Home Latest News EAC NA SADC NI SAYARI TOFAUTI KWA ECOWAS

EAC NA SADC NI SAYARI TOFAUTI KWA ECOWAS

1036
0
SHARE
Rais wa Gambia Yahya Jammeh, akiondoka nchini humo baada ya kutangaza kung'atuka madarakani

NA HILAL K. SUED,

Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara lina jumuiya tatu kuu za kikanda zinazoshikisha nchi za kanda zao – Jumiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi Magharibi mwa Afrika (ECOWAS na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo nimezipanga kwa umri zilivyoanzishwa.

Wakati ECOWAS inaanzishwa mwaka 1975 kulikuwapo jumuiya nyingine kubwa ya kikanda upande wa Mashariki – yaani EAC iliyoanzishwa miaka minane kabla. Na mapema mwaka 1980 nchi za Kusini (na za kati) Barani zilianzisha SADCC ambayo mwaka 1992 ilibadili jina na kuitwa SADC.

Kwa kiasi kikubwa kuanzishwa kwa ECOWAS kulisukumwa na uwepo wa EAC kwani nchi za Magharibi mwa Bara la Afrika waliona umuhimu na wao pia kuwa na chombo cha ushirikiano baina yao – hasa kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.

Lakini matumaini ya ECOWAS kuifanya EAC kama mwongozo na dira yake yalipata pigo kubwa pale EAC ilianza kuugua na hatimaye ikafa miaka miwili baadaye. Jumuiya hiyo ilikuwa ya kipekee kabisa duniani, kimuundo na kiutendaji kwani ushirikiano baina ya nchi hizo ulikuwa mkubwa na wa karibu mno kuliko hata uliopo ndani ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) sasa hivi.

Mbali na kuendesha pamoja mashirika ya kutoa huduma kama vile usafiri wa reli, ndege, shughuli za posta na simu na uendeshaji wa bandari, pia kulikuwapo mahakama moja ya rufaa kwa nchi zote tatu – Court of Appeal for East Africa – na uendeshaji wa pamoja wataasisi kadha kama vile za utafiti wa malaria, uvuvi na uthibiti wa wadudu waharibifu wa mimea.

Ilikuwa ni kazi ngumu kuvunja jumuiya yenye mshikamano kama ule, lakini siku zote wanasiasa si watu wa kuchezea hata kidogo. Matarajio ya wananchi wengi yalikuwa ni kwa Jumuiya hiyo kukua, siyo kufa. Hata hivyo ilifufuka tena miaka 23 baadaye (2000) ingawa tofauti kimfumo na kimkakati kuliko ile ya awali ingawa umbo na ukubwa ulikuwa ule ule.

Na baadaye zikaongezeka nchi za Burundi na Rwanda (2007) katika Jumuiya hiyo na mwaka jana Sudan ya Kusini nayo ilijiunga, pamoja na matatizo yao yote hususan yale ya kisissa.

Katika miaka ya mwanzo ya Milenia hii  aliyekuwa Katibu Mkuu wa EAC Amanya Mushegga wa kutoka Uganda aliwahi kusema kwamba iwapo Burundi na Rwanda wangeruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ile ya zamani na iwapo Jumuiya hiyo isingeachiwa kuvunjika mwaka 1977, matatizo ya kikabila yasingejitokeza katika nchi hizi mbili na kwamba hata mauaji ya kimbari ya Rwanda yasingetokea mwaka 1994.

Lakini kauli hiyo ilikuwa ni ya kufikirika (hypothetical) tu kwani mwaka 2007 Rwanda na Burundi zilijiunga na Jumuiya (ya sasa) lakini bado hii haijasaidia kutuliza migongano ya kikabila na ya kisiasa ndani ya nchi hizo, hasa Burundi.

Hii ni pamoja na miaka kadha iliyopita kuanzishwa kwa mkataba wa pamoja (Protocol) wa kusimamia masuala ya utawala bora na utoaji wa maamuzi ya haraka kuhusu ya migogoro ya siasa, masuala ambayo yalitajwa kuwa muhimu katika ajenda ya ushirikiano wa kisiasa (political integration agenda) miongoni mwa nchi hizi.

Haya yalitarajiwa kutoa suluhisho la kudumu katika uendeshaji wa chaguzi – suala nyeti kwa nchi zote wanachama. Kwa mfano Ibara ya 2 na 3 ya Mkataba huo yalizitaka nchi wanachama kudumisha misingi ya demokrasia, kusimamia utawala wa katiba na kufanya chaguzi zilizo huru na haki na katika kubadilisha serikali kwa njia ya amani.

