Home Makala Kimataifa Demokrasia imesaidia kupunguza mapinduzi ya kijeshi Afrika

Demokrasia imesaidia kupunguza mapinduzi ya kijeshi Afrika

1903
0
SHARE

Wanajeshi waasi wa Gabon wakitangaza kumuondoa Rais Ali Bongo kupitia raduio na televisheni.

NA HILAL K SUED

Jaribio la mapinduzi lilidumu kwa masaa machache tu. Saa kumi na nusu usiku wa tarehe 7 Januari kikundi kidogo cha maafisa wa jeshi wa ngazi za chini walikikamata kituo cha taifa cha radio na televisheni cha Gabon, nchi tajiri yenye kuzalisha mafuta kwa wingi huko Afrika ya Kati na kutangaza kwamba wamefanya mapinduzi.

Walisema walikuwa wamesukumwa na “hali ya kusikitisha” ya Rais wa nchi hiyo Ali Bongo Ondimba mwenye umri wa miaka 59 akitoa hotuba yake kwa wananchi wake akiwa kitandani nchini Morocco alikokwenda tangu Novemba mwaka jana kutibiwa baada ya kuugua kiharusi.

Hata hivyo ilipofika saa sita mchana wengi wa askari hao waliojaribu kufanya mapinduzi walitiwa mbaroni na serikali ikaendelea na shughuli zake.

Kilichotokea Gabon ni kumbusho tu ya hali ilivyokuwa Barani Afrika miaka ya nyuma. Mapinduzi ya kijeshi Barani Afrika miaka hii yamekuwa adimu sana – thibitisho kwamba misingi ya kidemokrasia imeenea katika nchi nyingi kuliko hapo zamani.

Lakini hata hivyo bado kuna udhaifu katika kuyadhibiti madaraka ya urais, hivyo viongozi wengi wamekuwa waking’ang’ania madarakani kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyo katika nchi nyingine zenye ushindani wa kweli wa kisiasa.

Tangu 2010 viongozi watano wa nchi tofauti za Afrika wamefariki wakiwa madarakani – wote kutokana na maradhi. Na viongozi saba waliopo sasa hivi wamekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 20. Rais Bongo ambaye asili yake ni uimbaji wa nyimbo za ‘funk,’ na kabla ya urais alikuwa waziri wa ulinzi, amekuwa madarakani kwa miaka kumi tu, lakini familia yake imekuwa ikiiongoza Gabon tangu 1967 – zaidi ya miaka 50. Ali Bongo alitwaa urais baada ya kifo cha baba yake Omar Bongo mwaka 2009.

Ali Bongo si rais pekee Barani Afrika anayeendesha nchi akiwa akiugua. Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alitumia muda mrefu wa mwaka 2017 akiwa anatibiwa nchi za nje kwa maradhi ambayo hadi sasa hayajajulikana.

Mwezi uliopita Buhari alilazimika kukana kwamba alikuwa amekufa na kwamba aliye madarakani ni mtu mwingie anayefanana naye. Hata hivyo anagombea tena urais katika uchaguzi mkuu mwezi ujao (Februari).

Aidha wananchi wa Algeria mara kwa mara huzungumzia afya ya rais wao – Abdelaziz Bouteflika, mwenye umri wa miaka 81. Ni nadra sana kwa Bouteflika kuonekana hadharani, na baadaye mwaka huu anatarajiwa kugombea tena urais kuwania muhula wa tano wa utawala wake.

Katika miongo ya nyuma viongozi hawa wakongwe walikuwa wanalengwa sana na vijana waliokuwa wakipanga kufanya mapinduzi. Hata hivyo mapinduzi ya hivi karibuni yaliyofanikiwa Barani Afrika pale jeshi la Zimbabwe lilimuondoa madarakani Robert Mugabe (93) yalikuwa tofauti kidogo.

Kuanzia mwaka 1980 hadi 2000 kulitokea mapinduzi 38 Barani Afrika yaliyofanikiwa. Kuanzia hapo (mwaka 2000) hadi sasa kumetokea majaribiao 15 tu. Sababu moja ya hii ni kwamba marais wamekuwa stadi zaidi katika kulinda tawala zao dhidi ya wafanya mapinduzi watarajiwa. Marais wengi husimika watu wa karibu wa familia zao katika nyadhifa muhimu, na kulifanya jeshi kuwa dhaifu.

Kuenea kwa demokrasia Barani Afrika nako kumepunguza kasi na idadi ya matukio ya mapinduzi. Umoja wa Afrika (AU) umeweka sera hasi dhidi ya mapinduzi ya kijeshi kewa kutoyavumilia kabisa ingawa imekuwa ikifumbia jicho pale itapatiwa sababu za kuridhisha za kufanya mapinduzi.

Zimbabwe kwa mfano, hatua ya majenerali ya kumzuilia nyumbani kwake Robert Mugabe waliieleza ni kwa ajili kumlinda, kuliko kumpindua. AU haikuoana kwanba hayo yalikuwa mapinduzi kwa tafsiri yoyote -inawezekana sababu ni kwamba Mugabe tayari alikuwa amepoteza umaarufu wake machoni mwa wengi.

Na katika nchi nyingine, ingawa msimamo wa AU umesaidia katika kuzuia kufanyika mapinduzi, pia umeyatibua mengine yaliyofanyika. Nchini Burkina Faso kwa mfano, AU ilihusika pakubwa katika kuwalazimisha wanajeshi kurudisha madaraka kwa viongozi wa kiraia baada ya kumuondoa madarakani Blaise Compaore mwaka 2015.

Hata hivyo kupungua kwa matukio ya mapinduzi ya kijeshi ni jambo jema, ingawa ushindani wa kisiasa katika nchi nyingi bado umebanwa. Nchi nyingi Barani Afrika zimejiwekea ukomo wa vipindi vya urais katika katiba lakini tangu mwaka 2000 nchi 10 zimebadilisha katiba zao kuwawezesha marais waliopo kuendelea kukaa madarakani.

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir ambaye ametawala tangu 1989 hivi karibuni naye ameweka dhamira ya kufanya hivyo, pamoja na maandamano yanayoendelea sasa hivi dhidi ya utawala wake – yuanayomtaka ang’atuke.

Kutokana na hali ilivyo Barani Afrika, wastani wa umri wa viongozi walio madarakani umekuwa ukiongezeka maradufu kuanzia miaka 52 mwaka 1980 hadi miaka 66 sasa hivi. Hii haitokani na sababu viongozi wanaishi maisha marefu. Katika demokrasia za ushindani mkubwa pia, vyama vya siasa huongozwa na watu wenye umri mkubwa ambao husita sana kuondoka uwanja wa siasa.

Kwa mfano sasa hivi mpinzani mkuu wa Buhari katika uchaguzi ujao nchini Nigeria ni mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 70, na alishagombea urais mara nne huko nyuma.

Mwaka 2014 nchi ya Tunisia ilimbadili kidemokrasia rais wake wa umri wa miaka 69 kwa mwingine wa umri wa miaka 88. Viongozi wakongwe barani Afrika hawana haraka ya kuondoka madarakani.