Home Makala Kimataifa David Cameron amewapa ukiwa Waingereza

David Cameron amewapa ukiwa Waingereza

983
0
SHARE

Na Karrima Carter, Norwich

JUNI 23, mwaka huu wananchi wa Uingereza tulipiga kura ya maoni (referendum) na kufanya maamuzi magumu ya kubaki au kujitoa katika jumuiya ya umoja wa Ulaya (EU).

Juni 24, matokeo yalitangazwa na kuonyesha asilimia 51 ya Waingereza wameamua kupiga kura ya kujitoa katika uanachama huo.

Kuna mengi ya kuzungumzia kuhusu uamuzi huo. Kubwa zaidi lililowafanya wananchi kupiga kura hiyo ni idadi ya wahamiaji walioingia nchini Uingereza kila mwaka. Wahamiaji wengi wanatoka nchi za mashariki za Ulaya ambazo zina hali duni kiuchumi au kimaisha, kama Poland na Romania.

Kwa vile nchi ikiwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya ni lazma ufuate kanuni na itikadi zilizowekwa na umoja huo, mojawapo ni kufungua mipaka yenu na kupokea wakimbizi watokao nchi tofauti, iwe zilizoathirika kwa vita au kiuchumi.

Wote tunafahamu kuwa Uingereza ni nchi mojawapo duniani itoayo misaada mikubwa kwa madhumuni ya kumudu maisha kwa hali ya unafuu na kuondoa bughudha ya umaskini. Ndio maana wakimbizi wengi wanakimbilia hapa Uingereza.

Wapiga kura  hao asilimia 51 lalamiko lao kubwa ni kuhusu sera hiyo ya uhamiaji ambayo imekuwa kubwa mno nchini kwetu, na inasababisha sisi wenyewe wananchi tujitahidi na kukubali upungufu wa fedha tupewazo na serikali (kwa wasiofanya kazi au walipwao kiwango cha chini katika mishahara) ni sawa na Tanzania ikimbiliwe na wageni wengi kutoka vijijini, itabidi iwalishe na kuwapa makazi. Lakini kama wewe una utajiri kama Bakharesa itakushinda kuwalisha watu 10? Sidhani.

Aidha, tusisahau kuwa Ufaransa wanatulindia mpaka wetu ambao una wakimbizi zaidi ya 900, 000 au 1000,000 ambao wanataka kuingia hapa Uingereza. Sasa hivi Wafaransa wakiamua kutususia ulinzi huo na kusema; “waingereza si mmejitoa, sasa na sisi tunatimua katika mpaka wenu”

Kwa hakika uamuzi huo ukifanyika Uingereza itavamiwa na wakimbizi kama nzige kwenye mazao. Wananchi walalamikao kuhusu wakimbizi bado hawajaona mafuriko ya wahamiaji kabisa!

Pili, jambo kuu pia lililowapotezea uaminifu wa uanachama ni ada tunayotoa kila wiki kwa Umoja wa Ulaya ambayo ni zaidi ya pauni milioni 350 (£ Mil.350).

Ada hiyo ya pauni milioni 350 na zaidi tutumiazo kila wiki kuwepo katika uanachama wa Umoja wa Ulaya ukichambua kiundani zaidi na kwa akili ya kiuhasibu (Accountants) utaona Uingereza tunapokea misaada mara 10 ya hiyo fedha tulipayo EU.

Wafanyabiashara wengi (Small Businesses) wanategemea mikopo kutoka EU. Na kampuni hizi huajiri wafanyakazi wengi, kwa hivyo wote watakosa ajira. Na baadhi ya vitu tuvizalishavyo tunaviuza huko nchi za EU kwa bei nzuri sana, hivyo inaboresha uchumi wetu na kutoa ajira kwa asilimia fulani ya wananchi.

Pia twategemea malighafi nyingi kutoka Ulaya kwani nchi yetu kimazingira au kihali ya hewa hatuwezi kuzalisha hizo bidhaa, kwa hivyo hatuna budi ila kuzalisha mali hizo nchi jirani zilizobarikiwa na sifa za hali ya hewa nzuri na uzalishaji mkubwa ambao unatugharimu bei ya chini kabisa, kwa vile sisi na wanachama.

Mfano kama mwanajeshi wa Tanzania  awe na kadi maalumu  ya punguzo bei ya asilimia 20 kwa kila anunuacho pale maduka ya jeshini.  Mwanajeshi huyo ataona afueni kubwa ya matumizi yake kuliko raia wa kawaida anunuae bidhaa hizo hizo ila kwa kiwango kisichokuwa na punguzo la asilimia 20.

Mbaya zaidi kile walicholisema (hizo milioni 350 na zaidi) zitakwenda kwenye shirika la afya ili kuboresha matibabu, lakini mara baada ya tangazo la matokeo ya kura, EU ilitugeuzia kibao, kwa kutoa taarifa kuwa fedha zilizotakiwa kuletwa hapa Uingereza hazikuletwa tena. Sasa wapo waliopiga kura kwa sarafu hiyo tu ya uboreshaji wa NHS (National Health Service).

Wapiga kura walioamua kujitoa katika umoja huu hawakufikiria athari muhimu sana iwapo tutajitoa. Mojawapo ni iwapo wewe ni mwanachama utapata taarifa za kiusalama ambazo ni nyeti sana ni katika sakata la upambanaji wa ugaidi duniani, unapaswa kushirikiana na nchi wanachama.

