Home Habari Figisu zaanza Uchaguzi Serikali za Mitaa

Figisu zaanza Uchaguzi Serikali za Mitaa

1046
0
SHARE

CCM waanza kupigana vikumbo, wapinzani watamba kwenda na ajenda tatu

FARAJA MASINDE – DAR ES SALAAM

JOTO la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji linazidi kupanda, huku figisu zikianza kutawala ndani ya vyama kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi za uenyekiti na kamati ya mtaa.

Hatua hiyo inatokana na baadhi ya wanachama wanaotajwa kugombea nafasi hizo ndani ya CCM kuanza figisu za uchaguzi ikiwamo kucheza rafu.

Taarifa zinaeleza kuwa vurugu zimetokea katika Mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Makurumla, Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam ambako mmoja ya wana-CCM wanaotajwa kutaka kugombea uenyekiti wa mtaa, amekuwa akigawa vinywaji kwa vijana kwa lengo la kujenga ushawishi kwa wapigakura wa ndani ya chama.

Hatua hiyo inaelezwa ilikwenda sambamba na vijana kupita mitaani na kuanza kuwashambulia wana-CCM wenzao kwa maneno na matusi ya nguoni kwamba hawatakiwi.

Wakati hayo yakiendelea, ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), inaonyesha leo utafanyika uteuzi wa maofisa uandikishaji wapigakura nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa sheria, Tamisemi kupitia waziri mwenye dhamana, Selemani Jafo, ndio wasimamizi wa uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo, utawala wa kijiji hutajwa kuwa miongoni mwa tawala katika Serikali za mitaa nchini.

Pia uongozi wa ngazi ya mtaa hutajwa kama utawala wa chini kabisa kimuundo ukitanguliwa na utawala wa kitongoji.

Ratiba hiyo ya uchaguzi inaonyesha kuwa kwa upande wa CCM uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba kugombea uenyekiti wa mtaa unaanza Oktoba 7 hadi 12.

“Kamati za siasa za matawi zitajadili wagomnbea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati ya siasa ya kata Oktoba 13, mwaka huu.

“Pia Kamati ya Siasa ya Kata itajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Siasa ya Wilaya Oktoba 14 na 15, mwaka huu.

“Oktoba 19 hadi 20 mikutano ya kura za maoni ya nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa/Kijiji ambapo wahusika ni wanachama wote wa CCM wa kila tawi,” ilieleza ratiba ya CCM ambayo imeshushwa kwa viongozi wote wa matawi.

Ratiba ya Serikali inaonyesha kwamba Oktoba 8 hadi 14 kazi ya uandikishaji wapigakura itafanyika kwa muda siku saba kwa wakazi wa mtaa husika.

Baada ya hapo, Oktoba 20 itaanza kazi ya kuchukua fomu za wagombea wa nafasi ya mwenyekiti wa mtaa na kutakiwa kurejesha mwisho Novemba 4.

KAULI YA CCM

RAI ilimtafuta Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni CCM, Pereira Ame Silima, ambaye alikiri kupokea malalamiko ya baadhi ya viongozi wa kata na matawi kudaiwa kuandaa watu pamoja na kuwachafua wengine.

Alisema kuwa CCM ina kanuni zake ambazo zinatosha kushughulikia suala hilo.

“Ni kweli tumepokea malalamiko yaliyowasilishwa na baadhi ya wanachama wetu wakiwataja baadhi ya viongozi kuandaa watu na kuchafuliwa, lakini kanuni zetu tulizonazo zinatosha namna ya kushughulikia suala hili,” alisema Silima.

SIFA ZA WAGOMBEA

Desemba 30, mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally alitaja sifa za wana-CCM ambao watateuliwa kuwania nafasi za uongozi wa kitongoji, kijiji na mtaa.

Dk. Bashiru alisema mwanachama atakayejihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa chama hicho tawala kusaka wagombea wake katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, atapoteza sifa za kugombea.

Alisema kila kiongozi wa CCM atakayejitokeza kugombea uenyekiti wa kijiji au mtaa, lazima awe mwadilifu na mwaminifu.

Alibainisha kuwa baadhi ya wagombea wanatumia majukwaa kupinga rushwa licha ya kuwa wanajihusisha nayo, ikiwa ni pamoja na kukiuka maadili ndani ya chama.

