Home Makala FIDEL CASTRO 1926 – 2016: AMEACHA THIBA YA MAPINDUZI ITAKAYODUMU KARNE...

FIDEL CASTRO 1926 – 2016: AMEACHA THIBA YA MAPINDUZI ITAKAYODUMU KARNE NYINGI

678
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Fidel Castro alitumia kipindi cha maisha yake yote kupambana na ‘dola’ kubwa ya ubeberu, udhalimu na ukandamizaji. Ingawa kifo chake wiki iliyopita kinaweza kuwa alama ya mwisho wa yeye kama binadamu, hakika kinazalisha thiba (legacy) ambayo bila shaka itadumu kwa karne kadha zijazo.

Itakuwa vigumu kuelewa kikamilifu uzito wa thiba aliyoiacha Castro kutokana na ukubwa wa kile alichokuwa akikisimamia na kukitetea – hasa katika kukata minyororo ya mamilioni ya watu wa mataifa mbali mbali katika Ulimwengu wa Tatu – minyororo iliyokuwa imewafunga kifikra na kihalisia.

Aliweza kufanya hivyo huku akijua anawakasirisha mabeberu, wabaguzi wa rangi na watetezi wa itikadi hiyo duniani kote

Kuanzia pale alipoongoza mapinduzi yaliyofanikiwa kumng’oa dikteta swahiba mkuu wa utawala wa Washington – Fulgencio Batista mwaka 1959, si tu aliendelea kuandika historia, bali hasa kuijenga na kuirutubisha historia hiyo kwa miongo kadha iliyofuatia.

Mara ya kwanza kabisa alipopanda kwenye jukwaa la siasa za dunia akiwa na umri wa miaka 30 tu kama kiongozi wa Mapinduzi ya Cuba, akiingia mji wake mkuu wa Havana akiwa juu ya kifaru alichokiteka huku akiwa hakunyoa ndevu na nywele hazikuchanwa, haidhaniwi iwapo yeye na wanamapinduzi wenziwe walijisimika kama waanzilishi wa ukurasa mpya katika kuuendeleza itikadi ya nchi za Dunia ya Kusini (Global South).

Wakiwa na uthubutu mkubwa, ushujaa na imani iliyopitiliza, waliweza kuhakikisha kwamba minyororo ya unyonyaji, dhulma na ukandamizaji, ambayo ilikuwa imeweka makovu katika maisha ya vizazi vingi vya nyuma kabla yao inakatika, na badala yake kuweka mazingira ya uwepo wa haki, heshima na udugu miongoni mwao.

Mwaka 1959 Dwight Eisenhower ndiyo alikuwa Rais wa Marekani na ilikuwa bado miaka miwili kuzaliwa kwa Rais wa sasa, Barack Obama. Tangu hapo marais kumi wa Marekani wamepita na majaribio mia kadha ya kutaka kumuua Castro yalifanyika, lakini yote hayo yalishindwa kumshinda.

Baadhi ya majaribio hayo yalikuwa ya ajabu sana. Kwa mfano katika miaka ya 60 Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ilipanga jaribio la kumpulizia dawa ndevu zake ili zisiote tena, kwani walidhani ndevu zake ndizo zilikuwa zinamfanya apendwe na watu wake.

Isitoshe hata dakika moja hakuogopa au kunywea na kurudi nyuma na hivyo kuachana na yote yale ambayo yeye na wenzake waliyasimamia katika kuwakomboa Wacuba kutoka katika pingu za kisiasa na za kiuchumi zilizokuwa zikiwekwa na watawala wa Washington.

Ushahidi kwamba moto wa mapinduzi na uthubutu wa Castro bado alikuwa nao pamoja na umri wake kuanza kumpa mkono, ulidhihirishwa wakati alipotoa karipio kali kama majibu kwa Obama baada ya rais huyo wa Marekani kutoa hotuba yake kwa viongozi wa Cuba alipotembelea nchi hiyo mapema mwaka huu kufuatia uimarishaji wa mahusiano baada ya miaka mingi ya sintofahamu baina ya nchi hizo mbili zinazotenganishwa na kilomita 200 tu za bahari.

Obama alionekana kutoa ‘somo’ kuhusu demokrasia na haki za binadamu kwa utawala wa Cuba na katika majibu yake katika makala yake ya maneno 1,500 yaliyochapishwa katika gazeti la serikali la ‘Granma’ Castro aliwakumbusha Wacuba na dunia nzima kwa ujumla kuhusu historia iliyojaa dhulma kubwa siyo tu kuhusu uhusiano wa Marekani na Cuba, na pia uhusiano wake na Bara la Afrika ambalo ni asili ya Obama mwenyewe.

