Home Latest News Dk. Mabula: Najivunia kutumia miaka mitatu kutatua changamoto ya miaka 40

Dk. Mabula: Najivunia kutumia miaka mitatu kutatua changamoto ya miaka 40

693
0
SHARE
Mwenyekiti  wa Umoja wa Vijana wa  Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa,  Kheri  James, (kulia) , akimnadi mgombea wa ubunge jimbo la Ilemela kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk. Angeline Mabula hivi karibuni jimboni humo kwenye uzinduzi wa kampeni za jimbo hilo zilizofanyika uwanja wa sabasaba kata ya Ilemela.

NA CLARA MATIMO

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Ilemela  kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Angeline Mabula, ni mwanamke pekee aliyepata ridhaa ya chama chake kupeperusha bendera katika kugombea nafasi ya ubunge kati ya majimbo tisa yaliyomo mkoani Mwanza.

Dk. Mabula anatetea nafasi yake ya ubunge ambayo aliipata mwaka 2015, hivyo akaweza kuwatumikia wananchi wa Ilemela kwa kipindi cha miaka mitano huku pia akiwa Naibu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiwa Naibu Waziri.

Dk. Mabula ambaye ni miongoni mwa mawaziri waliopata bahati ya kutotumbuliwa wala kubadilishiwa wizara tangu walipoteuliwa na Rais Dk. John Magufuli mwaka 2015 baada ya kuapishwa na kutangaza baraza lake la mawaziri, anasema kilichomsukuma zaidi kugombea nafasi hiyo mwaka 2015 na kuacha wadhifa aliokuwa nao kama Mkuu wa Wilaya ya Butiama iliyopo mkoani Mara ni changamoto mbalimbali ambazo wananchi wa jimbo hilo walikuwa wakikabiliana nazo.

Pamoja na mambo mengine, anasema changamoto kubwa ilikuwa ni migogoro ya ardhi na baadhi ya maeneo kutokuwa na usafiri wa kuaminika wakiwemo wakazi wa Kisiwa cha Bezi-Kayenze kilichopo Ziwa Victoria.

Kila mara alikuwa akisikia taarifa za matukio ya boti na mitumbwi waliokuwa wanaitumia wakazi wa Kisiwa cha Bezi-Kayenze kuvukia kukumbwa na upepo ziwani hivyo kupinduka na kusababisha vifo.

Taarifa hizo zilimwumiza sana akawaza fursa pekee atakayoweza kuitumia ni kuwa mbunge wa jimbo hilo, ili awe mwakilishi wa wananchi hao ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akawasemee changamoto zao  kwa niaba yao.

Anaeleza vifo hivyo pia viliwahusu wanafunzi ambao walikuwa wakitumia usafiri huo wa mitumbwi na boti kwenda shuleni hivyo akiwa mama alihisi anaweza akafanya jambo kwa ajili ya kuokoa maisha yao na watanzania wengine.

 “Nakumbuka nilipoenda kuomba kura kwa wananchi wa Bezi-Kayenze, niliahidi endapo nitashinda nitawajengea kivuko kwa sababu taarifa za vifo na matukio ya kuzama vyombo walivyokuwa wakivitumia kwa usafiri ambavyo ni mitumbwi ya mashuka,  kasia, injini na boti ziliniumiza sana ahadi hiyo haikuwamo kabisa ndani ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

“Shauku niliyokuwa nayo ya kuhakikisha nawatatulia changamoto hiyo, ndiyo iliyonisukuma niseme kwamba nitawajengea kivuko kwa sababu ilikuwa ni mojawapo ya sababu zilizonifanya nigombee nafasi ya ubunge maana  niliamini CCM itashinda na rais atanielewa tu nikimweleza adhima yangu ya kuomba kivuko kwa kuwa Watanzania wengi wanapoteza maisha,”anasema.

