Home Latest News CUF ISIWAHADAE WANACHAMA, UCHAGUZI NI 2020

CUF ISIWAHADAE WANACHAMA, UCHAGUZI NI 2020

856
0
SHARE

NA RASHID ABDALLAH

TANGU Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulipomalizika, mvutano ulioanzishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, bado hali ya siasa za Zanzibar haijapata kivuli cha kutulizana.

Mvutano huo ulitokea baada ya Mwenyekiti huyo kufuta matokeo ya uchaguzi Zanzibar, ambao waangalizi wa ndani na nje walikubali ulikuwa huru na haki.

Huenda masilahi ya kisiasa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio chanzo kikubwa cha matokeo yale kufutwa, kwa sababu katika jicho la kawaida hakukuwa na sababu nyingine ya msingi.

Hadithi ni ndefu na wengi tunaielewa, ikiwemo uchaguzi wa marudio ambao Chama cha Wananchi (CUF) kilisusa uchaguzi huo na kufanya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kukwama.

Tukapita katika kipindi cha kugomeana na kuchukiana, jirani hahudhurii harusi ya jirani yake kwa sababu ni chama tofauti na yeye. Mali za watu zikaharibiwa kwa sababu tu wanatoka chama fulani.

Ili mradi hali ilikuwa mkorogo, ile Zanzibar ya watu wanaounganishwa na dini moja, lugha moja na utamaduni wa aina moja unaopendeza hata kwa wageni, iliingia doa kwa sababu ya siasa.

Tunashukuru sasa hali inaonekana kutengemaa kwa kiasi kikubwa, watu wamerudi katika maisha yao ya kawaida, ingawa vumbi la kisiasa bado hutimka mara moja moja ila wakati mwingi hali ni shwari.

Bado kunabaki maswali mengi yasiyo na majibu imara, kutoka wakati ule hadi tulipo; nini kinafuata? Ile haki ambayo CUF wanaamini waliporwa wataipata? Je, hali itakuwaje 2020?

Sasa turudi katika moyo wa makala hii. Wakati CUF inatangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio, niliandika kupitia mtandao wa kijamii nikisema: “Ikiwa CUF wanasusia uchaguzi huu lakini wanazo njia mbadala za kuhakikisha wanakipata kile ambacho wanaamini ni haki yao iliyoporwa basi nitakuwa nyuma yao kama mpenda haki.

Hadi leo naendelea kusimamia maneno yangu, kinachoonekana sasa kwa CUF ni kutapatapa na kuhangaika, katika mikono ya siasa za kimafia za CCM.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim  Seif Sharif, amekuwa anawajaza  watu wake matumaini na ahadi ambazo mwisho wa siku hazitimii.

Tururudi nyuma kidogo. Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Maalim Seif aliahidi wafuasi wake kwamba baada ya miezi mitatu kupita wataona jinsi haki inavyopatikana yaani yeye kuapishwa, bahati mbaya miezi mitatu imeshakatika na hakuna jipya, zaidi ya utabiri ulioshindwa.

Amegeuka babu anayekusanya wajukuu zake kisha akawapa hadithi za uongo, mambo mazuri, hivi na vile lakini muda anaouahidi unapita na hakuna zuri linaloonekana.

CUF imeshindwa tu kuwaambia wafuasi wake waendelee na maisha yao wakisubiri 2020, binafsi si mabadiliko makubwa ya kisiasa Zanzibar kwamba eti yatatokea, hata ikitokea basi si mabadiliko ya Maalim kuapishwa kuwa rais.

Hayo ni maoni yangu binafsi, yawezekana huyapendi, yakakuchukiza lakini mimi ndivyo niaminivyo.

Maoni yangu yasitafsiriwe kwamba naunga mkono siasa za kimafia zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi. Sijawahi kuunga mkono siasa chafu hata siku moja.

Nasikitika kwamba CUF imeshindwa kuwika kwenye siasa hizi chafu kwa takribani miongo miwili sasa. Na hizi siasa chafu ndizo zinazomwingiza Maalim katika tamthilia ya kuwapa wafuasi wake matumaini yasiyotekelezeka.

