Home kitaifa CUF yakosolewa Zanzibar

CUF yakosolewa Zanzibar

1087
0
SHARE

seifNA UMAR MUKHTAR, ZANZIBAR

MWANASIASA mkongwe Hassan Mussa Takrima amesema chama chochote cha siasa ambacho ni imara na makini katu hakiwezi kukimbia na kususia uchaguzi au kuwa na hofu ya kushindwa.

Amesema chama kinachoweza kufanya hivyo ni chama legelege kinachopenda ushindi wa hila ndio maana kinapata hofu au wasiwasi wa kushiriki uchaguzi.

Takrima alitoa kauli hiyo mapema wiki hii katika mahojiano na RAI  yaliofanyika  nyumbani kwake huko Jumbi nje kidogo ya mji wa Unguja.

Alisema mwanasiasa au chama cha siasa chenye tabia ya kususia uchaguzi, hudhihirisha si makini na madhubuti pia  kinaweza kutafsirika mbele ya jamii.

Alisema ukiona chama cha siasa na viongozi wake wanapenda ulalamishi au kususa, huo ni ubabaishaji na aghalabu viongozi wa aina hiyo huota ndotoni  washike madaraka bila kutoa  jasho  la juhudi ya  kukinadi chama chao hadi kikubalike na kuchaguliwa kwa ridhaa  ya wananchi.

“Uchaguzi  mkuu wa Zanzibar mwaka huu umefutwa kisheria na chombo ambacho kina  dhamana kisheria, haukufutwa na chombo cha mitaani  kisicho na   nguvu  za kikatiba au kisheria, wanaosema ZEC imekosea meno  hebu wakasome tena katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa utulivu, umakini ili kuijua mipaka ya  zec ilivyo kisheria “. alieleza Takrima

Aidha, alisema historia ya ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi itaendelea kubaki pale pale kama ilivyotokea katika chaguzi kuu tatu kabla ya mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964.

Alisema  muendelezo  wa  ushindi wa CCM ambacho kimetokana na  ASP upande  wa Zanzibar, alidai  hayupo wa kukizuia kwa kuwa siasa za Zanzibar alidai huambatana na ukweli wa historia ya maisha ya watu wake kabla ujio wa wakoloni na baada ya kudondoshwa ufalme miaka 52 iliopita visiwani humu.

Akijibu mapigo ya mwanasiasa mwenzake Mzee Hassan Nassor Moyo ambaye amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema hatamuunga mkono Katibu mkuu wa CUF, Maalim  Seif Sharif Hamad ikiwa ataridhia matakwa ya kurudia uchaguzi, Takrima anasema huo ni ushauri mbovu usiofaa kufuatwa na kiongozi au chama makini chenye kujiamini kisera na kama kweli kina mtaji wa kuchaguliwa na kushinda.

Alisema mwaka 1957  ASP kiliishinda kwa kura 21,632 sawa na asilimia 60.1, ZNP kikapata kura 7761 sawa na asilimia 21. 6. ambapo uchaguzi mkuu  wa mwaka 1961, ASP  kilipata  kura 36, 698 sawa na asilimia 43, wakati  ZNP  kikikusanya kura 32,637 sawa na asilimia 38. 46  ambapo  kile cha ZPPP kikipata kura 15 ,5o5 sawa na asilimia 18.27.

“Tokea mwaka 1957 ASP kilikuwa kikiongoza kupata kura nyingi licha ya kutoruhusiwa kuunda dola kwa hila za watawala, akasema vile vya ZNP na ZPPP vilivyokuwa vikipata idadi haba ya kura, havikukata tamaa wala kususia chaguzi, nafikiri vilijiamini na kutambua kuna kushinda na kushindwa” alisema
Hata hivyo alisema katika uchaguzi mkuu wa mwisho wa mwaka  1963, ASP kilikusanya jumla ya kura 53, 232 sawa na asilimia 54. 2, huku ZNP kikiambulia  kura 26, 572 sawa na asilimia 29. 8 ambapo  kile cha ZPPP kikivuna  kura 4, 572 sawa na asilimia 15. 9

“Uchaguzi wa mwisho ndipo ZNP na ZPPP wakakubaliana kuungamisha viti ili kuunda serikali kwa lengo la kukikomoa ASP ambacho kilikuwa kikipata kura nyingi huku katika maeneo ambayo ASP ikikubalika na kwenye wananchi  wengi  yakawekwa majimbo machache kwa hila ya Sultan ” majimbo

Takrima alisema wenye dhamana ya kutangaza tarehe ya uchaguzi ni ZEC ambayo ndiyo yenye madaraka na mamlaka kisheria hivyo uamuzi wa chama chochote cha siasa aidha kuamua  kususa au kutoshiriki uchaguzi alisema huenda ni  uchanga wa kisiasa, upeo mdogo na ukomavu finyu wa mambo katika dhana ya maendeleo ya demokrasia.

SHARE
Previous articleMagufuli, Lowassa mtegoni
Next articleKATUNI