Home Latest News DR BASHIRU, MASUALA YA KIDIPLOMASIA WAACHIE WANADIPLOMASIA

DR BASHIRU, MASUALA YA KIDIPLOMASIA WAACHIE WANADIPLOMASIA

5815
0
SHARE

NA HILAL K. SUED


Ijumaa wiki iliyopita, alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa chama hicho tawala Dk Bashiru Ally aliwashangaa vijana hao kukaa kimya kutokana na kile alichokiita “mashambulizi ya Marekani dhidi ya demokrasia ya Tanzania.”

Kwanza turudi nyuma kidogo kuhusu hicho alichokiita “mashambulizi ya Marekani dhidi ya demokrasia ya Tanzania.”

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari nchini baada ya chaguzi ndogo mapema mwezi uliopita ukiwemo ule wa ubunge jimbo la Buyungu, Ubalozi wa Marekani hapa nchini pamoja na mambo mengine ulisema “Marekani imesikitishwa na uendeshaji wa chaguzi ndogo zilizofanyika nchini tarehe 12 Agosti 2018…..taarifa za kuaminika zinaonyesha kuwa chaguzi ziligubikwa na vurugu zilizohusiana na uchaguzi, ukiukwaji wa sheria za uchaguzi ikiwa pamoja na kukataa kwa baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi kuwasajili wagombea kutoka vyama vya upinzani, vitisho vya polisi dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani…

“…Mambo haya yanakwaza haki ambazo Katiba ya Tanzania imewapa raia wake na kuhatarisha amani, utulivu na usalama nchini na katika eneo lote la kanda.”

 

Nimelazimika kutaja kwa kifupi mambo ya msingi yaliyotajwa katika taarifa hiyo – mambo ambayo hata hivyo hayakuwa habari mpya kwani tayari yalikuwa yameripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii – ili tusipoteane njiani hasa katika hoja ya msingi.

 

Aidha Dr Bashiru binafsi amewahi kuligusia suala hili hili akiwa ziarani Visiwani alipotoa kauli ya kuyataka mataifa ya nje yaache tabia ya kuingilia siasa za ndani ya Tanzania, yaache kubeza ushindi wa CCM katika chaguzi, na badala yake yaangalie siasa za kwao na kuondosha migongano iliyopo. Hata hivyo hakuitaja Marekani moja kwa moja kama vile wiki iliyopita.

Kwa vyovyote vile inanibidi nimshangae Dr Bashiru Ally kwa kuusukuma tena mpira huo huo kwa vijana wa chama hicho, kwani alivyosema akiwa Visiwani ingetosha. Lakini suala si uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya nchi, bali je, ni sahihi kwa chama hicho kuijibu taarifa ya Marekani katika masuala ya chaguzi za ndani?

Tukumbuke kwamba ile taarifa ya Wamarekani hata sehemu moja haikuitaja CCM, wala kubeza ushindi wa chama hicho katika chaguzi zile. Haya masuala si yake, ni ya kidiplomasia na kuna utaratibu wake wa kuzishughulikia nchi zinaonekana kukiuka misingi ya uwakilishi wa kidiplomasia.

Tumeona hivi karibuni jinsi Dr Bashiru alivyo-panic pale alipoulizwa na mwandishi wa habari kuhusu suala ambalo liko moja kwa moja chini ya himaya yake — kwamba vipi chama chake hakifuati katiba na kanuni zake yenyewe kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge katika chaguzi hizi ndogo, kwani iwapo chama hicho kinakiuka katiba yake yenyewe, si pia kinaweza kukiuka katiba ya nchi?

Inashangaza kiongozi huyo mkuu wa chama hata siku moja hakuwa anatarajia kuulizwa kuhusu suala hilo – suala ambalo alijua lilikuwa gumzo kubwa katika medani ya siasa wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea. Hakuwa amejitayarisha kwa majibu – kwani hakujali iwapo chama kinaboronga katiba na kanuni zake kama ilivyo kwa serikali yake na wote wale wanaohoji wapuuzwe tu.

Aidha ku-panic kwake kunatoa maelezo ya madai kwamba wale wabunge na hata madiwani wa upinzani wanaohamia CCM hurubuniwa kufanya hivyo kwa ahadi mbali mbali ikiwemo ya kuteuliwa tena kugombea nafasi zao kupitia chama hicho, uteuzi ambao katika kuhakikisha unapatikana, sharti kanuni zilizowekwa za mchakato wa uteuzi uvurundwe.

