Home Makala ETHIOPIA NURU YA AFRIKA KWA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA

ETHIOPIA NURU YA AFRIKA KWA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA

4028
0
SHARE

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed (katikati) katika mazungumzo na ujumbe wa Kamati ya Bunge la Marekani mjini Addis Ababa mwezi uliopita.

NA HILAL K SUED


Nchi ya Ethiopia, mojawapo ya nchi yenye historia kubwa Barani Afrika, kama siyo ulimwenguni kote.

Lakini nchi hiyo imepitia misukosuko mingi na mikubwa katika miongo ya karibuni. Baada ya kuuong’oa utawala wa kifalme katika miaka ya 70 uliofanyika kwa umwagaji wa damu, tawala zilizofuata zilikuwa za kiimla hadi mapema mwaka huu pale ukombozi mpya ulionekana kutua nchini humo.

Je, nchi hii ambayo mji wake mkuu – Addis Ababa ni makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU), na mtangulizi wake Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) inaweza sasa kuchukua nafasi yake hiyo stahiki na kuanza kutoa nuru katika masuala ya demokrasia na utawala bora Barani Afrika, vitu ambavyo vimekuwa vikipondwapondwa na watawala kwa zaidi ya nusu karne, kuzidisha umasikini wa watu wake na vita vyta wenyewe kjwa wenyewe?

Upo uwezekano mkubwa hilo kutokea kutokana na ujio wa mtu mmoja, katika sehemu sahihi na wakati sahihi, kama nitakavyoeleza.

Baada ya ziara yake ya kutafuta ukweli nchini Ethiopia, tume ya kamati ya Bunge ya Baraza la Wawakilishi la Marekani chini ya Mwakilishi Christopher Smith, ilirudi Marekani na katika ripoti yake alisema tume yake ilikuwa imejiridhisha kwamba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inafanya maendeleo makubwa katika demokrasia ya kweli, chini ya uongozi mpya uliopo.

Smith ambaye ni wa kutoka Chama cha Republican na mwenyekiti a Kamati ya Bunge inayoshughulikia masuala ya Afrika, Haki za Binadamu Duniani na Taasisi za Kimataifa alitoa ripoti yake kwa Baraza la Wawakilishi wiki iliyopita kwa kusema:

“Waziri Mkuu Abiy Ahmed ni mtu sahihi katika wakati sahihihivyo anahitaji kuungwa mkono.”

Ukiwa Ethipoia ujumbe huo wa watu watano ulikutana na Waziri Mkuu Ahmed na maafisa wengine wa serikali, Wabunge, viongozi wa taasisi za haki za binadamu na pia wanasiasa na watu wengine waliokuwa kizuizini na kupitia mateso wakati wa utawala uliopita.

Smith ni muasisi wa Sheria ya ‘H.R. 128’ – sheria iliyopitishwa na Bunge la Marekani mapema mwaka huu iliyokuwa ikilaani ukiukwaji wa haki za kibinadamu nchini Ethiopia na kupendekeza mabadiliko kadha nchi hiyo ilipasa ifanye katika kukuza amani na demokrasia nchini humo.

Smith alimpongeza sana Abiy ambaye tangu ashike madaraka ya uwaziri mkuu amewaachia huru maelfu ya wafungwa wa kisiasa, ameondoa hali ya hatari iliyokuwapo kwa miezi kadha, na kuanzisha mkataba wa amani kati ya Ethiopoia na Eritrea.

KIONGOZI PEKEE BARANI AFRIKA ANAYEFUATILIWA ZAIDI

Abiy (42) ametokea kuwa kiongozi pekee barani Afrika anayefuatiliwa zaidi, mtu ambaye amesema anataka kuibadilisha nchi yake ndani nje tena kwa haraka iwezekanavyo.

Aidha ni kiongozi ambaye kwa kipindi kfupi tu ametoa matumaini kwa watu wa nchi kadha Baran Afrika kuwa itatoa mfano kwa nchi zao ambazo katika miaka ya karibuni tawala zake zimeanza kutumbukia katika uongozi wa kibabe na ukiukwaji wa haki za kibiunadamu na kuachana na misingi ya demokrasia na utawala bora.

Kazi mbele yake ni kubwa mno kwani Ethiopia ni nchi ya pili Barani Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu, ambao wanafikia 100 milioni. Mbali na hilo kuna hatari nyingine: mamilioni ya vijana hawana ajira, umasikini uliokithiri na hivyo ushindani mkubwa wa kuwania maliasili chache zilizopo.

Kuhusu vijana na ajira, Waziri Mkuu Abiy anashauriwa atoe kipaumbele katika sera zake na aachane na sera za watangulizi wake ambao walikazania sana ujenzi wa miundombinu na kuwasahau vijana.

