumia ripoti hiyo katika mikutano kama sehemu ya kumfanyia kampeni kiongozi huyo wa Chama cha ODM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. 

Aidha walipinga utaratibu wa kumkabidhi Raila mapendekezo ya wananchi wa kaunti husika ili awasilishe kwa jopo kazi ya BBI na namna ya uwepo wa ubaguzi kwa wanaopewa nafasi kuongea kwenye mikutano ya kuhamasisha ripoti ya BBI. 

Kulitarajiwa kuwe na mshikeshike katika kaunti ya Nakuru ambayo ni moja ya ngome ya Naibu Rais wakati wa mkutano wa BBI, lakini Serikali ikapiga marufuku mikusanyiko ya watu ikiwemo mikutano ya kuhamasisha BBI wakisema lengo ni kudhibiti kuenea maambukizi ya virusi vya corona. 

Hii ikawa ahueni kwa wakazi wa kaunti ya Nakuru kwa sababu kulikuwa na kila dalili ya ghasia ukizingatia kundi linalomuunga mkono Raila, walisema mkutano huo utafanyika kwa utaratibu wao wakipuuza wanasiasa wanaomuunga mkono Ruto waliosema hawatakubali kupangiwa masharti kwenye eneo lao. 

Swali sasa ni je, mkutano huo wa Nakuru utafanyika endapo janga la corona litapotea? Na vipi kuhusu uwepo wa upigaji kura ya maoni Juni mwaka huu? Serikali ya Kenya kupitia Wizara ya Afya imeweka mikakati kukabiliana na Covid-19, ikiwemo watu kuwepo nyumbani kuanzia saa 1 usiku hadi saa 11 alfajiri na kila mtu kujitahidi kuvaa barakoa. 

Kikwazo kinachoikabili utekelezaji wa ripoti ya BBI ukizingatia wanaoshabikia ripoti hiyo waliwaahidi Wakenya kufanyika kura ya maoni mwaka huu ni janga la virusi vya corona. 

Kamati hiyo ya BBI ilihitimisha ukusanyaji wa maoni mwezi uliopita na kwa mujibu wa Seneta Haji, walitakiwa kutoa mapendekezo yao katika awamu tatu ambayo ni mabadiliko ya kiutawala, kisheria na kura ya maoni. 

Huku taharuki ya covid-19 ikizidi kutanda, kuna uwezekano ikaingiliana na muda uliopangwa na kusababisha ucheleweshwaji wa ripoti ya BBI. 

Msisitizo wa Serikali ya watu kukaa nyumbani na ikiwezekana kufanya kazi wakiwa nyumbani kwa lengo la kuepusha mkusanyiko inaweza ikawalazimu kamati ya BBI kuendelea na majukumu yao hali ikishatulia.

Zoezi la kupiga kura ya maoni inawataka watu wajitokeze kwa wingi na hata kabla ya upigaji kura kuna kampeni zitafanyika. Hii yote kwa jinsi hali ilivyo sasa ni ngumu kufanyika na hata kama hali ya maambukizi yatashuka, bado kuna ule uoga wa mtu kujikuta kwenye mikusanyiko.

Mkurugenzi wa Uchaguzi ODM, Junet Mohamed, aliwahi kukaririwa akisema kura ya maoni itafanyika Juni mwaka huu lakini ni dhahiri anaweza kubadili kauli yake kwasasa kutokana na janga la covid-19.

Aidha Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru, ambaye naye pia amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono kura ya maoni kufanyika mwaka huu, alinukuliwa akisema kwasasa hilo sio jambo la msingi.

“Sasa tunapambana na masuala ya uhai na kifo. Lazima tuwe mstari wa mbele kuhakikisha usalama wa wananchi wetu na kusitisha kusambaa kwa ugonjwa huu. Na hiyo pekee kwasasa ndiyo malengo yetu,” alisema gavana huyo wa Kirinyaga.

Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa ODM, Opiyo Wandayi, alisema nchi imetambua BBI kama njia bora kutatua changamoto za utawala, kijamii na uchumi, na lazima safari yake ihitimishwe hata kama kuna virusi vya corona.

Wandayi anasisitiza kilichobakia hakihitaji mikusanyiko ya watu kwa madai mikutano ya usikilizwaji wa umma na kuhamasishana umeshapita hivyo kamati ya BBI jukumu lao ni kukusanya mapendekezo yaliyotolewa na kumaliza kazi yao ndani ya muda uliyopangwa.

Mwanasiasa huyo anaamini sahihi milioni moja zinaohitajika ili kuwepo kura ya maoni zinawea kupatikana ndani ya wiki moja.

“Tukumbuke kuwa IEBC (Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka) na mabunge ya kaunti yanafanya kazi hata kama kuna tishio la virusi vya corona. Kura ya maoni lazima ifanyike kabla ya Agosti,” alisema Wandayi.

Anachosahau Wandayi ni kwamba mabunge ya kaunti yamesitisha vikao vyao kutokana na wajumbe kutekeleza agizo la Serikali ya watu kukaa nyumbani. 

Mapambano dhidi ya covid-19 yanahitaji fedha hivyo kuna kila dalili mabilioni yaliyotengwa endapo kamati ya BBI itaridhia kufanyika kura ya maoni yaelekezwe kuboresha sekta ya afya ili kudhibiti virusi hivyo. 

Inaweza ikawa jambo la kushangaza kama wanasiasa na kamati ya BBI itashinikiza kuendelea na mchakato wa kura ya maoni kama janga hili halijadibitiwa, na kama mbaya zaidi maambukizi yatazidi kuongezeka.