Kwa sababu yeye huwa anaamini hakuna kitu kizuri duniani kama kuokoa maisha ya binadamu mwenzake, hivyo alimwomba Mungu kila wakati amsaidie ashinde ili akawatumikie watu wake.

“Hata nilipowaomba wanichague ili nikawajengee kivuko wananchi wenyewe wa eneo hilo, hawakunielewa nadhani walijua ni maneno ya wanasiasa hasa ukizingatia kwamba changamoto hiyo imedumu kwa zaidi ya miaka 40, lakini niliwahakikishia wanichague halafu wasubiri ndani ya miaka mitano waone,”anafafanua.

Mabula anasema baada ya kushinda uchaguzi alimfuata Rais Dk. John Magufuli akamweleza kuhusu ajali zinazotokea katika eneo la Bezi-kayenze ndani ya ziwa Victoria.

“Mheshimiwa Rais aliguswa sana akanikubalia ombi langu, akatenga Sh bilioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko cha wananchi wa kisiwa cha Bezi-Kayenze, niliamini sasa matukio ya vifo kutokana na kutumia usafiri wa boti na mitubwi yamefika mwisho,”anasema kwa furaha.

Anaendelea kufafanua kwamba changamoto hiyo aliitatua ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake, kivuko hicho kikaanza kujengwa ilipofika Februari mwaka huu Serikali ilikabidhiwa rasmi kivuko cha MV Ilemela kilichotengenezwa na Kampuni ya Songoro Marine  Transport Boatyard kwa gharama ya Sh bilioni 2.7 kwa ajili ya wananchi wa kisiwa cha Bezi-Kayenze mkoani Mwanza.

Kwa mujibu wa Mabula kivuko hicho kina  urefu wa mita  37, upana mita 10 na kitaelea ndani ya maji kati ya mita 0.75  hadi 1.4 kina uwezo wa kubeba tani 100 yaani abiri 200,  magari 10 na mizigo kwa wakati mmoja.

Kivuko hicho kina uwezo wa kufanya safari zake kati ya Mwanza-Ukerewe kupitia kisiwa cha Bezi na Kisorya, lakini cha faraja zaidi kwa watumiaji ni kwamba gharama za usafiri ni nafuu zaidi maana watatumia Sh 2,000 badala ya Sh 5,000 hadi 7000 walizokuwa wakitumia awali kwenye usafiri wa mitumbwi na boti.

“Huwezi amini siku hiyo pia ni miongoni mwa siku nilizofurahi sana, hakuna kitu kizuri kama kutimiza ahadi kwa binadamu mwenzako hasa ile ambayo kwake ni changamoto kubwa.

“Pia kivuko hicho ni miongoni mwa sababu zilizonifanya niombe ridhaa kwa chama changu kugombea, furaha zaidi niliipata kuona nimetekeleza ahadi ambayo haikuwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya chama changu.

“Ombi langu kwa wananchi wa Jimbo la Ilemela na Tanzania nzima wasihangaike kabisa kuchagua wagombea wa upinzani Oktoba 28 mwaka huu, wachague mafiga matatu kutoka CCM yaani rais, wabunge na madiwani ili tumrahisishie kazi Dk. Magufuli kuzidi kutuletea maendeleo, ni kiongozi msikivu.

“Hili limejidhihirisha pia kwenye ombi langu kwa kuwa ujenzi wa kivuko haukuwa kwenye ilani ya CCM, nilipoenda kumwomba awajengee wananchi wa Bezi-Kayenze kivuko hicho angeweza kukataa,”anabainisha.

Anasema ujio wa kivuko hicho umefungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo, kibiashara maana wana usafiri wa uhakika wa kutoka eneo moja kwenda lingine kufuata au kupeleka bidhaa mbalimbali za biashara.

Anasema wanafunzi nao sasa wanaenda shuleni wakiwa hawana hofu yoyote wana uhakika wa kwenda na kurudi katika makazi yao.