Mgeni yoyote anayefika mji mkuu wan chi hiyo – Addis Ababa anakumbana na uwanja wa ndege wa kisasa, barabara za upana wa njia hadi tano tano na ‘ma-fly-over’ kibao kiasi kwamba mtu anaweza kujihisi anaingia mji mkuu wan chi moja ya Ulaya.

Lakini mgeni huyo atoke nje kidogo tu ya Addis Ababa na aanze kukutana na wenyeji – hapo atapigwa butwaa kushuhudia umasikini wa kupindukia uliojikita katika maeneo yote.

KIBARUA KIGUMU NA CHANGAMOTO LUKUKI

Katika suala la kuendeleza demokrasia pia Abiy ana kibarua kikubwa pamoja na ahadi anazotoa. Kwa mfano wachunguzi wa mambo wanasema bado haifahamiki ni vipi anaweza kufanya uchaguzi huru na haki wa vyama vingi wakati serikali yake aliyoirithi, ambayo ni muungano wa vyama kadha, ndiyo inadhibiti karibu taasisi zote za umma na kushikilia viti vyote Bungeni?

Katika uchaguzi wa 2015 Muungano wa vyama chini ya Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF) kilichoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Hailemariam Desaleign ulikuwa umeshinda kwa kuzoa viti vyote 547 vya Bunge, tukio ambalo wengi hawakuamini kutokana na madai ya siku zote barani Afrika – ya wizi wa kura wa hali ya juu na uminywaji mkubwa wa demokrasia dhidi ya upinzani.

Lakini kama ilivyotabiriwa na wadadisi wa mambo ya siasa nchini humo, nchi ilishindwa kutawalika kutokana na uminywaji mkubwa wa haki na demokrasia, hali ambayo iliibua maandamano katika sehemu mbali mbali nchini karibu kila kukicha. Maandamano haya yalikuwa yanakabiliwa vikali na vyombo vya dola huku viongozi kadha wa vyama vya upinzani walitiwa mbaroni.

Hali hiyo ilijiri pamoja na kwamba utawala ulikuwa umezoa viti vyote vya Bunge na hivyo kuwa mwakilishi pekee ‘aliyekubalika’ kwa wananchi. Kwa tafsiri yoyote ile ushindi wake mkubwa katika uchaguzi ule ulikuwa bandia.

Hata hivyo Desalegn ni miongoni mwa viongozi wachache sana barani Afrika waliojiuzulu kwa hiari kutokana na changamoto nyingi nchini walizoshindwa kuzimudu. Mwingine ni Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Nyerere aliyeachia madaraka kwa hiari mwaka 1985, ingawa changamoto za nchi zilizomkabili wakati ule hazikufikia kiwango cha Ethiopia wakati wa Desalegn.

Abiy Ahmed, mrithi wa Desalegn, ni wa kutoka muungano wa vyama hivyo hivyo unaotawala na ambaye bila kusita alishika ‘tawi la mzeituni’ kwa wapinzani. Alianzisha kampeni kubwa ya maridhiano ya kisiasa na alianza kwa kuwaachia watu mbali mbali wa vyama vya upinzani – wakiwemo viongozi wa chama cha Oromo Federalist Congress Party, Merera Gudina na Bekele Gerba waliowekwa kizuizini na utawala uliopita wa Desalegn.

MKUTANO WA MARIDHIANO NA WAPINZANI

Aliwaita katika makazi yake ya Jubilee Palace mjini Addis Ababa viongozi wa vyama vya upinzani (wakiwemo wawili hao), viongozi wa dini, viongozi wa asasi za raia na watu wengine mashuhuri katika jamii.

Wote waliohdhuria walipongeza hatua hii ya kukutanishwa na waziri mkuu mpya kwa kusema kwamba ilikuwa ni njia sahihi na walimuomba kutimiza ahadi yake aliyoitoa katika hotuba yake baada ya kuapishwa kwake — ahadi ya kufungua wigo wa demokrasia nchini.

Katika hotuba ile Abiy Ahmed alikiri kwamba utamaduni wa demokrasia nchini humo haukuwa unaendelezwa jinsi inavyotakiwa. Alisema: “Nakiri nchi yetu haikufika mahali ambapo mitazamo tofauti ya kisiasa inavumiliwa, mahali ambapo usawa mbele ya sheria unahakikishwa kufuatana na katiba, na mahali ambapo iwapo kuna haki inayokiukwa na watawala, kuna utaratibu wa kuwawajibisha wanaofanya hivyo.”

Aliongeza: “Nchi yetu haikufika mahali ambapo haki za kisiasa na za kiraia kama vile haki ya uhuru wa mikusanyiko chini ya katiba inaheshimiwa.” Wadadisi wa mambo wanasema waziri Mkuu Ahmed ana vizheni kubwa iliyotakata kwani aliona nchi ilikuwa inaelekea kusiko.

