Home Makala Kimataifa DIANE RWIGARA MWANAMKE NGULI ANAYEPAMBANA NA SIASA ZA KAGAME

DIANE RWIGARA MWANAMKE NGULI ANAYEPAMBANA NA SIASA ZA KAGAME

1142
0
SHARE

NA MPOKI BUYAH

MWANASIASA Diane Rwigara Shima, amewahi kusema mbele ya vyombo vya habari kama Aljazeera na Reuters kwamba, katika taifa lake la Rwanda ni ‘rahisi sana kumpata mbuzi aliyepotea kuliko kumpata binadamu’. Rwigara anamaanisha kwamba, Rwanda mtu akipoteaa usihangaike kumtafuta maana hutampata kabisa lakini mbuzi akipotea au kuku mtafute huyo utampata.

Mbali na uongozi uliotukuka wa Paul Kagame, lakini taifa hilo linaongoza Afrika kwa kupoteza watu bila kujulikana walipo, katika hili viongozi wa Afrika wanapaswa kuliangalia vyema. Kupotea kwa watu au kufanyiwa unyama wa aina yoyote ile hakuwafanyi waogopwe bali kunawapotezea sifa ya kuwa viongozi bora.

Rais Yahaya Abdul Jameh, amewahi kushutumiwa kwa kutumia nguvu kubwa pamoja na kuwapoteza au kuwafunga vifungo vya muda mrefu zaidi pasipo kuwapeleka mahakamani.

Kinachomfanya Dianea Rwigira kusota na kufanyiwa kila aina ya dhuluma ni pale alipoenda kinyume na matakwa  ya Rais Kagame. Kinamchokabili mwanaharakati na mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Kagame ni pale alipogusa sehemu muhimu ya rais huyo ambaye ataongoza nchi mpaka 2034.

Diane Rwigara alizaliwa mwaka 1981 huko Kigali. Pengine unaweza ukasema ni Mhutu maana Wahutu wengi ndio wapinzani wakubwa wa Kagame, lakini huyu mtetezi wa wanyonge na mwenye kuhitaji kuona utawala wa sheria unatumika huko Rwanda anatoka kabila la Kituts, amekuwa akipinga utawala wa kimabavu usiojali haki za binadamu huko Rwanda na sasa amenasa kwenye mtego wa Rais Kagame.

Sijui kama atatoka salama maana Rwanda si sehemu salama kabisa kwa wasema kweli pengine kuliko taifa lolote lile Afrika, ukionekana wewe ni kikwazo katika Serikali basi unapotezwa wala kaburi au nguo zako hazitaonekana tena. Viongozi wa Afrika ni lini mtalifanya Bara la Afrika kuwa sehemu safi na salama kwa kuishi! Kabla hamjatuletea maji, barabara za flyover, shule, chakula, madawa na mengine, dumisheni amani na upendo dhidi ya raia mnaowaongoza. Kinachoendelea Rwanda si kigeni ila hofu ikizidi sana watu watakimbia na kwenda kuitafuta amani nje ya mataifa yao.

Diane ameanza kufuatiliwa na maofisa usalama wa taifa hilo baada ya kugoma kufanya kazi na kushirikiana na chama tawala – RPF. Mfanyabiashara huyo kijana kabisa barani Afrika ambaye amejitoa ufahamu kwa kupinga na kukosoa Serikali ya Kagame alianza kuchunguzwa baada ya kugoma kumuunga mkono Kagame.

Kumbe ukikataa kuunga mkono chama tawala wewe ni adui tayari, siasa za Afrika ni ngumu kuliko sehemu yoyote ile duniani. RPF walimwona Dianae kama kibaraka na hapo ndio chuki ilipoanza mpaka kufunguliwa mashtaka ya kutaka kuipindua Serikali ya Kagame. Na sasa akikutwa na hatia anaweza kuhukumiwa miaka 20 yeye na dada yake, Anne Rwigara na mama yao mzazi.

Huu ndio unaoitwa mkono wa chuma, katika maisha haya ya sasa Afrika inahitajika mabadiliko makubwa tena kwa haraka sana maana tunakoelekea ni kubaya zaidi kuliko tulikotoka, viongozi kumbukeni bila kudumisha amani na upendo na kuepuka kuwanyanyasa wanyonge kwa kuwa hawana kitu hata maendeleo mtakayoleta hayatakuwa na faida.

