Home Habari Daftari la wapiga kura kuzinduliwa leo

Daftari la wapiga kura kuzinduliwa leo

769
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaanza uboreshaji wa Daftari la mpiga kura ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Mwakani.

Uboreshaji huu unazinduliwa rasmi na Waziri Mkuu , Kassimu Majaliwa katika mikoa ya Kilimajaro na Arusha kisha uandikishaji huo kuendelea maeneo yote ya nchi.

Lengo la uboreshaji wa daftari hili ni kuruhusu uandikishwaji wa wapiga kura wapya ambao hawajawahi kujiandikisha katika daftari hilo, waliopoteza kadi zao pamoja na kuhuisha taarifa za wapiga kura waliofariki dunia.

Kutokana na uboreshaji huo Mkurugenzi Uchaguzi (NEC), Dk. Athuman Kihamia, amewataka wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, kutumia siku saba za uboreshwaji wa daftari hilo kujiandikisha na wasitarajie muda zaidi kuongezwa.

Dk. Kihamia amenukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa NEC imejipanga kikamilifu kuhakikisha shughuli nzima ya uboreshaji daftari hilo inakwenda vizuri kwa sababu wamejipanga  kuondoa kasoro zilizokuwapo kipindi cha nyuma.

“Tunataka maandalizi na shughuli nzima ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura iende vizuri, kwa baraka za Mwenyezi Mungu kama hakutakuwa na jambo lolote ambalo lipo nje uwezo wa kibinadamu, tutahakikisha uchaguzi unakua huru na haki na malalamiko yaliyokuwapo huko nyuma yamepungua kwa asilimia 90,” anasema Dk. Kihamia.

Ikimbukwe kuwa uboreshaji wa daftari hilo ni utimizaji wa matakwa ya sheria inayoelekeza uboreshaji huo kufanyia walau mara mbili katika kipindi cha kutoka ucaguzi mmoja hadi mwingine. Kwa kuwa ni matakwa ya sheria basi tume inatimiza wajibu wake kama inavyotakiwa.

Uboreshaji huu unakuja baada ya malalamiko kadhaa kutoka kwa wadau vikiwamo vyama vya siasa kulalamikia kutofanyika kwa uboreshaji huo. Pamoja na malalamiko hayo ni lazima kutambua kuwa sheria imeelekeza tu kufanyika kwa uboreshaji walau mara mbili kila baada ya uchaguzi na kabla ya uchaguzi mwingine lakini haijaelekeza ni lini maboresho hayo yafanyike.

Lakini kutokana na changamoto ambazo mara kadhaa zimekuwa zikijitokeza ni wazi kuwa iko haja sasa ya kufanya mabadiliko katika sheria hii ili kuongeza ufanisi wa tume katika uandikisha kutokana na ongezeko kubwa la waandikishaji wapya.

Kutokana na ongezeko hilo ni vema sheria sasa ikaelekeza mabadiliko hayo kuwa endelevu kama ilivyo kwa vitambulisho vya Taifa ambavyo ofisi zake ziko wazi wakati wote mtu anapohitaji, badala ya utaratibu wa sasa ambao unaweka vipindi maalumu vya kuandikisha.

Naamini utaratibu huu utapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa watu wakati wa kujiandikisha pamoja na changamoto za hapa na pale ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa kupiga kura.

Katika vipindi tofauti vya uchaguzi kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wananchi kulalamikia taarifa zao kutofautiana na zile za tume jambo ambalo huwakosesha sifa ya kupiga kura kuwachagua viongozi wao.

Kupitia uandikishaji endelevu ni wazi kuwa waandikishaji na waandikishwaji watakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa na kuingiza taarifa sahihi za kila mwananchi na hata kutoa nafasi ya kuzihakiki kabla ya kukamilisha mchakato wa uandikishaji.

Changamoto kubwa inayoweza kuibuliwa ni upungufu wa watendaji watakaofanya kazi hiyo. Lakini swali ni je hili la vitambulisho wa Taifa linawezekana vipi na hili la wapiga kura lishindikane? Mamlaka hizi zinaweza kuweka utaratibu utakaowezesha kazi hizi zote mbili kufanyika pamoja yaani watoaji wa vitambulisho vya Taifa pia wakatoa vitambulisho vya wapiga kura.

Hatua hii inaweza kuwa na mafanikio zaidi ya njia zinazotumika sasa na itawezaesha taarifa za uandikishaji katika kupiga kura kufanana na zile za kitambulisho cha Taifa.

Ni imani yangu kuwa utaratibu wa sasa wa uandikishaji ambao nautazama kama uandikishaji wa mtindo wa zimamoto kutokana na kufanyika kipindi kifupi kabla ya uchaguzi hauwezi kuwawezesha wananchi wote wenye sifa kuandikishwa na pia kuandiskishwa kwa usafi na ndiyo sababu ya vilio vya mara kwa mara kutofautiana kwa taarifa za mpiga kura.

Hebu fikiria ikiwa kwa mwaka mmoja tuvijana wapatao 427,181 au zaidi wanahitimu kidato cha nne, je idadi ya wapiga kura ni kubwa kwa kiasi gani. Nasema idadi hii ni kubwa kwa kuzingatia kuwa watu wanaokuwa katika umri wa kupiga kura ni wengi kuliko wale wanaohitimu kidato cha nne kwa mwaka mmoja.

Wahitimu wa kidato cha nne ni sehemu tu ya kundi kubwa la vijana wa umri huo kwa kuzingatia kuwa wako ambao hawakupata nafasi ya kuandikishwa shule, ambao hawakuendelea kidato cha kwanza baada ya kuhitimu darasa la saba, ambao waliachia katika masomo na ambao walijiunga katika mifumo mingine ya elimu isiyokuwa ya sekondari.

Kwa mantiki hiyo ni lazima Serikali ione haja ya maboresho katika eneo hilo hakuna sababu ya msingi ya kungoja karibu na wakati wa uchaguzi wananchi wanakurupushwa katika shughuli zao kwenda kupata foleni kusubiri kuandikishwa kupiga kura kana kwamba hawakuwa na taarifa kuwa daftari hilo linapaswa kuboreshwa.

Ni lazima kutambua kuwa jamii inayotafuta maendeleo ya Taifa ni lazima ianze na mabadiliko ya kifikra, kiutendaji na maendele ya mtu mmoja mmoja na hatimaye jamii nzima. Kuendelea kukumbatia sheria fulani ambazo hata zikibadilishwa haziwezi kuwa na athari hasi kwa Taifa ni kuamua kujichelewesha katika kuyasaka maendeleo ya kweli.

Ni lazima pia demokrasia ya kweli huanza kuhisiwa kuanzia katika masuala madogo kama hili la uandikishaji ambalo litawafanya wadau kuwa na imani kuwa wananchi wengi wamepata haki yao ya kuandikisha ili kupiga kura.

Kukosekama kwa imani hiyo kwa vyovyote vile inaweza kujenga dhana ya kuonewa kwa kuamini kuwa baadhi ya watu ambao walipaswa kupiga kura hawakupata nafasi hiyo.