Masuala ya siasa na amani, ambayo yana uhusiano mkubwa, ndiyo masuala yanayouumisha kichwa nchi nyingi Barani Afrika kwani migogoro mbali mbali ikiwamo ile inayozua vita vya wenyewe kwa wenyewe inakosa ufumbuzi – na hivyo kulifanya Bara la Afrika – pamoja na utajiri wake mkubwa wa mali ya asili – kubaki nyuma katika masuala mengi ya maendeleo. Hii huthibitishwa na takwimu mbali mbali zitolewazo kwa kulilinganisha na Mabara mengine.

Kwa kuhofia kile kinachoweza kuwafika kutoka kwa watawala watarajiwa, watawala wengi waliopo madarakani wamekuwa hawakubali katu kuachia ngazi hivi hivi, na demokrasia waliyolazimishwa baada ya miongo kadha ya utawala wa kidikteta wa chama kimoja wameifinyanga ili iwahakikishie kubakia madarakani. Wako tayari kuziingiza nchi zao katika mfarakano mkubwa, pamoja na vita ya wenyewe kwa wenyewe kuliko kuachia ngazi na hatimaye wakajikuta wanasimamishwa vizimbani.

AU YASHINDWA KUSIMAMIA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA

Umoja wa Afrika AU haiwezi kutatua mgogoro wowote Barani hapa kwani wengi wa viongozi wake wamejikita katika uporaji wa mali za wananchi wao. Umoja huo umeanza mtindo wa kulindana – yaani kama kiongozi mmoja wa nchi mwanachama kazusha mfarakano nyumbani kwake kutokana na masuala ya demokrasia na chaguzi, basi viongozi wenzake katika AU humlinda kwa kutumia njia ya kutomkaripia. Tofauti moja kubwa ilijitokeza kule Gambia.

Lakini hebu fikiria: Katika viongozi wa nchi 53 zinazounda Umoja huo, ni vigumu kupata angalau hata viongozi watano ambao wako madarakani nchini mwao kwa njia ya demokrasia iliyo ya wazi na inayokubalika, na kwamba uchaguzi wake ulikukuwa hauna dosari hata kidogo.

Na hapa neno “uchaguzi” namaananisha uhuru wa siasa katika uwanja ulio na usawa (level playing field) uandikishaji wa wapiga kura usio na dosari, tume huru za uchaguzi ambazo huendesha usimamizi wa haki wa uchaguzi — usimamizi usiokuwa na upendeleo, na kadhalika, na kadhalika.

Mimi nadhani idadi ya viongozi watano niliyotaja kwamba walipatikana kupitia uchaguzi halali ni wengi sana. Sasa kama hali ni hiyo, kuna kiongozi gani wa nchi mwanachama wa AU anayeweza kudiriki kumwambia mwenzake “wewe bwana uliiba kura nchini mwako.”

AU ilipoanzishwa, na kwa kuzingatia udhaifu na mapungufu yaliyokuwapo katika chombo kilichotangulia, yaani Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kulionekana umuhimu wa kuwapo kwa namna ya viongozi wa nchi kujiwekea nidhamu.

Ukawekwa mkataba wa hiari (Peer Review Mechanism) baina ya nchi wanachama kama mpango wa kujiratibu wenyewe kwa wenyewe kwa lengo la kuwepo kwa usawa katika masuala ya siasa, uendeshaji wa utawala bora na uchumi, na maadili yaliyo safi.

Kwa bahati mbaya mpango huu ulifeli mtihani wa kwanza kabisa wakati wa mgogoro wa uchaguzi nchini Madagascar mapema mwaka 2002. Mgogoro huo haukuwa na tofauti sana na ule wa Kenya wa 2007. Kiongozi wa zamani Didier Ratsiraka, aliyeshindwa uchaguzi na mpinzani wake Marc Ravalomanana, hakuonyesha maadili mema ya kuachia ngazi.

Na hata hivyo kulikuwepo mgawanyiko mkubwa ndani ya viongozi wa nchi wanachama wa AU kwani kuna baadhi yao, kama vile Rais Levy Mwanawasa wa Zambia (marehemu), walimmuunga mkono Ratsiraka.

Mgogoro ulikuja kutatuliwa na nchi iliyokuwa koloni la nchi hiyo, Ufaransa, ilipofanikiwa kumshawishi (pia inasemekana kwa kutumia misuli kidogo) Ratsiraka abakie uhamishoni nchini mwake (Ufaransa).

Hii inadhihirisha moja kwa moja kwamba nchi za nje, hususan za Magharibi na hasa zilizokuwa makoloni ndiyo bado zenye uwezo wa kutatua migogoro inayoanzishwa na watawala wa hovyo Barani humu. Ufaransa kwa mfano imekuwa inaingilia sana katika kutatua migogoro ya kisiasa katika makoloni yake ya zamanikama vile Mali na Chad.