Home Makala Kimataifa Ethiopia yawapa nafasi kubwa wapinzani

Ethiopia yawapa nafasi kubwa wapinzani

2553
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Katika hali ya kawaida iliyozoeleka Barani Afrika mtu anaweza kusema utawala wa sasa wa Ethiopia unazidi kufanya kufuru katika kuvunja, au tuseme kwenda kinyume na utamaduni na miiko ya tawala nyingi yanapokuja masuala ya demokrasia na uendeshaji wa chaguzi.

Katika mstuko mwingine wiki mbili zilizopita, utawala huo wa Addis Ababa, ulifanya kile kisichofikirika Barani Afrika – ulimteua kiongozi wa upinzani kuongoza Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Na nyuma ya mambo yote haya ya kushangaza ni kiongozi wa sasa, Waziri Mkuu Dr Abiy Ahmed ambaye viongozi wenzake wengi Barani humu wanaweza wakasema hakika huyu anatakiwa akapimwe akili, kwani si bure, atathubutuje kufanya ‘dhambi’ kubwa kama hii? Kuwapa wapinzani nyenzo kuu ya kushinda chaguzi na hata kutawala milele?

Lakini suala hilo ni moja tu miongoni mwa mengi yanayoshangaza medani ya demokrasia – si nchini Ethiopia tu, bali hadi nchi za nje – tangu kiongozi huyo ashike madaraka miezi saba tu iliyopita.

Ni kama vile Mwenyezi Mungu kaichagua Ethiopia kutoa nuru kwa nchi nyingine barani Afrika katika kuleta demokrasia halisi na kulinda haki za binadamu ili kupata maendeleo ya kweli katika bara ambalo limejaliwa maliasili nyingi lakini likakosa uongozi stahiki.

Ikumbukwe kwamba Waziri Mkuu aliyemtangulia lHailemariam Desalegn  alijiuzulu ghafla baada ya kushindwa kuiongoza nchi hiyo iliyokuwa inaelekea kukosa umoja na hivyo kuibua ghasia nyingi, pamoja na nguvu kubwa ya dola iliyotokana na chama chake cha EPRDF kushinda viti vyote vya Ubunge katika uchaguzi wa 2015, ushindi wengi waliuona ulitokana na hila, ghilba na wizi mkubwa wa kura. Viti vyote vya ubunge halafu hakuna umoja nchini?

Hatua nyingine alizochukua Dk Ahmed baada ya kushika madaraka ni kurudisha uhusiano na Eritrea, nchi ambayo ilipigana nayo vita vikali katika miaka ya 90, kuteua asilimia 50 ya wanawake katika Baraza la Mawaziri na mwanamke kuwa Mkuu wa Mahakama ya juu kabisa nchini humo (Supreme Court).

Tuendelee na maajabu ya kiongozi huyu kijana wa miaka 42 tu: Aliwafungulia viongozi wote wa kisiasa waliokuwa magerezani, akawaita kwenye mazungumzo katika Ikulu yake na pia kutoa wito wa kurejea nchini viongozi wote wapinzani waliokimbilia nchi za nje kwa sababu za kisiasa.

Miongoni mwao ni Bi Birtukan Mideksa, aliyewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, na baadaye kuwa kiongozi wa muungano wa vyama vikuu vya upinzani. Siasa za upinzani baadaye zilimlazimisha kukimbilia uhamishoni Marekani kwa miaka saba lakini sasa ndiyo ameteuliwa kuongoza Tume ya Uchaguzi, na hivyo atasimamia uchaguzi ujao wa 2020.

Mideksa alikuwa miongoni mwa viongozi kadha wa upinzani waliotiwa mbaroni na kuhukumiwa jela baada ya vurugu za uchaguzi wa 2005 ambao ulisababisha vifo vya mamia ya waandamanaji mjini Addis Ababa waliokuwa wakidai kuwepo kwa wizi wa kura. Wapinzani waliingia barabarani baada ya Kundi la Watazamaji wa EU kutangaza kwamba kulikuwa na udanyanyifu mkubwa katika uchaguzi ule.

Kuna watu wanaweza kudhani kwamba Birtukan Mideksa si kiongozi halisi wa upinzani – ni kibaraka tu wa utawala – sawasawa na viongozi wa upinzani ambao ni rafiki kwa utawala, na hivyo basi uteuzi wake ni kiini macho tu cha utawala kwa wapinzani. Lakini historia yake inapingana vikali na muono huo.

Ni mmoja wa waasisi wa muungano wa vyama vya upinzani (Coalition for Unity and Democracy – (CUD) – muungano ambao ulifanya vizuri katika uchaguzi wa 2005. Lakini hata hivyo alikamatwa na kushitakiwa kwa uhaini na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela. Wakati ule alionekana shujaa na kujichotea huruma kutoka kwa wengi – kwani akiwa gerezani alikuwa ametenganishwa na binti yake mchanga.

Julai 2007 aliachiwa huru baada ya kuwa jela miezi 18, kwa msamaha wa Rais lakini msamaha huo ulitenguliwa Desemba 2008 na hivyo kurudiswa tena gerezani ambako alikaa kwa miezi 21. Katika kipindi hiki inaelezwa mara kadha alikuwa akifungiwa kwa vipindi virefu kwenye chumba cha peke yake (solitary confinement).

Lakini kabla ya duru la pili la kifungo chake alianzisha chama cha upinzani cha (Democracy and Justice (UDJ). Aliachiwa kwa mara ya pili Oktoba 2010 miezi minne baada ya “ushindi wa kimbunga” wa chama tawala. Mwaka uliofuata alijiuzulu siasa na kwenda Marekani ambako alisoma katika chuo maarufu cha Harvard.

Baada ya kuteuliwa kwake kuwa mkuu wa tume ya uchaguzi Mideksa alisema ana imani uzoefu wake kama jaji wa mahakjama Kuu utamsaidia kutatua mizozo ambayo itaibuka katika wadhifa wake huo mpya na kwamba anaamini kabisa Waethiopia wengi wako tayari kwa mabadiliko – wako tayari katika kujenga mfumo wa kidemokrasia wanaoutaka na kuiwajibisha serikali. Alisema ana uhakika na hilo kutokana na hatua kadha ambazo zimechukuliwa kuelekea njia hiyo.

Alizitaja baadhi ya hatua hizo za serikali ya Dk Abiy ni pamoja na urekebishwaji wa mifumo ya taasisi za umma kuwa za nguvu katika utendaji wake bila ya hofu ya kuingiliwa na dola.

Baada ya uchaguzi wa 2005 uliofuatiwa na ghasia kubwa na mwingine miaka kumi baadaye (2015) ambao utawala ulizoa viti vyote vya Bunge, vyama vya upinzani vimekuwa vikidai marekebisho katika sheria za uchaguzi hususan katika kuipa Tume ya Uchaguzi hadhi inayostahiki, uhuru zaidi na kuwapa imani kwa wapigakura.

Na baada tu ya kuapishwa kwa Mikseda kama Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi, waziri Mkuu Dr Abiy aliwaita viongozi wa vyama vyote vya siasa katika mazungumzo yaliyohusu maandalizi ya uchaguzi ujao wa 2020.