Home Makala DK. HELEN KIJO BISIMBA: WATANZANIA TUSIOGOPE KUPIGANIA HAKI ZETU

DK. HELEN KIJO BISIMBA: WATANZANIA TUSIOGOPE KUPIGANIA HAKI ZETU

956
0
SHARE

NA HARRIETH MANDARI,

LINAPOTAJWA jina la Dk. Helen Kijo-Bisimba ni jina ambalo sio geni masikioni mwa wa Tanzania wengi hasa wale waishio vijijini kwa kuwa huwa mstari wa mbele kupitia Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC).

Wiki hii RAI imebisha hodi Dk. Bisimba ili kupata wasaaa wa kuzungumza naye kwa kina kuhusu jukumu la kituo hicho la kutetea haki hususani za wanawake.

RAI: Kwa kifupi watanzania wangependa kujua historia fupi ya safari yako ya kitaaluma hadi kufikia kuwa mtetezi wa  haki za binadamu.

HELEN: Nimezaliwa katika mkoa wa Kilimanjaro miaka ipatayo 63 iliyopita, ambapo mimi ni mchanganyiko wa makabila mawili baba yangu ni Mpare na mama ni Mchaga. Nilizaliwa huko huko Kilimanjaro na elimu yangu ya msingi niliipata katika shule ya Msingi ya  Majengo, nikaendela na elimu ya sekondari katika shule ya Weruweru (Awali ilijulikana kama Asunta College) na kuhitimu kisha nikachaguliwa kuendelea na elimu ya juu katika shule ya sekondari ya wasichana ya Korogwe mkoani Tanga.

Baada ya kumaliza elimu ya juu nilienda jeshini mwaka 1975  kwa mujibu wa sheria, ambapo ilikuwa ndiyo awamu ya kwanza katika mpango huo wa mafunzo ya ukakamavu nchini.

RAI: Baada ya kumaliza jeshi miezi sita ulibahatika kuajiriwa?

HELEN: Wakati huo sikupenda kuajiriwa moja kwa moja baada ya kumaliza elimu yangu kwa kuwa enzi hizo wale waliokuwa wakiajiriwa moja kwa moja walionekana kama vilaza (wavivu) badala yake niliamua kujiendelelza zaidi na nikajiunga na Chuo cha Ualimu cha Chang’ombe kwa ngazi ya stashahada.

RAI: Baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu ulianza kufundisha shule gani?

HELEN: Nilipata ajira katika shule ya masista ya Kurasini ambapo nilikuwa nafundisha somo la Kiswahili. Na baadaye nilihamia kufundisha katika shule ya sekondari ya Tambaza.

RAI: Ni nini kilikufanya ubadili taaluma kutoka kwenye Ualimu hadi Uanasheria 1985.

HELEN: Nilitaka kujiendelelza lakini nilifikia uamuzi wa kubadili fani kufuatia ushauri niliopata kutoka kwa walezi wangu hivyo kushawishika kusomea fani ya Sheria na nilibahatika kupata nafasi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kujiendelelza na fani ya sheria kwa ngazi ya Shahada kuanzia mwaka 1982 hadi 1985.

RAI: Kwa hiyo ulipomaliza ulianza kazi kama wakili?

HELEN: Hapana sikupenda sana kuwa mwanasheria kwani wakati wa mafunzo nilikuwa ninaona jinsi gani baadhi ya haki hasa za wasio na uwezo wa kifedha na waliokuwa wakikosa msaada wa utetezi walikuwa wakishindwa kesi kwa uonevu.

RAI: Unaweza kukumbuka ni kesi gani ambayo ilisababisha kushindwa kufanya kazi ya uanasheria au uwakili mahakamani?

HELEN: Sintosahau siku nilishuhudia moja ya kesi ambapo mtuhumiwa alikuwa daktari na mlalamikaji akiwa mwanamke ambapo daktari huyo alituhumiwa kumbaka mwanamke huyo aliyekuwa na hali mbaya na maumivu makali, na kwa kuwa alikuwa na wakili mzuri alitetewa kiasi ambacho unaona kabisa yule mwanamke ambaye alionekana kabisa kuwa alibakwa lakini aliishia kushindwa kesi, na alikuja kufariki siku mbili baada ya hukumu hiyo, hali hiyo ilinisononesha sana kwani napenda sana kuona haki za binadamu hasa kundi la wanawake na watoto wanatendewa haki zao za kibinadamu.

