Home Makala FEDHA NI NYENZO MUHIMU KWA VYAMA VYA SIASA

FEDHA NI NYENZO MUHIMU KWA VYAMA VYA SIASA

675
0
SHARE
Maandamano na mikutano ya kampeni na uhamasishaji wa wapigakura hutumia fedha nyingi kwa vyama husika.

NA HILAL K SUED


Kuna nukuu moja maarufu ya Groucho Marx, Mmarekani mcheza sinema mchekeshaji (comedian) aliyeishi karne iliyopita. Siku moja alikuta watu njiani ambao walitumia muda mwingi kuisifia nyumba moja ya kifahari iliyokuwa karibu na ufukwe wa bahari.

Baada ya muda aliwasogelea na kuwaambia: “Nawahakikishia hiyo nyumba si chochote si lolote. Hebu ondoa tu bahari, na uone iwapo uzuri wake utaendelea kuwepo.” Nitaeleza kwa nini nimeleta nukuu hii.

Miongoni mwa habari kuu zinazoenea kwenye vyombo vya habari – magazetini na kwenye mitandao ya jamii zikiwanukuu viongozi wa vyama vya upinzani na watu wengine ni kuhusu hali mbaya ya kifedha serikalini, ingawa serikali imekuwa inakana kuwepo kwa hali hiyo.

Hata hivyo wakati haya yakiendelea kuna gazeti moja maarufu (kwa maana la kuwepo miaka mingi) limekuwa na mtindo wa kila baada ya siku mbili hivi kuandika habari za ‘kufilisika’ kwa kiongozi mkuu wa chama kimoja cha upinzani.

Kwa mtazamo wangu naona harakati za gazeti hilo ni kujaribu ‘kuiosha’ serikali na/au kuhamisha mjadala – kutoka kile kinachozungumzwa kuhusu utawala – kwamba kama ni suala la kufilisika, basi kiongozi huyo wa upinzani na pengine chama chake ndiyo wanafilisika.

Nalazimika tu hapa kutaja kwamba gazeti hilo hivi karibuni limeokolewa na wamiliki wake kutokana na hali mbaya ya kifedha baada ya kuingilia kati mmiliki wake mkuu – chama kilichopo madarakani – CCM.

Hata hivyo nimelazimika kuweka kitangulizi hiki kutokana na ukweli kwamba fedha ndiyo msingi mkubwa wa kuendesha karibu kila kitu – serikali, makampuni, taasisi, familia na na vyama vya siasa pia. Pasipo na vyanzo vya uhakika vya mapato basi mambo yanakuwa si shwari.

Kuna usemi kwamba fedha si kila kitu – yaani huwezi kupata kila unachokitaka kwa pesa. Kwa upande mmoja huu ni ukweli pia, lakini pia ni ukweli kwamba ni bora ukawa na fedha kuliko kutokuwa nazo.

Kwa upande wa serikali si tatizo kubwa kwa sababu sheria zinaiwezesha kukusanya mapato kutoka vyanzo mbali mbali. Tatizo linakuja tu pale ambapo kunatokea usimamizi mbovu wa ukusanyaji kodi, sheria mbovu zisizokidhi hali, ufisadi pamoja na matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa.

Na kwa vyama vya siasa – bila fedha haviwezi kujiendesha kwa sababu ada kutoka kwa wanachama ni kitu kilichokuwapo enzi zilizopita – tena kwa vyama vyote. Angalia vile vyama vidogovidogo visivyokuwa na ruzuku kutoka serikalini. Vipo vipo tu, na baadhi yao vipo kwa sababu ya kutumika katika kazi fulani fulani tu, vinginevyo havina uhalali wowote wa kuwepo.

Wakati wa ujio wa vyama vingi serikali iliweka ruzuku kwa vyama baada ya kutimiza vigezo fulani kimojawapo ni kuwa na Wabunge. Lakini kwa ule uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi, mbali na CCM, vyama vya upinzani vilivyoanzishwa na kusajiliwa havikuwa na Wabunge hivyo serikali ilitoa fedha kwa vyama vilivyokuwa na usajili kamili na ambavyo vilisimamisha angalau wagombea wa Ubunge majimboni.