“Ahadi nyingine ninayojivunia kwa kipindi cha miaka mitano ya uwakilishi wangu wa wananchi wa Jimbo la Ilemela bungeni ni kutatua migogoro sugu ya ardhi, namshukuru Rais Dk.  Magufuli kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, niliitumia vizuri fursa hiyo jimbo letu linaongoza katika zoezi la urasimishaji makazi nchini.

Mgombea huyo anayetumia kauli mbiu ya ‘Ilemela ni yetu tushirikiane kuijenga’  anasema alipoingia madarakani alikuta jimbo hilo lina migogoro sugu ya ardhi zaidi ya 12 ambayo ilikuwa ina miaka zaidi ya 15  haijapatiwa ufumbuzi.

Kama kawaida yake alimfuata Rais Dk. Magufuli akamueleza kero hiyo naye akaahidi kuipatia ufumbuzi, akatoa zaidi ya Sh bilioni 3 zilizotumika kuwalipa fidia wananchi wa Ilemela na Nyagungulu.

“Leo hii ninapozungumza na wewe wananchi wa Lukobe na Nyanguku ambao maeneo yao yalikuwa yamechukuliwa na jeshi la wananchi wameishaanza kulipwa Sh bilioni 6 zimetengwa kwa ajili yao.

“Tulikuwa na mgogoro sugu eneo la mlima wa kigoto  wananchi kaya 614 walikuwa wameamliwa kutoka kwa sababu ni eneo la jeshi la  polisi, lakini Rais Dk. Magufuli aliagiza watu hao wamilikishwe na wafanyiwe zoezi la urasimishaji hadi sasa kazi hiyo tunaendelea kuifanya kwa hiyo hawatahama kwa ufupi nimetatua migogoro ya ardhi katika jimbo hili kwa asilimia 98.

“Niwape matumaini na matarajio makubwa wananchi na kata ambazo zilijengwa shule za kata miaka ya 2007, hii ni zaidi ya miaka 13 ambao walikuwa hawajalipwa fidia zao mwaka huu watalipwa, mwezi huu watalipwa watu wa Nyamanoro, Isenga na Nyamwilekelwa, haya yote yamefanikiwa kwa sababu waliniamini wakanichagua na Mheshimiwa Rais akanichagua kuwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Dk. Mabula anasema ahadi zingine zikiwemo barabara, elimu na afya amezitekeleza kwa kiwango cha juu kwa sababu zilikuwemo ndani ya ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020.

Kwa upande wa barabara anasema ndani ya miaka mitano amefanikisha kujenga kilomita 35 za lami na taa zinawaka pia amefungua njia za changarawe kilomita 51.

“Hizi barabara zimefunguliwa si kwa mfuko wa jimbo wala fedha za Dk. Magufuli ni kwa juhudi ya wananchi wenyewe wakishirikiana na mimi mbunge wao kazi hiyo tumeifanya chini ya uongozi wa madiwani na wenyeviti wa mitaa.

Mgombea Ubunge Jimbo la Ilemela, Dk. Angeline Mabula, akiwa katika mikutano yake ya kampeni jimboni humo hivi karibuni. wananchi hawapo pichani.

“Kwenye bajeti ya mwaka huu kilomita 27 za barabara tayari zimeingizwa kwenye mzunguko wa kukarabatiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(Tarura),”anafafanua.

Kwa upande wa elimu anasema baada ya kujadiliana na wananchi kuhusu umuhimu wa kuongeza shule wakazi hao wa Ilemela wamechangia zaidi ya Sh milioni 311 kuhakikisha miundombinu ya majengo ya shule inaendelea ambapo wamefanikisha kujenga shule tatu mpya za sekondari na tatu za msingi.

Anasema baada ya kuboresha miundombinu ya elimu Wilaya ya Ilemela imeshika nafasi ya kumi bora kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mara mbili ambapo mwaka  2018 ilishika nafasi ya sita na mwaka 2019 ilishika nafasi ya pili.

