Home Makala FCC: WATANZANIA WENGI WANANUNG’UNIKA BILA KUCHUKUA HATUA

FCC: WATANZANIA WENGI WANANUNG’UNIKA BILA KUCHUKUA HATUA

1385
0
SHARE
Baadhi ya maofisa wa FCC wakikagua mojawapo ya bidhaa bandia walizozikamata

NA GABRIEL MUSHI


MARA nyingi tunanunua vitu na bidhaa mbalimbali bila kuzifahamu au kuzichunguza vyema. Hili limesababisha watu wengi kununua bidhaa zisizofaa kwao au zenye madhara kwenye afya zao.

Kutokana na ukosefu wa elimu pamoja na kuishi kwa mazoea, watu wengi hawajui wala hawachunguzi vyema bidhaa wanazozinunua ili kuhakikisha ubora wake.

Matokeo yake watu wengi huishia kunung’unika kuwa bidhaa fulani si nzuri ni bandia, na mwisho wa siku hawachukui hatua yoyote.

Iwapo Watanzania wangekuwa na mazoea ya kulalamika na kuacha kunung’unika maana yake wangechukua hatua ikiwa ni pamoja na kuifanyia uchunguzi bidhaa husika na kuifikisha katika vyombo vya kiuchunguzi na kisheria kama vile Tume ya Ushindani nchini (FCC).

Kwa kuwa ni wachache wanaochukua hatua katika kuvisaidia vyombo husika kuzuia uingiaji na matumizi ya bidhaa bandia nchini, hali bado inakuwa tete kutokana na ukuaji wa teknolojia duniani.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na Shirikisho la viwanda (CTI) Juni mwaka jana, unaonesha kuwa asilimia 50 ya bidhaa kama vifaa vya maofisini, dawa,vyakula na vifaa vya ujenzi vinavyonunuliwa nje na kuingizwa Tanzania ni bandia.

Kaimu mwenyekiti wa CTI, Evasist Maembe alifafanua kuwa bidhaa hasa zinazonunuliwa kutoka China, Vietnam, Singapore, Afrika Kusini na kadhalika zimetambulika kutokuwa za asilia.

Katika kupunguza kasi ya ongezeko la bidhaa bandia nchini, Tume ya Ushindani nchini (FCC) imekuwa ikitoa elimu kwa wadau kada mbalimbali ikiwamo waandishi wa habari ili kuendeleza gurudumu la kuzuia na kutokomeza bidhaa bandia na kujenga mazingira shindanishi ya kibiashara nchini.

Ofisa Mtetezi wa Walaji Mwandamizi wa tume hiyo, Joshua Msoma anasema wateja wa bidhaa wanapaswa kuwa wadadisi ili kubaini bidhaa bandia zinazoingizwa kinyemela au kutengenezwa kwa kuiga.

Anasema FCC imebaini kuwa baadhi ya vifaa bandia vinavyoongoza kwa sasa ni vya ofisini (stationery) ambapo vinaongoza sokoni kwa asilimia 23 vikifuatiwa na vya ujenzi kwa asilimia 18 na umeme asilimia 16. Aina za bidhaa ambazo zinaongoza kwa kughushiwa ni wino wa printa, simu na televisheni.

Haki na wajibu wa mlaji

Aidha, pamoja na mambo mengine Msoma anasema mlaji au mteja anazo haki nane muhimu ambapo iwapo mlaji akizitambua vema huenda tatizo hilo la bidhaa bandia linaweza kupungua.

“Kwanza mlaji ana haki ya kupata mahitaji muhimu yanayomwezesha kuishi kama vile chakula, malazi na mavazi, haki ya usalama ambapo mlaji hulindwa dhidi ya bidhaa na huduma zisizo salama ambazo zinaweza kuangamiza mali zake, kumjeruhi na hata kuhatarisha afya na maisha yake.

“Pia ana haki ya kupata taarifa au maelezo sahihi na kamili kuhusu bei, ujazo na malighafi zinazounda bidhaa zinatakazomwezesha kufanya uchaguzi wa kununua bidhaa sahihi ya kulipia huduma bora badala ya kurubuniwa na matangazo na vifungashio vinavyopotosha.

“Haki ya kuchagua bidhaa na huduma mbalimbali katika soko, haki ya kusikilizwa katika masuala ya sera, mipango na maamuzi yanayowahusu au yanayoweza kumuathiri, haki ya kutatuliwa malalamiko yake kuhusu bidhaa na huduma hafifu, zisizo salama, ghali kupita kiasi na dhidi ya utendaji wa soko unaokandamiza.

“Haki ya mazingira mazuri na endelevu yasiyohatarisha maisha na uhai wake na mwisho haki ya kupata elimu itakayomwezesha kufanya muamuzi kuhusu bidhaa na huduma akiwa na ufahamu na uhakika wa maamuzi yake,” anasema.

