Home Latest News FRANK MWAKAJOKA: UTEKELEZAJI HAFIFU WA BAJETI CHANZO CHA KUDORORA KWA UCHUMI

FRANK MWAKAJOKA: UTEKELEZAJI HAFIFU WA BAJETI CHANZO CHA KUDORORA KWA UCHUMI

5622
0
SHARE
NA GABRIEL MUSHI    |  

FRANK Mwakajoka ni mmoja wa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Mendeleo (Chadema), ambao wamefanikiwa kunyakua majimbo yenye hamasa kubwa ya upinzani kwa sasa.

Mbunge huyo ni wa jimbo la Tunduma ambalo awali kati ya madiwani 20, madiwani 19 walikuwa wa Chadema na mmoja wa CCM, hii imeonesha wazi kuwa ni kwa namna gani jimbo hilo limekuwa ngome ya upinzani.

Hata hivyo, Tunduma wamesalia na wabunge 14 wa Chadema kutokana na sababu mbalimbali ambazo Mwakajoka anaendelea kuzidadavua katika mahojiano yafuatayo.

RAI: Uongozi wa Rais John Magufuli umetimiza miaka miwili na ushee, unazungumziaje hali ya kisiasa nchini?

MWAKAJOKA: Ni dhahiri kila Rais na zama zake, ila hali hivi sasa imekuwa tofauti sana. Ameminya demokrasia na zipo sababu nyingi ikiwamo uhuru wa kujieleza, vyama vya siasa kunyimwa fursa ya kufanya mikutano ya hadhara, ukikosoa serikali kwa njia yoyote kama kwenye mitandao unakamatwa. Nasema hivyo kwa sababu watu wengine tu wako rumande. Haya ni mambo yanadhibitisha demokrasia inaminywa.

Vilevile ukija kwenye suala la mikutano na Bunge kutooneshwa ‘live’ pia ni jambo ambalo limewanyima wananchi fursa ya kujua nini wawakilishi wao wanachozungumza ilhal yeye Rais kila anakokwenda anaoneshwa live. Ingawa wanasema wanarekodi alafu yanarushwa usiku naoana ni jambo la kulaghai wananchi kwa sababu saa nne usiku sio wote wataweza kutazama.

RAI: Vikao vya Bunge la bajeti vinaendelea sasa kwa wizara kuwasilisha bajeti za mwaka 2018/19, ni ipi tathmini yako kuhusu bajeti ya mwaka 2017/18?

MWAKAJOKA: Hakuna kinachoendelea katika utekelezaji wa bajeti hizo, kwa mfano mwaka jana kwenye bajeti ya wizara ya afya mwaka uliopita 2017/18 tunaona kuwa vifo vya mama na mtoto vingepaswa kupungua kutoka 444 hadi 229 katika kila vizazi 100,000.

Lakini huwezi kuamini katika bajeti hii vifo vimeongezeka na kuwa 556, ina maana ukipeleka kina mama 100,000 zaidi ya 444 wanaoenda kujifungua hufariki. Sasa bajeti imeleta manufaa gani hapo.

Ukiangalia kwenye bajeti hiyohiyo tulitenga Sh bilioni 10 kwa ajili ya watu wenye VVU ila cha ajabu hakuna hata senti tano iliyotolewa. Hii yote ni utekelezaji wa chini ya kiwango kabisa. Bajeti hii kwa ujumla imetekelezwa kwa asilimia 23. Sasa hatuoni umuhimu wala sababu ya kusema serikali inakwenda vizuri.

Ukija kwenye bajeti ya wizara ya ujenzi, fedha nyingi zilitengwa ila nyingi hazikutolewa na hazina licha ya kwamba sekta ya mawasiliano na uchukuzi inachangia Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 29. Huwezi kuamini mwaka jana kwenye sekta ya mawasilianio tulitenga bilioni 14 lakini haikutolewa hata shilingi moja.

Hii ni dalili mbaya kabisa na inaonesha serikali haina malengo ya kutatua kero za wananchi ikiwamo kubadilisha hali zao za umaskini wa watanzania.

Kwa mfano Shirika la ATCL inafahamika tangu mwaka 2015 limeingiza hasara kubwa Taifa, lakini bado wanajaza fedha kule na bajeti ya mwaka jana lilitengewa bilioni 500 na mwaka huu limetengewa Sh bilioni 495.

Ni kweli tunahitaji ndege ila majukumu mengine lazima yaendelee kutekelezwa hasa ukizingatia asilimia 75 ya watanzania ni wakulima.

Ukija tena kwenye sekta ya kilimo mwaka 2017/18, tulitenga bilioni 101 lakini walipewa bilioni tatu tu. Sasa iweje kwenye ATCL utenge bilioni 500 alafu kilimo utoe bilioni tatu hii ina maana kuwa bajeti ya kilimo imetekelezwa kwa asilimia 11 tu.  Sijui hii serikali ni wanyinge wa aina gani inataka kuwasaidia.

