Home Makala DEVOTHA MINZI: Mkufunzi ujasiriamali asiyejuta kuacha kazi BoT

DEVOTHA MINZI: Mkufunzi ujasiriamali asiyejuta kuacha kazi BoT

980
0
SHARE

NA ESTHER MBUSSI

-DAR ES SALAAM

UNAWEZA kudhani ni hadhi ya juu kiasi gani kufanya kazi katika taasisi kubwa nchini yenye dhamana ya fedha kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT). 

Unaweza kudhani mtu anaweza kuacha kazi katika taasisi hiyo nyeti bila kufukuzwa kazi eti kisa tu akafanye ujasiriamali.

Mama Devotha Minzi aliyefanya kazi katika taasisi hiyo kwa miaka 24, aliacha kazi ili tu akawe mjasiriamali.

Baada ya kuacha kazi mwaka 2008, alifungua kampuni yake aliyoipa jina la K-Finance yeye akiwa Mwenyekiti wa Bodi, ambayo inajishughulisha na kutoa mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali.

Anasema kampuni hiyo ambayo imefanya kazi kwa karibu na wajasiriamali, lakini wiki iliyopita kampuni hiyo iliamua kwenda mbali zaidi na kutoa mafunzo rasmi kwa wajasiriamali wanawake zaidi ya 100.

Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, yaliitikiwa vizuri na wanawake hao ambapo mada mbalimbali ikiwamo namna ya kumfanya mjasiriamali kutumia mtaji wake vizuri na kuiongezea thamani biashara yake na uhuru kwa lengo la kumfundisha mjasiriamali kuelekea kwenye uhuru wa fikra ya kiuchumi, ziliwasilishwa na Devotha pamoja na kupata uzoefu kwa watu waliofanikiwa.

“K-Finance lengo lake ni kumfanya mjasiriamali aweze kutumia mtaji wake vizuri. Tuliona tukusanye huu uzoefu ili tujue wakati tunafundisha, tusifundishe nadharia sasa huu ni mwaka wa 12 na tunatimiza muhula wetu wa pili kufundisha uhuru wa fikra.

“Haya mafunzo yetu tumeyaita ‘Ignite Business Clinic’ kwa misingi kwamba ni Kliniki ya kiuchumi, kliniki ya utajirisho, hapa tunatengeneza jukwaa la majadiliano, kuna mambo mengi ambayo Watanzania tunayachukua kwa juu juu tu.

“Kwa mfano hatuheshimu watu waliofanikiwa katika jasho na damu watu wanafanya kazi ndiyo wanafanikiwa lakini utasikia mtu anazungumzia mambo kirahisi rahisi tu, unapiga dili kupata fedha, sisi hiyo tunataka tuikemee fedha zinapatikana katika kazi, katika kuongeza thamani ya bidhaa yako.

“Tuliona wakati wanafundisha tusifundishe nadharia tu, sasa huu ni mwaka wa 12 na tunatimiza muhula wetu wa pili kwa hiyo katika mafunzo haya ambayyo tumeanza kwa kina mama lakini tutaenda kwa kina baba na vijana pia, tunataka kubadilisha fikra za Watanzania.

“Tumeanza na wamama kwa kuwa tunatambua mchango wa wanawake katika jamii, mwanamke akishajua kwamba hapa ni kazi na kazi kimpango kazi anaifanya kwa usahihi na pia kwa sababu wao ni walimu,”anasema Devotha.

Pamoja na mambo mengine, anasema mafunzo hayo pia malengo yake ni kumfanya mjasiriamali aweze kutumia mtaji wake vizuri kwa sababu kumekuwa na matumizi mabaya ya neno ujasiriamali kuwa mjasiriamali ni kama mtu mwenye biashara ndogo ndogo lakini ukweli ni kwamba ujasiriamali si biashara ndogo ni namna ya ufanyaji biashara wenye tija.

Anasema mafunzo hayo yatakuwa endelevu ambapo wanapanga kuwa na semina zenye wazo kuu moja kila baada ya mwezi mmoja, mada ikiwa ni kujitathimini na kujitambua.

