Home Makala Dunia imeanza kumwelewa Rais Magufuli

Dunia imeanza kumwelewa Rais Magufuli

597
0
SHARE
Rais Magufuli akizungumza na wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wilayani Chato hivi karibuni.

NA GALILA WABANHU

APRILI 22 mwaka huu wakati Rais John Magufuli akizungumza na wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wilayani Chato katika Mkoa wa Geita alizungumza mambo mbalimbali kuhusu janga la virusi vya ugonjwa wa Corona linaloendelea kuua maelfu kwa maelfu na kuathiri mamilioni ya watu kote duniani. 

Moja ya jambo alilolizungumza kwenye hotuba yake hiyo ukiachana na mambo mengine lilikuwa ni suala la kupulizia dawa ya kuua wadudu maarufu kwa ‘fumigation’ iliyoaminika kwamba inaweza kuua virusi vya Corona.

Rais Magufuli alisema kitendo kilichokuwa kinafanyika kwa baadhi ya maeneo hapa nchini kupulizia dawa kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye mabasi na kwingineko kama njia ya kuua virusi vya Corona hakikuwa sahihi na kwamba hakuna Fumigation yoyote inayoweza kuua virusi vya Corona. 

Mkuu huyo wa nchi kwa msisitizo zaidi kwa alichokuwa anakizungumza alienda mbali kwa kusema jambo hilo lilikuwa la kipuuzi kabisa.

Sasa baada ya kauli hiyo ya mkuu wa nchi, vijana wa upinzani walilipuka mitandaoni kwa kusambaza wakidai suala la fumigation lilikuwa sahihi kwa sababu ya kwamba eti mbona lilifanywa pia na mataifa mengine makubwa duniani kama China, Uingereza, Marekani, Canada na mengine mengi waliyoyataja huku wakihoji kama lilikuwa jambo la kipuuzi basi mataifa hayo makubwa kabisa duniani na yenyewe yasingefanya suala hilo.

Kwa mawazo na akili zao walidhani jambo likifanywa na mataifa makubwa basi hilo ni lazima liwe sawa na haliwezi kabisa kutokuwa sahihi kamwe.

Sasa wenye mamlaka yao ya afya duniani, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kupitia kwa mtaalamu wake wa masuala ya dharura, Dk. Michael Ryan Mei 5 mwaka huu lilisema dawa inayopulizwa mitaani kwenye baadhi ya nchi kama njia ya kujikinga na Corona wala haisaidii chochote kwenye kuua virusi hivyo vya Corona. 

Shirika hilo la afya ulimwenguni lilienda mbali zaidi kwa kusema kwamba kupuliza dawa hizo mitaani kunaweza kuleta athari na hatari tu kwa watu kuugua magonjwa mengine yatokanayo na kuvuta hewa ya dawa hizo zenye kemikali.

Hayo yanajiri siku 25 tu tangu Rais Magufuli akiwa Chato mkoani Geita akatae upuliziaji wa dawa hizo na kusema fumigation haiwezi kuua virusi vya Corona kamwe.

TUNAJIFUNZA NINI KWENYE MKASA HUU

Mosi; Watanzania tuone aina ya Rais tuliyenaye. Hili linaweza kuwa funzo la kwanza kabisa kwenye kisa hiki. Tunaweza kuona aina ya Rais tuliyenaye na jinsi alivyo na uwezo mkubwa wa kung’amua mambo yenye faida na hasara kwa nchi yake. 

Si kweli kwamba kila jambo linalofanyika nje au na mataifa makubwa basi ni jema na linafaa kuigwa na kufanywa hapa kwetu. Hii si kweli na si sawa hata kidogo. Si sheria kwamba mkubwa hakosei. Akili na maono yanahitajika sana kipindi hiki tukipambana na janga hili la Corona. Yatakuja mengi lakini si kila litakalokuja na kulisikia ni la kweli na la kulifuata. Mhenga wetu wa Pwani mzee Jakaya Kikwete (Rais mstaafu), anasisitiza sana kuhusu akili za kuambiwa kuchanganya na za kwako. Hapa Rais amechanganya na zake kuliepusha taifa kuingia hasara ya kupuliza dawa hizo na zaidi kuwaepusha Watanzania na hatari ya magonjwa iliyotolewa na WHO hasa baada ya mtu kuvuta hewa ya kemikali kutoka kwa dawa hizo za kupulizia (fumigation).

Pili; Kujifunza aina ya upinzani wa Tanzania. Hii ni moja ya changamoto kubwa sana hapa nchini kwetu. Hapa kwetu pametengenezwa aina fulani ya kupinga kila jambo linalofanyika kwa mwamvuli wa upinzani. Ukienda kwa majirani zetu kwa mfano wa Kenya huwezi kukuta upinzani huo. Walishavuka huko. Wao wanaiangalia Kenya kwanza kabla ya siasa na masilahi yao. Uhuru Kenyatta na Raila Odinga sasa wako pamoja wanajenga nchi. Hapa kwetu upinzani ni taswira ya kupinga, kukosoa na kubisha kila jambo hata kama lina masilahi ya taifa ama hasara kwa taifa. Jambo hata kama ni baya litatengenezewa picha lionekane ni zuri na kama ni zuri basi litatafutiwa kila aina ya propaganda ili lionekane baya. Ndipo tulipofikia hapa Tanzania. Hii ni funzo kwa Watanzania.

Tatu; Dunia imeanza kumwelewa mwana wa Afrika. Hii ni ishara tosha kwamba maono ya Rais Magufuli sasa yanatumika na kugombaniwa kote duniani. Leo WHO inathibitisha fumigation ni upuuzi na ni hatari kwa watu. Tayari msimamo wa Rais Magufuli wa hakuna lockdown unaendelea kufuatwa kote duniani. 

Leo Afrika imeshindwa kuwafungia watu wake ndani sababu ya njaa. Nchi nyingi za Afrika zimeshindwa na sasa inasisitiza zaidi watu kuchukua tahadhari. Marekani, Uingereza, Italia, India, Brazil wanaanza kulegeza masharti ya kutotoka nje kwa kuhamasisha zaidi watu kuchukua tahadhari kuliko kuwafungia huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi kuitaka serikali kuwafungulia. 

Marekani, Uingereza na Brazil kuna maandamano makubwa sana ya watu. Haya yote Rais Magufuli amekuwa akiyahubiri kila kukicha. Taratibu wanaanza kumwelewa anachomaanisha Rais. Corona ni vita ya aina nyingine, inahitaji umakini na akili kuipigana. Kila mtu ashinde za kwake halafu tutahesabiana baadaye. Rais Magufuli songa mbele sisi vijana wako tupo na tupo pamoja na wewe kwa vitendo na Watanzania na dunia yote wamekuelewa.