Na kama wewe si mwanachama lazima kuwe na kiwango fulani cha kupunjwa taarifa za kiusalama. Sasa baada ya kujitoa Uingereza itabaki ukiwa, itapunjwa sana taarifa za kiusalama. Na hii yaweza kutupa mitihani migumu katika upambanaji wa ugaidi nchini kwetu. Kwani tayari tumeona tatizo kubwa la ugaidi mnamo kama shambulizi la kigaidi la Julai 7, 2005 lililotoka mjini London.

Itachukua takriban miaka miwili hadi tuweke mikakati na makubaliano mapya katika viwanja, mashirika ya nchi za Ulaya, na si hasha tukatozwa pesa za juu zaidi kwa kila tutakacho kununua kutoka huko. Mwisho wa siku twaweza jikuta tumekomboa milioni 350 ila tunalipa billion 1 kwa huduma zile zile tulizokuwa tunazipata, na yote hayo kisa tumeomba ile karatasi ya talaka.

 

MASHARTI YA IBARA YA 50

Kama nilivyotangulia kusema itachukua miaka miwili hadi kuweka makubaliano na nchi za Ulaya, nikiwa na maana ya kuzingatia Katiba iliyoanzishwa Jumuiya yenyewe.

Masharti mapya kulingana na Ibara ya 50 ya Mkataba wa EU wa Lisbon, Ureno yanailazimisha Uingereza kusubiri hadi miaka miwili  kamili hadi kukamilika kwa talaka ya kujitoa EU.

Kwanza kutakuwa na mkutano wa Mawaziri wa mambo ya Nje wan chi wanachama wa EU unaofanyika huko Burssels nchini Ubelgiji kisha Wakuu wa nchi za EU wiki ijayo watakutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron ambaye atapeleka taarifa rasmi ya kuwafahamisha kuwa wananchi wameamua kujiondoa.

Ibara ya 50 ni kipengele kwenye mkataba wa Umoja wa Ulaya kuhusu nchi mwanachama kujiondoa EU. Kinamtaka nchi mwanachama, kwa mfano Waziri Mkuu David Cameron anatakiwa kufuata utaratibu wa hiyo ibara kwa kuandika barua rasmi kwa Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo, kambi iliyoshinda ya akina Nigel Farage na Boris Johnson ina mpango wa mkakati ambao umeweka utaratibu wanaotaka wao kuhusu namna ya kujiondoa rasmi. Mkakati wa akina Garage na Johnson wanataka kuona Uingereza inatumia miaka mitatu na miezi kumi hadi kukamilika mpango wa kujitoa unachana wa EU.

Endapo mpango huo utakubaliwa badala ya ibara ya 50, baadhi ya mabadiliko yataanza mara moja kwa mfano, haki ya ukazi ya raia wa Ulaya inaweza kusitishwa moja kwa moja, sheria za uhamiaji zitabadilishwa, na mikataba mbalimbali ya biashara.

NANI KUWA WAZIRI MKUU?

Na sasa jukumu la kukamilisha kujitoa kwenye Jumuiya ya Ulaya halikuwa mikononi mwa David Cameron ambaye anatarajiwa kujiuzulu ifikapo Oktoba mwaka huu. Swali limebakia, nani atakuwa waziri mkuu baada ya kuondoka Cameron?

Inatarajiwa kuwa Meya wa zamani wa jiji la London na kiongozi Mkuu wa kampeni ya Uingereza kujitoa EU, Boris Johnson, atakuwa Waziri Mkuu baada ya David Cameron.

VUGUVU LA UTAIFA

Uingereza  inaundwa au ni mkusanyiko wa mataifa ya England, Wales, Scotland na Ireland Kaskazini. Sasa kwa mujibu wa matokeo ya kura, Scotland na Ireland Kaskazini walipiga kura kubaki EU, wakati England na Wales wamepiga kura kujiondoa EU.

Tayari Scotland wanasema wanaona hatima ya maisha yao  imo ndani ya EU na sio nje. Pia wamesema matokeo ya kura hiyo yanawapa haki ya kupiga kura nyingine ya maoni ya kudai uhuru kutoka Muungano wa Uingereza.

Hali kama hiyo imejitokeza pia huko Ireland Kaskazini ambao chama cha Sinn Fein kinataka Ireland ya Kaskazini ijitoe kwenye Muungano wa Uingereza kisha iungane na  Jamhuri ya Ireland.

Awali nchi zote mbili zilikuwa wanachama wa EU, sasa ni tofauti. Tatizo la mipaka pia linagusa mpaka wa Uingereza na Ufaransa katika mji wa Calais ambayo Wafaransa wanaulinda kwa niaba ya Uingereza kama nilivyoeleza hapo mwanzoni. Vuguvugu la utaifa limezikumba Ireland, kaskazini na Scotland.

Aidha, waziri mkuu wa Scotland, Nicola Sturgeon anayekiongoza chama cha SNP ametangaza kupambana ili kuzuia Uingereza kujitoa kwenye EU, vinginevyo na wao watadai kujitoa kwenye muungano ili baadaye wajiunge na EU wakiwa taifa huru.
KUCHUKUA AJENDA YA UKIP

Ninachokiona katika uongozi wa David Cameron ni kufanya maksoa wakati akigombea uwaziri mkuu kwa mara ya pili. Wakati wa kampeni mwaka jana David Cameron aliona njia ya kudhibiti umaarufu wa Chama cha UKIP ni kwa yeye kutoa ahadi kwenye kampeni kuwa akiingia madarakani ataitisha kura ya maoni kuhusu kubaki au kutoka EU wakati yeye ni miongoni mwa waliotaka Uingereza ibaki kwa hiyo katika kampeni hizi alihangaika upande wa kupinga isitoke. Hili ni kosa la kisiasa kuchukua ajenda za watu bila kuzielewa.