“Makatibu wa CCM kila ngazi hata nyie msiwe wa kupokea rushwa kupitisha majina ya wagombea wasiokuwa na sifa, lazima kiongozi afuate miiko na ahadi za mwanachama,” alisema Dk. Bashiru.

KAULI YA JPM

Julai mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa Katoro na Buseresere mkoani Geita, Rais Dk. John Magufuli aliwataka Watanzania kutumia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 kuwachagua viongozi wazuri na si watoa rushwa.

“Mwaka huu tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, chagueni viongozi wazuri, msichague viongozi wanaowapa rushwa, mkikosea kuchagua madhara yake ni makubwa.

“Mkasimame imara katika kuchagua viongozi ambao mnafikiri wataweza kunisaidia pia, na kunishauri vizuri,” alisema Rais Magufuli.

SERIKALI YA MTAA

Utawala wa Serikali ya Mtaa huelekeza wananchi katika kutumia madaraka yao ya kidemokrasia kuamua juu ya mambo yanayowahusu kama wanakijiji moja kwa moja bila kupitia mlolongo au urasimu mrefu.

Kwa mujibu wa sheria, inaelekezwa kwamba kila baada ya miaka mitano kunakuwa na Mkutano Mkuu Maalumu wa Uchaguzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji au Mtaa.

Mkazi wa kijiji au mtaa anayegombea nafasi ya uongozi kwenye halmashauri ya kijiji au uenyekiti wa kijiji lazima awe na umri usiopungua miaka 21.

HOJA ZA UPINZANI

Akizungumzia uchaguzi huo ikiwamo suala la kuanza kwa uandikishaji, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji,  alisema kuwa kama chama wanaamini kuwa ratiba itafanyiwa kazi kama ilivyotolewa na kwamba hawatarajii mambo kwenda kinyume.

“Sisi kama Chadema tumejiandaa vizuri kuelekea kwenye uchaguzi huu ambao tayari kipyenga chake kimepulizwa, hivyo tunaendelea kufuatilia ratiba ya uchaguzi kama inavyoelekeza, kwa hiyo hatuna hofu kabisa.

“Hivyo kwa kuwa uchaguzi tayari umepangwa, sisi kama Chadema tuna mikakati minne tu ya kuingia kwenye uchaguzi huu, kwanza ni chama cha siasa ambacho tayari tunacho, hivyo lazima tushiriki uchaguzi, pili ni wagombea tulionao, ambapo tumepanga kuweka wagombea hadi vijijini bila hata ya kuacha mtaa.

“Lakini mkakati wa tatu ni ajenda, kwani tuna ajenda nzuri ambayo ninaamini kuwa itakuwa na mashiko zaidi kwa Watanzania ambayo ni Freedom democracy and Market Economy (uhuru wa demokrasi na uchumi na masoko) pamoja na mkakati wa mwisho ambao ni rasilimali fedha,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema pia kwa sasa wapo katika harakati za kuunganisha nguvu na vyama vingine vya siasa ambavyo vitakuwa vimekosa wagombea katika uchaguzi huo.

CUF NA KUENGULIWA

Mkurugenzi wa Habari, Itikadi na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya, alisema hawatarajii kuona muujiza wowote ukitendeka dhidi yao kwa kile alichodai kuwa asilimia kubwa ya waandikishaji hao wanatoka CCM.

“Tunajua kuwa hakuna jambo jipya ambalo litafanyika kwa haki dhidi yetu, kwani tunafahamu fika kuwa hata hawa waandikishaji wenyewe ni wale wale wana-CCM, lakini haina maana kwamba hatushiriki uchaguzi, hapana, kwani kama unavyojua CUF ni chama kikubwa na tuna wabunge wengi maeneo mbalimbali. ikiwamo Pemba na maeneo mengine, hivyo hatuwezi kuacha nafasi,” alisema Kambaya.

Alisema shaka yao kubwa imekuwa ni juu ya kuenguliwa kwa wagombea wao jambo ambalo anaamini kuwa litatokea tu kutokana na rekodi.

“Unajua ni lazima niwe mkweli kwenye hili, kwani kuna utamaduni ambao ni kama umeanza kuzoeleka kuona kwamba CCM imekuwa na mchezo wa kuengua wagombea wa vyama pinzani kwa madai kuwa hawana sifa za kushiriki uchaguzi na hayo ndiyo mashaka yetu makubwa, lakini kama hawatatumia mbinu hiyo basi tunao uhakika wa kufanya vizuri,” alisema.