Home Latest News ‘Driverless Car’ ni hatari inayotusubiri ulimwengu ujao?

‘Driverless Car’ ni hatari inayotusubiri ulimwengu ujao?

2128
0
SHARE

NA LAMECK KUMBUKA

GENEVA

MWANZONI mwa wiki hii kwa mara ya kwanza kabisa nilipanda gari linalojiendesha lenyewe hapa ninapoishi mjini Geneva nchini Uswisi. Kwa lugha ya kimombo magari hayo yanaitwa ‘Driverless Car’. Kimsingi dunia ilainza kuwa na wazo la kuunda magari ya namna hiyo katika miaka 1920, maendeleo kasi ya teknolojia kwa sasa yameweza kulitekeleza na watu wanatumia bila wasiwasi.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2015 baadhi ya majimbo ya California, Florida, Michigan, Nevada, Virginia na Washington D.C nchini Marekani yaliruhusu matumizi ya majaribio ya magari hayo katika barabara za umma. Lengo lao lilikuwa kufanya tathmini juu ya utendaji wake wa kazi. Namna yanavyomudu kutoa huduma na vigezo vyote ambavyo wanatakiwa kwenye sekta ya usafirishaji nchini humo.

Kwa hapa nchi ya Uswisi kwa ujumla wake mradi wa magari yasiyotumia dereva yaani kujiendesha yenyewe, majaribio yanafanyika kwenye mtaa ninaoishi jijini Geneva, hivyo basi nimelipanda kwa mara yangu ya kwanza, licha ya kila siku kushuhudia linapita katika safari zake.

Siku zote nilikuwa naogopa kutumia usafiri huo, nikihofia usalama wangu na pia sikufahamu namna linavyofanya kazi. Kwahiyo nikakata shauri ya kupanda. Hata hivyo, sitaongelea namna inavyofanya kazi, linajuaje kama kuna matuta ili lipunguze mwendo, au inavyopishana na magari mengine barabarani au kushika breki ama kusimama yenyewe kwenye kituo husika ambacho abiria mwingine anaingia au kushuka.

Niwaambie watanzania wenzangu kuwa ninachotaka kuongelea hapa ni tafsiri yake katika ulimwengu ujao wa kazi. Upo wasiwasi mkubwa uliotanda duniani kuhusu teknolojia ya magari ya kujiendesha yenyewe.

Wataalamu na watu wengine wote wanajiuliza, je mashine ama Roboti zinaenda kuwa mbadala wa watu katika ufranyaji wa kazi kuanzia ofisini, mitaani na kwingineko unakokujua? Vilevile vipi majukumu ya askari wetu wa barabarani yaani Trafiki katika ukaguzi wa magari na kutoa faini kwa yale yanayokutwa na makosa, ikiwa yatatoweka duniani?

Hii maana yake inagusa hadi kwenye vyuo vyetu nchini Tanzania ambavyo vinatoa mafunzo ya udereva au fani husika. Vipi wale wanaotegemea kazi ya udereva watafanya kazi gani iwapo magari ya kujiendesha yeneywe yatasambaa duniani?

Je wale madereva waliomo kwenye huduma za Hoteli au wale wanaofagia? Si tu kazi kama hizo, sasa hivi hata lugha  inaweza kufundishwa kwa njia ya mashine hasa kwa wanasheria. Mashine zitaweza kuchambua, kusimamia kesi zote kwa ufasaha kabisa kuliko nguvu za mwanandamu.k

Sekta ya uhasibu nayo hapo ndipo mashine zitakuwa zinatumika zaidi kuliko nguvu za binadamu. Kwenye uhasibu binadamu hagusi kabisa. Katibu Muhtasi huko tayari kazi zilishaanza kupotea na nafasiz ao zinachukuliwa na mashine.

Je yatupasa kuogopa hali hii?

Watafiti wengi kutoka vyuo vilivyobobea vya teknolojia kama vile Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts yaani MIT(Massachusetts Institute of Technology). Wanazuoni kutoka MIT wamesisitiza kuwa mashine hazitakuja kamwe kuwa mbadala wa nguvu za binadamu.

Changamoto pekee iliyopo ni namna ya kutengeneza mashine ambayo itakuwa msaidizi mzuri wa binadamu. Kwa tafsiri nyingine ni kuwa Roboti zipo kwa ajili ya kutusaidia na kamwe si kuwa mbadala wetu. Kuna mifano mingi inayo dadavua na kusimamia hii hoja.

Je tufanye nini ?

Kitu pekee ambacho mashine au roboti haitakuja kuwa nacho ni hisia. Kuna tafiti zinajaribu kuonesha namna ambavyo roboti zitaweza kusoma hisia yako msomaji na kukuhudumia kwa kadiri ya unavyojisikia, hata hivyo hisia na huruma ya mwanadamu haitokuja kupatikana kwa mashine yoyote duniani.

Je ni ujuzi gani utakaotupatia kazi hapo baadaye?

Tunafahamu kuwa kasi ya mashine kuchukua ajira za binadamu ni kubwa. Kwahiyo ili binadamu aendelee kubaki kwenye kazi au soko la ajira anatakiwa kufikiria ujuzi unaofaa. Je, ni ujuzi upi unafaa wakati mashine zitakapokuwa zimechukua kazi zote?

Haistajabishi mtu akidhani kuwa ni mapema sana kufikiri hili hasa kwa bara letu la Afrika. Lakini muda unakimbia. Tafiti mbalimbali za hivi karibuni zimejikita kutafuta ufumbuzi katika suala hili. Kuna makala,vitabu,majarida na blogu maelfu na maelfu kuhusu haya lakini zote zinakubaliana katika sehemu zinazohusiana na Ujuzi wa mtu.

Sehemu hizo ni kama vile Ubunifu, kwenda na wakati au mazingira/hali, kujali muda,hisia,huruma na mitandao ya watu (creativity, adaptation to environment/situation, time management,feelings, empathy and networking)

Katika kila kitu unachokifanya hapa duniani hakikisha unajaribu kuhusisha mambo hayo. Sio rahisi, kwa sababu vingine havifundishwi shuleni wala vyuoni bali ni vipaji, lakini ni vema kujaribu kukuza ama kuendeleza ujuzi wako mara kwa mara katika maeneo tajwa.

Leo naishia hapa kwa ufupi. Mungu akitujalia wiki ijayo nitaongelea moja baada ya nyingine kwa ufupi kuhusiana na suala zima la mashine na nafasi ya mwanadamu pamoja na sisi wenyewe kufuatilia yote muhimu katika utendaji wa kazi.