Na hatujui hizi fedha zinakwenda wapi. Ndio maana hata ukiangalia kwenye taarifa za CAG mapendekezo aliyotoa hayafanyiwi kazi. Kwa wastani tunaona mapendekezo anayoyatoa CAG hayatekelezwi kwa sababu ukiangalia ripoti ya mwaka 2017/18 kati ya maagizo 38 ni manne tu yametekelezwa tena yale yasiyokuwa na athari kubwa.

RAI: Katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliani mwaka huu 2018/19, ilikumbwa na vikwazo vingi ikiwamo baadhi ya wabunge kudai ujenzi wa reli ya kisasa umekiuka malengo ya awali. Hili unalionaje?

MWAKAJOKA: Ninaona kwanza kuna athari kubwa kwa Taifa, kwa sababu huko tunapoelekea tutatumia fedha nyingi halafu tutashindwa kupata faida kutokana na reli hii.

Awali reli ilipangwa kuishia Msongati lakini sasa wanapeleka hadi Rwanda tena kwa kulenga eneo la DRC kaskazini ambako hakuna hali ya usalama, ni dhahiri kuna ushawishi mkubwa wa wenzetu umefanyika lakini ni ukweli usiopingika kuwa kutoka Rwanda kuelekea Kongo kuna vita kubwa hakupitiki, hivyo naona bado itakuwa hasara kubwa kwetu.

RAI: Unazungumziaji utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano?

MWAKAJOKA: Utendaji wa Rais Magufuli bado naona uko chini ya kiwango kwa sababu utendaji si kusema maneno au kuonesha huruma kwa jambo ulilolitekeleza, tunapenda rais anasema na kumaanisha. Kama utekelezaji wa bajeti, kuwepo na uwazi, kwa mfano ukiangalia Bunge la bajeti wabunge wa CCM wamefungwa midomo hawawezi kusema, wengi wanashika shilingi (wanataka kuzuia bajeti) lakini mwishoni wanaachia kwa shingo upande unawaona kabisa kwa sababu sio kwamba hawana akili.

Ukiangalia CAG mapendekezo yake hataki kuyajibu badala ya kupeleka fedha kwenye kilimo unaenda kununua ndege wakati wananchi wako hawana masoko ya mazao, hawana pembejeo sasa ndege za nini.

Kwa mfao ukiangalia suala la viwanda, wanalazimisha mifuko ya hifadhi ya jamii kuwekeza kwenye viwanda wakati ukiangalia uwezekano wa viwanda kufa upo, je, vikifa hizi fedha za wanachama zitarudishwaje, haya ni baadhi ya mambo ya kujiuliza kuhusu maamuzi yake.

Kuhusu sera ya viwanda, kwanza niseme wazi kuwa hakuna mtu asiyependa viwanda, kwani vinaongeza pato la nchi na ajira, lakini usitamke tu kuwa unataka kuwekeza kwenye viwanda lazima kuwepo na mazingira wezeshi kwani tukiangalia leo mazingira ya kibiashara yamekuwa magumu.

Kwa mfano wafanyabiashara wanahama nchi, sio kwamba wanakimbia nchi hapana!  wanahamishia biashara zao Zambia. Watanzania wengi wanahamia katika miji ya Lusaka, Kitwe, Mwinilunga ambako wametengewa maeneo maalumu na kupewa miundombinu yote.

Ukienda pale Tunduma pale Idara ya Uhamiaji unakuta msururu wa Watanzania waliovuka kwenda Zambia. Zambis wameweka masharti nafuu kwa wafanyabiashara.

Ili kufanikisha uwekezaji kwanza ni kuweka mazingira mazuri kwa sababu mwekezaji akija hapa akiuliza hali ya biashara tu anapata jibu kuwa hali ni mbaya kuanzia mahotelini mpaka kwa hata mama ntilie.

Bado kuna migogoro mikubwa kati ya wafanyabiashara na serikali. Mfumo wa kodi bado haupo wazi, hivyo kwa hali kama hiyo usitegemee kuwa na viwanda.

RAI: Kumekuwapo na wimbi la watu kutekwa na wengine kudaiwa kuuawa, hii inaleta taswira gani kwako kama mmoja wa wabunge wa upinzani?

MWAKAJOKA: Tunaamini serikali hii haitaki kukosolewa, kwani licha ya watu kutishiwa au kuuawa cha ajabu hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.  Ukiangalia ni kweli kila mtu anatishiwa baada ya kuisema serikali ndani ya Bunge, ni dhahiri serikali inataka kuwafunga watu midomo, haina uwazi na ukweli ndio maana inazuia watu kusema kwa sababu kama ina uwazi haiwezi kuzuia watu kusema

RAI: Unazungumziaje tukio la mdogo wake Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche kuuawa?

MWAKAJOKA: Ni tukio baya halina ishara nzuri kwenye nchi kama kweli polisi wanaweza kumkamata mwananchi wakaondoka naye halafu akauawa tena kwa kuchomwa kisu,  ni dhahiri tulipofikia inaonesha uweledi wa jeshi  letu haupo sawasawa. Hilo ni tendo la ajabu sana kwani kwa askari ambaye amefunzwa haiwezekani kutenda tendo la aina hii.