Baada ya uchaguzi huo ruzuku ilikuwa inatolewa tu kwa vyama vyenye Wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na kiwango kilitegemea idadi hiyo pamoja na idadi ya kura za mgombea urais wa Jamhuri katika uchaguzi uliopita. Serikali ya CCM iliweka uwepo wa ruzuku bila shaka baada ya kukifikiria chama chake kwanza (CCM) – wapi kitakuwa kinapata fedha za kujiendesha. Kwani huko nyuma enzi wa mfumo wa chama kimoja CCM ilikuwa inapewa fedha kutoka Hazina.

Na ndiyo maana nasema ingelikuwa sasa hivi CCM ina mapato yake yenyewe ya uhakika ya kujiendesha, utawala wa Awamu hii ya John Magufuli, kutokana na azma yake ya kubana matumizi ya serikali ingefutilia mbali ruzuku kwa vyama. Hata hivyo pengine ni mapema mno kuyasema haya.

Lengo kuu bila shaka ingekuwa kuhakikisha kwamba kama njia nyingine za kukwamisha maendeleo na ukuaji wa vyama vya upinzani hasa katika siasa za nguvu ya hoja zikishindikana, basi silaha iliyobaki ni kuona vinakauka kifedha.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 iliyoppita CCM ndiyo kilikuwa kinatamba katika medani ya siasa nchini kutokana na nguvu ya fedha. Katika chaguzi zote zilizopita fedha ndiyo ilikuwa inaamua mshindi, katika ngazi zote za uchaguzi kuanzia udiwani kwenda juu. Lakini kutokana na nukuu ile ya Groucho Marx hebu fikiria tu iwapo chama hicho kisingekuwa na fedha.

Nitatoa mfano. Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Chadema haikuwa na fedha za kukiwezesha kuweka wagombea katika majimbo yote 239 ya uchaguzi, wakati CCM iliweza kufanya hivyo. Chadema iliambulia kupata viti 24 tu vya ubunge wa majimbo.

Lakini kutokana na kura alizopata mgombea wake wa urais – Dk Wilbrod Slaa – chama hicho kiliweza kujihakikishia ruzuku kutoka serikalini ya zaidi ya sh 200 milion kwa mwezi – kutoka shs 31 milioni ilizokuwa ikipata nyuma – yaani kabla ya 2010.

Ghafla chama hicho kiliweza kuboresha uwezo wake wa kujieneza na kugombea nafasi mbali mbali hususan katika chaguzi ndogo ndogo za Ubunge na Udiwani kwa kutoa ushindani mkali kwa CCM.

Baada ya uchaguzi wa mwaka juzi 2015 ruzuku kwa Chadema iliongezeka maradufu ya ile iliyopita kutokana uwingi wa Wabunge waliopatikana na kura za mgombea wake wa urais.

 

Inaelezwa kwamba mwishoni mwa miaka ya 90, ujumbe wa UNIP – chama kilichokuwa kikiongozwa na Kenneth Kaunda nchini Zambia, na kilichokuwa chama swahiba kwa CCM, kilialikwa kuhudhuria mkutano wa vyama vya siasa katika nchi moja Barani Afrika (sitaitaja jina). Ujumbe huo ulifikia katika hoteli moja ya daraja la nne katika eneo la hali ya chini la mji husika.

Ujumbe wa CCM (ambao pia ulikuwa unahudhuria mkutano) ulipofahamu habari hizi, ulifanya kila waliloweza kuwahamisha wajumbe wale wa UNIP na kuwaweka katika hoteli na sehemu nzuri.

Hata kama stori hii haina ukweli, lakini ukweli ni kwamba chama hicho (UNIP) kiko nyikani kisiasa, na hakitaweza kurudia hali yake ya zamani kilipokuwa madarakani – kikiitisha mikutano mikubwa mikubwa ya enzi za ‘Mulungushi’ ya kutumia mamilioni ya fedha. Sasa hivi kwa kuwa hakipo madarakani, basi hakina fedha – na kinyume chake pia – kwamba kwa kuwa hakina fedha basi pengine ndiyo kinashindwa kuingia madarakani. Nukuu ya Groucho Marx ya nyumbo kando ya bahari.

Hakika mfano huo wa UNIP umekuwa somo kubwa kwa CCM, chama kilichokuwa swahiba wake na hivyo kinafanya kila namna nacho kisijikute katika hiyo hali.