Home Habari kuu Elimu kuhusu corona inahitajika zaidi

Elimu kuhusu corona inahitajika zaidi

1132
0
SHARE

JAVIUS KAIJAGE

BAADA ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kutangaza mgonjwa wa kwanza wa virusi vya corona mkoani Arusha mapema mwezi huu, wananchi walipatwa na wameendelea kupatwa na taharuki kubwa huku kila mmoja akiwa anaongea ya kwake.

Licha ya virusi hivi kuwa tishio na hatimaye kutangazwa na shirika la Afya Duniani (WHO), kuwa ni janga la kimataifa lakini bado naamini kabisa taharuki hii huenda inasababishwa na mambo mengi kama ifuatavyo.

Kwanza inatakiwa ikumbukwe kuwa ingawa kwa mujibu wa wataalamu na historia inaonyesha kuwa jamii ya virusi hivi iligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1960, hata hivyo aina hii ya COVID-19 ambayo inasemekana kutokea kwake ni mlipuko wa awamu ya tatu, bado imeonekana kuwa tishio kuliko jamii nyingine ya corona iliyowahi kujitokeza.

Ni tishio kwa maana ya kwamba tangu kugundulika kwake nchini China tangu Desemba mwaka jana, virusi hivyo vimeweza kusambaa kwa haraka takribani mabara yote ya dunia huku idadi kubwa ya waathirika na vifo vikizidi kuongezeka ukilinganisha na virusi vingine mfano HIV na ebola.

Sababu ya pili ambayo huenda  inasababisha taharuki ni ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi ambao kutokana na kuibuka kwa virusi hivi na hatimaye kusambaa kwa haraka kuliko idhaniwavyo, inaweza kuwa chanzo cha hofu kwani wananchi walikuwa hawajapata muda wa kutosha ili waelimishwe kama ilivyokuwa  kwa virusi hatari vya ebola.

Utoaji wa awali usiyo sahihi dhidi ya virusi hivi hasa katika kipindi hiki cha dunia ambayo imeshuhudia maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano ni sababu nyingine inayoweza kusambaza taharuki.

Mbali na vyombo vya habari vya asili ambavyo tulikuwa tumevizoea mfano redio, luninga na magazeti, kwa hivi sasa kuna vyombo vipya vya kisasa vya habari kwa maana ya mitandao ya kijamii.

Kimsingi mitandao ya kijamii kama njia mojawapo ya mawasiliano si mibaya bali inageuka kuwa mwiba hasa pale inapotumika vibaya kwa lengo la kupotosha umma.

Ni ukweli usiopingika dunia ya sasa hivi huhitaji kusubiri mtangazaji aingie kwenye chumba cha redio au luninga ili kukupasha tukio lililotokea bali kupitia mitandao ya kijamii taarifa husambaa haraka zaidi kuliko kawaida.

Dunia ya sasa huhitaji mwandishi aingie mitaani kutafuta habari na hatimaye kutumia kalamu yake kuiandika kwenye gazeti ndipo ujulishwe bali kupitia mitandao ya kijamii watu hujikuta wakipashana habari kwa haraka zaidi.