Home Makala ELIMU BURE NI KAA LA MOTO

ELIMU BURE NI KAA LA MOTO

853
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


SHULE nyingi za Msingi na Sekondari sasa hivi ziko katika kukamilisha mhula wa mwisho na hivyo zoezi la kufungwa kwa ajili ya likizo ya mwisho wa mwaka kufanyika.

Wakati wa mwisho wa muhula, wanafunzi na walimu huwa katika hekaheka za kufanya mitihani na kisha kuisahihisha, na kwa wanafunzi hiki ni kipindi kizuri kwao kujua maendeleo yao kitaaluma.

Wakati hayo yakiendelea, upande wa wazazi nao kazi ya kuwaza kuhusu maendeleo ya watoto wao nayo huchukua hatamu. Kwanza, wazazi huwaza kuhusu maendeleo ya kitaaluma kwa kuangalia alama ambazo watoto wao watapata katika mitihani hii ya mwisho. Na pili watakuwa na kazi ya kuangalia kama kweli watoto hao wana sifa ya kwenda daraja linalofuata.

Kwa wazazi makini wanaofahamu nini maana ya kuwa na watoto, kipindi hiki kwao ni kigumu mno. Kipindi hiki kinaambatana na kuwaza kuhusu gharama za shule baada ya kufunguliwa. Hiki ni kipindi ambacho kina sikukuu nyingi za mwisho wa mwaka, na kwa wafanyakazi ni kipindi pia ambacho kinaambatana na likizo.

Kwa upande wa wakulima na wafugaji, aina yao ya kazi huwafanya kuwa na kazi hasa za uandaaji mashamba, palizi na hata kutafutia malisho mifugo. Kwa wafanyabishara, kipindi cha mwisho wa mwaka huendana na manunuzi mengi japokuwa katika mwaka huu uliopo sasa, hali inaweza kuwa tofauti.

Suala la ulipaji ada kwanza linamfanya mzazi kutambua wajibu wake kwa mtoto wake. Dunia inazidi kubadilika na hivyo wazazi wanajikuta nao wakikumbushwa wajibu wa kuwa na idadi ya watoto ambayo wanaweza kweli kuihudumia.

Kitendo cha siku za hivi karibuni cha serikali kutangaza kuwa imefuta ada na kisha michango mingine kwa shule za Msingi, kwa namna moja ama nyingine kinaweza kuwa ni hatua nzuri kwa wazazi, lakini kitendo hicho ukikitafakari kinaleta hali ya mkwamo katika elimu. Ebu tafakari, kama mzazi kashindwa kusomesha mwanaye ada ndogo ya shule ya Msingi kweli huyu atamudu kumlipia gharama za Elimu ya Juu?

Ukitafakari upya unabaini kuwa bado serikali inatakiwa kuwaacha wazazi kuchangia huduma za elimu kwa watoto wao, nayo ikajikita katika eneo la Elimu ya Juu ambako huko gharama huwa kubwa na wazazi wengi kwa kuzingatia vipato vyao hawawezi kumudu.

Ndio maana unajiuliza swali, kuhusu hali iliyopo leo kuhusu vipaumbele vyetu kama nchi na mwisho unabaki kutazama kuwa huenda hatuna vipaumbele. Elimu ya Msingi inajumuisha idadi kubwa sana ya wanafunzi. Kutokana na idadi hii suala la wajibu wa wazazi kwa watoto wao na shule wanazosoma watoto hao haliwezi kubebwa na serikali peke yake.

Tena hali hii haiwezi kufanyika sasa ambapo eneo la elimu limekithiri ushindani na wazazi walio makini wanaangalia suala la ubora na viwango vya elimu katika shule kabla ya kupeleka watoto wao. Ni kweli serikali inayo nia njema ambayo inalenga kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeweza kuachwa bila kusoma, lakini mfumo unaotumika katika kuwapata wanafunzi kwenye bodi ya mikopo, ungeweza kutumika ili kubaini wapi hasa wana uhitaji ili wazazi waweze kuendelea  kutambua wajibu wao kwa watoto wao.

Serikali ingezidi kujikita katika kuboresha viwango, kulipa walimu tena kwa mishahara inayoendana na maisha pamoja na kuongeza zana za za kufundishia zikiwemo maabara. Lakini sasa nini kinapatikana? Ni idadi ya wanafunzi kuwa kubwa. Ni idadi ambayo ukiipima haina uwezo wa kushindana.

Tena lipo tatizo la elimu yetu kuendeshwa kisiasa zaidi kuliko ilivyokuwa awali wakati wa awamu ya kwanza. Waziri wa Elimu anayo mamlaka makubwa mno katika kuharibu ama kujenga elimu yetu. Uzoefu unaonesha kuwa Mawaziri wengi waliopitia eneo hili waliishia kuharibu. Hata sasa unashuhudia kauli ambazo zinalenga kuharibu na sio kupeleka elimu yetu mbele zaidi.

Ili twende mbele, tunahitaji kukubali kujumuisha wadau wote wa elimu ili wachambue maeneo ya muhimu ya kutuondoa tulipokwama. Tunayo matatizo ya walimu, si kwa sababu ya idadi la hasha! Aina ya walimu wanaofundisha. Je, wanaandaliwa vema, yapi mazingira ya kuwaandaa, vigezo vya nani aende chuo cha ualimu na je, nani mkufunzi wa chuo cha Ualimu?

Tunalo tatizo la zana za kufundishia. Je, vitabu vya kiada vinakidhi mahitaji ya soko la elimu kwa sasa na kwa miaka mingine mingi ijayo. Je, vitabu vipi vya ziada vinapelekwa katika shule zetu. Je, masomo ya lazima ni yapi na kwa sababu gani? Na je, masomo ya ziada ni yapi na yana faida gani?

Ukiachilia hoja hizo, jiulize pia kuhusu mitihani yetu. Je, inaandaliwa vizuri. Je, inalenga kutahini wanafunzi wetu na kuwapa uwezo wa kufahamu zaidi masuala wanayotakiwa kuyafahamu? Na je, baada ya mitihani hiyo nini kinafuata?

Lipo suala la usahihishaji wa mitihani hiyo. Je, unafanyika pasipo misukumo. Je, unafanyika kwa haki na kwa wakati? Je, wanaosahihisha mitihani hiyo wanahudumiwa ipasavyo ili kuifanya kazi hiyo kwa weledi umahiri na uadilifu?

Kisha tutafakari maisha ya sasa na makuzi ya sayansi na teknolojia. Je, kama nchi tunataka wananchi wetu waishi vipi. Nani mshindani wetu na yeye anafunza wanafunzi wake kwa aina gani? Je, elimu tunayotoa inakidhi kuwafanya wanafunzi kuhitimu na kukabiliana na maisha ya sasa?

Maswali haya na mengine kama aina ya shule tulizonazo, vifaa vilivyopo katika shule hizo. Mambo mengine ya msingi kama viwanja na vifaa vya michezo na tamaduni kweli vipo na vinatumika? Ili tufanikiwe tunahitaji mjadala mpana. Na ili tufanikiwe zaidi tunahitaji Elimu yetu kuiondoa kuwa chini ya Waziri na badala yake ijengewe mfumo ambao ndio utaingoza. Inahitaji sera zinazoakisi maisha ya sasa na huko tuendako, sera zinazotabiri yale yatakayokuja na sera zinazoelezea taifa hili litakuwa wapi lini.