Home Habari Elimu inahitajika kuhusu likizo katika ajira

Elimu inahitajika kuhusu likizo katika ajira

3160
0
SHARE

ANNA HENGA

LIKIZO imekuwa ikileta migogoro katika sehemu ya kazi kati ya waajiri na waajiriwa. Migogoro mingi inatokana na elimu finyu juu ya sheria na kanuni zinazosimamia masuala ya kazi kati ya waajiri na waajiriwa.

Halikadhalika sababu ya kiuchumi ni miongoni mwa sababu ambayo mwajiri huitumia katika kukiuka haki ya likizo kwa wafanyakazi. Wakati mwingine waajiri huchukua faida ya waajiriwa kuwa na shida za kiuchumi, hivyo kuwatishia endapo watadai likizo wataachishwa kazi. Katika makala hii tutaangalia aina mbalimbali za likizo kama zilivyoainishwa kwenye sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004.

LIKIZO YA MWAKA

Mwajiri anatakiwa kumpa mwajiriwa likizo ya siku 28 mfululizo katika kila mwaka yaani kipindi cha miezi 12 katika mzunguko wa ajira. Lakini hapa ifahamike kuwa siku za likizo zinaweza kupungua endapo mwajiriwa alishawahi kuomba likizo za dharura mbalimbali katika mwaka husika.

Vilevile sheria inamkataza mwajiri kumnyima mwajiriwa kwenda likizo yake ya mwaka, endapo itatokea mwajiriwa alishawahi kwenda au anatarajia kwenda likizo nyingine ambayo inatambulika kisheria. 

Kwenye aina hii ya likizo waajiri wengi wamekuwa hawawalipi waajiriwa malipo ya likizo pindi wanapokwenda likizo. Wengi wamekuwa wakiwaambia kuwa kwa kuwa wanalipwa mshahara kwenye mwezi husika basi hawatakiwi kulipwa malipo hayo ya likizo.

Hii ni kinyume cha sheria kwani mwajiri analazimika kumlimpa mwajirwa malipo ya likizo pamoja na mshahara wa kawaida wa mwezi husika ambao atakuwa likizo.

LIKIZO YA UGONJWA

Sheria ya ajira na mahusiano kazini, inaeleza wazi kwamba mwajiriwa atatakiwa kupata likizo ya ugonjwa pindi atakapokuwa anaumwa. Mwajiriwa anatakiwa kupata likizo ya ugonjwa kwa siku 126 katika mzunguko wa likizo.

Siku 63 za kwanza mwajiriwa atatakiwa kulipwa mshahara wake kama kawaida na kama ataendelea kuumwa, mwajiri atatakiwa kumlipa mwajiriwa nusu mshahara katika siku 63 za pili.

Kwenye likizo hii mwajiriwa anatakiwa kuonyesha kwa mwajiri cheti cha matibabu ili aweze kulipwa malipo ya likizo ya ugonjwa ikiwa kama atatakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria yoyote au makubaliano ya pamoja kati ya mwajiri na mwajiriwa.

LIKIZO YA UZAZI

Kuhusu likizo ya uzazi kwa mwanamke; atatakiwa kupata likizo ya uzazi ya siku 84 ikiwa amejifungua mtoto mmoja au siku 100 kama atakuwa amejifungua mtoto zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.

Lakini kama mtoto atakuwa amefariki ndani ya mwaka mmoja basi mwajiriwa atatakiwa kupata likizo ya siku 84 za nyongeza. Kabla ya likizo ya uzazi kuchukuliwa mwajiriwa ana wajibu wa kutoa taarifa (notisi) kwa mwajiri miezi mitatu kabla ya tarehe anayotarajiwa kujifungua.

Notisi itatakiwa kuambatanishwa na cheti cha daktari. Mwajiriwa anaweza akaanza likizo ya uzazi wiki nne, kabla ya tarehe ya kujifungua au anaweza akaanza likizo mapema zaidi lakini mpaka ithibitishwe na daktari kwamba kuna haja ya kufanya hivyo ili kulinda afya ya mtoto au mama.

Mwajiri haruhusiwi kumtaka mwajiriwa kufanya kazi wiki sita baada ya kujifungua lakini anaweza kuruhusiwa tu endapo daktari atathibitisha kuwa anaweza kufanya kazi. Mwajiriwa anapomaliza likizo yake ya uzazi anaweza kurudi kazini kwa vigezo na masharti yaleyale aliyoajiriwa nayo.