CCM ya Zanzibar hawana uungwana huo kwamba eti uapishwe baada ya miezi mitatu, watu wanakula viapo majukwaani kwamba wao ni lazima washinde, mambo si mepesi kama watu wanavyoyatazama.

Kususia uchaguzi wa marudio kisha ikakosekana njia mbadala za kupata kile mnachoamini ni haki yenu mliyoporwa, inadhihirisha ukweli unaouma kwamba CCM kwa miaka 20 sasa wanaendelea kuwashinda kwa mbinu zao chafu.

Si ajabu hata hiyo 2020 utakapokuja uchaguzi mwingine pengine mkashinda uchaguzi lakini wao wakawashinda kwa mbinu, wakaendelea kubaki madarakani na CUF ikaendelea kulalamika mitandaoni.

Hizi ndio shida ya siasa za kimafia, CCM wanaendesha siasa chafu, kwa hiyo ukiwa na siasa safi mbele ya mwenye siasa chafu huenda itakuchukua muda hadi kufanikiwa.

Sisemi kwamba kama wao wanatumia siasa chafu na CUF itumie siasa chafu. Unaweza kutumia siasa safi lakini hakuna ulazima wa ahadi hewa na uongo.

Juzi wakati nikipita katika mtandao mmoja wa kijamii kusoma, nilikuta tangazo jingine limewekwa na mkereketwa wa CUF.

Mwezi mmoja nyuma nilikuta tangazo lenye maneno mengi lakini mwisho wake anasema Maalim ataapishwa kabla ya Novemba mwaka huu. Sasa tunaenda Desemba!

Wakati mwingine ukishasoma matangazo kama haya inabidi utabasamu kisha uendelee na maisha, ni kweli binadamu hawatakiwi kukata tamaa, lakini tukikuona unataka kudondosha shina la mbuyu kwa kiwembe hata kama hukati tamaa lakini tutakuhesabu umeanza kuchanganyikiwa.

Wiki kadhaa nyuma nilimtembelea rafiki yangu, ni mpenzi mkubwa wa CUF, ilikuwa ni siku chache baada ya ile miezi mitatu aliyoitangaza Maalim kuisha, nilipomuuliza vipi mbona hujaangusha mbuzi.

Alibaki tu kuniangalia akicheka, mwisho akaniambia; “Na mimi nimeanza kupoteza matumaini sasa.”

Waliopoteza matumaini na hizi ahadi ni wengi sasa, hivyo CUF ni bora kutafuta lugha nzuri ya kuzungumza na wafuasi wao ambao ni watu wazima kuliko kuzungumza nao kwa lugha ya kitoto.

Pengine mtu atahoji, kwa hiyo CUF inapaswa kufanya nini?  Mimi si mwanasiasa, japo nafuatilia siasa, naamini CUF wanaweza kuwa na jawabu zuri kwa swali hilo kuliko hata mimi, ingawa uzuri wa jawabu lao si lazima nikubaliane nalo.

Ambalo mimi nitalisema ni hili; ikiwa CUF kwa uhalisia wameshindwa kuirudisha haki yao basi wanapaswa kuwaeleza ukweli wafuasi wa chama hicho na si kuwapa ahadi kapa, maanake ukimpa ahadi ya uongo mtu mzima mwenzako inasababisha aanze kupoteza uaminifu kwako.

Wakishawaeleza ukweli, waanze kujipanga na uchaguzi wa 2020, miaka hiyo waingie katika uchaguzi wakielewa wanapambana na chama kilichosheheni mbinu na wao waingie uchaguzini wakisaka ushindi huku wakizuia hizi mbinu zisije kufanikiwa na kuwakosesha ushindi, kama ilivyotokea 2015.

Kufutwa kwa uchaguzi uliopita ambao waangalizi walirithi ulikuwa uhuru na haki, ilikuwa ni moja ya mbinu za CCM katika dakika za mwisho mara baada ya mbinu zao kushindwa katika matawi ya chini.

Nikimalizia maoni yangu, kwa upande mwingine ikiwa wanaamini bado wanao uwezo hadi sasa wa kuurudisha ule ushindi wanaoamini wamepokwa, basi waendelee na kazi hiyo lakini ahadi za uongo wazisitishe, kwanza dhambi kisha hazina manufaa endelevu katika siasa.