Home Makala Eti nani anaandika hotuba ya Rais?

Eti nani anaandika hotuba ya Rais?

1338
0
SHARE

Na MARKUS MPANGALA

WATU 12 wameniuliza swali moja; hivi ni nani anaandika hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli. Watu 10 wameniulzia kupitia simu ya mkononi, wakitaka kumjua mtu anayeandika hotuba ya Rais wa awamu ya tano.

Miongoni mwao mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, ambaye katika moja ya mijadala yetu aliuliza swali hilo; nani anamwandikia hotuba Rais Magufuli? Ingawaje mhadhiri huyo mwenye kiwango cha Uprofesa hakuelekeza swali hilo moja kwa moja kwangu, lakini nilikuwa miongoni mwa walengwa kwenye mjadala huo kwani alihitaji majibu yangu pia.

Hata hivyo sikuwa na jawabu maridhawa la kuwaridhisha watu hao, badala yake nami nikaanza kufikiri jambo hilo; eti nani anaandika hotuba za Rais Magufuli? Sikupata jibu, ila nilianza kufuatilia ili nijiridhishe.

Kati ya watu hao ni mmoja pekee ambaye alinifuata kwa maongezi ya ana kwa ana.  Ilikuwa Alhamis Septemba 15, mwaka huu ambapo Mchungaji mmoja alipofanya ziara ya ghafla ofisini kwangu. Mchungaji huyo ni rafiki yangu wa siku nyingi, lakini hakunifahamisha kuwa angenitembelea.

Baada ya salamu za, ndipo alinibandika swali lilelile ambalo watu 11 walioniuliza awali. Mchungaji huyo alikuwa mtu wa 12 kati ya walioniuliza; nani mwandishi wa hotuba za Rais Magufuli? Aliniambia ile hotuba ya Rais Magufuli aliyoitoa Kisiwani Zanzibar husuani ziara ya Pemba ilikuwa mbovu.

Sikuweza kutoa jawabu la moja kwa moja zaidi ya kuinamisha kichwa changu chini ili kuvuta tafakuri jadidi, sambamba na kutafuta jawabu la kumridhisha mchungaji huyo. Natambua kuwa licha ya uchungaji ni miongoni mwa vijana wenye upeo mkubwa wa kufikiri na mchambuzi mahiri wa masuala ya kijamii, kiroho, kisiasa, utamaduni na uchumi.

Aghalabu amekuwa akichambua masuala mbalimbali kila anapopata wasaa. Lakini ajenda yake ya swali la mwandikaji wa hotuba ya Rais lilinipa wakati mgumu. Upesi nilifikiria wale 11 ambao waliniuliza jambo hilo, lakini hadi leo sikuwahi kuwapa jawabu.

Nitawapa jawabu gani kama sijui nani anaandika hotuba za Rais? Nitawapa jawabu gani nami siyo mwanasiasa, maana wao hawakosi majibu hata kama yanakuwa mabovu na upuuzi. Nami nimebeba ujumbe wa watu hao 12 na kuwawekea leo wasomaji wa safu hii; eti nani anaandika hotuba za Rais Magufuli?

Wakati ninauliza swali hilo, wengine walinikumbusha juu ya Hotuba ya kwanza ya Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005. Walinikumbusha jina la Januari Makamba, kwamba ndiye alikuwa mwandishi wa hotuba za Rais katika awamu ya kwanza ya miaka mitano (2005-2010).

Baadaye Januari Makamba aliondoka Ikulu na kugombea ubunge katika jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu waziri wa Sayansi na Teknolojia.

Mwaka 2015 Januari Makamba aliwania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM, lakini aliishia kuingia tano bora ambayo iliwajumuisha Bernard Membe, Balozi Amina Salum, Dk. Asha-rose Migiro na John Magufuli.

Kwa sasa Januari Makamba ni Mbunge wa Bumbuli na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Muungano na mambo ya mazingira akisaidia na kijana mwenzake, Luhaga Mpina.

Wakati ninakumbushwa nafasi ya awali ya Januari Makamba, nikaelezwa pia aliyekuja kuchukua nafasi yake ni nani? Hata hivyo nilikosa jawabu kwakuwa moyoni sikupata kulifahamu jina lake zaidi ya kuambiwa kuwa alitokea Chuo cha Diplomasia na kuwa msaidizi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe kabla ya kijana huyo kupelekwa kuwa msaidizi na mwandishi wa hotuba za Rais.

Nisingeweza kutoa majibu hayo moja kwa moja kwakuwa isingelikuwa jambo lenye afya njema kuwahadaa waulizaji. Nilibaki na tafakuri hii moyoni, wala halikuwa lengo langu kuliandika kwenye safu hii.

Kutokana na mgandamizo wa mawazo ya swali hilo, na namna ambavyo hotuba za Magufuli zinavyotolewa nimeonelea isiwe vibaya msomaji wangu na mimi tukitafakari hilo kwa leo. Ni matumaini yangu kuwa waulizaji wanayo nia nzuri kwa Rais wao Magufuli. Kama wanayo madukuduku yao mioyoni kwa hakika siwezi kukata kiu zao bila kuwashirikisha wasomaji wengine wa hapa safuni.

Kwamba kwanini watu hawa wamtafute mwandishi wa hotuba za Rais Magufuli? Je hotuba za Rais Magufuli ni mbovu kwa kiwango gani? Eti ni kweli Rais anafoka na kukaripia au kutishi chochote? Ama niambiwe kuwa Rais anatoa kauli thabiti na msimamo wake binafsi badala ya serikali yote?

Je, mwandishi wa hotuba za Rais ndiye anamwambia kuwa Rais awe anatoa hotuba za binafsi badala ya ujumla wa ‘serikali yetu’? Kwamba wananiambia mwandishi wa hotuba za Rais ndiye anayemwambia Rais aseme “serikali yangu”?

Nami najiuliza kwani maneno ya ‘serikali yangu’ au ‘serikali yetu’ yanabadilisha mantiki ya kile anachowasilisha? Hivi mwandishi wa hotuba za Rais anayo nafasi gani kwa umma? Kwamba anawezaje kumharibu Rais katika hotuba zake? Kwamba anawezaje kumfanya Rais kuwa mahiri kwenye hotuba? Je umahiri wa Rais kwenye hotuba zake ndiyo jawabu la mwisho la ubora wa kazi zake?

Tujiulize, kama upo umuhimu wa mwandikaji wa hotuba za rais basi tuambizane faida na hasara zake. Tuambizane ubovu wa hotuba ya Rais unatokana na nini; Rais mwenyewe au mwandikaji wa hotuba?

Na kama mwandikaji wa hotuba hapewi nafasi yake ipasavyo kumsimamia Rais kutoa hotuba murua, inayobembeleza, kulainisha, kuhuzunisha, kufurahisha au namna nyingine yoyote tutamlaumu au kumpongeza Rais? Chukulia mfano Rais anatoa hotuba isiyoandikwa kokote, je nini jukumu la mwandishi wa hotuba za rais kumpika bosi wake awe anatoa hotuba zenye umahiri hata upande mwingine wakapiga makofi na kushangilia?

Je, hotuba pekee inamfanya Rais kuwa mahiri? Sina jawabu la uhakika, kwakuwa ninaendelea kutafakari kama hotuba za Rais wetu Magufuli ni mbovu au mahiri. Sina jawabu kama mwandikaji wa hotuba za Rais ni mahiri au hafai. Nabaki kutafakari, ni nani huyo anayeandika hotuba za Rais John Magufuli? Anapewa umuhimu wake? Anatekelezaje majukumu yake? Na hapo ndipo tunapoishi Mawazoni.