Home Michezo Dili zilizoota mbawa usajili Januari

Dili zilizoota mbawa usajili Januari

1219
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

DIRISHA dogo la usajili la Januari lilifungwa mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni baada ya takribani mwezi mmoja tangu lilipofunguliwa.

Kilikuwa ni kipindi kigumu kwa makocha na mabosi wa klabu mbalimbali barani Ulaya kuvifanyia marekebisho vikosi vyao kuelekea mwishoni mwa msimu huu.

Klabu zote 20 za Ligi Kuu ya England (EPL) zimetumia fedha kiduchu, Pauni milioni 180, likiwa ni anguko kubwa ikilinganishwa na miaka sita iliyopita.

Mara ya mwisho kwa EPL kuwa na utumizi mdogo wa fedha kwenye soko la usajili ilikuwa Januari, 2012, ambapo ghadi dirisha linafungwa ni Pauni milioni 60 tu zilizokuwa zimenunua wachezaji.

Hata hivyo, zikiwa zimebaki saa chache kabla ya usajili wa safari hii kufungwa, zilikuwapo dili zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu lakini kwa bahati mbaya zilishindwa kukamilika.

Nyota wa Chelsea, Willian, alikaribia kujiunga na wababe wa soka la Ufaransa, PSG, kabla ya dili kuota mbawa na kujikuta amebaki Stamford Bridge.

PSG waliamini Mbrazil huyo aliyetua Blues mwaka 2013 akitokea Ukraine alikokuwa akiichezea Shakhtar Donetsk, ndiye anayeweza kuvivaa viatu vya Neymar atakayekuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi akiuguza ‘enka’.

Mazungumzo ya dakika za mwisho yalikwama baada ya Chelsea kuiambia PSG iweke mezani kitita cha Pauni milioni 40 kumchukua Willian mwenye umri wa miaka 30.

Olivier Giroud naye alikaribia kwenda Magharibi mwa Jiji la London kujiunga na mahasimu wakubwa wa Chelsea, West Ham. Ujio wa Gonzalo Higuain, umeonekana kumnyima raha Giroud, hivyo alitaka kutimka zake.

West Ham walipeleka ombi lao la kutaka kumchukua Giroud kwa lengo la kumsaidia mshambuliaji wao hatari, Marko Arnautovic, na hadi dakika za mwisho kabla ya usajili kufungwa, iliaminika angekwenda huko lakini Blues waligoma.

Arsenal walipania kumchukua kwa mkopo mshambuliaji wa pembeni wa Inter Milan, Ivan Perisic.

Kuonesha ni kwa kiasi gani mwanasoka huyo wa kimataifa wa Croatia alikaribia kutua Emirates, tayari alishawaandikia barua mabosi wake wa Inter akiwaambia anataka kuondoka.

Kilichokwamisha mpango huo dakika za mwisho ni kwamba, wakati Arsenal wakiwa wanamtaka kwa mkopo, Inter waligoma, wakisema imnunue moja kwa moja.

Ni kama Gunners walikuwa na mkosi kwani hata usajili wa kiungo wa Kibelgiji anayekipiga China, Yannick Carrasco, ukiishia kuwa tetesi.

Klabu yake ya Dalian Yifang ilikuwa kwenye mazungumzo na Arsenal lakini ‘Washika Bunduki’ walikataa kutoa kiasi fulani kilichokuwa kikitakiwa na Wachina hao.

Bayern Munich nao waliambulia patupu katika harakati zake za kuifukuzia saini ya kinda mwenye umri wa miaka 18 katika klabu ya Chelsea, Callum Hudson-Odoi.

Mashabiki wa Blues walichimba mkwara waliposikia klabu yao inataka kumwachia Hudson-Odoi aende Bayern iliyokuwa imeshapeleka ofa nne Stamford Bridge.

Ukiacha kumhakikishia namba kwenye kikosi cha mwisho, kete ya mwisho ya Bayern ilikuwa ni kuitangazia Blues kiasi cha Pauni milioni 35 lakini ‘dogo’ amebaki Chelsea.

Dili jingine ni la Shinji Kagawa wa Borussia Dortmund kwenda Monaco. Kagawa aliyewahi kuichezea Manchester United, hana namba Dortmund, hivyo kutakiwa Monaco ilikuwa habari njema kwake.

Lakini sasa, dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, nyota huyo wa kimataifa wa Japan alijiunga na Besiktas, moja kati ya klabu kongwe huko Uturuki.

Idrissa Gueye naye alinukia PSG lakini mwishowe Msenegal huyo alibaki katika klabu yake ya Everton. PSG walimtaka Gueye kwa kuwa eneo lao la kiungo haliko sawa.

Marco Verratti na Lass Diarra ni majeruhi, huku Adrien Rabiot akionekana kutofurahia maisha klabuni hapo baada ya kukataa mkataba mpya.

Itakumbukwa kuwa ofa ya mwisho ya PSG iliyokataliwa na mabosi wa Everton ni ile ya kitita cha Pauni milioni 21 (zaidi ya Sh bil. 63 za Tanzania).

West Ham walikaribia kumpoteza mpachikaji mabao wao hatari raia wa Austria, Marko Arnautovic. Nyota huyo alikuwa akiwaniwa na Shanghai SIPG ya China.

Ofa nyingi za Wachina zilikataliwa lakini ya mwisho, ambayo ingemfanya mchezaji huyo awe anapokea mshahara wa Pauni 200,000 (zaidi ya Sh mil. 600 za Tanzania) kwa wiki, ilikuwa hatari zaidi.