Home kitaifa Demokrasia ya kupayuka inamsaidiaje mwananchi?

Demokrasia ya kupayuka inamsaidiaje mwananchi?

2575
0
SHARE
Viongozi wakuu wa Chadema, wakiwa wameshikana mikono baada ya kutangaza oparesheni UKUTA

WIKI iliyopita tulishuhudia katika vyombo vya habari takriban vyote jinsi mvutano kati ya Rais John Magufuli na wanasiasa wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ulivyokuwa mkali na wakati mwingine wa kutisha.

Mvutano wenyewe umetokana na uamuzi wa viongozi wakuu wa vyama vya upinzani kuamua kwamba wanataka kuitisha na kuhamasisha wananchi kote nchini kujitokeza katika maandamano ya kupinga kile wanachodai kwamba ni viashiria vya udikteta katika staili ya utawala ya Rais Magufuli.

Katika azima hiyo ya kutaka kupingana na staili ya uongozi ya Rais Magufuli na kaulimbiu yake ya HapaKaziTu viongozi hao wakisaidiwa na baadhi ya wasaidizi wao wametangaza kufanya maandamano waliyoyaita UKUTA wakimaanisha Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania.

Kwa mtazamamo wao ambao wana haki nao ya kikatiba ni kwamba kaulimbiu ya Rais Magufuli ambayo haiwezi kutekelezeka bila ya kuwa na nidhamu ya hali ya juu ni udikteta.

Hili la udikteta wa Rais Magufuli naliacha kama lilivyo kwani linajadilika katika duru za falsafa ya siasa na najua kwamba si rahisi sana kufikia muafaka. Hata hivyo kuna umuhimu wa kuangalia mambo kadhaa ili kuweka kila kitu mahali pake.

Rais Magufuli anatawala nchi hii kwa kufuata Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kwa mujibu wa kitabu hicho ambacho ni sheria mama kuna maelekezo ya nini kinatakiwa kufanyika kama kiongozi aliyepo madarakani anaivunja Katiba hiyo.

Kuhamasisha wananchi kujitokeza eti kupiga viashiria vya udikteta wa Rais ni kwenda kinyume kabisa na Katiba hiyo kwani ndani yake kuna utaratibu wa jinsi ya kumchukulia hatua Rais endapo atavunja Katiba.

Aidha, katika hoja ambayo Rais Magufuli anaitumia ni kwamba maandamano si tatizo hata kidogo. Tatizo ni kwamba yeye hakubaliani na utaratibu wa wanasiasa kuondoka katika majimbo yao ya uchaguzi na kuingia katika majimbo yasiyowahusu moja kwa moja na kuwahamasisha wananchi kuandamana.

Msisitizo wa Rais Magufuli ni nidhamu katika kila jambo ambalo tunalifanya lakini zaidi ni nidhamu ya kazi. Sasa kama wanasiasa watakuwa wanawahimiza wananchi kuandamana na kuacha kufanya kazi kwa kisingizio kwamba Rais ambaye wamemchagua miezi takriban tisa iliyopita eti ni dikteta hilo ni jambo lisilokubalika.

Aidha, Rais Magufuli anawaasa wanasiasa kuitisha maandamano na mikutano ya hadhara ndani ya majimbo yao ili kupeleka ujumbe wanaoutaka badala ya kuwaingiza watu ambao kama tukirejea katika matokeo ya uchaguzi walimpigia yeye kura kuwa rais wao na wanasubiri kuona huyu waliyempigia kura anawapa nini.

Haiyumkiniki hata kidogo hata kabla hajakalia kiti cha urais na kujiweka sawa badala ya kumsaidia ili aweze kuongoza vizuri wanamvuta shati.

Nani asiyejua kiwango cha utovu na ukosefu wa nidhamu ambao umetamalaki katika nchi hii. Nani asiyejua kwamba ufisadi na wizi wa kila aina umeota mizizi kiasi kwamba kufanya kazi kukachukuliwa kwamba ni ubwege na ufisadi ukawa ndio unaopigiwa mfano na kushangiliwa.

Inakuwaje katika nchi ambayo wananchi walikwisha kufikia hatua ya kukata tamaa na kutaka mabadiliko yoyote yale ilimradi si ya kuendelea na kinaichoitwa business as usual leo kikundi cha waliokuwa walalamikaji wakuu na waliokuwa wakiomba ridhaa ya kuingia Ikulu ili waibadilishe hali hiyo sasa hawataki tena hayo mabadiliko.

Ukiangalia na kufuatilia hicho kinachoitwa udikteta au viashiria vya udikteta ni hatua ambazo Rais Magufuli anazichukua katika jitihada za kurudisha heshima ya kazi na kwa njia hiyo heshima ya Mtanzania na Tanzania.

Tuligeuka kuwa nchi ya watumishi wa umma wezi wa mali ya umma kwa kushirikiana na wafanyabiashara. Watumishi wa umma walijigeuza miungu na wanachoamua wao ndicho kinachofanyika na wananchi walikuwa ni mabwege tu mbele ya wateule hao.

Ajira zilikuwa zinatolewa kwa watu wasiostahili, vyeti vya kughushi vikajipenyeza kila kona, shahada za karatasi zikawa ndizo zinazotumika kugawa nafasi za ajira jambo ambalo limesababisha hasara kubwa kwa serikali si kwa upande wa mishahara na marupurupu tu bali hata kwenye upande wa maamuzi yasiyokuwa sahihi kutokana na uwezo mdogo wa watumishi hao wenye taaluma feki.