Aidha, baada ya kuhitimu masomo nilianza kufanya kazi katika Taasisi ya Elimu ya Watu wazima kitengo cha masomo ya sheria lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza hasa kwa upande ukosefu wa fedha za uendeshaji na vitendea kazi niliamua kutafuta ufadhili wa masomo  nchini Uingereza lakini nilishauriwa kusomea hapahapa kwa kuwa fani hiyo kwa ngazi ya Shahada ya pili (Masters) inapatikana hapa. Nilipata nafasi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kusoma kuanzia mwaka 1991 hadi 1994

RAI: Kwa hiyo uliamua kuwa mtoa huduma za kisheria kwa upande gani?

DK.HELEN: Niliona ni vyema kuwa mtetezi wa haki za binadamu kwa kuwa bado naipenda sana fani ya Ualimu niliona katika kituo kama LHRC patanifanya nifanye kazi kwa furaha kwani ninakuwa mwalimu ambaye anafundisha sheria kwa wananchi kwa vitendo zaidi, ninaweza kuonana na watu wazima ambao bado hawajui haki zao  hasa wa kipato cha chini na wenye uhitaji wa msaada wa kisheria moja kwa moja badala ya Ualimu wa  kufundisha watoto wadogo mashuleni pekee.

RAI: Ulijiunga na  LHRC mwaka gani?

HELEN: Mwaka 1996 wakati kinaanzishwa kituo hicho na mimi nilibahatika kuwa mmoja wa wajumbe wa bodi na mwaka huo huo nilichaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC.

RAI: Ni changamoto gani ambazo umeziona tangu uingie kwenye harakati  za kutetea haki za binadamu nchini?

HELEN: Kwanza kabisa watanzania wengi ambao tumekuwa tukiwasaidia ni vigeugeu unakuta mwanamke katendewa ukatili labda kupigwa au kubakwa inapokuja suala la kufungua kesi wanasema wanafuta kesi na kwamba wanamalizana nje ya mahakama jambo ambalo linazidi kumdidimiza mwanamke.

Changamoto nyingine ni utoaji na upokeaji rushwa ambapo walalamikiwa hutoa rushwa aidha kwa mahakimu au hata kwa walalamikaji

Vilevile kwa upande wetu sisi wanasheria watetezi tunapata vitisho kutoka kwa watuhumiwa hivyo kutuhatarishia maisha yetu. Pia jamii wakati mwingine huwa hawaelewi nia yetu wakati wa kutafuta haki kwa mfano ilipotokea mgomo wa madaktari nia ya kituo chetu ilikua kuishinikiza serikali kuwasikiliza madatari kilio chao ili kupata suluhu ya kudumu badala yake baadhi ya wananchi walianza kutuchukia na kusema kuwa tunasababisha wagonjwa wanakufa.

RAI: Ni tukio gani ambalo hutolisahau tangu ulipoanza majukumu yako?

HELEN: Sitosahahu matukio mengi tu lakini mojawapo ni lile la shauri la watoto wa Kimasai kule Morogoro ambapo walitoroka kukwepa kukeketwa, kisha kukimbilia kwa Padri mmoja aliyekuwa akitoa huduma kitongojini pale, katika harakati za kutafuta salama ya watoto hao hawakuwa wakikijua kituo cha LHRC hivyo walipeleka shauri wilayani na watendaji walilipeleka polisi.

Wakati huohuo, wazazi wa watoto hao walikimbilia polisi na kuripoti kuwa wametekwa na ndipo Polisi walimkamata Padri huyo na kumtesa kisha kuwarudisha watoto hao kwa wazazi wao ambao walikeketwa, hali ambayo ilinisononesha sana.

RAI: Kwa mtazamo na uzoefu wako hali ya uelewa wa haki za wananchi ukoje nchini?

HELEN: Uelewa umeongezeka ijapokuwa si sana lakini sasa wananchi wanajua ni hatua gani wachukue linapotokea tatizo la ukiukwaji wa haki za binadamu katika maeneo yao.

RAI: Ni kesi za aina gani ambazo mnaletewa kituoni?

HELEN: Kesi za migogororo ya ardhi zimekuwa nyingi sana siku hizi pia ukatili uliokithiri kwa wanawake na watoto.

RAI: Ni nini rai yako kwa watanzania kuhusu umuhimu wa kujua haki zao za msingi?

HELEN: Watanzania ni vyema tujiamini hasa inapotokea kupigania haki zetu, tusirudi nyuma, kwani unapoogopa kupigania haki yako si tu unaleta athari kwako na jamii inayokuzunguka, ila athari yake ni kubwa hata kwa kizazi kijacho.