Home Habari kuu Dk. Mahiga ni mfano wa viongozi kuhimili vishindo vya wanahabari

Dk. Mahiga ni mfano wa viongozi kuhimili vishindo vya wanahabari

735
0
SHARE

JAVIUS KAIJAGE

MIONGONI mwa mambo ambayo wanasiasia na viongozi wengi hupata changamoto, ni namna ya kuhimili vishindo na mihemuko ya waandishi wa habari, hasa wakati wanapokuwa wanahitaji habari ya kuujuza umma juu ya masuala fulani.

Kushindwa kwa wanasiasa na viongozi katika kustahimili majukumu ya waandishi wa habari au vyombo vya habari, hutokana na hofu inayozaliwa na kutojiamini.

Hata hivyo, kuna suala la kujiuliza kwamba hofu hiyo ya viongozi na wanasiasa inayozaliwa na kutojiamini chanzo chake halisi ni nini?

Ni vigumu kutambua chanzo chake, lakini zipo sababu kadhaa ambazo wanasiasa au viongozi hujikuta ni maadui kwa waandishi wa habari au vyombo vya habari.

Kwanza ipo dhana imejengeka kuwa ili kiongozi aongoze vizuri, ni lazima ahakikishe kuwa waandishi wa habari au vyombo vya habari havipati fursa ya kutangaza habari zake.

Pili viongozi au wanasiasa walio waoga huwa hawapendi kuwapa nafasi waandishi wa habari waweze kuwakosoa na hatimaye kurudi kwenye mstari.

Wanasiasa au viongozi wenye kutojiamini katika maamuzi, huwa hawapendi vyombo vya habari vyenye kuhoji mara kwa mara hasa linapokuja suala la masilahi binafsi.

Hizo zikiwa ni sababu chache kati ya nyingi ambazo huwafanya wanasiasa wawachukulie waandishi wa habari kama simba, bado wapo wenye uwezo wa kuwachukulia kama fursa au bidhaa hadimu na mfano mmojawapo ni Balozi Dk. Augustine Mahiga.

Dk. Mahiga akiwa ni msomi aliyebobea katika masuala ya uhusiano wa kimataifa, amebahatika kutumia taaluma yake ipasavyo kwa kufanya shughuli za kimataifa kwa muda mrefu na hivyo kujijenga.

Mbali na taaluma, lakini ni dhahiri historia ya msomi huyu imetukuka sana na vigumu kuiilezea na kuimaliza kwani kutokana uadilifu wake usio na shaka, alianza kuwa mtumishi wa umma tangu awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere kwani mwaka 1975 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya kuhitimu shahada yake ya uzamivu (PhD) alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Na sasa akiwa na umri wa takribani miaka 74, Dk. Mahiga anaendelea kufanya kazi katika Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Joseph Magufuli akiwa ni Waziri wa Sheria na Katiba akitokea Wizara ya Mambo ya Nje.

Kwa wanaomfahamu vizuri Dk. Mahiga, wanasema ni kiongozi msikivu, asiyekurupuka katika ulimi na matendo yake, anayejiamini, lakini pia akiwa ni mwenye huruma, sifa ambazo kimsingi humfanya awe mtu wa watu wakiwemo waandishi wa habari.

Uwezo wake wa kuzungumza na kujenga hoja kwa kujiamini humfanya awe tayari kukabiliana na maswali ya waandishi wa habari, hasa wanapokuwa wanahitaji kujuzwa suala fulani kwa manufaa ya umma.

Ikumbukwe kuwa wakati mwingine waandishi wa habari huwa wana maswali yenye mtego au yenye kuudhi na hivyo kwa kiongozi asiyejiamini na mwenye fikra za kuhisi kudharauliwa,  hujikuta akiangukia katika mtego wa ubabe badala ya kutumia akili kupangua hoja au maswali yaliyoko mbele yake.

Dk. Mahiga kutokana na kutulia kwake kunakomwezesha kufanya tafakuri tunduizi, humfanya asiweweseke wakati anapojibu maswali ya waandishi wa habari na hii ni kwa mujibu wa wanaomfahamu kwa karibu.

Inasemekana Dk. Mahiga hakurupuki katika ulimi wake kwani kwa kila utakalomuuliza lazima aweke ‘Why? What? When? Where? Which? na Who’?

Mimi binafsi nikiwa katika shughuli zangu za kitaaluma, nilibahatika kukutana na Dk. Mahiga mwaka huu alipokuja Mwanza katika ziara ya shughuli za Serikali baada ya kuwa ameishateuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Ni dhahiri ukimsikiliza anapokuwa akiongea na wananchi au waandishi wa habari, utabaini ya kwamba ni kiongozi mwenye vitu vya pekee na ziada.

Aonyeshi sura ya kukasirika au kuhamaki hata akiulizwa kuhusu suala lolote linalohusu Serikali au yeye binafsi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya ustawi wa jamii, kila binadamu ni mpekee na ni wa aina yake na hivi ndivyo ilivyo kwa Dk. Mahiga.

Inaweza kuwa vigumu kumfananisha Dk. Mahiga na wengine, lakini kuna haja ya viongozi kubadilika katika zama hizi za utandawazi.

Nasema kuna haja ya kubadilika kwa maana ya kwamba yapo masuala ya kimazingira ambayo si ya kimaumbile, kwamba kwa binadamu mwenye akili timamu anaweza akajifunza kama si kuiga.

Hivi kama Dk. Mahiga ni kiongozi wa aina hii kwanini viongozi wengine wasiige au kujifunza nyendo zake?

Inashangaza kuona kiongozi anajenga uadui na vyombo vya habari au waandishi wa habari kisa amekosolewa.

Inatia huruma kiongozi kumchukulia mwandishi wa habari kama adui kisa kafichua habari za rushwa, ufisadi na kujilimbikizia mali.

Ni usaliti ulioje kiongozi kushindwa kutoa taarifa kwa mwandishi wa habari kisa anahofia mambo yake mabaya yatawekwa hadharani na hivyo kuziba riziki.

Ni dhambi kubwa kwa kiongozi kumtafutia mwandishi wa habari makosa ya kubambizia kisa katangaza au kuandika habari ambazo ni kinyume na mtazamo wake.

La kujiuliza hapa ni kwamba iweje mwandishi wa habari akiandika habari zenye kumsifia kiongozi hata kama ni za uongo hachukuliwi hatua, lakini akiripoti habari zilizo kinyume atafuatiliwa sana hata kama habari hizo ni za kweli.

Viongozi wakiondoa dhana ya kwamba ili wananchi waongozwe vizuri ni lazimua wafichwe habari fulani, itawasaidia kuwachukulia waandishi wa habari watu wema wanaowasaidia kufanikisha shughuli zao.

Ni dhahiri maendeleo ya nchi huwa makubwa pale wananchi wanapopewa habari sahihi na kwa wakati sahihi na sehemu sahihi, na ndiyo maana mataifa mengi yaliyoendelea uhuru wa habari unalindwa kwa gharama yoyote ile hata kama bado kuna vizingiti kadhaa kutokana na sababu mbalimbali.

Katika karne hii ya sayansi na tekonolojia ambayo wananchi wana uelewa mkubwa katika masuala yahusuyo maisha yao, hakuhitajiki viongozi wanaoogopa vyombo vya habari, waandishi wa habari au kutoa taarifa sahihi.

Kama Dk. Mahiga anaweza  kumsaidia vizuri  Rais Magufuli, huku akihimili vishindo vya waandishi wa habari, naamini  hata viongozi wengine wanaweza kufanya hivyo.