Pamoja na kutambua haki zao, pia mlaji anapaswa kutambua wajibu wake ili kusaidia FCC na  mamlaka nyingine kuzibaini bidhaa hizo bandia na kuziteketeza kwa mujibu wa sheria, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha afya za walaji.

Akifafanua kuhusu wajibu wa mlaji anasema kwanza mlaji anapaswa kuwa makini na kuuliza maswali kuhusu bei na ubora wa bidha na huduma ili kuhakikisha kuwa anatendewa haki katika kununua bidhaa na huduma, kutumia bidhaa na huduma inavyostahili jkwa kuzingatia athari katika mazingira zinazotokana na mfumo wa matumizi ya bidhaa na huduma.

“Mlaji ana wajibu wa kujenga uwezo wa ushawishi na utetezi kwa mlaji, kusoma maelekezo na kuchukua tahadhari ili kuzingatia usalama wake wakati anapotumia bidhaa na huduma kama ilivyoelekezwa, kutafuta na kutumia taarifa kabla ya kufanya manunuzi ili kuhakikisha kuwa wakati wote anafanya maamuzi ya kununua baada ya kupata taarifa kamili kuhusu bidhaa au huduma husika.

“Pia anapaswa kufanya juhudi za kuwezesha maoni yake kufahamika kupitia vyama vinavyotetea masilahi ya mlaji, kupigania kuzingatiwa kwa uborawa bidhaa kupitia utaratibu thabiti wa uwasilishaji wa malalamiko na kugoma kununua bidhaa hafifu.

“Mwisho kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kuwa makini katika kuchagua na kutumia huduma na bidhaa. Hii inahusisha pia kuchukua hatua za kupunguza taka na kubadili matumizi ya taka kwa ajili ya matumizi mengine pale inapowezekana.

Msoma anabainisha kwamba umakini wa aina hiyo utasaidia kulinda masilahi ya walaji kwa sababu watanzania wengi wananunua bidhaa kwa kuwa wana fedha.

“Ndio maana walaji au watanzania wengi ni wanung’unikaji si walalamikaji kwa sababu mlalamikaji huchukua hatua dhidi ya vitendo dhaifu. Yaani hawatafuti taarifa za bidhaa kama bei halisi, ubora, ila hulalamika wanapobaini tofauti na walichokitarajia. Ni wajibu wao kufahamu kila kitu kuhusu chochote wanachonunua,” anasema.

Jinsi ya kutambua bidhaa bandia

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Utetezi wa Mlaji na Bidhaa Bandia kutoka FCC, Godfrey Gabriel anasema udhibiti wa bidhaa bandia nchini unatekelezwa kwa mujibu wa sheria ya alama za bidhaa ya mwaka 1963.

Anasema bidhaa hizo zimeainishwa kuwa ni matumizi yasiyosahihi ya jina au kifupi cha jina katika bidhaa, maelezo ya bidhaa yasiyo sahihi na matumizi ya alama zilizoghushiwa au alama za udanganyifu katika bidhaa.

Aidha, anafafanua kuwa mambo yafuatayo ni muhimu katika kukagua uhalisia wa bidhaa ambayo ni ufungashaji wa bidhaa, uandishi wa jina la bidhaa au nembo, usanifu wa mwishi wa bidhaa, bei ya bidhaa ambazo mara nyingi huwa na punguzo la bei, maelezo ya bidhaa ambapo mara nyingi bidhaa bandia hukosa maelezo muhimu.

“Alama maalumu za utambulisho hukosewa pamoja na malalamiko kutoka kwa mzalishaji asilia kwani mara nyingi bidhaa zinazolalamikiwa na mzalishaji asili huwa hazijatengenezwa na wazalishaji halisi.

Mikakati ya udhibiti wa bidhaa bandia

Katika kuendeleza kudhibiti uingiaji wa bidhaa bandia nchini, Afisa Mwandamizi, Elimu kwa mlaji na mawasiliano kutoka FCC, Franki Mdimi anasema kwa kuwa wananchi wengi hutegemea zaidi vyombo vya habari katika kufikia maamuzi ya msingi yanayowaathiri katika maisha yao, ni wajibu wa vyombo vya habari kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu athari, udadisi na haki za mlaji kuhusu matumizi ya bidhaa mbalimbali wanazozitumia.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Dk. John Mduma anasema pamoja mambo mengine, katika kuhakikisha kuwa mlaji analindwa vema aidi Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendesha mashauriano na jadiliano kwa ajili ya kutunga sera ya Taifa ya mlaji ityakayotoa dira ya masuala ya msingi ya kuboresha muundo wa utetezi wa mlaji nchini.

“Matarajio ya matokeo ya mchakato huo ni pamoja na kupunguza kujirudiarudia kwa majukumu katika eneo la utetezi wa mlaji katika taasisi za serikali zinazoshughulikia utetezi wa mlaji,” anasema.