“Hakuna mtu anayeweza kuwaambia ufanye biashara gani, ni lazima ujitambue kwanza, yaani tutumie nafasi tulizo nazo kujidadavua sisi ni nani. Tunaanzia kwenye uhuru wa fikra kwa sababu ndiyo uhuru wa kila kitu kuelekea uhuru wa kiuchumi.

“Uhuru wa kiuchumi ni ile hali ya kutengeneza kipato endelevu kinachokidhi mahitaji yako na uhuru wa kiuchumi unapatikana katika kazi na nguvu ya kiuchumi inaendana na kujiajiri,” anasema mama Devotha.

CHIMBUKO LA MAFUNZO YA IBC

Mama Devotha anazungumzia chimbuko la mafunzo ya ujasiriamali ya IBC, anaeleza amepata kuwa mjumbe wa mabodi kadhaa akishiriki kusimamia na kuongoza makampuni ambapo kupitia elimu na kazi yake ameweza kuufahamu vizuri uchumi wa Tanzania.

“Kupitia uzoefu huo, nimeweza kuelewa fursa na changamoto zilizopo kiuchumi. Natambua wapi tupo kiuchumi na wapi tunatakiwa kwenda.

“Katika uzoefu wangu huo pia niligundua wasomi ndiyo kabisa hawako kwenye biashara, nilitambua pia kuendesha biashara kunahitaji akili nyingi na maono makubwa ili kuwa bosi wako mwenyewe.

“Biashara tumeiachia watu majasiri wakiwa na changamoto  kubwa za kielimu na kimikakati,” anaeleza.

KUACHA KAZI BoT

Wakati anaacha kazi BoT, mwaka 2008 akiwa na miaka 48, watu wengi walimshangaa lakini hakusubiri ushauri wao kwani wengi wao wamekuwa wakimkatisha tamaa.

Anasema aliamua kuwa msuluhishi wa yale aliyoyaona kuwa changamoto ambapo aliamua kutumia elimu yake kama mchumi na mtafiti na kufungua kampuni yake hiyo ya K-Finance Ltd.

“Wengi wameniuliza maana ya K, sikuwa wazi na imekuwa siri kubwa moyoni mwangu lakini maana yake ni inamaanisha Kwanza kwani niliamini siku moja kampuni yangu itakuwa top number one (Namba moja) kwa kile ninachokifanya. 

“Ndoto yangu kubwa ni kuona K-Finance inaheshimika kwa mchango wake kwa kuwaunga mkono wajasiriamali Tanzania na kuongeza mchango wa wazawa katika taifa letu,” anasema.

UZOEFU WA UJASIRIAMALI

Kuhusu uzoefu wake katika ujasiriamali, Mama Devotha anasema kujishughulisha na wajasiriamali kumemfundisha kuwa ukosefu wa elimu na ufahamu juu ya dhana nzima ya biashara ni tatizo kubwa sana.

“Huenda ni kubwa kuliko la mitaji kama tunavyoamini, hapa sizungumzii elimu ya darasani, madigrii wala madiploma.

“Kama jamii tunahurumia sana umaskini bila kukemea na kuondoa visababishi vya umaskini huo. Jamii haimpi kibano na maswali magumu asiyekuwa nacho na hatuwajibishani kwa dhati kuondoa mzizi wa tatizo  na hii imekuwa ni sehemu ya utamaduni wetu na inatugharimu sana,” anasema.

Anazungumzia vijana kuwa wanaacha kazi kwa sababu za kipuuzi wakitegemea kuishi kama tegemezi na wanaachwa hivyo huku akifafanua tatizo la ajira haliendani na bidii na umakini unaowekwa katika kazi.

NINI KIFANYIKE?

Mama Devotha pia hasiti kutoa suluhu ya changamoto hizo ambapo anasema mabadiliko ni lazima na kitafutwe chanzo cha mkwamo huo.

“Bila kutambua chanzo na kubadili tabia, hutoki. Jamii inawaheshimu waliofanikiwa kwa juhudi na maarifa. Tuwatambue wapambanaji kiuchumi na kuwapa heshima yao tukiiga mifano ya nchi za magharibi.

“Tundokane na dhana potofu ya kufikiri watu wanafanikiwa kibahati. Maandiko yote matakatifu yamesisitiza kuwa mafanikio yanatokana na kazi na juhudi,” anasema.