Home Makala DK. SEMBOJA: BENKI ZINAPITIA KIPINDI CHA MPITO TU

DK. SEMBOJA: BENKI ZINAPITIA KIPINDI CHA MPITO TU

541
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE

BENKI nyingi nchini sasa zinapitia kwenye kipindi kigumu cha uendeshaji hali ambayo imepelekea kuwapo kwa mabadiliko makubwa kwenye utoaji wa huduma zake zikiwa na lengo la kujinasua.

Itakumbukwa mapema mwaka huu mataifa kama Kenya na kwingine yalikumbwa na msukosuko huu wa kuporomoka kwa mabenki na hivyo kujikuta nyingine zikipunguza wafanyakazi huku baadhi zikifungwa kabisa.

Hali hiyo ndiyo iliyopo pia nchini sasa jambo ambalo linatazamwa na wataalamu wa mambo ya uchumi kama ni ya mpito tu kama anavyofafanua, Mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja.

Mtazamo huu wa Dk. Semboja unakuja ikiwani ni miezi kadhaa tangu baadhi ya benki hapa nchini ikiwamo CRDB kutangaza kusitisha utoaji mikopo kwa baadhi ya makundi ili kuweza kujinusuru.

Mbobezi huyo wa Uchumi anasema kuwa kuanguka kwa mabenki siyo nchini tu bali hata kwenye kwenye mataifa makubwa hali si shwari.

Dk. Semboja anabainisha baadhi ya athari za  kuyumba kwa mabenki hapa nchini zilianza kuonekana mara tu baada ya kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Hata hivyo anaielezea kuwa hali ya kiuchumia inaweza kubadilika kulingana na maendeleo ya nchi na dunia kwa ujumla.

Ambapo hilo linapimwa kwenye maeneo mengi yakiwamo yale ya uzalishaji na mengine.

“Kutetereka kwa maeneo kama ya utalii, idadi kubwa ya watu wasio na ajira, kuyumba kwa biashara ikiwamo usafiri wa anga, kupunguza wafanyakazi na kuwapo kwa mdororo wa pato la taifa ni moja ya mambo ambayo yanafanya nchi kupitia kipindi hiki kigumu hasa mabenki.

“Hii inatokana kwamba serikali imeamua kuziondoa fedha zote na kuziingiza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini baada ya muda itazirejesha tena kwani haiwezi kusimama yenyewe bila kuwepo kwa sekta binafsi.

“Hivyo hiki ni kipindi cha mpito ambacho benki zinapitia lakini baada ya muda zitarejea kwenye hali yake ya kawaida,” anasema Dk. Semboja.

Dk. Semboja anabainisha kuwa, ishara ya kuwapo kwa tetemeko hilo la kiuchumi ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwenye sekta ya benki na kifedha kwa ujumla zimekuwapo tangu mwishoni mwa mwaka jana ambazo zinahusisha kupungua kwa ajira na kupungua kwa vipato vya wananchi.

“Ni wazi kuwa kwenye sekta nyingi hasa zisizo rasmi nchini ni lazima zikumbe na hakli ngumu ya kifedha ilinganishwa kuwa ni eneo ambalo wengi wamewekeza.

“Hivyo tunatazamia kuwa baada ya kipindi kifupi cha serikali kukamilisha mikakati yake ni lazima kutakuwa na hali njema ya kiuchumi ikiwamo kuboreshwa kwa huduma za kibenki kwani serikali ni lazima itarejea kushirikiana nao bega kwa bega.

“Hivyo sasa ni lazima tutaendelea kuona miamala ya simu ndiyo ikichukua nafasi zaidi kushinda mabenki licha ya ukweli kuwa hali hii itaimarika baadaye,” anasema Dk. Semboja.

Upande mwingine, Dk. Semboja, anatazama athari nyingine ambazo zinaweza kutokea kwasasa kutokana na hali hii ya kiuchumi kuwa ni kuendelea kushamiri kwa vitendo vya, uhalifu, na tabia mbaya za ulevi na utamaduni wa kisasa.

Huku akifafanua hali ya benki nyingi kushindwa kutoa mikopo kwa wanchi kwasasa.

“Kwasasa ni kweli kuwa benki haziwezi kutoa miko[po kulingana na changamoto ya uendeshaji wa biashara kwa wateja wake hivyo inakuwa ni ngumu mno kuweza kurejesha mkopo husika.

“Hivyo kumekuwapo na hali ya hofu kubwa ambayo imetanda kwenye benki nyingi sasa ambayo itaenda kwa kipindi fulani kisha itarejea kwenye hali ya kwaida,” anaema Dk. Semboja.

Anabainisha kuwa kufuatia kushuka kwa bei na wingi wa uzalishaji wa bidhaa za kilimo cha biashara za nje ya nchi, ni wazi kuwa pato la Serikali, Pato la Taifa (GDP), kupungua kwa ajira na kuongezeka kwa umasikini ni mambo yatakayoliumiza taifa kwasasa.

“Ni vema kutambua kuwa pamoja na kuwa Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama nyingi, pwani nzuri, kisiwa cha Zanzibar na Pemba, utalii wetu uko chini, mdogo na ukuaji wake ni dhaifu ukilinganisha na nchi kama vile Kenya na Afrika Kusini.

“Sababu kubwa ya utalii duni hapa nchini ni pamoja na kuwa na miundombinu mibovu, kodi kubwa, huduma na bei mbaya za hoteli na usafiri na gharama kubwa kwa watalii.

“Hivyo, mtikisiko wa kiuchumi utaweza kuwa na athari kubwa katika maeneo ambayo watalii wataona kuwa fedha zao hazitapata huduma bora wanazohitaji.”

Pia kuna maeneo mengine yanyodhorotesha mabenki nkama kushuka kwa bei za madini na kupunguka kwa mahitaji vimeathiri shughuli za uchimbaji, biashara na uwekezaji katika sekta hiyo.

Kwani baadhi ya kampuni za uchimbaji wa dhahabu zimeanza kupunguza shughuli na ajira kama mikakati ya kupunguza gharama za uendeshaji.

“Hali ikiwa mbaya zaidi kwenye nchi kama, Marekani, Ulaya, China na India zinaweza kusitisha uwekezaji wa moja kwa moja nchini kwa kuhofia kupotea kwa mitaji na kupata hasara, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania haina mazingara endelevu ya uzalishaji na kibiashara.

Dk. Semboja anabainisha kuwa hali ya mpito inayoyakabili mabenki siyo ya ndani tu bali hata ya kigeni pia yanapaswa kuchukua tahadhari.

“Mabenki ya biashara ya kigeni yaliyomo nchini yameanza kupata joto la kutakiwa kuwa makini katika kutoa mikopo midogo kwa ajili ya shughuli za biashara ndogondogo hapa nchini.

“Hapo awali walikuwa wepesi kutoa mikopo aina ya msaada kwa ajili ya sekta binafsi inayoendeshwa na wazalendo, tofauti na sasa. Hii itachangia kusimamisha uwekezaji wa wazalendo kwa ajili ya maendeleo yao.

Hivyo kwa vyovyote ni lazima benki na watanzania watambue kuwa kipindi hiki nichampito tu kwani uchumi ni lazima utaimarika na kurejea kwenye hali yake licha ya ukweli kuwa itachukua muda kuweza kulifanikisha hili.