Home Afrika Mashariki DALILI ZA UCHOYO, UBINAFSI WA ‘PANGU PAKAVU’ UNAANZA KUIBOMOA EAC

DALILI ZA UCHOYO, UBINAFSI WA ‘PANGU PAKAVU’ UNAANZA KUIBOMOA EAC

1108
0
SHARE

 

NA BALINAGWE MWAMBUNGU

WAVULANA wawili waligongana kwa msichana mmoja na kila mvulana alipeleka barua ya posa. Msichana huyo anajulikana kwa jina la Bomba binti Mafuta, anaishi nchini Uganda. Wavulana hao mmoja anatoka Kenya na mwingine Tanzania.

Tanzania na Kenya ni marafiki wa miaka mingi na wanategemeana katika mambo mengi ikiwamo biashara, lakini msichana Bomba aliharibu uhusiano huo.

Biashara kati ya Tanzania na Kenya imekuwa ikiongezeka na Kenya ndiyo ilikuwa inafaidika zaidi kwa kuwa ilikuwa inauza zaidi Tanzania. Kenya iliuza Tanzania bidhaa zenye thamani ya shilingi ya Kenya bilioni 19.9 mwaka 2005 na biashara hiyo iliongezeka na kufikia shilingi ya Kenya bilioni 41.05 mwaka 2011.

Katika kipindi hicho hicho, Kenya ilinunua bidhaa kutoka Tanzania zenye thamani ya shilingi ya Kenya bilioni 2.9 na 15.58. Kenya inauza Tanzania mchanganyiko wa bidhaa ikiwa ni pamoja na sabuni, mafuta ya michikichi, dawa aina mbalimbali, sukari ya viwandani, vyombo vya nyumbani, siagi, na chuma bapa (flat rolled iron).

Tanzania inauza Kenya bidhaa mbalimbali pia, ikiwa ni pamoja na karatasi ngumu (paper board), mahindi, mchele, nguo, transfoma, tube na mabomba, unga, mazao ya mifugo, mbogamboga na mafuta yatokanayo na mbegu.

Lakini biashara baina ya nchi hizi mbili ilishuka kwa muda mfupi kutokana na kugombea ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda. Wakenya ambao wanajiona wajanja na bora kuliko Watanzania, kama wajinga, walizidiwa kete.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, wakubaliana katika mazungumzo ya awali kwamba, bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1403 kutoka Hoima, lingejengwa kwenye ardhi ya Kenya hadi Bandari ya Lamu nchini Kenya. Baadaye baada ya wataalamu wa Tanzania kukutana na wale wa Uganda na Kenya, wakakubalina kwamba bomba hilo ambalo gharama yake ni $4billioni lipite Tanzania kwa sababu si tu litapunguza bali litapungua umbali kutoka kilometa 1403 hadi 1,120, bali pia gharama. Inaeleza kwamba ujumbe wa Kenya ulisusa kusaini muhtasari wa majadiliano.

Rais John Magufuli, haraka haraka akaenda Uganda na kuonana na Rais Museven na ikatangazwa rasmi kwamba bomba hilo litapita Tanzania. Rais Kenyatta akakimbilia Paris Ufaransa kujaribu kuwashawishi viongozi wa kampuni ya mafuta ya Total ambayo ndiyo itakayochimba mafuta katika Ziwa Albert, nako akagonga mwamba. Kama kwamba haikuridhika, Gazeti la Standard la Kenya, liliripoti kwamba nchi hiyo ilituma ujumbe wa kiserikali, ukiongozwa na Waziri wa Nishati, Charles Keter, lakini ulikataliwa kuingia kwenda kuangalia mazingira ya Bandari ya Tanga—sehemu ambayo imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya mafuta ghafi kutoka Uganda.

Baada ya bifu hilo kati ya Kenya na Tanzania, Shirika la Viwango la Kenya (KNSB), lilitangaza kwamba, mauzo ya bidhaa kwenda Tanzania, yalishuka kwa asilimia 27—kiasi cha KShilingi 42.7bilioni mwaka 2013 na kufikia KShilingi33.7 mwaka 2015.

Tanzania, ambayo ni muagizaji wa pili kwa ukubwa, biashara ilishuka kutoka KShilingi 18.36 mwaka 2014, hadi KShilingi 16.9bilioni mwaka 2015.

Kenya ikaanza bifu na Tanzania na hadi sasa bado zimesigana. Kana kwamba hiyo haitoshi, Kenya kwa kutaka kuiyumbisha Tanzania, ikakiuka makubaliano ya Mkataba wa Afrika Mashariki wa mwaka 2005 uliosainiwa na marais wanzilishi—Yoweri Museveni wa Uganda, Rais wa Kenya, Daniel arap Moi na Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa—kwamba mambo ya kisera na mipango, lazima yazingatiwe kwa matakwa ya wanajumuia.

Kenyatta akasusa kuja Dar es Salaam kwenye mkutano wa viongozi wa Jumuia, akamtuma Makamu wa Rais, William Rutto baada ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Magufuli, kuzishawishi nchi wanachama wa EAC kutosaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi—Economic Partnership Agreement (EPA). Kenya ikaenda kinyume ikasaini mkataba huo.

Sasa haieleweki itakuwaje, maana nchi zote za EAC zilitakiwa zisaini mkataba wa EPA kama kundi moja. Kenya imeingia mkataba huo kwa kutazama masilahi yake na Bunge la Tanzania limekwisha pigilia msumari wa mwisho kwa kukataa kuidhinisha mkataba huo uliobuniwa na Jumuia ya Ulaya.

Msuguano ulianzia wakati wa utawala wa Rais Mkapa ambaye aliuelezea mkataba wa EPA kama ukoloni mambo leo—kwamba Wazungu kwa kupitia mkataba huo wanataka kunyang’anyana Afrika kama walivyofanya kwenye Mkutano wa Berlin, mwaka 1884.

Mwalimu wa Sheria, Chuo Kikuu cha Iringa, Pius Shirima, ameifungulia mashita Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki kwa kusaini mkataba wa EPA. Anasema Mkataba wa EPA una madhara makubwa kwa uzalishaji wa bidhaa za Afrika Mashariki kwa kuwa zitakosa soko.

Katika hali kama hii, tutegemee nini kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki? Jumuiya ya awali ya 1967 iliyoundwa na Rais Julius Nyerere (Tanzania), Dk. Milton Obote (Uganda) na Jomo Kenyatta (Kenya), ilivunjika kutokana na chochoko kama hizi. Kenya wakajitapa kwamba wao ndio injini ya Jumuiya.

Kupinduliwa kwa aliyekuwa Rais Obote na Jenerali Idd Amin, kulimkasirisha Mwalimu Nyerere, akasema hataweza kukaa meza moja na Amin. Kwa upande wa Kenya, viongozi ambao walikuwa wanazitolea jicho la husda mali za Jumuiya, wakatumia uzee wa Rais Kenyatta, kuivuruga Jumuiya. Viongozi wakuu wa Jumuiya, ambao ndio Mamlaka ya Jumuiya inayoidhinisha bajeti, hawakukutana kwa muda wa miaka sita (1971-77). Jumuiya ikafa. Naanza kuziona dalili za mwanzo wa mfarakano zinazotokana na uchoyo na ubinafsi wa ‘pangu pakavu’.