Pindi mwajiriwa ambaye ni mzazi anaporudi kazini, mwajiri haruhusiwi kumruhusu au kumtaka afanye kazi ambazo zitakuwa na madhara kwa afya yake au ya mtoto.

Kama itatokea mwajiriwa anafanya kazi katika mazingira hatarishi basi sheria, inamtaka mwajiri kumpangia mwajiriwa nafasi nyingine ambayo haitadhuru afya yake na mtoto kwa kuzingatia vigezo na masharti yaleyale aliyoajiriwa nayo.

Na vilevile sheria inamtaka mwajiri kumpa mwajiriwa ambaye ananyonyesha masaa yasiyopungua mawili ya muda wa kazi ili aweze kumnyonyesha mtoto.  

Likizo ya uzazi kwa mwanaume; hii ni likizo ambayo inatolewa kwa mwajiriwa mwanaume ambaye mkewe amejifungua. Ili kupata likizo hii mwajiriwa anatakiwa aiombe ndani ya siku saba toka siku ambayo mtoto amezaliwa na vilevile anatakiwa awe baba wa mtoto husika.

Katika likizo hii mwajiriwa atapewa siku zisizozidi 3 za mapumziko bila kujali idadi ya watoto waliozaliwa. Mwajiri anaweza kuomba uthibitisho wa kuzaliwa mtoto kabla hajatoa ruhusa ya likizo.

LIKIZO YA HURUMA

Likizo hii hutolewa kwa sababu za kibinadamu pale ambapo mwajiriwa anapokuwa amefiwa au kuuguliwa na ndugu. Hapa mwajiriwa atapewa likizo hii endapo atakuwa amefiwa au kuuguliwa na mtoto au kufiwa na mke au mume, mzazi, babu au bibi, mjukuu, kaka au dada. Likizo hii hutolewa siku nne kwa kila mzunguko wa likizo.

Ingawa sheria za kazi zimeweka wazi taratibu za utoaji wa likizo kwa waajiriwa, bado waajiri wengi wamekuwa na kiburi katika kuzifuata. Katika likizo ya mwaka, uzoefu unaonyesha kuwa waajiriwa wengi hawalipwi posho zao za likizo ya mwaka. Wamekuwa wakipewa mshahara wa mwezi husika tu na wakati mwingine hata huo mshahara kutopewa kabisa kwa madai ya kutokufanya kazi kwa mwezi husika.

Vilevile akina mama wengi, wamekuwa wakinyimwa mishahara yao au wakati mwingine kufukuzwa kazi wanapokuwa katika likizo ya uzazi kitu ambacho ni kinyume cha sheria kwani ni ubaguzi wa kijinsia.

Lakini maofisa wa kazi ambao wamepewa jukumu la kufanya ukaguzi katika maeneo ya kazi wameshindwa kuwabana na kuwawajibisha waajiri ambao hawafuati taratibu za kisheria. Kwa upande mwingine wengi wa waajiriwa wana uelewa mdogo wa sheria za kazi, hivyo kutokujua kitu gani wafanye pale haki zao zinapovunjwa wawapo katika mahala pa kazi.

Wakati mwingine, waajiriwa wanafahamu taratibu zipi za kufuata pindi haki zao zinapovunjwa lakini wamekuwa waoga kufanya hivyo kwa kuhofia kupoteza ajira zao.

Hata vyama vya wafanyakazi vingeweza kuwa na msaada mkubwa katika kutatua kero za wafanyakazi kwani wao wako karibu na waajiriwa na waajiri katika maeneo ya kazi.

Lakini bado hawajaweza kuwa msaada kwa wanachama wao kwani matatizo hayashughulikiwi kikamilifu. Hii inaweza kuthibitika na wafanyakazi wengi ambao ni wanachama wa vyama vya wafanyakazi wamekuwa wakija katika taasisi zisizo za kiserikali zinazotoa misaada ya kisheria kama vile Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ili kupata ushauri wa kisheria.

Hivyo, elimu zaidi inahitajika kwa wafanyakazi ili watambue stahiki zao wawapo mahala pa kazi na hata pale ajira zao zinapositishwa bila kufuata taratibu watambue hatua zipi za kuchukua.

Mashirika yasiyo ya kiserikali, Serikali, vyama vya wafanyakazi, vyombo vya habari na wadau wengine ni wakati muafaka wa kuchukua hatua kwa kutoa elimu kwa wananchi ili haki iweze kutendeka katika maeneo ya kazi.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).