Kama nilivyotaja hapo mbele CCM si mamlaka sahihi kuijibu taarifa hiyo ya kibalozi. Nasema hivi kwa sababu kama ubalozi umelalamika, au umesikitishwa (neno ililotumia) kuhusu uendeshaji wa chaguzi, basi ubalozi ulikuwa unailalamikia serikali, kwa maana kwamba serikali ndiyo mamlaka ambayo kikatiba inayoendesha chaguzi kupitia taasisi zake kama vile Tume ya Uchaguzi (NEC), na vyombo vyake vingine vinavyosimamia usalama wa raia kama vile polisi – ambavyo vyote hivyo vina bajeti ya serikali inayotokana na walipa kodi – na pengine kutoka kwa wafadhili wa nje ikiwemo Marekani.

CCM kama chama, hakiendeshi chaguzi hizi za kitaifa, kwa hivyo mlengwa wa taarifa ya Wamerakani ni serikali – siyo CCM, ambayo pamoja na kitengo chake cha vijana, ilikuwa sahihi kukaa kimya. Hata watu wa Tume yenyewe (NEC) hawakupaswa kujibu taarifa ile, na kama walikerwa na taarifa hiyo basi wangeelekeza malalamiko yao kwa mamlaka sahihi ya kujibu, ambayo ni serikali kupitia wizara yake ya Mambo ya Nje.

Na serikali imeshawahi kufanya hivyo huko nyuma. Katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nne, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo Bernard Membe aliwakemea hadharani mabalozi wa nchi za magharibi hapa nchini pale alipowaita ofisini kwake na ‘kuwapa somo’ namna ya kuziwasilisha nchi zao katika ardhi ya Tanzania.

Dhambi yao ilikuwa kujipa ‘uthubutu’ wa kuiambia serikali yetu kuanza kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wakuu wa serikali na taasisi zake wanaotuhumiwa kwa ufisadi na wizi wa fedha na rasilimali za taifa. Membe alikuwa amesahau kuwa baadhi ya fedha hizo ni zile zilizotoka kwa wafadhili hao kama misaada.

Aliyeongoza katika thubutu hiyo ya kuiambia serikali kufanya kile cha msingi na kwa nia njema kabisa ni aliyekuwa Balozi wa Marekani hapa nchini Michael Retzer. Katika hotuba yake ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini mwishoni mwa 2007 Retzer alisema imefikia wakati sasa kwa serikali kuwachukulia hatua za kisheria ‘mapapa’ wa ufisadi, badala ya kukimbizana na ‘vidagaa’ vya ufisadi.

Lakini Waziri Membe, kwa niaba ya serikali yake alikwenda mbali zaidi – pale aliposisitiza hatua ya mabalozi hao kuingilia masuala ya ndani ya nchi na hapo hapo kunukuu vipengele vya Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) kuhusu kanuni za mahusiano ya kibalozi.

Mkataba wa Vienna ni makubaliano baina ya nchi za kimataifa kuhusu mahusiano yao ulioratibiwa na Umoja wa Mataifa mapema mwaka 1961 wakati bado nchi yetu haijapata uhuru lakini baadaye uliuafiki na kutia saini.

Swali ambalo nilikuwa najiuliza ni kwamba hivi yote hayo yalikuwa ni lazima? Kulikuwa na haja ya kwenda mbali namna hiyo katika kuwadhalilisha marafiki zetu ambao ‘dhambi’ yao ni kutamka yale ambayo mtu yoyote yule wa barabarani anaona ni kweli tupu na kuyaafiki na hutamkwa kila siku kwa sauti kubwa? Vienna inakujaje hapa?

Mambe hakuishia kwa hilo tu. Itakumbukwa alizikaripia tena nchi za Magharibi kwa kuzisaidia kifedha asasi za jamii na mashirika yasiyo ya kiserikali (CSOs and NGOs) katika kampeni zao za kupinga uanzishwaji wa mifuko ya maendeleo ya majimbo yaani Constituency Development Fund (CDF) na kwamba waache kufanya hivyo mara moja. Bahati nzuri mara hii hakunukuu Mkataba wa Vienna.

Ni kweli Membe alikuwa na ushahidi wa tuhuma zake kwani karibu CSOs na NGOs zote hupata misaada kutoka kwa wafadhili wa nje, siyo tu kwa ajili ya kampeni dhidi ya CDF, bali pia kwa karibu shughuli zao zote. Kama jinsi wafadhili hao hao wanapofadhili shughuli nyingi za serikali.