“Lakini tuliweka ahadi baada ya Dk. Magufuli kufanya ukarabati katika shule kongwe za sekondari za Serikali watoto waliahidi wanafuta sufuri na  kupunguza daraja la nne, mwaka huu tuna division one 122 Bwiru girls,  tuna division two 155, division three 95 na four watatu hatuna zero.

“Hii yote imetokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika sekta ya elimu, wengi wamefaidi elimu bure bila malipo tumeletewa zaid ya Sh bilioni  2.7 katika shule za msingi na bilioni 7.3 shule za sekondari, pongezi nyingi ziende kwa walimu ambao wanazisimamia vizuri sana fedha hizo.

Anasema kwa upande wa afya, wamefanikiwa kuboresha Kituo cha Afya Buzuruga kwa gharama ya Sh milini 400 pamoja na kuwepo uhakika wa dawa katika hospitali za Serikali.

Kuhusu kuwainua wananchi kiuchumi, anasema wakati anaingia madarakani alikuta fedha inayotolewa katika mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ilikuwa haizidi Sh milioni 220 lakini sasa wanapata Sh bilioni 1.4.

Kwa mujibu wa Dk. Mabula zaidi ya vikundi 112 vya vijana wameishachukua fedha zaidi ya Sh milioni 286, vikundi 414 vya wanawake wameishakopeshwa zaidi ya Sh bilioni 1.1 na watu wenye ulemavu wamekopeshwa Sh milioni 33.

Analishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutunga sheria  ya kuzitaka kila halmashauri kutenga asilimia kumi kwa ajili ya makundi maalumu, hiyo imesaidia kuufanya mfuko huo uwe wa kisheria zaidi kwa sababu awali baadhi ya wakurugenzi walikuwa hawatimizi takwa hilo hivyo kuwanyima haki wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia mapato ya ndani ya maeneo yao lakini sasa madiwani hawawezi kupitisha matumizi yoyote bila kuona asilimia kumi zilizotengwa kwa ajili ya vijana asilimia nne, wanawake asilimia nne na asilimia mbili watu wenye ulemavu.

“Si jambo dogo kupata mkopo wa Sh bilioni 1.4 kutoka Sh milioni 220  hili kwangu ni faraja kubwa sana, unapoona watu wako unaowatetea wanafanikiwa lazima ufurahi kwa sababu lengo la mbunge yeyote anayeingia madarakani akiwa na nia ya kuwawakilisha wananchi wa eneo husika hawaweki mbele masilahi yake anaangalia ya watu wake kwanza,”anasema.

Anasema ujenzi wa stendi kubwa ya mabasi na malori katika eneo la Nyamhongolo itakayogharimu Sh bilioni 28 imetoa ajira zaidi ya 200, ombi lake ni wananchi kuwaamini wagombea wa CCM maana wanadhamira ya dhati ya kuendeleza taifa.

“Wananchi wote wameshiriki katika kulifikisha taifa kwenye uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025, niwaombe waniamini mimi ni kiungo mchezeshaji ninacheza mbele ninacheza nyuma kuhakikisha napokea kutoka kwa Rais Dk. Magufuli nashusha kwa diwani, naye anafikisha kwa mwenyekiti wa mtaa unawafikia wananchi kazi zinasonga mbele.

“Nitumieni sita ni ya kwangu nane ni ya kwangu kiungo mshambuliaji ambaye pia nina uwezo wa kuzuia magoli yasiingie,”anasema.

Anaeleza kwamba Wilaya ya Ilemela ina kilomita za mraba 1080 lakini zaidi ya asilimia 80 ni eneo la maji hivyo wakazi wengi wanajishughulisha na uvuvi kwa hiyo tayari Sh milioni 250 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha mialo mitatu  ya samaki ambayo ni  Kayenze, Igombe na Miham lengo ni kuwa na uvuvi endelevu.