Vijana ambao wote tunakubaliana kwamba wana tatizo kubwa la ajira, badala ya waliopo madarakani kuwasaidia kwanza kwa kuwasimamisha kwenye msitari wa nidhamu binafsi kama msingi muhimu katika mazingira yoyote yale ya kupata ufumbuzi wa tatizo, wakasambaziwa viroba kila kona ya nchi hadi vijijini temna kwa bei ya hadi shilingi 100 kimoja.

Taratibu taifa likaanza kugeuka la vijana walevi, wasiokuwa na muda wa kufikiri jinsi ya kujipenyeza kwenye uchumi wa taifa kwa kutarajia na kutegemea kwamba watapata ajira kutoka serikalini.

Badala ya viongozi kutafuta namna ya kushirikiana na vijana hao kubunia namna ambayo wangeliweza kujitumbukiza kwenye uchumi mkuu wanaendelea kuwatumia kama mtaji wa kisiasa, wa kuwalisha uongo kwamba wanao uwezo wa kuwapatia ajira ili mradi tu wawe nao na wahakikishe kwamba wanapigana ili wapate kura na kuingia madarakani.

Rais Magufuli amepokea nchi ambayo hata wasomi wake wanaohitimu wana mapungufu makubwa katika elimu waliyoipata kwani wanategemea na kutarajia kuajiriwa na serikali au sekta binafsi ili mradi ni ajira.

Kwamba usomi ni pamoja na kuweza kutambua namna unavyoweza kuitumia elimu uliyoipata ili kujipatia kipato na wakati huo huo ukitatua matatizo ambayo yapo katika jamii kwa njia moja au nyingine.

Udikteta unaozungumziwa na ambao ndio unaowafanya baadhi ya viongozi kuhamaki ni hatua ambazo Rais Mgufuli anazichukua ili kuibadili hali hasi iliyokuwepo nchini na kuwafanya wananchi watambue kwamba kazi ndio msingi wa kila aina ya mafanikio katika jamii na kwamba njia za mkato za kupata fedha si tu kwamba ni kuvunja sheria bali hazina tija.

Taifa ambalo watu wake wanaiona kazi kuwa ni adhabu na ambalo linawavulia kofia na kuwapisha viti mafisadi haliwezi kujivuna kwamba lipo sawasawa. Ni taifa la watu hatari sana.

Katika kuitekeleza azima ya kuirejesha nchi kwenye mstari unaotakiwa bila shaka Rais Magufuli atafanya makosa hapa na pale. Haiyumkiniki kumkwaza asiirejeshe nchi kwenye mstari eti kwa kuchelea tu kwamba inawezekana ikafanyika tafsiri hasi ya vitendo vyake.

Hiyo demokrasia inayozungumziwa kwamba anaikwaza ni lazima ikwazike kwa sababu tayari ilikwisha kuvurugwa katika kipindi cha myumbo katika nchi yetu.

Kwamba tunaona ni afadhali kuwa na uhuru wa kupayuka sana hata kama kupayuka huko hakusaidii kurejesha matumaini ya walio wengi ya kuondokana na ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma, wizi, upendeleo na kila aina ya madhila katika jamii. Kwangu  mimi haiingii akilini kwamba eti ni afadhali tuishi katika mazingira ovu ili mradi tunaweza kupayuka. Haiingii akilini hata kidogo.

Demokrasia gani hiyo tunayoipigania ambayo haiweki mkazo kisawasawa katika ufanyaji kazi kwa wote wenye uwezo wa kufanya hivyo? Demokrasia gani hiyo ambayo inatoa fursa ya kutukana na kupayuka utakavyo na upendavyo lakini haibadilishi chochote kwa sababu wizi upo pale pale, ubadhirifu kama kazi, ufisadi ndiyo usiseme, kughushi vyeti ndiyo mchezo wa kila mwenye kompyuta, wizi wa fedha za umma kwa kutumia wafanyakazi hewa ndiyo mchezo wa kila siku, kuwapora wananchi ardhi na kuwakabidhi wanaoitwa wawekezaji kama kawa, wakubwa kujimilikisha ardhi za vijiji na kuwatimua kama mbwa koko wanavijiji na mikopo ya elimu ya juu kutolewa kwa wenye uwezo na kuachwa wanaohitaji. Demokrasia ya aina hiyo kamwe haifai, haitakiwi na haiwezi kuwa na nafasi.

Demokrasia anayoitaka Rais Magufuli ni ya kuhakikisha kwamba ufisadi, wizi na ubadhirifu wote wa mali ya umma unakoma mara moja. Rais Magufuli anataka demokrasia ya kuhakikisha kwamba ardhi inarejeshwa kwa wamiliki wake halali ambao ni wananchi.

Anachotaka Rais Magufuli ni kuhakikisha mikopo ya elimu ya juu inatolewa kwa wanaohitaji kweli. Anachotaka Rais Magufuli ni demokrasia ya kweli na si ya kuachia kupayuka na kutukana bila ya mabadiliko yoyote.

Rais Magufuli kasema kweli wanaotaka kuandamana na wafanye hivyo kwenye majimbo yao ya uchaguzi badala ya kuwavuruga watu ambao wanataka kufanya kazi kwa utulivu na kutumia demokrasia yao kuzalisha mali. HapaKaziTu!

DK. GIDEON SHOO, +255 784 222 293 /drgshoo@gmail.com