RAI: Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hadi mwaka huu tumeshuhudia wimbi kubwa la wapinzani kuhamia CCM kwa madai ya kumuunga mkono Rais Magufuli, vipi kwa upande wa jimboni kwako hali ipoje?

MWAKAJOKA: Hizi siasa za kijinga kwa sababu serikali iliyopo madarakani ingeleta siasa za kiushindani na si kununua madiwani. Hali hii inaleta picha kwamba serikali ya CCM imeamini wapinzani wana nguvu, kwani tuna uhakika madiwani wananunuliwa.

Tunduru wamenunuliwa madiwani watano, kati ya madiwani 19 wa upinzani na sasa wamebaki 14. Tulikuwa na madiwani jumla 20 akiwamo wa CCM mmoja ambaye sasa amepata wengine watano walionunuliwa kwetu.

Jana nimeambiwa bado wanaendelea kuwashawishi madiwani wahamie CCM, sasa kinachonichangaza ni kwamba nchi hii wanaiongoza wao, wana rais, mawaziri wakuu na wabunge.

Wabunge tuko wote pamoja bungeni tunasimamia serikali eti mtu anajitokeza anasema namuunga mkono Magufuli wakati maiaka 56 sasa hakuna kilichopatikana chini ya CCM. Naona kama wanafanya utani kwani nchi hii isipojengwa lazima CCM ilaumiwe.

RAI: Ni ahadi gani ulizoahidi wananchi wako na umefanikiw akuzitekeleza?

MWAKAJOKA: Niliahidi kuwa muumini wa elimu kwenye jimbo langu, na mpaka sasa tumejenga shule za msingi nane na shule za sekondari nne, pia nimenunua mifuko 250 ya saruji kwa ajili ya ukarabati wa shule mbalimbali.

Hizi shule nne za sekondari hazijaanza kutumika kwa sababu mbalimbali ikiwamo mgogoro uliokuwapo wa baraza la madiwani.

Kikao cha baraza la madiwani hakijakaa tangu mwaka jana Agosti  kwa sababu mkuu wa wilaya kwa kushirikiana na mkuu wa mkoa walimwambia mkurugenzi asitishe vikao vya baraza kwa sababu ya kutoelewana kati ya mwenyekiti wa baraza na mkuu wa wilaya.

Kwa mujibu wa sheria, serikali za mitaa sio wakala wa serikali kuu, ni serikali kamili ambazo hukaa na kuiamua mambo yao wenyewe, kwa mujibu wa katiba zimeweka mamlaka ya mipaka na ambao watakuwa wanasimami serikali za mitaa ni madiwani katika maeneo yao.

Baraza la mji wa Tunduma walitengeneza bajeti ya mwaka 2017/18, ikapitishwa kuanzia vikao vya serikali za mitaa, ODC, Halmashauri, DCC vya mkuu wa wilaya na RCC – mkuu wa mkoa ambaye pia ana ushauri wake kuhusu vipaumbele vya serikali.

Hivyo kama kuna marekebisho tunaweza kuwasiliana na mkuu wa mkoa kwani mbunge na mwenyekiti wa baraza la madiwani wanaingia kwenye kikao cha RCC. Licha ya kwamba vipaumbele vyetu vilipitishwa na Bunge na RCC lakini Mkuu wa wilaya akataka kubadilisha jambo ambalo halikuwezekana kwani huwezi kubadilisha muelekeo wa bajeti wakati imeshapitishwa labda mpaka Bunge lijadili tena upya.

Ndipo vikao vikasitishwa, ila sasa waziri mkuu ameshazungumza na waziri wa Tamisemi na ameagiza baraza lianze mwezi ujao ambapo tayari maagizo yametoka na waziri husika amenihakikishia kuwa wiki ijayo baraza linaanza kukaa vikao vyake.

Sasa haya ni mambo yanayokwamisha kwa sababu tu wanaona mji unaongozwa na upinzani, ni moja ya mambo yanayokwamisha maendeleo ili tu kuwalazimisha madiwani wahamie upande wa CCM. Na kama tunavyoona sasa hizi shule hazikumaliziwa kwa sababu ya mambo kama haya.

Kuna suala la huduma za maji, Mji wa Tunduma kwa kweli kuna shida ya maji, licha ya kuomba miradi mikubwa ya maji hadi sasa miradi mikubwa haikufanikiwa na imefanikiwa miradi midogo midogo saba ambayo kwa hakika naona bado haiwezi kutatua taizo la maji Tunduma.

Vilevile kwenye barabara licha ya kupigania upanuzi wa barabara na kutengeneza barabara mpya zaidi ya 33 bado hakuna fedha ya kukarabati barabara hizi kwa sababui wakala ambao ni Tarura wanapewa fedha ndogo sana, asilimia 30 ilihali Tanroad asilimia 70.