NA SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM
JUMAMOSI iliyopita, Klabu ya Yanga ilifanya harambee kubwa ya kuchangisha fedha iliyopewa jina la ‘Kubwa Kuliko’, kwa ajili ya kutumika kufanya usajili wa wachezaji wa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.
Kwa hakika lengo kuu la harambee hiyo, lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa, kwani wapenzi na wasio wapenzi wa klabu hiyo, walionekana kuitikia kwa kutoa michango ya fedha taslimu na ahadi.
Wazo la kufanya harambee hiyo lilikuja, baada ya klabu hiyo kupitia nyakati ngumu kiuchumi, tangu aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuph Manji alipoamua kujiweka kando na kiti hicho.
Mkwamo huo wa kiuchumi ulioikumba Yanga kwa misimu miwili mfululizo, ulisababisha ishindwe kumudu kulipa mishahara ya wachezaji na wafanyakazi wengine wa klabu hiyo kwa wakati , lakini pia kutokuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wenye ubora wanaoendana na hadhi ya klabu hiyo.
Kwa hakika hili liliisumbua sana Yanga, na kibaya zaidi upande wa pili yaani kwa wapinzani wao Simba, mambo yalionekana kuwa mazuri tangu ilipoamua kuhama kutoka mfumo wa umiliki wa kadi za uanachama hadi kuwa umiliki wa hisa ambao uliotoa fursa kwa bilionea na mwanachama wake, Mohamed Dewji ‘Mo’ kuwekeza.
Hali hiyo mbaya ya kiuchumi, pia imesababisha Yanga kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu miwili mfululizo, huku pia ikinusurika kukosa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa, kabla ya kufanikiwa kuipata, baada ya Shirikisho la Soka Afrika(CAF), kuipa Tanzania nafasi nne za uwakilishi katika mashindano yake.
CAF imetoa nafasi hiyo, baada ya Simba kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo ilifika hatua ya robo fainali, kabla ya kutupwa nje na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo(DRC). Yanga kupitia bahati hiyo, iliyotokana na jitihada za Simba, itashiriki ligi ijayo ya Mabingwa Afrika.
Lakini kupitia harambee ya Kubwa Kuliko, Yanga ilifanikiwa kuvuna mamilioni ya fedha.
Bahati nzuri tukio lenyewe lilionyeshwa moja kwa moja yaani ‘Live’ kwenye televisheni, hivyo kila kitu kilikuwa wazi.
Kupitia harambee hiyo, ni dhahiri mashabiki, wapenzi, wanachama na wadau wengine wa soka,watakuwa na matumaini mapya ya kuiona Yanga iking’ara upya katika ligi ya ndani na kimataifa.
Ifahamike kwamba, katika misimu hii miwili migumu ambayo Yanga imekumbana nayo, timu hiyo ilikuwa ikijiendesha kwa kutegemea fadhila za michango ya wapenzi wake, pamoja na udhamini mdogo ambao hata hivyo haukuwa unakidhi mahitaji.
Lakini harambee ya Kubwa Kuliko imeonekana kama mkombozi wa kurudisha furaha za wapenzi wa Yanga.
Hiki kilichofanywa na wapenzi wa Yanga na wadau wengine wa soka cha kuitikia kwa nguvu wito wa kuichangia timu hiyo, nina kitafsiri kama deni kwa uongozi wa klabu hiyo, chini ya mwenyekiti wake Dk Mshindo Msola.
Ukiondoa wachache, naamini wapenzi wengi wa soka walioichangia Yanga ni watu wenye vipato vya kawaida tu na sio matajiri.
Kilichowafanya kwa moyo mmoja kutoa fedha zao na kuichangia ni mapenzi yao kwa mchezo wa soka na kwa klabu hiyo.
Kikubwa wanachosubiri au kukihitaji baada ya kujitoa kwao kuichangia klabu hiyo ni kuishuhudia ikiwa ikicheza kwa kiwango bora lakini pia ikipata matokeo mazuri dimbani.
Kama hivi vitu viwili watavipata, maana yake vitawafanya wawe na furaha na kutojutia fedha zao walizo changa.
Lakini tofauti na hapo, uongozi wa Dk Msola na wenzake ujiandae kuhojiwa na wale waliojitoa kuichangia klabu hiyo fedha.
Pia itashangaza kama uongozi wa Dk Msola utaibuka tena na kuomba michango kutoka kwa wapenzi wake na wadau wengine wa soka badala ya kutafuta njia nyingine ya kupata suluhisho la kudumu.
Ukweli ni kwamba, fedha zilizochangwa na wapenzi wa klabu hiyo pamoja na wadau wengine wa soka ni suluhisho la muda mfupi, haziwezi kutosheleza kuendelea shughuli za kila siku za klabu hiyo, hivyo ni wajibu wa uongozi wa Dk Msola na wenzake kubuni vyao vingine vya mapato na kuvisimamia ili kuhakikisha hali inaendelea kuwa nzuri.
Hili lililofanywa katika harambee ya Kubwa Kuliko litumike kama kianzio tu cha mapambano ya kusaka fedha zaidi kupitia fursa tofauti ilizonazo klabu ya Yanga.
Hakika kama hili litafanikiwa, naamini hakuna mpenzi wa soka wa klabu ya Yanga atakayetamani kuhoji ziliko fedha zilizochangwa kupitia harambee ya Kubwa Kuliko, kwakua kile alichokuwa anakitarajia atakuwa amekipata.