Je haya yanatokea? La hasha, migogoro ya kisiasa kuhusiana masuala ya uchaguzi yamekuwa ya kawaida katika kila nchi za EAC na hakuna nchi nyingine ya kumnyooshea kidole mwenzake – eti kufanya hivyo ni kuingilia masuala ya ndani. Sasa ile Protocal iliyosainiwa ina maana gani iwapo inavunjwa na kila nchi?

Migogoro na ghasia wakati na baada ya chaguzi kutokana na chaguzi zisizo huru yamekuwa ni masuala ya kawaida. Tanzania pia ina sehemu yake ya siasa haribifu pamoja na majigambo ya majukwaani kwamba ni kisiwa cha amani katika bahari ya machafuko.

Suala lilitokana na kufutwa ghafla kwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar yaliyoonyesha kuupa ushindi upinzani ni mfano mmoja. Pengine mgogoro huu haukufikia kiwango cha kutaka kuingiliwa na viongozi wengine wa Jumuiya, lakini mbegu mbaya imeshapandwa na huko tuendako Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye.

Kwa upande wa SADCC migogoro itokanayo na chaguzi na ambayo iliingiliwa na Jumuiya hiyo katika kupata suluhu ni pamoja na Madagascar, Zimbabwe na Lesotho. Lakini suluhu hizi zilikuwa za namna ya kuzifanya pande zinazohusika zielewane zaidi na hata ikiwezekana kushirikiana kimadaraka, kwa muda, (Transitional power sharing) kuliko kutumia nguvu za kijeshi.

Tukiacha pembeni SADC, nimeleta habari ya hali ilivyo ndani ya jumuiya yetu ya EAC kwa lengo la kulinganisha na ile ya wenzetu ECOWAS. Pamoja na jumuiya hiyo kuwa na nchi wanachama wengi zaidi (15) kuliko sisi, lakini wamepata mafanikio makubwa katika masuala ya kukuza na kulinda demokrasia miongoni mwao. Wamekuwa na uthubutu wa kuonyeshana kidole kwa kiongozi yoyote anayekwenda kinyume na hata kuchukua au kutishia kuchukua hatua za kijeshi. Inatajwa kwamba ECOWAS huchukua hatua kali kama hizi kutokana na historia ya umwagaji damu katika kanda hiyo ya Afrika hasa katika nchi za Nigeria (vita ya Biafra ya miaka ya 60), Sierra Leone, Liberia, Guinea na Mali.

Kabla ya mgogoro wa kisiasa wa Gambia ECOWAS imewahi kuingilia kati migogoro ya kisiasa ikiwemo ile iliyosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya nchi nilizotaja kama vile Sierra Leone, Liberia, Ivory Coast na Mali.

Katika migogoro ya miaka ya karibuni Ivory Coast, Mali na Gambia ni mifano mizuri pale msukumo ya pamoja kutoka nchi wanachama waliweza kuwang’oa viongozi ambao walikuwa wamepora demokrasia wakati wa uchaguzi.

Huko Ivory Coast nguvu za wanachma wa ECOWAS zilifanikiwa kumpeleka mporaji wa demokrasia Laurent Gbagbo katika Mahakama ya ICC kule The Hague, Uholanzi, wakati Yahya Jammeh wa Gambia hatimaye amesalimu amri na kukubali kuondoka nchini na kumwachia madaraka mshindi halali wa uchaguzi Adama Barrow.

Isitoshe, popote panapotokea mgogoro unaotokana na uporaji wa ushindi, viongozi wa ECOWAS huwa hawakubaliani na mtindo wa serikali za mpito ambazo pia hushirikisha vyama vya upinzani – kama vile ilivyotokea Kenya baada ya uchaguzi wao wa 2007 au hata Zimbabwe (mwanachama wa SADC) baada ya uchaguzi wao wa 2008. Utamaduni wa ECOWAS ni kwamba ikithibitika uliiba ushindi, basi unaondoka, hakuna namna ingine.

Matunda ya jitihada za namna hii zinaanza kupatikana – mfano katika chaguzi nchini Nigeria na Ghana ambapo marais waliokuwa madarakani (incumbents) walioshindwa walikubali kushindwa. Au tuseme kutokana na hofu ya kile kinachoweza kutokea dhidi yao viongozi wa nchi za Jumuiya hiyo wameanza kujenga utamaduni wa kutowaza kuendesha chaguzi za hadaa ili kujipatia ushindi. Wameanza kuogopa.

Huku Mashariki mwa Afrika bado viongozi wanaendeleza utamaduni wa chaguzi za hadaa na usanii mtupu ili kuendelea kubaki madarakani – kama si wao wenyewe, basi vyama vyao. Masuala ya EAC kuwaingilia kati – tupa kule.