Home Latest News England imemaliza kazi moja bado nyingine

England imemaliza kazi moja bado nyingine

1487
0
SHARE

englandKELVIN LYAMUYA NA MITANDAO

KWA kipindi kirefu timu ya soka ya Taifa ya England imekuwa na desturi ya kuwatia moyo mashabiki wake na kujisifu kulikopitiliza kwamba wana wachezaji bora kuliko hata kunyakua mataji makubwa duniani.

Nadhani ukihesabu majigambo hayo katika miaka yote waliyoshiriki kwenye michuano mbalimbali basi timu hii itakuwa imejaza mataji ya kujigamba katika kabati lao.

Ukirudi nyuma katika michezo kadhaa waliyoshinda ya kujipima nguvu ukiwemo ushindi wa juzi wa mabao 3-2 dhidi ya Ujerumani jijini Berlin, nitakuelezea jinsi gani kocha wa timu hiyo, Roy Hodgson, anavyofurahia na kujipa matumaini huku ukweli akibaki nao moyoni mwake.

England huwa ni timu tofauti linapokuja suala la mechi za kirafiki, hucheza kwa kiwango kinachoweza kukupa mwanga wa wapi wanaweza kufika mbali katika mashindano.

Mwaka 2006, kabla ya michuano ya Kombe la Dunia haijaanza kutimua vumbi nchini Ujerumani, England iliwapa matumaini makubwa mashabiki wake baada ya kuichapa Argentina mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki, shukrani kwa mfungaji wa mabao hayo, Michael Owen. Lakini mbio zao katika michuano hiyo ziliishia robo fainali baada ya kukubali kipigo kutoka kwa Ureno.

Kabla ya michuano ya Euro 2012, England pia iliwachapa mabingwa wa dunia mwaka 2010, Hispania kwa bao 1-0 kwenye dimba la Wembley, huku ushindi dhidi ya Ujerumani juzi ulikuwa ni wa tatu katika ardhi ya nchi hiyo.

Yote kwa yote, ushindi katika michezo yote hiyo ya kirafiki itakuwa na maana gani kwa taifa hilo ambapo michuano ya Euro 2016 inategemewa kuwa ni yenye ushindani mkubwa kuliko iliyopita? Na je, ushiriki wa nchi hiyo utakuwa tofauti msimu huu?

Ukianza kukichambua kikosi chao kilichosheheni vijana wenye kipaji na walioonesha juhudi na kupata ushindi dhidi ya mabingwa wa dunia, hautaweza kung’amua haraka ni namna gani muunganiko huo wa wachezaji wenye kufurahisha ukiwaangalia jinsi watakavyoweza kutoa upinzani.

Harry Kane, Dele Alli na Jamie Vardy, wachezaji ambao msimu huu wanafanya makubwa katika klabu zao, waliilaza na viatu timu bora duniani, upande mwingine mfungaji wao bora mwenye mabao saba katika michezo ya kufuzu na nahodha, Wayne Rooney, naye hayupo kikosini, unaachaje kuwa na matumaini?

Siku za hivi karibuni katika soka kuna vitu vingi ambavyo vinachukuliwa kwa mtazamo hasi, kwa hiyo vema kuwasamehe tu mashabiki wa England ambao walijipa asilimia 100 ya kuiona timu yao inafanikiwa msimu huu hasa baada ya kiwango walichokionesha Berlin.

England inatakiwa kufuta kabisa ndoto wanazoziota na kuishi katika dunia halisi, katika muda huu ambao michuano ya Euro itakayofanyika Ufaransa ipo mbioni kuanza.

Jipu katika safu ya ulinzi ndilo linalotakiwa kutumbuliwa haraka iwezekanavyo na hawatakiwi kujipa matumaini ya kupata raha msimu huu kama watadharau jambo hilo.

Anayetaka kuwatetea England na aendelee tu lakini ukiangalia jinsi walivyofungwa dhidi ya Ujerumani hasa mabao mawili yaliyowahusisha Mesut Ozil, Marco Reus, Thomas Muller na Mario Gomez, utaona jinsi gani safu yao ya ulinzi ilivyo na mapungufu mengi ya kufanyiwa kazi.

Ujerumani wanasifika kwa aina ya ushambuliaji wao wa nguvu, lakini kwa timu kubwa na yenye jina kama England haikuonesha umakini wa kutosha kuhakikisha haiwaachii nafasi kubwa wachezaji wa timu hiyo pale walipokuwa wakilifikia lango lao.

Mabao mawili yaliyofungwa na Toni Kroos na Gomez yote yalikuwa katika mazingira ya wazi, ilionekana ni kama kupiga ngumi fuko lililojaa makaratasi.

Mabeki waliosimama kati walikuwa ni Chris Smalling na Gary Cahill, ambao kiwango chao msimu huu kimekuwa ni cha kupanda na kushuka, wakati mabeki wa pembeni walikuwa ni Danny Rose, Nathaniel Clyne ambao licha ya kusaidia safu ya ushambuliaji kwa kiasi fulani hawakufanya kazi ya ulinzi kwa kiwango cha kuridhisha.

Hodgson ana upungufu mkubwa wa mabeki wa kati wenye uwezo wa kupambana na washambuliaji wakali msimu huu kama Lewandowski, Ronaldo, Griezman na Reus, sio kama kipindi kile ambacho England ilikuwa na utitiri wa mabeki wa kati.

Kwa mbali, beki mwingine wa kati mwenye uwezo wa kuingia katika kikosi cha kwanza ni John Stones wa Everton ambaye hata hivyo bado ana vitu vingi vya kuongeza katika kiwango chake.

Hodgson mwenyewe anamwamini beki huyu ambapo anamtaja kama ni kijana mwenye kipaji kikubwa na anayeweza kuwa msaada katika kikosi chake.

Kipaji ni kipaji, lakini Stones ameshindwa hata kumwaminisha kocha wake Everton na hajacheza katika michezo michache iliyopita huku rekodi zikionesha kuwa beki huyo ameruhusu mabao mengi ya ligi kuliko wote pale Everton, ukizitoa timu nne zilizo katika janga la kushukua daraja pamoja na Bournemouth.

Lakini bado Stones anaonekana kama ni beki bora katika akili ya Hodgson, ambaye baada ya mchezo dhidi ya Ujerumani alisema anawataka mabeki wake kujiamini hata wanapofanya kosa lolote uwanjani.

Stones anaweza kuyafurahia maneno hayo, lakini pia unaweza kushangaa ni kwa namna gani anaweza kufikiri huku bado kwa upande wa klabu yake hauoneshi kumwamini kwa asilimia zote baada ya kipindi kifupi tu cha kuaminiwa na kila mtu pale Merseyside?

Kinadharia, Stones anawapa matumaini makubwa England katika safu ya ulinzi, lakini bado wanahitaji kiongozi katika eneo hilo, mtu atakayehakikisha hakuna makosa ya kijinga.

Habari mbaya zaidi kwa Hodgson ni kwamba mchezaji huyo bado hajaweza kujitambulisha kama ni beki bora kabisa duniani, bado ni chipukizi na tayari anaonekana kuharibiwa kiwango na majigambo ya Waingereza, kwa hiyo atakuwa na jukumu lake mwenyewe la kujitambulisha katika ulimwengu wa soka kabla ya michuano ya Euro kuanza.

England imemaliza kazi moja, nayo ni safu ya ushambuliaji ambayo imekamilika na yenye makali ya kuridhisha. Sasa kazi iliyobakia ni kwa safu ya ulinzi na hapo ndipo wataweza kujigamba vizuri.