Home kitaifa Dk.Tulia umeletwa kuua Demokrasia?

Dk.Tulia umeletwa kuua Demokrasia?

951
0
SHARE

tulia katuniTANGU Dk. Tulia Ackson alipozawadiwa ubunge wa kuteuliwa na Rais John Magufuli nilianza kupata shaka kuhusu utendaji wake kama ataweza kusimamia majukumu yake kwa haki.

Shaka yangu haihitaji mtu mwenye shahada ya chuo kikuu kutafakari ilikuwa ni ngumu kwa Dk. Tulia kusimama kidete kuisimamia serikali kwa haki kwa maana kwamba bila upendeleo.

Ni ngumu mtu kupewa cheo cha hisani na kupambana kutetea haki za wanyonge dhidi ya mteuzi wako aliyekuwezesha kushika wadhifa husika.

Niliamini kabisa kile anachokifanya Dk. Tulia cha kuwabana wabunge wa upinzani ni kulinda maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ya Magufuli kingetokea.

Hilo linadhihirisha kwamba kila jambo linaloletwa huletwa kwa mkakati hivyo ujio wa Naibu Spika huyo haukuwa wa bahati mbaya bali mkakati anaoutimiza hivi sasa.

Ingekuwa jambo la kushangaza iwapo Dk. Tulia angeweza kusimamia haki wakati akijua kabisa ameteuliwa kwa kazi ya kukilinda Chama tawala ambacho kimekuwa kikipoteza umaarufu siku hadi siku tangu kuasisiwa kwake.

Ulipaji wa hisani umemfanya Dk. Tulia kuonekana kama kiongozi mwenye upande hali inayoashiria udhaifu anapokuwa amekalia kiti cha uspika.

Tangu alipoteuliwa amekuwa akifanya mambo mbalimbali yanayoashiria kuvunja sheria na kanuni za Bunge hali inayozua maswali mengi.

Wapo baadhi waliokuwa wakihoji huenda ni ugeni wake katika nafasi husika aliyopewa au ni makusudi ya kulinda serikali badala ya kuisimamia kama madhumuni yanavyotaka.

Amekuwa akiwapendeleo wabunge wa chama chake moja kwa moja huku akijua kuwa anavunja kanuni ya 8 (b) inayokataza upendeleo sambamba na kanuni ya 5 (1) inayomtaka Spika kuzingatia mila na desturi na uamuzi wa maspika wa mabunge mengine.

Mara kadhaa amekuwa akipigiwa kelele kwa tabia yake ya kuvunja kanuni hizo hali inayosababisha baadhi ya wabunge kuchukua uamuzi mgumu wa kutaka kumng’oa kwa kutumia kanuni ya 138 (1).

Kanuni hiyo inaeleza “Utaratibu wa kumwondoa madarakani Naibu Spika chini ya Ibara ya 85 (4) (c) ya Katiba utakuwa kama ule wa kumwondoa Spika, isipokuwa tu, taarifa ya kusudio la kumwondoa Naibu Spika madarakani inayoeleza sababu kamili za kuleta hoja hiyo  itapelekwa kwa Spika ambaye ataiwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kujadili.

Sababu kubwa ambazo zinalalamikiwa na wabunge hao ni namna ambavyo naibu spika huyo anavyoweka mbele maslahi ya CCM, kuliko maslahi ya Bunge kinyume na kanuni ya 8 (b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Uamuzi wa kumng’oa umepelekwa hata kama hatang’oka ujumbe utakuwa umefika ukionyesha kwamba wabunge wa upinzani wamechukizwa na upendeleo anaoonyesha.

Kwa mfano Mei 6, 2016 alitumia vibaya madaraka yake ya kiti cha uspika kwa kutoa uamuzi wa mwongozo ambao ulikuwa unakiuka Ibara ya 12 (2) ya Katiba inayosema: “Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”.

Mwongozo huo uliokuwa unapinga udhalilishaji wa wabunge wanawake wa upinzani na mmoja wa wabunge lakini hakuheshimu hilo hali iliyosababisha wabunge hao kutoka nje ya Bunge bila ya kujali hata jinsia yake.

Aliendelea na uvunjaji huo wa kanuni ili kukinusuru CCM, Aprili 28, 2016 alivunja kanuni ya 64 (1) zinazokataza mbunge kutumia lugha ya matusi kwa mbunge au mtu mwingine yeyote na kukataza matumizi ya lugha ya kuudhi au kudhalilisha watu wengine, lakini Naibu Spika alinukuliwa akimtusi mbunge: “Mheshimiwa Bwege, usionyeshe ubwege wako humu ndani…”

Hakuishia hapo kuwasakama wabunge wa upinzani kwani Mei 30, 2016 aliamua kwa makusudi kuvunja ibara ya 63 (2) ya Katiba kwa kutumia vibaya kanuni ya 69 (2) na 47 (4) kwa kumhusisha mbunge Joshua Nassari kwa upande mmoja na Bunge zima kwa upande wa pili kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali.

Wabunge wote wangeshikamana pasipo kuangalia vyama vyao kukemea uovu huo waziwazi kama alivyokuwa akifanya Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa akikemea vitendo vya kidikteta, unyonyaji na ubaguzi wa rangi kabla na baada ya kupata uhuru.

Iwapo wabunge wa CCM wataruhusu kutumia mchezo huo ndani ya Bunge kwa kuruhusu ubaguzi wajue kabisa watakuwa wanahatarisha amani ya Taifa.

Serikali hii inayoongozwa na CCM naipatia ushauri wa bure kwamba iache kubaka demokrasia na iache kubariki uvunjifu wa demokrasia kwani kwa kufanya hivyo itakuwa inabariki uvunjifu wa haki za binadamu.

Nchi nyingi ambazo zimetumbukia kwenye machafuko ambayo siyaombei ni zile zilizojaribu kupuuza haki za wananchi wake ikiwemo ya kidemokrasia.

Dk. Tulia anatakiwa kusimamia sheria na kanuni ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa watu wanaofikiri kwa jicho la tatu kwamba amekuja kuua demokrasia ili aweze kulipa hisani aliyopewa na chama chake na Rais Magufuli.