Diane kosa alilolifanya mpaka leo anaonekana kibaraka na kusota mahabusu yeye, dada yake Anne pamoja na mama yao mzazi ni baada ya kutaka kufanyika upya kwa upelelezi juu ya kifo cha baba yake mzazi, Assinol Rwigara, aliyefariki kwa kupata ajali baada ya gari lake dogo kugongana na lori kitu ambacho wanadai kulikuwa na upotoshaji wa taarifa maana lori liligonga upande wa abiria inakuaje Assinol Rwigara afariki!

Lakini pia Rwigara anafafanua kwamba, baba yake alifunikwa na kitu kizito kilichomfanya akose pumzi, lakini pia baada ya ajali hiyo walikumkuta ameharibiwa vibaya mno sehemu za kifuani na usoni. Hivyo Dianne amekuwa akimwomba Kagame kufanyika upya uchunguzi juu ya kifo cha baba yake mzazi kilichotokea mwaka 2015 na kuituhumu Serikali ya Kagame kwamba ilihusika katika kumuua mzee Assino  kitu ambacho, wachambuzi  wa nchi hiyo wanaamini hayo ni moja ya sababu zinazomfanya leo anauvaa mkono wa chuma wa Kagame.

Pia Diane sasa yupo matatani baada ya kumkosoa waziwazi Kagame kuwa anaminya uhuru wa raia wake na ukandamizaji wa haki za binadamu ikiwemo kupotezwa kwa wapinzani tangu mwaka 1994. Kaka yake Diane, aliwaambia Aljazeera kuwa baada ya dada yake kuanza kukosoa na kuhoji juu ya ukandamizaji wa haki za binadamu, wamekuwa wakifuatiliwa na kukaguliwa mara kwa mara na maofisa wa polisi.

Kwa mantiki hiyo Afrika si sehemu salama kusema ukweli na kuzikosoa Serikali zilizopo madarakani. Imekuwa hivyo kwa muda wa miaka mingi, viongozi wengi hawataki kukosolewa maana hawajui umuhimu wa kukosolewa na hiki ndicho kinachomfanya Dianne akutane na mkono wa chuma ambao umeshutumiwa vikali na mataifa ya Uingereza na Marekani juu ya kukamatwa kwake.

Unapozungumzia siasa, unazungumzia maisha na mali za watu  kwa ujumla wake, matetemeko ya kisiasa yameanza kumkumba Diane na Anne Rwigara pamoja na mama yao Adeline, baada ya kutangaza nia ya kugombea urais mnamo Julai mwaka huu. Chama tawala cha RPF hakikupendezwa na hatua hiyo na baada ya saa 72 kupita maofisa usalama wa nchi hiyo walitoa picha za utupu za Dianne ili kumchafulia, picha hizo nyingi zilimwonyesha akiwa uchi wa mnyama ijapokuwa yeye mwenyewe amepinga kwamba picha hizo hazikuwa zake bali zilihaririwa kwa ustadi wa hali ya juu.

Bado Dianne aliendelea na mapambano na kukusanya saini za wadhamini ambapo alifikisha 958 na kuongezea nyingine 120, tume ya uchaguzi walisema saini hizo ni za uongo kwamba ameghushi na kuongeza kuwa kudai kwamba baadhi ya wadhamini wake walishakufa hivyo alifunguliwa kesi mahakamani kwa kosa la kughushi.

Kupambana na Serikali iliyopo madarakani ni kazi ngumu sana ambayo inahitaji kuwa na moyo mgumu kama wakina Ondimba Toivo ya Toivo wa Namibia au Ernesty Che Guevara au ambaye mwaka huu ametimiza miaka 50 tangu kifo chake kilichotokea mwaka 1967 huko Bolvia. Guevara alipinga vikali dhuluma na ukandamizaji wa watu wanyonge alikuwa mtetezi ambaye hakuwa na mipaka ambaye miaka ya 1960 alifika mpaka Congo.

Mwanamama Dianne pia anashutumiwa kwa kutaka kuipindua Serikali ya Kagame ingawa familia yake inapinga vikali shutuma hizo huku wakidai kwamba wamebambikiziwa hizo kesi baada ya mtoto wao kutangaza nia ya kugombea urais ambapo Kagame alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 99.

Mamlaka za ukusanyaji wa mapato nchini Rwanda pia zimemfungulia kesi Dianne kwa makosa ya ukwepaji kodi katika biashara zake kwamba hajalipa kodi kwa muda wa miaka zaidi ya mitano hivyo anashtakiwa kwa kosa la ukwepaji kodi. Mahakama nchini humo zinadai kwamba endapo atakutwa na hatia basi atahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kufilisiwa mali zake zote pamoja na za familia yake. 0762155025,mpokibuya@gmail.com

Itaendelea wiki ijayo.