Mbali na kuboresha mialo hiyo pia Sh milioni 50 zimeishatengwa kwa ajili ya kutoa mafunzo  kwa wavuvi ya ufugaji wa vizimba  ili wavue muda wote bila kutegemea mwanga wa jua, mwezi au urefu wa kina cha samaki.

“Unapokuwa na uwekezaji mkubwa katika maeneo ni wazi maendeleo ya haraka yanapatikana wavuvi tumewaboreshea miundombinu ikiwemo upanuzi wa uwanja wandege sasa wanasafirisha samaki zao moja kwa moja bila kupita nchi jirani,”anaeleza.

Anasema anaielewa vizuri miradi hiyo  kwa sababu aliwaahidi wananchi mwaka 2015 alipoenda kuwaomba kura, anatambua wazi kwamba wavuvi wakitegemea  uvuvi ndani ya ziwa viktoria itafikia mahali samamki zitakwisha na hakutakuwa na uvuvi endelevu familia zao zitahangaika ndiyo maana akahakikisha miradi hiyo inapatikana.

“Nitumie fursa hii kuwaomba sana wananchi wakisikia mafunzo yameanza kutolewa waende wakajifunze ufugaji wa vizimba ili tuwe na uvuvi endelevu unapofuga kwa vizimba utajua umepanda vifaranga lini na unavuna baada ya muda gani

“Huo unakuwa ufugaji endelevu sio ule wa kutegemea leo mvua imenyesha sana samaki zimepotea leo kuna giza dagaa wapo wengi, kuna mwanga dagaa hakuna,”anasema.

Mabula anasema hapendi mtu yeyote anayedharau jinsia ya kike wakati wanawake ni walezi wakubwa waf amilia, ndiyo wanaokesha na mtoto tangu akiwa mdogo hadi anapokuwa na  wanahakikisha wanampa malezi yaliyo bora.

Anasema kitu anachokipenda ni haki,  amani, kusaidia kutatua changamoto za binadamu wenzake ambazo ziko ndani ya uwezo wake na kushirikiana na jamii katika masuala ya maendeleo.

Anaeleza kwamba katika uongozi wake akiwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeo ya Makazi hajakutana na changamoto nyingi kwa ajili ya jinsia yake kwa sababu alifanya kazi kwa weledi pia alisikiliza na kufuata ushauri alioona unafaa kwa masilahi ya taifa alipopewa na watu mbalimbali.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kisiwa cha Bezi –Kayenze kilichopo Ziwa Viktoria, wanasema hawakuamini walipoona ujenzi wa kivuko hicho umeanza walijua hizo ni njia za wanasiasa kuwadanganya wananchi ili muda wa uchaguzi utakapofika wawahadae wawapigie kura kwa kusema kwamba wameanza ujenzi.

Maganga Simon na Getruda Mateso wanasema hawakutarajia  kama watakuwa na kivuko cha kisasa chenye kutoa huduma za usafiri wa majini za uhakika  maana wameteseka zaidi ya miaka 40 kila kipindi cha uchaguzi kilipofika wagombea walienda kuwahadaa na sera hiyo kwamba wakiwachagua watawajengea kivuko lakini baada ya kushinda hawakutekeleza ahadi hiyo.

“Zaidi ya miaka 40 tumekuwa tukitumia usafiri wa mitumbwi ya mashuka, mitumbwi ya kasia, mitumbwi ya injini na boti,  usafiri huu umesababisha tupoteze ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi sana kwa kweli Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mungu ambariki kwa kadri amuombavyo,”anasema Getruda.

Simon yeye anamshukuru Mabula huku akibainisha kwamba sasa anauhakika wa kwenda  Bezi  kufanya shughuli zake za uzalishaji na kurudi Kayenze bila mashaka yoyote kwa sababu kuna usafiri wa uhakika.