Castro aliandika: “Hakuna mtu atakayeweza kujifanya haoni na kupuuza tunu za utajiri mkubwa wa kiroho ambayo Wacuba wamefaidika kutokana na maendeleo katika nyanja za elimu, sayansi na utamaduni.

“Pia napenda kuonya kwamba tuna uwezo wa kuzalisha chakula cha kututosheleza kutokana na uwezo mkubwa wa watu wetu na rasilimali zilizopo. Hatuhitaji hata dola moja ya Marekani au kutupatia kitu chochote.”

Hata alipoanza kufikia mwisho wa maisha yake Castro hakuwa na muafaka wowote kuhusu maelewano mazuri na Marekani. Angebadilisha vipi msimamo wake wakati uzoefu wake wa miaka mingi ulikuwa ni wa kuona harakati za Marekani katika kukandamiza maisha na uhuru wa mamilioni ya watu duniani, wengi wao wakiwa watu wa rangi na dini nyingine?

Ukubwa wa ‘kivuli’ cha Castro kilichofunika matukio ya dunia katika kipindi cha zaidi ya nusu karne ni ushahidi tosha wa yeye alivyokuwa mshawishi mkubwa katika masuala mbali mbali ya dunia hii.

Na hakuna zao kubwa la ushawishi huu kama lile lililotokana na mchango mkubwa wa Cuba katika kuutokomeza ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini.

Ingawa kwa sababu zinazoeleweka Cuba haitajwi kwenye historia rasmi inayotambuliwa na nchi za magharibi kuhusu mapambano dhidi ya ubaguzi ya nchi hiyo, ukweli ni kwamba ni vigumu sana kupuuza mchango wa Fidel Castro na Cuba. Na hakuna mtu mwingine pasi Nelson Mandela mwenyewe, hadi anaingia kaburini alikuwa anaupigia saluti mchango wa Castro katika ukombozi wa nchi yake.

Na kama Mandela mwenyewe alivyosema alipotembelea Cuba mwaka 1991 wiki chache baada tu ya kutoka kifungoni: “Watu wa Cuba wametwaa sehemu maalum katika mioyo ya watu wa bara la Afrika. Wanamapinduzi wa Cuba wamechangia sana katika harakati za ukombozi wa Afrika, na kuwepo kwa haki na uhuru.”

Vikosi vya kijeshi vya Cuba vilivyopelekwa Angola katika miaka ya 70 na 80 na mafanikio yao katika kuuvunja ubabe wa siasa za kibaguzi wa Weupe wachache uliokuwa ukiungwa mkono na Marekani na nchi nyingine za Magharibi ni mfano wa mchango mkubwa wa Cuba kwa wanaukombozi wote dunuiani.

Kiukweli kabisa kuna mifano mingi sana ya kuonyesha msimamo wa Castro isiyoyumbishwa katika uungaji wake mkono wakandamizwaji dhidi ya wakandamizaji na pengine itahitaji kitabu kizima kuyaelezea yote hayo.

Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba, Nelson Mandela, Malcolm X, Che Guevara, Camilo Cienfuegos, Bobby Sands, Ben Bella – orodha ya wanamapinduzi kutoka sehemu mbali mbali waliojitokeza na kuondoka duniani wakati wa uhai wa Fidel Castro ni ushahidi mwingine tosha wa ushawishi mkubwa aliokuwa nao Castro wakati wa uhai wake.

Lakini pengine sehemu kubwa ya thiba ya Castro ni namna alivyoweza kubadilisha maisha ya mamilioni ya Wacuba katika nyanja za elimu, sayansi, afya, na utamaduni wakati huo huo kukiwepo vikwazo vikubwa vilivyowekwa na Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa lengo la kuipigisha magoti nchi hiyo ya kisiwa.

Na hata baada ya kusambaratika kwa iliyokuwa Urusi ya Kisoviet mapema miaka ya 90 – nchi ambayo ilikuwa ni swahiba wake mkubwa na hivyo kuifanya Cuba isimame peke yake katika ‘bahari’ ya ubepari, mapinduzi ya nchi hiyo yalidumu bila kutetereka.

Na hiki ni kielelezo cha jamii ambayo Cuba ilizalisha – jamii ambayo watu wake walielewa tofauti kati ya kugawana kile walichobakiza na kugawana kile waliokuwa nacho.

Alisema Fidel Castro: “Mapinduzi ni mapambano hadi kufa baina ya wakati ujao na wakati uliopita.”

Ingawa kiongozi huyo amefariki, mawazo yake ambayo aliyapigania katika maisha yake yote bado yataendelea kuishi, siyo nchini mwake tu, bali popote pale ambako ubeberu na unyonyaji wa watu dhaifu unaofanywa na wenye nguvu ndiyo hali ya maisha.

 

  • Makala hii imetayarishwa kwa msaada wa vyanzo mbali mbali vya Intaneti.